Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Wizara ya Ardhi.
Kwanza nawashukuru Wizara kwa maana ya Waziri, Naibu, Makatibu wake na wote walioko hapo kwenye maeneo ya ardhi kwenye Wizara ya Ardhi. Nimshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kweli kimsingi toka Rais amekamata hii nchi imekaa vizuri sana na inakaa vizuri inaendelea vizuri. Mheshimiwa Rais amefuata misingi ya Baba wa Taifa, anaijenga nchi katika misingi isiyo ya matabaka na wale wanaohubiri matabaka watakuja kuona kwamba hii nchi imejengwa kwa matabaka na haiwezi kuwa matabaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mtaniwia radhi tu yaani tu, yaani kusema lazima niseme tu. Katika Wizara sielewi kabisa ni Wizara ya Ardhi yaani sielewi, yaani sielewi, yaani sielewi naanza moja/mbili wapi, sielewi yaani ni Wizara ya Ardhi na kusema kweli kipindi hiki naunga mkono ila bajeti ijayo nitakuja na hoja binafsi ya kuichunguza Wizara ya Ardhi. Kabisa yaani sielewi, haitokei kichwani yaani. Wizara ambayo ina Mkurugenzi wa Ardhi, Kamishna wa Ardhi, Katibu Mkuu Ardhi, msaidizi gani - ardhi. Wana mipango, wana wasomi, wana maprofesa, wana makamishna wa mikoa, wana wa ardhi wa wilaya. Hakuna migogoro mahali popote imeisha, yaani hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mabula mimi niulize swali; hivi kweli kwa mfano ulikuwa Naibu, umekuwa Waziri, hivi kweli hata kwenye majiji yetu basi, tuseme leo Dar es Salaam migogoro imepungua imebaki asilimia labda 10, 15; Jiji la Mbeya imebaki lazima asilimia ngapi; Jiji la Mwanza yaani hakuna mahali unaenda ukute ardhi sasa imepunguza migogoro. Sasa tunajiuliza, sasa humu ndani kuna nini kinaendelea? Nenda kwenye mipaka ya nchi migogoro, mipaka ya vijiji migogoro, kila mahali migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jamani mambo gani haya? Kwa kweli mimi niombe na nikuombe mama yangu nikuombe kwa kweli ujitahidi. Mimi nadhani kuna matatizo kwenye hii Wizara na matatizo makubwa ni mipango ya Wizara hii. Sijui kama inaenda vizuri, sielewi yaani sielewi kama inaenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano mimi nikienda benki nataka kufanya biashara, mimi ni mfugaji labda nataka kufanya biashara ya ng’ombe wakanipa shilingi milioni 300 halafu milioni 300 nikapita barabara nimetoka Dar es Salaam nikatamani gari nikanunua shilingi milioni 200. Jamani, mambo ya ajabu haya. Mmepewa shilingi bilioni 350, badala ya kwenda kupima viwanja mpewe hela za kudumu miaka yote, mnajenga majengo. Hayo majengo si yapo? Yako pale Bunda yamejengwa, majengo ya ardhi yapo, yako kila mahali. Juzi juzi hapa mmejenga mmetengeneza mtandao pale Dar es Salaam mzuri kabisa mmepewa sijui mkopo kutoka nje. Migogoro imeisha? Mimi nadhani kuna shida, kuna shida.
Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri ufanye kazi ya kutosha kwenye Wizara yako. Ukiona imekushinda, hivi kwetu hapa hakuna mtu kujiuzuru? Si inakuwa imekushinda tu unasema Mheshimiwa Rais hii Wizara imenishinda basi. Kwa hiyo mimi nikafikiri kwamba hii hali ni hali ngumu sana ya Wizara hii.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere namomba upokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba naomba tukumbuke kwamba migogoro hii haijaanza hivi karibuni na mnakumbuka kabisa kuna Kamati ya Mawaziri nane iliundwa kwa ajili ya kutembelea kila eneo kuangalia changamoto zilizopo za migogoro ya ardhi na sasa kamati hii iko kwenye utekelezaji. Sasa inapofika mahali inaonekana kwamba kipindi hiki ndiyo migogoro imekuwa mikubwa, siyo kweli. Migogoro hii ni chimbuko la kuundwa kwa Kamati ya Mawaziri nane. Nataka hili Waheshimiwa walitambue, ahsante.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere unapokea taarifa?
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niendelee na uchangiaji wangu kwa sababu mimi sijazungumza hakuna Wizara inaitwa Kamati ya Mawaziri. Wizara inaitwa Wizara ya Ardhi, hakuna Wizara ya makamati ya Mawaziri. Kwa hiyo, mimi niendelee na mchango wangu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunapozungumza ukweli kwenye jambo hili tunataka Waziri au Wizara hiyo ijirekebishe basi au kama kuna matatizo imalize. Kuna migogoro ya kudumu ya muda mrefu ni kweli, lakini kuna migogoro ya viwanja kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa yale yote ambayo Wabunge wamejadili humu wamemuomba aende atekeleze ikiwa ni pamoja na kutazama hizi fedha za kujenga majengo badala ya kwenda kupima viwanja. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa kweli hili ulitazame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea haya kusema kweli kwa sababu hatuwezi kuwa na miaka 60 tuna Wizara halafu hakuna eneo, hakuna hata mkoa mmoja ambao tunasema sasa huu mkoa uko nafuu labda twende Dodoma hapa iko nafuu. Hata tunakoishi hapa ni shida. Nenda pale kwenye Wizara ya Ardhi hapo, watu wanazunguka tu wamejaa kila mahali, ni shida. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hili nalo tulitazame tuone tunafanyaje ili tuweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Bunda nimeomba nimeandika barua ya kupima vijiji 30, sijawahi kupata majibu, lakini Mheshimiwa Waziri wewe ulikuwa Mara na mimi nakujua ni mkakamavu, mimi sijui Mawizara humu yanakuwaje mimi sielewi, lakini wewe ni mkakamavu kweli kweli yaani sasa sielewi ukifika Wizara fulani sijui ni watu wamekushinda akili sijui nieleweje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ulikuja pale unajua mgogoro wa Mkomariro, siyo mgogoro sasa hivi ni changamoto; za Mkomariro, Sirorisimba, Mgonyamirwa na Kijiji cha Mahanga na Manchimweru kuna migogoro ile ambayo iko kwenye mipaka. Siyo sana kama ilivyo huko nyuma lakini tupeni fedha, wanahitaji shilingi milioni 60 tu kupima hata hati za kimila wawape ili kila mtu awe na ardhi yake wapunguze migogoro. Nikuombe kwenye hilo nitakuja ofisini kwako niweze kukuomba ili uweze kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumza hapa ni suala la Nyatwali. Sasa Mheshimiwa Waziri ulikuja Nyatwali nikakusikiliza na tukakufuata, tukakuuliza kwa nini wananchi wa Nyatwali ambao wana GN ya vijiji vyao mnawahamisha kinyemela tu bila kuwapa fedha shilingi bilioni mbili au laki mbili au laki ngapi wafanye kazi. Mheshimiwa Waziri ukasema unajua Sheria za Valuation zinasema hivi, zinasema hivi.
Sasa nataka nijiulize, hivi wananchi wa Nyatwali wao ni Warundi au ni watu gani? Wana tofauti gani na watu wa Ngorongoro waliohamishwa ambao tena hawakuwa na registration yoyote, wakapewa fedha, wakapewa nyumba, wakapewa mashamba, wakapewa vitu vya, wakapewa umeme, wakapewa, yaani wana tofauti gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli hivi Mama Samia analijua hili kweli? Mimi nimuombe mama kwa sababu mama watu wote ni watu wake. Aliwaonea huruma watu wa Ngorongoro wanavyoteseka na leo wanasifia sana kila mahali. Kwa nini hatuwaonei huruma watu wa Nyatwali? Hivi unamhamishaje mtu Mheshimiwa Waziri unasema Sheria ya Valuation inasema hivyo? Pale ni shilingi laki saba, sijui heka laki ngapi? Hivi Ngorongoro hakuna hiyo sheria? Hapo Ngorongoro sheria ilipotea? Ni watu ni wale wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo hata mimi ungeniuliza Nyatwali wahame wasihame, ningewaambia wahame kwa sababu si tunataka tuweke Hifadhi ya Serengeti iwe mbuga ya maajabu? Si unataka ishikane na Ziwa Victoria? Sasa wale watu tumekwenda kuwahamisha kwa hiari yao, kwa nini tulete kutumia sheria na wamekubali kuhama, kwa nini? Nikuombe Mheshimiwa Waziri unajua mimi huwa najiuliza swali moja huwa najiuliza sana, hivi Wabunge mbona Wabunge mkiwa siyo Mawaziri naona kama vile mna-act vizuri, mkiwa Mawaziri mnakaa pembeni. Mkitenguliwa mnaanza na maneno, hivi mkoje ninyi? Kwa nini msihurumie watu? Yaani mkitenguliwa ndiyo mnajua huruma ya wananchi, mkiwa kwenye Uwaziri huruma hamuioni. Hivi mkoje ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini msione huruma ya wale watu? Nenda kawatembelee mama wale watu. Wale watu wa shilingi milioni moja, milioni mbili, milioni tatu waone. Wale waliopata mabilioni, mabilioni achana nao. Muone basi wa kuwaona. Kwa nini huwaonei huruma, hivi siku nyingine mama wewe ni wa pale. Hivi siku ile unapita pale watu wanalia machozi, wanajigaragaza, mmekwenda kuwahamisha kwa hiari yao halafu mnawalipa shilingi laki moja, laki mbili, laki tatu? Jamani kwa kweli hii kwamba hiyo haiko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Rais hili kwa kweli alione, mimi sijui kama analifahamu vizuri, mimi sifahamu. Mimi nadhani kwamba sasa tumebaki tutafute alternative mtuombee wananchi na wazee sisi wa kule tumuombe tumwone mama na tumwambie mama watuongeze basi badala hata ya shilingi milioni mbili iwe milioni tatu. Hivi shilingi milioni mbili unaenda kununua; kiwanja bure ni shilingi milioni nne, unaenda kununua nini? Huna mahali pakwenda, hujapewa eneo, hujapewa chochote, yaani wahame tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe kwa kweli hiki kitu hakiko sawa. Nikuombe tutamuomba Mheshimiwa Rais hili ataliona aweze kutusaidia kwamba hii hali itakwendaje kwenye jambo hili ambalo siyo zuri kwa kweli, halina wema wowote.
Mheshimiwa Waziri hivi mipaka hii sasa, mipaka ya vijiji mimi niwaombe na nikuombe na Wizara yako, wakati fulani msitumie ramani kwa sababu unaweza kutumia ramani kwa sababu walikuja siku moja kutumia ramani Kijiji cha Tiling’ati wakakuta kijiji hicho kiko Butiama, siyo Bunda. Ukaenda sehemu nyingine kuangalia ramani kijiji kiko Serengeti siyo Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani kwenye migogoro ya muda mrefu nendeni mkajiridhishe, wewe unaishi hapa mwaka gani? Miaka fulani, wewe unaishi hapa miaka gani? Miaka fulani basi mnapima mnaachana nao. Kwa nini hatufanyi hiyo akili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna mtu mmoja anaitwa Albert Einstein alisema akili ni kile ambacho wewe umetolewa vitu vyote ulivyojazwa kichwani ukabaki nacho, hicho ndiyo akili. Kwa nini watu wazito wa busara? Kwa hiyo muende kwenye maeneo ambayo watu wamekaa kwa muda mrefu muwasaidie, muangalie uhalisia wao siyo kufuata ramani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)