Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

Hon. Amour Khamis Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii kuwa mchangiaji wa mwanzo kabisa katika jambo hili la Kamati hii ya Kudumu ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Allah Subhana Wa ta’ala muumba mbingu na ardhi, akatuwezesha sisi kuwa Wabunge mahiri tunaofanya kazi zetu kwa umakini sana. Lakini pia nitumie fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Amefika kila eneo, kila jimbo, kila kata kupeleka maendeleo. Tunamshukuru sana, tunampongeza sana, tunampa moyo sana, ili aendelee kufanya kazi hii adhimu ya Taifa hili, kazi ya uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashukuru pia kuwemo kwenye Kamati hii, Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo. Katika vipengele ambavyo vimetajwa leo hapo na Mwenyekiti wakati akiwasilisha mada yake ni kutokutekelezwa kwa Maazimio ya Bunge. Sisi hapa tumekaa tunapitisha maazimio leo. Mfano leo, tumeshasoma na tutapitisha maazimio, kama yalivyoelekezwa katika uwasilishaji wake, na Bunge linaazimia kwamba, jambo hili lirekebishwe, litengenezwe, halafu anatokea mtu hafanyi hilo jambo kwa hiyo, hatekelezi Maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siamini kwamba kuna mtu ana nguvu hiyo, lakini labda huwa nafikiri labda amesahau au hakusikia au sijui niseme neno gani zuri. Maana maazimio tunayatoa kwa pamoja tunakuwepo humu Bungeni, watu wanasikia, wafau wenzetu wanasheria wanayachukua wanakubaliana na sisi, miezi inapita, mitatu, minne, mpaka miezi sita hajatekeleza, lengo lake huwa ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, labda wanafikiria kwamba Kamati hii ya Sheria Ndogo labda si Kamati ya kisekta, mimi huwa nafikiria vitu kama hivyo, labda si Kamati ya kisekta kwa hiyo, hawajibiki sana hivi, hana wajibu wa kuwajibika wa kutekeleza Maazimio ya Bunge kwa sababu ni watu wa sheria ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike kwamba, Kamati ya Sheria Ndogo ni sawa na kamati nyingine yoyote ya Bunge na tunaliwakilisha Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, siamini na wala sitaki kuamini kwamba kuna mtu anatubeza kiasi hicho. Sasa, kama yupo tunamuomba aache hilo jambo, aache kabisa, kwa sababu hizi tunazozitengeneza ni sheria na tunazitengeneza kwa ajili ya wananchi wenzetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora ni utawala wa sheria. Maana yake ni kwamba, kama sheria ni mbovu, zimerekebishwa na wewe hautaki, maana yake ni kwamba unabomoa utawala wa sheria ambao ndio utawala bora, kazi ambayo itakuwa inatukwaza, si jambo zuri. Na bahati nzuri sana ni kwamba, hizi sheria tayari ziko mtaani na zinawaumiza watu, ni wananchi wenzetu na sisi ni miongoni mwa wananchi. Kwa hiyo tunawaomba wale wanaohusika, wale wadau wenzetu wa sheria wanaohusika na kurekebisha warekebishe. Si vizuri mpaka Bunge lingine linakuja maazimio ya Bunge hayajatekelezwa, si jambo zuri. Lakini mimi ninaamini labda watu wanafanya hivyo kwa sababu ya yale madaraka yao, labda wale wanataka kuyalinda yale madaraka, kwamba hiyo sheria ikibadilishwa inamfanya madaraka yake yapotee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba tena kwa heshima na taadhima wale wanaohusika na kutekeleza Maazimio ya Bunge baada ya Bunge kupitisha maazimio hayo wayatekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo naunga mkono hoja na ninakushukuru kwa nafasi; ahsante. (Makofi)