Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtambile
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-wa-ta‟ala amenijalia uzima na afya njema, nikapata nafasi au fursa ya kuchangia machache kwenye hotuba hizi mbili; hotuba ya Mheshimiwa George Boniface Simbachawene na Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nataka nimkumbushe ndugu yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, wakati akitoa maelezo kwamba Bunge lililopita tulipitisha sheria kwamba Bunge hili lisioneshwe live, watu waliokwambia walikudanganya. Siyo kweli, ulikuwa ni uongo wa mchana kweupe bila giza. Hakuna mahali iliyopita hata mara moja kwamba ilifika wakati sisi kuna taarifa hiyo ilipita, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nashukuru sana kwa mujibu wa kitabu cha Mheshimiwa George Boniface Simbachawene ukurasa wa 74, ameelezea mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ufuatiliwaji wa taarifa za fedha juu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; pili, Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti...
KUHUSU UTARATIBU....
MWENYEKITI: Sawa. Mheshimiwa Masoud tuendelee, utatoa baadaye uthibitisho huo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kutokana na tabia hiyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo kwenye kitabu cha Mheshimiwa George, Waziri huyu ameelezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna tatizo kubwa ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; Serikali Kuu ukurasa wa 304 imeelezea kilio, deni ambalo Tanzania tunatakiwa tulipe la shilingi bilioni 90 juu ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kulipa kampuni ta China ya Wallys.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jipu la kwenye kichogo au kisogo, kwa maana nyingine jipu hili halionekani. ATCL iliingia mkataba na kampuni ya Sonangol kutoka China katika miaka iliyopita kwamba ingeleta ndege saba, tano zikiwa aina ya airbus na ndege mbili ndogo. Baadaye kampuni hii ya Kichina ya Sonangol ilimtaarifu kampuni mwenzake ya Wallys kwamba iweze kuleta ndege hapa Tanzania, lakini nini ambacho kilitokea? Ndege iliyofika ilikuwa moja tu aina ya airbus na ndani ya hapo ndege hiyo ilipofika hapa Tanzania ilikaa kwa muda wa miezi sita kwa sababu ndege hiyo ilikuwa ni mbovu. Baadaye hiyo ndege ikachukuliwa mkaipeleka Ufaransa; kufika Ufaransa ndege hiyo mpaka leo haijarudi. Ndege hiyo iko wapi Serikali? Mtuambie ndege hiyo mpaka leo iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi kufika Ufaransa ndege hiyo ilipakwa rangi nyingine kwa nchi ya Guinea na rangi tunaambiwa iliyopakwa hatuelewi kama ilikuwa ni ya kijani au manjano, hatuelewi. Baadaye mtatuambia; lakini ndege hiyo ilipakwa rangi nyingine na ndege hiyo mpaka leo haikurudi, lakini cha kujiuliza ni kitu gani? Ni kwa nini kulikuwa na uharaka mkubwa kupita kiasi katika mikataba hii? Ina maana tunadaiwa shilingi bilioni 90 hivi sasa. Hilo ni jipu kubwa, kwa nini mnalifumbia macho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaposema sisi upande huu wa pili tunaambiwa kwamba ninyi mnapinga hiyo ndiyo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2015 kwenye Serikali kuu ukurasa wa 304. Hilo ni jipu, tumbueni au ni upele hamwezi kuukuna. Wahusika wapo, Mheshimiwa Waziri Simbachawene kwa nini hadi leo walioko Hazina, walioko ATCL hakuna hata mmoja aliyeulizwa? Kwa nini? Tunaambiwa tulipe sisi shilingi bilioni 90.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, nenda kwenye ukurasa wa 282 ambapo inaelezea juu ya wizi, ubadhirifu na ufisadi mkubwa kabisa. Ripoti inaeleza kwenye Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma ambapo mwenyewe Mheshimiwa Waziri ndipo anapotoka, kuna ufisadi, wizi na ubadhirifu wa shilingi bilioni 912 kwa mambo yafuatayo; hilo ni jipu au ni upele au ni uvimbe? Mtasema wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, sikiliza kwa makini sana; kuna salio ya shilingi 571,498,633 la vifaa vya dawa, mafuta na vifaa vingine vinavyotumika mara kwa mara havikuingizwa kwenye taarifa za fedha; ufisadi wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili, kuna mali zenye thamani ya shilingi 209,809,780 zilizidishwa kwa taarifa za fedha na hakuna marekebisho yaliyofanywa; ubadhirifu wa pili Mkoa wa Dodoma kwenye Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi, hapa hapa mchana kweupe.
La tatu, kuna matumizi yaliyolipwa zaidi kwa shilingi 131,049,085 kama madai ya mwaka 2014/2015 yameingizwa kwa malipo mengineyo; ufisadi mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaosema sisi tunapiga kelele, tunapinga kila kitu, hatupingi kila kitu, tuna ushahidi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, inaonesha kuna wizi, kuna ubadhirifu, ufisadi wa kutisha na hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sisi tukasemee wapi wakati Serikali ndiyo ninyi? Tutasema hapa hapa kweupe wala hatuvumilii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine haya yamekuwa ni mazoea. Mimi nikiwa Mbunge wa Bunge la Nane kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2005 jumla ya fedha ambazo zilisababishwa na wizi, ubadhirifu na ufisadi ilikuwa shilingi bilioni 4,403; watu waliopelekwa mahakamani ilikuwa ni 321; lakini cha kustaajabisha walipofika mahakamani waliambiwa kwamba wahusika hawa hawana kesi, wametoroka. Aliwatorosha nani? Walitoroka kwenye vyombo vya dola. Sasa hili ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 shilingi bilioni 2.3; mwaka 2007 shilingi bilioni 3.5; mwaka 2008 shilingi bilioni 3.1; mwaka 2009 shilingi bilioni 11.1; mwaka 2010 shilingi bilioni 12.9; wote huu ni ufisadi wa kutisha unaofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sisi tukayaseme wapi haya? Leo tunapoelezea mambo kama haya watu hawako serious, umakini wa Serikali uko wapi? Lazima tuyaseme haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora uko wapi? Tumekuwa tukisema mambo mengi ya msingi; leo hii ukiangalia manyanyaso ambayo yanatokea kwa watu wetu kule Tumbatu; na naomba nisome kwenye Ibara ya 13; “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.” Wananchi wa Tumbatu makosa yao ni nini? Unguja wamekuwa nyumba zao zikitiwa moto, hawana pa kushitaki. Lolote wanalolifanya wao kwao ni baya. Tatizo la Tumbatu ni kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ni lazima nao walindwe. Inakuwaje leo watu wetu hawa wa Tumbatu kila siku wananyanyaswa na baadhi ya watu ambao wanajulikana lakini hakuna hatua. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, fanya ziara yako uende Tumbatu. Hali hairidhishi. Hili ni jambo kubwa sana na nadhani Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani utalichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuje kwenye mafao. Ni mara kadhaa ambapo inaonekana kwamba mafao ya wastaafu wakati wa kupata haki zao wanapunjwa na hili ni tatizo kubwa. Sasa inakuwaje leo mnasema kwamba kwa mujibu wa ripoti iliyomaliza juzi mwaka 2015 kati ya majalada 1,683 wastaafu 200 wamepunjwa shilingi 385,304; je, hamjui kukokotoa? Angalieni ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ukurasa wa 99, kwa nini mwapunje na kwa nini msiwazidishie?
Mheshimiwa Kairuki, kwa nini msiwazidishie? Sasa huu ni ufisadi au siyo ufisadi? Mnawapunja, lakini watakapokufa wastaafu wale wengine ambao wana heshima zao mnakwenda pale na risala ya kutoa machozi ya uongo mtupu kweupe mchana, Marehemu alikuwa hodari, shupavu, jasiri mwaminifu na mtiifu; yeye atakumbukwa, atathaminiwa, mbona walipokuwa hai hamkuwathamini mliwapunja ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufisadi wa kutisha ni wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kama hata wastaafu hamwathamini pia mnawapunja...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Masoud muda wako umeisha, naomba ukae.