Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia uhai mpaka tumefika hatua hii tunapokwenda kuhitimisha hoja ya bajeti ya Wizara ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee kabisa niwapongeze na kuwashukuru Wabunge wote ambao kwa namna walivyochangia Wizara hii ya Ardhi. Wengi wamechangia kwa uchungu sana na wamechangia wakiwa na imani ya kwamba kile wanachokizungumza kikifanyiwa kazi maana yake Watanzania wengi wataweza kuwa na amani. Nina washukuru sana kwa sababu ni dhamira njema ya Serikali kuhakikisha kwamba watu wao wanaishi kwa amani na hili sisi kama Wizara tumelichukua, tunaona ni jambo la msingi na michango yote iliyotolewa yote ilikuwa ni michango ya busara ambayo inahitaji kuifanyia kazi kwa namna moja ama nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nishukuru pongezi mlizozitoa kwa Wizara na Serikali hasa kwa Mheshimiwa Rais. Kwa kweli kama ni pongezi zote mlizozitoa kwa Mheshimiwa Rais ni hakika zinamstahili, kwa sababu katika mageuzi makubwa yanayofanyika ndani ya Wizara kuna mkono asilimia 100 kutoka Mheshimiwa Rais. Wote mnajua Wizara ilikotoka na Wizara ilipo sasa kwa kwa uhakika Wizara ilipo sasa haianzishi migogoro mipya, bali inahangaika na migogoro ambayoo imekuwepo ya miaka nenda-rudi, lakini kwa miundombinu ambayo tunakwenda kuwekeza tuna imani tutakwenda kuimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchangiaji jumla ya Wabunge 34 wamechangia 30 wakiwa wamechangia kwa kuwaongea na wanne wamechangia kwa maandishi, niombe kutolea ufafanuzi kwa hoja za Wabunge ambazo wamezitoa katika mjadala huu ambao ulikuwa unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na lile ambalo lilikuwa linaongelewa ya kwamba Serikali ilikosea sana kuwahamisha watumishi wa TAMISEMI na kuwapeleka Wizara ya Ardhi.

Naomba niseme tu kwamba sababu za msingi zilizopelekea Serikali kufanya jambo hilo ni kwamba sheria zote zinazohusu masuala ya ardhi zimekasimiwa mamlaka na usimamizi wa ardhi kutoka kwa Waziri mwenye dhamana. Sasa hawezi kuwa Waziri mwenye dhamana wakati wale ambao unawasimamia hawako kwako wewe siyo mamlaka ya nidhamu, wakifanya kosa la kiutalamu, wakifanya kosa la kiutumishi, huna mamlaka ya kuweza kuwagusa, lakini wanachokifanya ni kile ambacho wewe umepewa dhamana ya kusimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kitendo cha kuwahamisha kuwaleta katika Wizara, Serikali ilikuwa na lengo zuri la kutaka kuwaweka katika mstari ambao utaweza kusimamiwa kitaaluma, kwanza kutoka kwa Waziri mwenye dhamana mwenyewe, lakini pia katika usimamizi wao kuna bodi ambazo zinawasimamia na zote ziko chini ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia Sheria ya Ardhi Sura 113 kifungu cha 8 cha sheria hiyo na kifungu cha 5 cha Mipango Miji kwenye Sheria Namba Nane ya mwaka 2007 aya ya 18.11 na bahati nzuri mtoa hoja alikuwa ni mwanasheria anajua hii. Kwa hiyo, Serikali imeweka hiyo kuhakikisha ya kwamba haya yanakwenda katika utaratibu huo. Lakini pia majukumu ya Wizara wameainishwa kwenye Tamko la Mheshimiwa Rais Namba 385 la tarehe 7 Mei, 2021 na Waraka huu wa Utumishi Namba 01 wa mwaka 1998 ulifanyiwa marekebisho mwaka 2019 na katika kufanya hivyo sekta tatu zilitolewa kwa wakati mmoja; maji, barabara pamoja na ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara ya Maji, niwapongeze pia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambao tayari waliunda vitengo. Sasa ukiangalia namna bora ya utoaji huduma kwa maji ndiyo hiyo hiyo inatakiwa ikawe bora katika sekta ya ardhi ambayo ni Wizara wezeshi katika suala zima la kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa hiyo, katika hiki ambacho tunakifanya sisi sasa ni kwamba watumishi wameletwa Wizarani waweze kusimamiwa na hatua mbalimbali zimechukuliwa katika wale ambao wamesababisha migogoro ikiwepo hapa Mkoa wa Dodoma watumishi wengi wameachishwa kazi na wengine wamepewa maonyo kwa sababu tu ya kukiuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama huyo mtu hauko nae ndani ya Wizara yako anayefanya sekta yako huwezi kumsimamia, lakini hatua hiyo pia ilikuwa imelenga suala zima la kuboresha na tunavyokwenda hata mabadiliko ambayo Mheshimiwa Hawa Mwaifunga ameyasema, yanafanyika kwa nia njema na dhamira njema ya kuwasikiliza Waheshimiwa Wabunge analalamikia labda mtu huyu hafanyi kazi vizuri, unachunguza unakuta labda kazi haiendi vizuri, lakini wakati mwingine anafanya vizuri katika kuboresha zaidi unamtoa pale alipo, unapeleka kwenye changamoto nyingi ili aweze kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano yule wa Tabora ametoka Tabora ameletwa Dodoma na anafanya kazi nzuri sana. Aliyekuwepo Dodoma hapa naye amepanda cheo kafika hatua ya kwenye nafasi nyingine nzuri zaidi. Kwa hiyo, ni kwamba tunapeleka huduma hii kulingana na uhitaji uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nitamuomba tu aliyetoa hoja hiyo atuletee watumishi au Halmashauri zilizogoma kufanya kazi kwa sababu tu zimehamishiwa Wizara ya Ardhi. Sisi kama Wizara hatuna taarifa wala nyaraka zozote za watumishi kuamua kuacha kazi au kugomea kazi, kwa sababu tu wametoka katika Wizara ya TAMISEMI na kupelekwa Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaomba sana hilo tulipate kwa maandishi ili tuweze kufuatilia hao na tujue kwa nini wametoka maana hatuna taarifa hiyo tumeisikia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala lingine ambalo amelizungumza Mheshimiwa Mtemvu; mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Mtemvu amekuwa akiliongelea sana suala hili la maeneo ambayo yamechakaa na kutaka pengine kufanya miji yetu ipendeze. Niseme kwa Watanzania hii ni fursa ambayo hata yule Mtanzania wa kawaida mwenye ardhi yake mjini ambaye ana nyumba yake ya toka mwaka 1947 lakini unapoangalia mipango ya majiji yetu na miji yetu pale alipo sasa hapatakiwi kuwa na jengo kama lile. Niwaombe sana wasiuze maeneo na kuondoka, lakini watumie ardhi zao kuwezesha kujinufaisha na kuleta utajiri, waingie kwenye ubia kama una jenga ghorofa tano pale mwenye hati ni mimi nina jengo langu la kawaida wewe jenga ghorofa zako tano tukubaliane zangu ni ngapi? Maisha yanaendelea mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumejitokeza wahuni wachache wanaenda katika maeneo hayo hasa kwa akinamama waliozeeka zaidi wanawadanganya, wanawanyang’anya zile ardhi na mtu anajenga jumba pale anaendelea na kufaidika, lakini yule aliyoitunza ile ardhi kwa muda mrefu anakosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Jiji la Dar es salaam kumekuwa na mipango mingi zaidi ya kumi ambayo imefanyika tulikuwa na Buguruni Development Plan ya 2014-2024 inakwenda kuisha na hali inayokwenda katika uendelezaji bado ni wa kusuasua. Kuna Kurasini Development, kuna Dar es salaam Central Area Development Scheme ya 2018 – 2028; kuna Magomeni ambayo imeshaanza sasa hivi ile Magomeni Quarter tunaona inavyokwenda na ndiyo muelekeo. Kwa hiyo, plan ziko nyingi kinachotakiwa ni zile Mamlaka za Usimamizi za Upangaji kuweza kutekeleza hiyo mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wakati mwingine tunachanganya, sisi kama Wizara tunasimamia sera, kanuni na miongozo mbalimbali suala la uendelezaji miji lina mamlaka yake ya kusimamia, lakini kwa sababu Serikali ni moja na tunafanya kazi moja, ukiona mambo hayaendi vizuri unatia mkono katika kuhakikisha kwamba suala hili linakwenda vizuri.

Kwa hiyo, katika mambo ya ushauri mliyoyatoa tunayachukua na nimshukuru sana Mheshimiwa Angellah Kairuki anayesimamia mamlaka za upangaji, amejibu suala la migogoro na mambo mengine ambayo pengine mamlaka za upangaji zinatakiwa kuisimamia kwa karibu hasa walioko kule chini Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mtemvu ameenda mbali zaidi akasema tuangalie namna bora ya kuendeleza maeneo ambayo pengine yamechakaa kwa kutumia National Housing. Mpaka sasa National Housing kazi inayofanyika ni nzuri na katika ufanyaji kazi wake tayari wameishaingia katika mikataba mbalimbali wakati wa hotuba yangu nilizungumza na hiyo haiishii katika wafanyabiashara tu, inakwenda pia katika kubadilisha kabisa maeneo mengine ambayo yapo na tayari katika mipango yao wamefungua milango ili watu waweze kuingia, na Mheshimiwa Rais kafungua milango kuruhusu wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi wachukue fursa hiyo sasa kwa sababu suala la uendelezaji milki bado liko chini sana tunahitaji kuongeza kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, milango imefunguliwa kwa hiyo anatakiwa kuingia kusaidiana na Shirika la Nyumba, lakini bado anaweza akaingia na mtu binafsi kama nilivyosema, lakini bado hata kama wewe Mheshimiwa Mbunge una ardhi yako bado ni ruksa kuingia katika makubaliano na likaendelezwa tukabdilisha sura ya miji yetu. Magomeni Quarter ni mfano mzuri na tumekwenda kujifunza hata kwa wenzetu Morocco walikuwa wanakweneda block kwa block wanaondoa zile squatters wanajenga majengo, lakini wale walioko pale hawaondolewi, wanatolewa kwa muda wanakaa sehemu baadaye majengo yakikamilika wanaingia na maisha yanakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Halima Mdee amezungumzia habari ya National Housing katika mradi ule wa Kawe Seven Eleven pamoja na ile miradi mingine ambayo ameitaja. Naomba tu niseme ya kwamba ni kweli NHC kuna kipindi walisimamishwa kuchukua mikopo wasiendeleze maeneo yao na wakati wanasimamishwa kulikuwa na miradi mikubwa inaendelea pamoja na Mororcco Square ambayo sasa imekamilika. Kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Shirika lenyewe la Nyumba katika suala zima la kuondokana na hili suala Mheshimiwa Rais ameridhia National Housing waendelee kukopa na wameshakopeshwa, wamekubaliwa kukopa shilingi bilioni 173 ambazo sasa zinakwenda kukamilisha ile na hao ambao miradi yao ilikuwa imesimama ambao pengine wangeweza kuidai National Housing, tayari tuko nao katika mazungumzo kuweza kuona ni kwa namna gani pengine ubia uliokuwa unaendelea katika kufanya kazi au ule ukandarasi uliokuwa unaendelea utaendelea bila kuingiaza hasara National Housing kwa sababu kosa lile halikuwa la National Housing na ndio maana Serikali imeingia kwa karibu sana kuweza kulizungumza suala hili liweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la migogoro ambayo imezungumzwa na Mheshimiwa Mwita Waitara, Mheshimiwa Bahati, Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Ester Bulaya, Mheshimiwa Yahaya, Mheshimiwa Ally Makoa na Mheshimiwa Robert nadhani Wabunge kama kumi hivi wamezungumzia suala la migogoro hasa ya vijiji 975. Nimshukuru sana Mheshimiwa Mary Masanja ameweza kujibu kwa namna nyingne ambayo imekwenda kulizungumzia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu, migogoro hii kama tulivyosema ni ya muda mrefu, lakini imekuwa sugu kwa sababu kule chini ambako ndio mgogoro unaanzia, wanaacha mgogoro unaanza mpaka unafukuta unafikia mahali ambako hauwezi tena kusuluhishwa. Lakini kama tungekuwa tunafanya kazi kule, bahati nzuri sisi wote ni Madiwani na migogoro yote hii iko kwenye maeneo yetu, tunasikia mpaka hapa na hapa kuna kelele, lakini tumekaa kimya tunasubiri kuyaleta kwenye Bunge. Tukiyasimamia kule kule chini hasa wale watendaji wetu, kwa sababu ndio jukumu lao, kama GN imezungumza habari ya maeneo ya utawala na kazi ya Wizara ya Ardhi ni kutafsiri GN, kazi yake ni kutafsiri GN ambayo mipaka inakuwa imewekwa inaweza ikawekwa kwa features zilizoko ardhini au kwa kufata coordinates na katika maeneo ambayo tunafata coordinates peke yake wananchi wengi wanakataa, lakini ukienda kwenye milima ukienda kwenye mito, mito inahama leo ulikuwa umeweka coordinates kesho inakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo matokeo yake ni kwamba tunakwenda na vyote viwili kunakuwa na coordinates lakini na zile features zilizoko ardhini. Lakini sasa wananchi wetu mara nyingi wengi hawataki kukubali ule ukweli hata wale walioingia katika maeneo hawataki kukubali ukweli na sheria haiwezi kusema uongo katika masuala ya tafsiri. Bahati nzuri ukienda kwenye migogoro wanakwambia tafsiri iliyoko kwenye GN au GN iliyoko wanaitambua. Ukisema unaenda kufanya tafsiri kwenye ardhi anakataa, sasa tunataka kujiuliza katika hilo kipi ambacho unakiona kinafaa? Ukienda kwenye ramani iko sawa, lakini mwananchi anasema hapana sisi hapa kulikuwa na mto, lakini mto haupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima tufate taratibu zile zote za kitaalamu na haya yameweza kupelekea Mheshimiwa Rais aridhie kwa sababu ya wananchi ambao walikuwa wamekaa maeneo mengi, ameweza kuridhia ekari 2,385,316 kuwapa wananchi pamoja na kwamba waliingia katika maeneo ambayo hayapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika hili kwa sababu amepunguza migogoro na kero za wananchi. Niwaombe tu Watanzania wenzangu pale ambapo Mheshimiwa Rais amesharidhia, mipaka tumeshaibadilisha, tumeshaweka mipya na tumeshaweka zile alama kwa maana ya beacon tuheshimu, kwa sababu changamoto nyingine zinakuja mpaka umewekwa na unaonekana, lakini mtu anavuka anaingia kule ndani. Ukienda kule unaingia kijinai, maana yake wewe ni mhalifu kama wahalifu wengine. Lakini tukisema siku zote tusitekeleze kile ambacho kiko kisheria inaweza ikatuletea shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ya migogoro ambayo ipo mimi nitoe rai tu kwa Watanzania wenzangu wote tutii sheria bila shuruti kwa sababu ardhi ndio wezeshi katika shughuli zote za kimaendeleo, ukiwa na mgogoro huwezi kwenda popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Nyatwali na fidia; bahati nzuri alilianzisha Mheshimiwa Halima akalizungumza, akaja Mheshimiwa Ester mtoto wa pale pale akalizungumza, akaja na Mheshimiwa Getere naye akalizungumza. Wamelizungumza kwa uchungu sana na sisi tunakubaliana na hisia wanayokuwa nayo, lakini Serikali inachokifanya haina maana yoyote, yaani haina lengo la kudhulumu mwananchi yoyote. Katika masuala mazima ambayo yamefanyika hakuna mwananchi aliyedhulumiwa. Kabla ya kufanya uthamini kuna utafiti unafanyika, bahati nzuri wanasheria wanajua wanazisoma sana hizi sheria, kile ambacho wananchi walikuwa wanauziana na kile ambacho Serikali inatoa ni vitu viwili tofauti. Serikali imetoa kikubwa kuliko kile walichokuwa wanauziana, kwa hiyo, kinachofanyika pale wananchi tunayo na mikataba yao walikuwa wanauziana wengine ekari moja shilingi 500,000 wameenda sana mpaka shilingi 1,500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikaongeza pale top-up pale ya shilingi 500,000 lakini thamani ya ardhi ya pale haifiki ile thamani ambayo wamepewa. Kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba Serikali haina dhamira ya kumnyanyasa Mtanzania lakini Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba inalinda pia maisha ya Mtanzania katika kuwezesha kuweza kumlipa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bahati amezungumza kwa kirefu sana amesema nisipotaja maeneo ambayo yametolewa kwa sababu amekuwa akisikia Waziri Mkuu kasema hivi, statement ya Waziri Mkuu na tunayosema Wizara ni ile ile wala haina tofauti yoyote. Katika eneo la Hifadhi ya Ruaha kule Mbarali jumla ya vijiji 13 vimeondolewa katika maeneo ya hifadhi ambavyo ulitaka tuvitaje ni Azimio, Igava, Ruiwa - Mahango, Mapogoro, Mbalino, Miyombweni, Mlungu, mpolo, Mwatenga, Nyakazobe, Magululu, Sonyanga na majina magumu kweli kweli, lakini ndiyo hivyo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo vyote vimebaki I mean vinatakiwa kutoka kwa 100% kwa maana ya vijiji ni Kijiji cha Msanga, Iyala, Makulusi, Kilambo na Luhanga. Lakini katika hivi vijiji vitongoji katika haya maeneo vitongoji 38 katika vijiji 16 vya Mwanavala, Imalilosongwe, Warumba, Igulunya, Vikai, Ikunda, Ihuta, Iwalanje, Magigiwa, Mkuya, Mahango, Nyamakuyu, Ukwavila, Mvunguni, Isimike na Ruanze vitaondolewa kupisha shughuli za hifadhi. Kati ya 38 kuna hivyo ambavyo vinaondoka.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu alichosema, alisema kwa idadi ya vijiji lakini kuna vijiji ambavyo sehemu yake ya vitongoji vinaondoka kwa maana ya kwamba havijaathiriwa na hifadhi na sehemu ambayo inaingia kwenye hifadhi yenyewe itabidi waondolewe. Kwa hiyo, vimewekwa kwa maana vijiji ni vitano, lakini vingine ni sehemu ya vitongoji ambayo vinabaki kwenye hifadhi. Pori la Swagaswaga ameshalizungumzia sitaki kulirudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye eneo ambalo limeleta changamoto kubwa kwa Wabunge wote wamelizungumza.

Kwanza naomba nikiri wazi tu kwamba mradi huu siyo mradi wa leo, mradi ulianza mwaka 2016 kwa maana ya kuanza mchakato. Mwaka 2018 ndio discussion zikaanza na wenzetu wa World Bank, mwaka 2021 wakakubali ku–finance na mradi huu uli–appear kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021, ume–appear kwenye Bajeti ya 2021/2022 na sasa 2022/2023 ndio tumeanza kuutekeleza. Lakini mradi huo wakati wa makubaliano ulivyokuwa vijiji vilikuwa vimepangwa vilikuwa ni 250.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Kamati ninawashukuru walipiga kelele sana katika hili wakasema haiwezekani mnapeleka kwenye miundombinu pesa nyingi na nini tunataka vijiji viongezwe. Wizara ikaenda ikakaa, tukafanya mawasiliano na wenzetu ratiba zao kidogo zikawa haziko sawa sawa kwa sababu huwezi kufanya mabadiliko katika mkataba ambao mmeingia na World Bank bila kukaa nao na kuridhia. Lakini tuliangalia ndani ya mkataba ulivyokuwa na kwa sababu tulikuwa na ule mradi wa kuimarisha suala la upimaji kulikuwa na pesa ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kununua ramani. Sasa mradi huu kama unafanya maana yake huhitaji kununua ramani, unaweza ukatengeneza mwenyewe. Tukahamisha zile pesa tukaenda kuongeza vikawa vijiji 250 suala ambalo tulitoa taarifa na walikubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Waheshimiwa Wabunge naomba niwaambie, tumekaa miaka yote ya uhuru ambayo tunaizungumza vijiji 12,000 tunavyo 319 sasa ni 318 baada ya kijiji kimoja kuondoka. Lakini vijiji zaidi ya 10,000 vimepimwa na vina vyeti; vyenye mpango wa matumizi ni 2,675 kwa nini ni vichache? Kwa sababu hakuna miundombinu ya kurahisha upimaji na hiki kinachotakiwa kufanyika kinafanyika once and for all maana yake ni kwamba ukishasimika miundombinu ile ya upimaji, ukarahishisha ile distance ya upimaji kutoka kwenye kilometa 90 zikwa kilometa 20, 25 kasi ya kupima itaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kuongeza kasi ya kupima hata ule uzalishaji wa viwanja, uzalishaji wa kupanga matumizi ya ardhi utakuwa mkubwa kwa sababu muda utakuwa ni mfupi na gharama itakuwa ni ndogo. Tukisema tuhamishe pesa tupeleke tukapime leo, bado kasi itakuwa ni ile ile ni ndogo utapeleka pesa lakini huna nyenzo za ku-speed up kazi yako. Bado utapima vijiji 50, utapima vijiji sijui vingapi kwa mwaka ambayo haifadhiliwi pia.

Kwa hiyo, kinachofanyika ndani ya Wizara ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na miundombinu ya uhakika ambayo haitaturudisha nyuma kwenye kasi, ukishaiweka maana yake sasa ni kazi ya kubanana kila mwaka hatuitaji kwenda kuweka miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo zile points ambazo zinatumika katika suala zima la upimaji ambazo zilikuwa tatu tu, sasa hivi tunaenda kuweka nyingine 30 na mradi unaweka 22 tunakwenda kuwa na kama 25 ambazo zile zinakurahishia katika kazi ya upimaji. Ukishaweka zile ndugu zangu kazi itakayobaki sasa kufanyika ni kazi ya kupima tu uwandani hata kama watafanya usiku na mchana, lakini wana uhakika na nyezo zile wanazozitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili tutapeleka pesa ndio, lakini wana uwezo gani? Hawana vitendea kazi, zile mashine za kupimia za kileo, wanahangaika na total station, wanahangaika sijui na vitu gani, ambayo hayawezi kufanya kazi ile inayokusudiwa na lengo letu tupime vijiji vingi kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia pia tuna Dar es Salaam na Dodoma peke yake ambapo sasa tumewekea Mfumo wa ILMIS, tunakwenda kuweka Mfumo wa ILMIS kwa nchi nzima katika mikoa yote na ile inaweza kurahisisha sasa wale watendajii wanaokwenda kutumia hiyo mifumo hawana huo uelewa wa kuweza kuingia kwenye mfumo na kufanya kazi ile na ndio maana sasa hivi tuna timu ya wataalamu ambayo inahakikisha kwamba inaweka mfumo vizuri ina-clear data zote, halafu tunakwenda kusimika mifumo katika kila mikoa. Mifumo ile itatusaidia kuongeza kasi ya upimaji, kuongeza kasi ya upangaji, lakini kutunza kumbukumbu za kila mmiliki wa ardhi kiasi kwamba hatuwezi kuwa tena na kelele za double allocation, hatuwezi kuwa na kelele za upandanaji wa ramani hapa na pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kufanya data conversion limefanyika kwa kiasi kikubwa 100% ramani za mipango miji pamoja na ile ambayo inakwenda kwenye ramani za upimaji wa ardhi, sasa usipokuwa na hiyo huwezi kwenda. Waheshimiwa Wabunge, tunaheshimu kile mnachokizungumza, wala hakuna ambaye hakiheshimu na ndio muelekeo tunaotaka sisi Watanzania wetu waweze kufikiwa, lakini tutaenda kwa kusuasua mpaka lini? Mimi nadhani hili mkiipa nafasi Serikali, halafu mkaja kuihoji hapa itakuwa ni vizuri zaidi, lakini ile dharura mnayoisema tunasahau kwamba hii ni fedha za kideni, kuna fluctuation ya currency na mpaka tunapoongea sasa hivi hizo dola mnazozisema hazipo, zimeshaliwa na mfumuko wa bei, kwa hiyo sio kwamba ni cash imewekwa ya dharura kwamba labda tutajisikia kama Wizara sasa tumepungukiwa tuchukue Hapana. Ile imewekwa kwa sababu kuu ya kuangalia mabadiliko ya currency zetu kwa maana ya inflation ambayo inakuwepo. Kwa hiyo, ni vitu ambavyo siyo kwamba tunaila sisi, na ukienda leo pesa imeingia toka mwaka jana jinsi ilivyokuja, ukienda sasa hivi siyo shilingi bilioni 345 tunazozisema leo, zimeshashuka kwa sababu siyo tena dola za Kimarekani milioni 150 kwa sababu ya suala la kibenki pia, kwa hiyo, ile siyo dharura ya kwamba inakwenda mfukoni kwa Waziri au kwa nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala haya niongelee suala zima la shamba lile la DDC la Mlolo Mheshimiwa Halima amesema. Mheshimiwa Halima wewe ni wakili, wewe ni wakili msomi na hili unalijua. Hivi kisheria unapokuwa na umiliki wa ardhi unaweza ukaukataa katika njia ipi? Una nyaraka ndio makaratasi sawa, lakini mwenye umiliki halali ana hati yake toka mwaka 1998 na bahati nzuri Mheshimiwa Gwajima leo hayuko hapa, wameshafanya vikao zaidi ya mara tatu wakishirikiana na wale DDC wenyewe pamoja na Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Dar es Salaam, walianzia shilingi 8,000 kwa square meter wananchi wakagoma, wakaja 6,000 wakagoma, wamekwenda kushuka kwa makubaliano wenyewe mpaka shilingi 4,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Halima unalolizungumza wale watu hawatalipa wasipimiwe ndio maana yake ile ardhi hawana faida nayo, hawawezi kuitumia mahala popote. Lengo la Serikali ni kuhakikisha wanamwezesha anapata hati na anakuwa mmiliki halali sio sasa leo unaambiwa ya DDC, kesho unatolewa na hayo hayo yako kule Chasimba Chachui.

Mheshimiwa Halima wananchi wamevamia maeneo lakini mtu tayari ana hukumu ya mahakama anatakiwa awaondoe, hasa katika kuwaondoa Serikali ime–intervene ikasema hebu tukae mezani, basi ninyi mmeshavamia hebu mrudishieni huyu hela yake ya ardhi aweze kuchukua ardhi nyingine na ninyi mmilikishwe muweze kutumia ardhi zile kisheria na kuweza kufanya kile ambacho kinaweza kuwasaidia katika maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuwaombe wananchi wetu kwanza wasivamie maeneo, kama wanataka kujenga wajenge maeneo kwa kufuata taratibu na kwa kutumia mamlaka za upangaji, asiingie kwenye eneo eti ni shamba limekuwa pori kwa muda mrefu halafu akasema kwamba hili sasa mwenyewe hayupo mimi naingia, tutakuwa tunafanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Kitandula namshukuru kwa hoja yake ambayo ilikuwa supported pia na Mwenyekiti wangu wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizara tunapokea kile ambacho kimekuja kwa maana ya notice zinapokuja na kama zina kila ushahidi hamna tatizo. Sasa unapokuja shamba limepewa notice sawa muda umetosha anatakiwa kunyang’anywa, lakini hati yake iko kwenye benki. Sasa lazima taratibu nyingine za kifedha zifanyike, na huyu bahati mbaya zaidi amekopa benki ya nje na ndio maana kama mtakumbuka miaka mitatu iliyopita tulibadilisha sheria hapa kwamba ardhi ya Tanzania kama unataka kukopa ukope ndani ya nchi na ukaendeleze hapa hapa ndani ya nchi, kwa sababu tumekuta wengi walikuwa wamekopa zamani kwa kutumia mashamba hayo hayo na hawayaendelezi nawamekopa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pale tulikuwa tunaweka dhamana mbaya kwa Tanzania yetu kwamba ardhi yetu tunayo kubwa, lakini kwa sehemu tayari imeshawekwa dhamana nje ya nchi. Akishindwa kulipa huyo mtu anakuja na hati yake anadai ardhi yake, huwezi kukataa. Tukabdilisha sheria hapa nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge mlisaidia tulibadilisha sheria.

Kwa hiyo, mimi niwaombe tu Mheshimiwa Kitandula kwa sababu masuala mengine lazima yafate taratibu, tutalifuata tu kama ambavyo lilivyo na tutafikia maamuzi na Mheshimiwa Rais sasa hivi ukimplekea hati za kufuta wala haichukui muda, amefuta amshamba zaidi ya 11 Morogoro na wakarudishiwa wananchi pale kawa ajili ya kupanga matumizi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hilo tunasema likishakamilika Mheshimiwa Rais hana neno na sisi kama Wizara, mimi kama mshauri nitapeleka kwa ajili ya kumshauri sasa afute ili ipangiwe matumizi mengine. Kwa hiyo, niwaombe tu kwamba maeneo yote hayo ambayo mnayazungumzia kwamba pengine mlishaomba yafutwe lakini hayajafanyika ni taratibu tu zikikamilka tunafuta. Changamoto tunayoipata tukiwarudishia kwenye Halmashauri/Mamlaka za Upangaji mnataka kupima viwanja vyote, mnasahau kwamba tunahitaji kuwa na mashamba. Kuna maeneo mengine hayatakiwi kuendelezwa I mean kurudishiwa ukapanga viwanja, bado lilikuwa ni shamba limeshindwa kuendelezwa na halijaharibiwa mle ndani kwa maana watu wameweka miundombinu ya kudumu labda majengo bado unaweza ukalitumia kama shamba na kwa mjini pia urban farming inakubalika heka tatu unalima. Sasa tutajikuta mjini kote tunajaza viwanja, viwanja halafu mashamba yanakosekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna mahali pengine pia tukiwaletea kwa ajili ya kufanya mpango wa matumizi basi tuombe tu tuangalie kama kweli tunatoka kwenye shamba tunaingia kwenye mji au tunafanyaje, lakini lengo la Serikali, lengo la Wizara ni kuhakikisha haya yote tunayafanya katika utaratibu ambao ni mzuri na haumuumizi mtu yeyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ambazo zimezungumzwa zingine tutazileta kwa maandishi kwa sababu zilikuwa ni hoja nyingi, lakini nirudie kwa kusema tunaheshimu michango yenu na bahati nzuri katika lile suala la mradi Kamati ya Bajeti pia ilishalichukua na walikuwa wanalifanyia kazi. Kwa hiyo, tuna imani ya kwamba kile tulichiokieleza na kama kutakuwa na changamoto nyingine yoyote katika suala zima hili tutaweza kuona tunafanyaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chege naye aliongea kwa uchungu sana suala la Utege, naomba tu nimwambie ya kwamba, sisi tutakuwa tayari kwa wakati wowote kuweza kuona ni jinsi gani tunaweza kutatua matatizo hayo bila kuwa na shida yoyote. Lengo letu ni kumsikiliza mwananchi aseme anachokisema na Serikali itaeleza kwa nini inataka kutwaa eneo lile, ili wote tuwe katika win-win situation kwa sababu, hakuna anayetaka kumuumiza mwenzie. Kwa hiyo, tukishamaliza hivyo maana yake mtu anapewa haki yake anayostahili na tunaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu ya kwamba kwa Wabunge wote changamoto zote mlizonazo tumezipokea. Kule tutakakotakiwa kufika tutafika, tutashirikiana na wenzetu wa mamlaka za upangaji kuhakikisha kwamba migogoro inatatuliwa. Hatuhitaji migogoro mipya, tunahitaji kumaliza iliyopo na kwa sababu tunaingia kwenye digitali, taarifa zote mtazipata kiganjani na haya ni mabadiliko makubwa chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Ardhi inakwenda kuwa Wizara wezeshi kikweli kweli na sio Wizara ya migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.