Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii na mimi kuwa sehemu ya wachangiaji wa hoja iliyopo mezani, lakini nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na leo hii tuko mbele ya Bunge lako tukufu kwa ajili ya kupangilia maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwa mara ya kwanza kusimama na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kwa jinsi alivyoniamini nahaidi kwenda kufanya kazi ya kuishauri Wizara kwa maana ya Waziri, lakini na kutoa matokeo ambayo ni matarajio ya waliyo wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana sana familia yangu kwa utulivu, kwa sababu muda mwingi siko nayo, waendelee kuwa wavumilivu wakati huu tunapotekeleza majukumu ya kuiendeleza nchi. Niwashukuru wapiga kura wangu kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa mwakilishi wao na baadaye kutokana na hayo ndiyo nikaaminiwa kuwa kwenye nafasi hizi ambazo ni za kiutendaji Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwashukuru Wabunge wote mliopata nafasi ya kutoa michango yenu. Watu karibu 30 na zaidi mmechangia kwa uzito wa hali ya juu masuala yote yaliyowasilishwa ambayo yanaisoma bajeti yetu kwa mwaka huu ambao ni mwaka tarajiwa unaokuja na kimsingi mawazo yote ni ya muhimu sana sisi kuyazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Kamati kwa kuonesha ule uelekeo wa nini ambacho kama Wizara tunatakiwa tulibebe na mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote, maoni na mapendekezo na maelekezo ambayo mmetupatia kama Wizara itakuwa ni ajabu sana tukatoka nje ya maoni yenu tukaenda kufanya vitu vingine ambavyo vitakuwa haviendi sambamba na maelekozo ya nchi ambayo ndiyo mwelekeo wa nchi yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ukienda kwenye hili eneo la migogoro, migogoro hii ina sura mpaka tatu; tunayo migogoro ya ndani ambayo hii ni mimi nimeibiwa kiwanja, mimi nimefanya nini, nimecheleweshewa hati nimefanya nini? Hii ni migogoro ambayo iko kwenye eneo la utendaji wa Wizara katika kusimamia watendaji wetu kufanya kazi zao kwa uadilifu na uaminifu na ninashukukuru sana Waheshimiwa Wabunge wengi mmeungana na sisi katika mabadiliko mbalimbali ambayo tumeendelea kuyafanya ndani ya Wizara katika kuimarisha utendaji. Mojawapo ni lile lile la kutambua hata watumishi wetu ambao walikuwa wanafanya kazi moja kwa moja kwenye halmashauri, lakini badaye Serikali iliamua kuwarudisha na kuwa chini ya Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niwatoe wasiwasi kwamba kurudi kwao Wizarani bado hakutafisha au kudhoofisha utendaji katika maeneo yote ya Serikali yetu kwa maana ya halmashauri na hii itasaidia sana kuimarisha usimamizi kwa sababu kama mtabaini katika muundo wa utumishi ukitoka ngazi ya Waziri mpaka Kamishna wa Mkoa palikuwa pana gap kubwa sana kwenda kukuta watendaji wetu ambao wako kwenye halmashauri, lakini sasa tunakwenda kuhakikisha kwamba hawa wanarudi kwenye nguvu ya Wizara ili usimamizi wao uwe karibu zaidi ili waweze kuwajibika ipasavyo, hii itatusaidia sana kutoka matokeo, kwa sababu taasisi nyingine zote zilifanya hivyo hata TAMISEMI yenyewe ilitambua kwa mfano Mamlaka kama za TARURA kwa ajili ya kuongeza usimamizi mzuri. Hata sisi Wizara ya Ardhi tunaendelea kutengeneza mpango ambao utaletwa mbele ya Bunge lako tukufu kwa maana ya kutengeneza Kamisheni ya Ardhi ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya kusimamia shughuli za ardhi hapa nchini na inaweza ikaleta ufanisi mkubwa sana ambao ndiyo matarajio ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye migogoro; kuna migogoro ambayo ni ya kati kati hapa na migogoro mingi ni kwa muda mfupi niliyokaa Wizara hii migogoro hii ya kati ambayo inasababishwa na mgongano wa kimipaka ndani ya nchi, ndani ya wilaya na wilaya, ndani ya kijiji na kijiji na hii inayohusisha kwa maeneo ya hifadhi tunajaribu kupitia vilevile hata sheria zetu kuziangalia. Kwa sababu utaona kuna kachangamoto kadogo unaweza ukakaona ni kama ni kadogo lakini kanagonganisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano zile GN zinazosomwa katika kila maeneo ni mamlaka tatu zimepewa mamlaka ya kutoa GN ambazo ukiliangalia unaweza ukakuta linaleta mgongano ule ambao unasababisha migogoro kwa wananchi wengine, kwa mfano TAMISEMI kwenye kupima vijiji imepewa mamlaka ya kutoa GN, Maliasili imepewa mamlaka ya kutoa GN, Ardhi ambao ndiyo wasimamizi halisi wa ardhi nao wanatoa GN. Sasa mgongano huu lazima tukae, tutakaa katika Wizara hizi ili tuweze kutafsiri nani hasa awe wa mwisho kwenye kuzungumza juu ya matumizi ya ardhi kitu ambacho kitasaidia sana kuondoa hii matatizo makubwa ambayo yanatukabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano niwape mfano mdogo tu hapa Wilaya ya..., I mean mgongano uliyopo kati ya Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara eneo moja linaitwa Mkungunero. Mkungunero TAMISEMI ilienda ikatambua vijiji, baadaye Maliasili ikatambua maeneo ya hifadhi, sisi tukaenda tukaweka mpaka wa mkoa; ule Mkoa kimsingi umesoma vijiji vingine ulikata ule vijiji ile alama ya mkoa imeacha vijiji vingine Dodoma, vingine Manyara.
Sasa migongano kama hii tusipo ikalia pamoja tukaiweka vizuri migogoro hii haitaisha, lakini ndani ya migongano hiyo ya kimpaka mingine ipo kwenye wajibu tu wa viongozi wa maeneo, tunaikuza sana sana mpaka ikapelekewa na Mawaziri nane na nini, lakini kwa mtazamo halisi unaona kabisa DC wa eneo anahusika, Mbunge wa eneo anahusika, Mwenyekiti wa Kijiji anahusika, yangeishia kwenye level hiyo wala kusingekuwa na mgongano, lakini kule nimeona kabisa na kubaini kuna baadhi maeneo mengine watu wanakimbiana, hawakai pamoja kuzungumzia matatizo ya wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo gani kati ya mwananchi ambaye amepitiwa na mpaka wa Mkoa analima Mkoa wa Manyara anakaa Mkoa wa Dodoma, kuna tatizo gani huyu mwananchi kuachwa katika muundo huo wa kutumia ile ardhi na badala yake tunaandamana. Mimi niwaombe kwenye eneo hili mamlaka za maeneo zisimame imara kuzungumza mambo haya hadharani, yakija huku Wizara, huku tunafuata sheria, hata tukienda na sheria zetu pale hazitatanzua mgogoro kama ambavyo tungekaa huko katika ustaarabu wetu wa maisha yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti mimi niwaombe ndugu Waheshimiwa Wajumbe na Wabunge wenzangu, tuzungumze, kwenye maeneo haya tuzungumze kwa uwazi kabisa. Tunafanya juhudi mbalimbali na kimsingi lazima muone namna ambavyo Serikali inafanya juhudi za kujaribu kutatua migogoro, lakini migogoro mingi haiwezi kutatuliwa kama viongozi wa maeneo husika wao wenyewe hawawi sehemu ya kumaliza migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lipo hili tatizo la mipaka ya nchi, hilo tunaendelea nalo na Waheshimiwa Wabunge tunaendelea na kutambua mipaka, kuna maeneo mengine bado kuna mvutano kidogo ila yanaenda kumalizika hivi karibuni na nchi nyingine tumeendelea kuzungumza nao kwa ajili ya kunyoosha mapito, kwa sababu Tanzania na majirani zake hatuna mgogoro wowote wa kimahusiano, kwa hiyo, masuala haya yanakwenda vizuri na ni wahakikishie kabisa kwa mfano hili eneo la Mheshimiwa Kitandula kule juu baharini wala asiwe na wasiwasi kwa sababu mazungumzo ya Kenya na Tanzania ni ya karibu mno kuliko hata mataifa mengine kwenye suala la mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la mabaraza; hili suala la mabaraza Waheshimiwa Wabunge mmetoa mawazo kuhusu uimarishwaji wa mabaraza, ni kweli hata sisi tumeliona na tumeunda timu maalum ipitie. Hata hivyo Serikali Kuu jambo hili lilikwenda kwenye Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuangaliwa, je, lirudi mahakamani au liendelee kuwa Wizara ya Ardhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa upande wote kwa sababu ni watu ambao tunasubiri maelekezo sisi tumeendelea kujiandaa upande wetu kuimarisha haya mabaraza na mwaka huu wa fedha ambao leo tumewaletea bajeti hapa tunakwenda kwa ajili ile tofauti ya mabaraza 47.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo tu, ahsante, wale wanao kosekana kwenye halmashauri karibu 47 tunakwenda kuwaajiri mwaka huu wa fedha kwenye zile wilaya ambazo bado hazijapata Wenyeviti, tunaenda kuajiri. Vilevile tuwaombe mshikamano wenu kwamba tunakwenda kuleta wale watendaji lakini tunahitaji maeneo ya kufanyia kazi ambayo kimsingi tunapata msaada kutoka TAMISEMI kwa maana ya maeneo yale ya ofisi za mahakama hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sera tumeshaanza kuipitia kwa uzito wa kutosha, hata hili suala la diaspora linakwenda kuisha kwa sababu hatuoni kama tunaweza tukaendelea kuwa na msimamo wa kutokutambua Watanzania wenzetu ambao wakija kujenga nyumba Tanzania hawahami nayo. Wakija kuwekeza Tanzania maana yake wanarudisha nguvu walizozikusanya nje nchini mwao, Serikali imeliona na sasa liko katika hatua za mwisho na hawa Watanzania wenzetu wataenda kunufaika na hii huduma ambayo ni ya kupata ardhi na kuwekeza nchini Tanzania na hii ndiyo mataifa mengi yanafanya kuwatumia watu wao ambao wako nje kwa maendeleo yao hata ukienda Ethiopia pale utakuta wazamiaji wengi ndiyo wanajenga majengo kule ya maana kabisa. (Makofi)
MWENYEKITI: shsante sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Geophrey Mizengo Pinda.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)