Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Allah Subhanhu Wataallah kwa kutujaalia uzima, salama na kuendelea kuijalia nchi yetu kuendelea kuwa na usalama na kutamalaki kwa maisha mema nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependaa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya yeye pamoja na Naibu Waziri Ndugu Pinda, pamoja na timu nzima ya watendaji, kwa kweli mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Tumeona maendeleo makubwa tu katika mabadiliko ya ardhi na hili nafikiria ni register shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifaya na inaonesha wazi Mheshimiwa Rais, kwa kweli anapita katika nyanja zilezile ambazo alipita Hayati Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Hayati Abeid Amani Karume, kwa kuweka usalama wa matumizi bora ya ardhi na kuwamilikisha wazawa na wananchi wanyonge kuendelea kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuelekeza mchango wangu katika maeneo matatu makubwa; la kwanza, mwenzangu jana Mheshimiwa Chege aliligusia kidogo kuhusu suala la sera. Nafikiria ni kipindi kirefu kidogo tumekuwa tukizungumzia suala la kukamilisha Sera ya Maendeleo ya Ardhi pamoja na Sera ya Maendeleo ya Makazi nchini, na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na timu yake wamefanya kazi nzuri katika hili na hadi sasa tayari rasimu ipo na kuna mabadiliko machache ambayo yanasubiriwa hasa katika suala la diaspora pamoja na watu wa real estate kuweza kulikamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa nina ushauri hapa; ushauri wangu ni kwamba nimuombe tu Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa zile changamoto ambazo zinaonekana ni ngumu kidogo kuweza kukamilika kwa haraka na kuikamilisha rasimu hii ya sera. Basi tungeendelea na mchakato tukaja tukaweka provision katika maeneo ya sheria katika maeneo ya sheria kwa kuja kuitayarisha kanuni ambayo itakuja kuwasaidia wenzetu wa diaspora pamoja na usimamizi mzima wa masuala la real estate. Hii itafanya tukamilishe hii sera haraka na kuanza kuitekeleza ili iende ikasaidie zile changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge hapa wamekuwa wakizungumza kila mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la pili nigusie kidogo kuhusu suala zima la mipaka ya kimataifa; kazi nzuri imekuwa ikifanywa katika kuainisha na kuweka mipaka katika maeneo mbalimbali lakini bado hatuendi kwa kasi. Kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba tu, Mheshimiwa Waziri na hivi zaidi tusimlauimu Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ni Waziri wa Fedha, kwa sababu wao wanafanya kazi kulingana na kiwango cha fedha ambazo wanakasimiwa. Sasa ningeomba tu Waziri wa fedha akatenga fedha za kutosha ili hili zoezi la kuainisha na kuweka mipaka ya kimataifa kwa haraka basi likaenda kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea fedha kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha nafikiri hayupo, lakini anatusikia huko aliko, kwamba tuisaidie fedha hii Wizara ya Ardhi, kwa sababu hawawezi wakafanya miujiza kama hawana fedha za kutosha katika kulifikia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi pia nilikuwa na ombi moja hapa. Mheshimiwa Waziri najua tunashughulika na mipaka zaidi ya kimataifa lakini na mipaka ya ndani vilevile tuiangalie na haswa masuala ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wenzetu wa usimamizi hasa baharini wanapata shida wakati mwingine katika kusimamizi wa rasilimali za bahari na rasilimali nyingine za uvuvi na ulinzi kwa sababu mipaka ya Zanzibar na Tanzania Bara hasa katika eneo la bahari vilevile nalo ni kiini macho, kwa hiyo, ningeliomba na hili nalo tukaliingiza katika kuweka mipaka, basi na hili pia nalo tukaliingiza katika kubainisha ule mpaka hasa tukajua tukawasaidia watendaji wetu wa uvuvi, watendaji wetu wa kilimo, watendaji wetu wa Serikali kwa ujumla wakajua ile mipaka ili usimamizi wao na utendaji kazi wao tukaurahisisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala la tatu nigusie katika suala zima la upimaji na usimamizi mzima wa ardhi; changamoto nyingi zimekuwa zikizungumzwa hapa kwamba mipaka imekuwa ina shida lakini pia upimaji hauendi kwa kasi. Lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kweli tumeona kuna maendeleo makubwa yamekuwa yakiendelea katika sekta nzima ya upimaji wa ardhi Tanzania na kwa kweli nimpongeze sana mpima na zaidi Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Upimaji ya Ardhi nchini, anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa na mapendekezo machache; kwanza, tukaangalie migogoro ambayo kwa kipindi kirefu imetamalaki Tanzania. Kuna mgogoro wa Tarime. Mipaka inajulikana toka mwaka1968 na wameenda watendaji kule wakiongozwa na mwenyewe mwenye hatimiliki ya kuainisha na kutafsiri mipaka Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, lakini ameondoka kule bado shida ameiacha iko vilevile. Lakini pia juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu amenda Mbarali nako vilevile akaenda akatoa maeneo na maeneo yale kwa kweli maeno oevu, maeneo ya majimaji, ya chemchem, lakini pia tukawa tume–risk, tukawapa wananchi lakini alipoondoka yale maeneo ambayo tumekubaliana watu wakaanza kuvamia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali kadhalika kuna hekta karibu 950,000 tumezitoa tukawapa wananchi na tumeyakata maeneo ya hifadhi, hifadhi nyingine tumeziondoa, hifadhi nyingine tumezimega tukawapa wananchi, lakini bado matatizo ya ardhi yanaendelea. Kwa hiyo, hapa tatizo la migogoro ya ardhi tuliweka kama ni suala ambalo litaendelea kwa miaka mingi itakayokuja. Tuweke utaratibu wa watu kuweza kwanza, kuwa wazalendo na kutii sheria hili la muhimu na tukiweka utaratibu Mheshimiwa Waziri wa kwamba kila mtu tumridhishe kwa atavyotaka basi nchi nzima itakuwa ni kama vile uwanja wa mpira tunanyang’anyana tu mpira utacheza wewe kwa atakayekuwa na nguvu ndio atafunga goli, kama Mayele ana nguvu nzuri zaidi ana magoli 16 sasa. Kwa hiyo itakuwa mwenye nguvu ndio anashinda sasa unaona. (Makofi)

Kwa hiyo mimi ninaloomba tuendeleze utii wa sheria kwa wananchi wetu. Mipaka ikishakutafsiriwa na Mheshimiwa Waziri ambaye ndio tumempa nafasi hii ya yeye ndio atafsiri mipaka ya ardhi ya nchi yetu, akishatafsiri basi pande nyingine ziridhike. Lakini leo Mheshimiwa Waziri unaitwa uende na timu yako wanakwenda sio kwamba ukafanye utatuzi, unaitwa uende ukatoe haki kwa upande ambao watu wangependelea uwape, siyo kwa sababu ya kwamba ukafanye haki kwamba tunavyoona mimi mpaka uko hapa, nyie kuweni huku. Kwa mfano, kama Tarime, Tarime Mheshimiwa Rais amefanya favour mpaka buffer area ya zile mita 500 zile amewapa wananchi, baada ya kusema kwamba nusu tuwape hifadhi na nusu tuwape wananchi Mheshimiwa Rais amesema zote wapeni wananchi. Ametoa favour kubwa lakini bado tatizo linaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba mipaka hii ya ardhi itaendelea kuwepo, lakini Serikali isimame katikati, itoe haki kama inavyohitajika na mimi nitoe ushauri nimalizie kwa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza huu mradi ambao wa usalama wa miliki za ardhi Mheshimiwa Waziri twende tukaushughulikie na tukausimamie ipasavyo, kwa sababu una malengo mazuri na mimi nimeusoma mradi mzima ule nimeusoma vizuri. Tunakwenda kuandaa hati milioni mbili kwa wakazi wa mijini na tunakwenda kuandaa hati 500,000 zile hati za kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunakwenda kuandaa miundombinu ya kidijitali ambayo itarahisisha kufanya shughuli zetu kwa haraka. Sasa hivi ni 10% ya mradi tunaenda kupima, lakini tukiumaliza mradi tutakuwa tumeandaa miundombinu ya kuweza kusaidia upimaji kwa haraka zaidi na hivi Mheshimiwa Waziri ningependa sana utakapokuja hapa ukawaeleza wananchi huu mradi una tija kiasi ngapi? Kwa sababu wananchi wengi hasa Waheshimiwa Wabunge bado hawajaelewa pamoja na semina ambayo umetufanyia pale Msekwa bado hawajaelewa tija ya huu mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia tija ya matokeo ya huu mradi unakwenda kumaliza tatizo la upimaji wa ardhi nchini, unakwenda kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi nchini. Hebu Waheshimiwa Wabunge wenzangu tumpe muda Mheshimiwa Waziri na timu yake wakatekeleze huu mradi kwa sababu tunasema huu mradi fedha nyingi zimewekwa kwenye uratibu. Uratibu ukijenga ofisi nao ni uratibu, ukienda kutayarisha miunombinu ya communication ikawa mawasiliano mikoa kwa mikoa nao ni uratibu. Isionekane kwamba labda shilingi bilioni 45 zinaenda kwenye uratibu kwamba hizi fedha labda ni watu watakuwa wakikaa kitako ndio wanatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naangalia mradi mzima sikuangalia lile jedwali la fedha tu. Nimengalia mradi mzima in totality, nimeona kwamba kwa kweli mradi huu una tija na Mheshimiwa Waziri tukiushughulikia basi utakwenda kutuvusha katika suala zima la migogoro ya ardhi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)