Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kusema kwa kifupi kabisa, kuchangia hii hoja iliyoletwa na Kamati ya Sheria Ndogo na suala mahususi ambalo linahusu marekebisho waliyoagiza Wizara ifanye kwenye kanuni ya ushirikishwaji wa Serikali katika biashara ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, napenda kuipongeza Kamati kwa sababu wanafanya kazi nzuri sana na walitupa fursa ya kuja kuelezea utekelezaji wa hoja hizi ambazo wamezileta leo mbele ya Bunge lako Tukufu, nasi kwa heshima kubwa kabisa tuliwaomba baada ya muda wa wiki moja na nusu tuwaite kwenye semina ambapo tutaitumia kuelezea kuhusu hizi kanuni za ushiriki wa Serikali za mwaka 2022, sambamba na kupewa majibu ya utekelezaji wa hoja ambazo walitupatia tufanye marekebisho kwenye kanuni hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya tarehe 31 mwezi wa Nane, tulipata hiyo fursa tukatoa elimu na tukawaeleza kwamba marekebisho yote tuliyoagizwa tuyafanyie kazi, tumeshayafanyia kazi, zimepita kwenye mchakato mzima wa kuhakikiwa mpaka na AG na zikarudishwa kwetu kwa ajili ya Waziri kutia Saini ili ziweze kutangazwa katika Gazeti la Serikali kupitia GN. Kwa bahati nzuri, maana sitaki kusema kwamba ni mbaya, siku ile ambayo Waziri alikuwa atoke akazisaini, Mungu akamjalia, akamwonekania, akateuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ile shughuli ya kusaini ili ziende kwenye Tangazo la Serikali likawa limesimama, na ndani ya muda huu mfupi basi, leo tumejikuta tena tupo mbele ya Bunge lako tukufu kujibu hoja ya kuonekana kama tumepuuza maagizo ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ukweli ambao Mungu anaujua, tulipokaa nao tarehe 31, tuliwaridhisha kwamba tumetekeleza, imebaki tu utaratibu wa kutangaza. Nami nafahamu kwamba Kamati hii inafanya kazi nzuri nasi tunaiheshimu kazi yao na Wizara siku zote imekuwa ushirikiano kwa Kamati za Bunge inapohitajika. Kwa hiyo, nitumie tu jukwaa hili kuihakikishia Kamati hii na Bunge lako tukufu kwamba kazi waliyotutuma tukaifanye, tumeifanya kikamilifu na kwa uadilifu wote, sema tu imechelewa kumalizika na kuja Mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na hoja ndogo ya maoni ya wadau wengine kuhusiana na kanuni hizo ambazo tulianza kuzifanyia kazi. Mwanzoni tulidhani tutatoa tangazo moja na marekebisho yote ya Kamati na wadau wengine mbalimbali yangeweza kuingizwa, lakini baada ya kuona kwamba Kamati inataka kuona utekelezaji wa jambo lao tukazileta hizo hoja zao tatu mbele, tukafanyia marekebisho iende kwenye GN ambayo ingetoka ambapo baadaye tungetoa nyingine ya ku-accommodate maoni mbalimbali ambayo wadau waliendelea kutoa kuhusiana na kanuni hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi tu, nilihakikishie Bunge lako kwamba sisi tumefanya kazi marekebisho yaliyoelekezwa na ndani ya muda mfupi tangazo hilo litakapotoka tutaweza kuziweka mbele ya Bunge lako tukufu ili wajiridhishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)