Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

Hon. Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi leo nikawa mchangiaji katika Taarifa hii ya Kamati yangu ya Sheria Ndogo.

Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kunijalia nikapata pumzi hii ya kusimama hapa leo. Nisiende mbali sana kwa wingi wa shukrani hizo, naenda moja kwa moja, nijielekeze katika mchango wangu niliokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tumesikia hapa wakati Mwenyekiti wa Kamati anatuwasilishia Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo. Ni maswali ambayo hata mimi najiuliza sana, sijui ni kwa mujibu wa jina la Kamati lilivyowekwa, Sheria Ndogo, ndiyo tunapata mwanya wa kuzipuuza hizi sheria au sijui ni kitu gani kinatufanya tunapata huu mwanya wa kuzipuuza sheria hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Azimio lililotolewa na Bunge kwenye Mkutano wa Nane na wa Tisa, wote tunaweza kuona ni gap la kiasi gani hapa ambalo Wizara husika zilitakiwa kuchukua hatua na mpaka kufikia leo zilitakiwa ziwe tayari zimekamilisha. Cha kusikitisha tunamaliza Mkutano wa 10, ni miezi kadhaa hapo imepita, lakini ukiangalia bado changamoto hizi zinawakumba wananchi wetu walio kule chini, ni wapigakura wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo la wazi lisiloweza kufichika, lazima tuwe makini katika utendaji wa kazi zetu hususan kwenye sheria. Kwa mfano mmoja ambao nitautumia, katika dosari hizi ambazo zimewasilishwa hapa leo, dosari nyingi zinatoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kitu ambacho Ofisi ya Rais, TAMISEMI ndiyo wanaogusa wananchi wetu katika majukumu ya kila siku. Hakuna siku itapita mwananchi asiweze kuigusa Ofisi ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Ofisi hii ya TAMISEMI ndiyo hiyo ambayo ina mkanganyiko mkubwa na mlundikano wa sheria hizi ambazo dosari hawajataka kuzifanyia kazi. Mfano mmoja niutumie, Sheria Ndogo ya Afya ya Usafi wa Mazingira ya Halmashauri ya Igunga, Tangazo la sheria lilikuwa Na. 555 ndani ya Mkutano wa Nane wa Bunge. Kifungu cha 14(3) kinaeleza; “Iwapo abiria atatupa taka nje ya chombo cha usafiri, kosa litachukuliwa limetendwa na mmiliki wa gari, dereva ama kondakta wake.”

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho yakatakiwa ibadilishwe na kuwa hivi; “Marekebisho yafanyike katika sheria ndogo hii ili kuhakikisha mkosaji anatumikia adhabu kutokana na kosa alilotenda.” Azimio tayari hapa limeshaweka wazi. Sasa sijui Wizara ni kitu gani ambacho ilikuwa inakihitaji zaidi. Si Azimio limeshasema kwamba tuondoe mmiliki wa gari, dereva na kondakta, tumlete mtenda kosa awajibike kutumikia kosa lake. Ni nini changamoto? Kila kitu kimeshafafanuliwa tayari. Ndiyo pale pale tunarudi tunasema labda ni kwa sababu imeitwa Sheria Ndogo, lakini si inatumika kama sheria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kubwa zaidi ambayo naiona ni kwamba, bado Tanzania tunatunga sheria kwa kuangalia hapa tu. Hatutungi sheria zitakazoangalia mwaka 2025, 2026 mpaka 2030. Kwa sababu, kama ingekuwa tukitunga sheria zetu tunaangalia kitu kinachokuja mbeleni, huu mkanganyiko wa marekebisho ya Sheria Ndogo ya kila wakati, tungepunguza gap kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti kampongeza na anayo kila haki ya kupongezwa kwa ajili ya utendaji wake wa kazi. Mimi sijawahi kuwasiliana naye, sijawahi kumtafuta, lakini mchangiaji mwenzangu mmoja hapa alisema kwamba, hata ukimtafuta muda wowote ule anakuwa yupo tayari kwa ushirikiano. Ni sawa, lakini twende tukatunge sheria ambazo zitatupunguzia gap la Sheria Ndogo. Hizi Sheria Ndogo na Kanuni tuzipunguze kwa kutunga sheria zinazoendana na muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuzipe gap sheria zetu ili isiwe kila siku, kila Bunge litakalofuata tuna Sheria Ndogo. Kila siku idadi ya Sheria Ndogo inaongezeka. Nina uhakika hata kama hizi ambazo zinafanyiwa kazi ziko nyingi huku nyuma, kila siku tutaendelea kupitia sheria? Ni wakati wetu sasa, twende tukatunge sheria zitakazoendana na Tanzania ya baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, naenda kwenye Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini nayo wana jukumu kubwa sana katika nchi yetu, mapato makubwa asilimia kubwa yanatokana na Wizara ya Madini, lakini nao sheria tatu ambazo bado hazijafanyiwa kazi na ukiangalia hakuna sababu ya msingi ya kutokufanyiwa kazi sheria hizo. Mfano, kifungu cha 15 kimeweka sharti la muuzaji ama mchimbaji anapotafuta leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, samahani, Wizara ya Madini, Kanuni ya 6(2) inamtaka mtu yeyote mwenye leseni ya uchimbaji madini atoe notice ndani ya siku 90, tangu tarehe ya kutangazwa kwa Kanuni hizi ili hatua nyingine zichukuliwe, ili kuipa nafasi Wizara iweze kutangaza katika Serikali na kuhakikisha Serikali inapata hisa katika mgao huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuangalie hapa, hii imewekwa kwamba ndani ya siku 90 lakini baadaye kwenye azimio ikasema hapa kikubwa kinachotakiwa ni kitu kidogo tu, sawa! Wameweka ndani ya siku 90 lakini nini azimio lilishauri? Je, kama hizo siku 90 hakufanya hivyo? Itatakiwa kwamba Kanuni ifanyiwe marekebisho kwa kuongeza kifungu kitakachoonesha adhabu kwa kushindwa kutoa notice ndani ya siku hizo 90, jamani mambo yapo wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inarekebishwa sheria, inatangazwa, Bunge linaanza kuleta maazimio, kwa nini Wizara isitimize wajibu wao?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono Azimio la Kamati. (Makofi)