Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye aliyetuumba, ametupa uzima na uhai, siku hii ya leo ametutunza na tuko Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba niunge mkono asilimia mia kwa mia bajeti hii iliyopo mbele yetu.
Ninaomba nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwapa imani Watanzania, kwa elimu bure, Watanzania wameona matunda yake, vilevile Watanzania wote wanampongeza jinsi anavyofanya kazi nzuri ya kutumbua majipu, Watanzania wanaona, wanafurahi na jinsi ya kubana matumizi. Zile pesa zinawaendea wenyewe kwa ajili ya matatizo yao na kuwapa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wa haki na uhuru. Jana nilikuwa Zanzibar, kuna amani tosha. Nimepata marashi ya karafuu murua kwa ajili ya Watanzania jinsi tunavyoishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mawaziri wote wanavyofanya kazi vizuri na yaliyokuwa mbele yetu kwa ajili ya Taifa letu, kwa ajili ya kutimiza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Endeleeni, kazeni buti, mnafanya kazi nzuri ambayo sasa hivi kila mtu anaona jitihada zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende upande wa Halmashauri kupitia elimu. Shule zetu zimezeeka sana ambazo ziko upande wa kijijini, zina nyufa, chini sakafu hakuna, ninaomba basi miundombinu hiyo itengenezwe na Halmashauri zetu sasa zifanye mikakati mikubwa na mipango mizuri ya kuboresha shule zetu kila mwaka waweze kujenga madarasa manne au mawili kwa ajili ya uboreshaji wa shule zetu za primary, pamoja na kuanza kujenga kwa kasi kubwa…
TAARIFA...
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siikubali taarifa yake kwa sababu mimi nilikuwa Zanzibar, nimekaa siku nne, kuna amani na utulivu, na uchaguzi umefanyika kwa haki. Kama kuna mabomu yeye anafanya nini humu ndani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar ni tulivu kabisa, hakuna mabomu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo maana yeye yuko humu ndani, anakula upepo, ina maana kama uchaguzi usingefanyika wa haki yeye asingekuwepo hapa. Demokrasia imechukua mkondo wake, Wazanzibari wamefanya kazi yao nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Precision Air inaanza kwenda Pemba, safari ya Dar es Salaam, Unguja - Pemba, naomba nimpe taarifa hiyo, kwa sababu ya amani na utulivu wa nchi hii.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji vingine havina shule kabisa ya primary, ninaomba Serikali iangalie kupitia Halmashauri zake, vile vijiji ambavyo havina shule za msingi ziweze kujengwa. Pia shule za sekondari, zipo shule za sekondari ambazo hazikujengwa kwa kiwango leo hii ukienda zina ufa, ninaomba zichukuliwe hatua ambazo zitaboresha shule zile pamoja na nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la afya. Tuna Bima ya Afya ambayo tumewahamasisha wananchi wetu ambao Wabunge wengi wamezungumzia. Ninaomba Bima ya Afya ni matatizo makubwa sana kwa wananchi wetu. Wakienda hospitali kwenda kuchukua dawa wanaambiwa dawa hakuna waende kununua dawa. Tunaomba mikakati mizuri ya Bima ya Afya iwekwe vizuri ili wananchi wetu waweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya hasa Wilaya ya Mpanda vimekaa vibaya. Ukienda Kituo cha Afya Kalema, Mwese na Mishamo ni distance ndefu mno, hatuna gari hata moja. Ndiyo maana tumepata matatizo makubwa sana, asilimia ya vifo vya wanawake wajawazato mwezi wa nane na mwezi wa tisa, kila mwezi tulikuwa tunapoteza akina mama 40 wanaokufa kutokana na vifo. Tunaomba sana mtuangalie kwa jicho la huruma, mtupe ambulance za kuweza kusaidia akina mama Wilaya ya Mpanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye zahanati unakuta muuguzi mmoja tu, hakuna msaidizi, matokeo yake muuguzi yule akiondoka, maana muuguzi huyo ndiye daktari, ndiye nesi, ndiye mhudumu. Ina maana akitoka akina mama wakienda pale au mgonjwa akiwa serious hatapata huduma kutokana na muuguzi kuchoka, hayupo, amekwenda kunywa chai, matokeo yake tunapata matatizo mengi makubwa ya vifo ambavyo hatukuweza kuvitegemea. Ninaomba tuweke mikakati mizuri, tutengeneze kila Mkoa, tuwe na vyuo ambavyo ni vya kuwa na wahudumu wetu pamoja na manesi, tuibue manesi kila Mkoa ili waweze kusaidia vituo vyetu vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda zahanati nyingi, watu wengi wamesema, zahanati nyingi, shule nyingi hazina maji safi na salama ni shida. Tunaomba Serikali ijiwekee mikakati mizuri kwa ajili ya maeneo ya zahanati na shule zetu za msingi na shule zetu za sekondari kuwe na maji safi na salama kwa ajili ya watoto wetu. Unakwenda unakuta vyoo hakuna, vyoo vingi vimechakaa, vyoo vingi vimeshaanza kutitia. Tunaomba uboreshaji kwenye shule zetu za primary na sekondari vyoo vijengwe upya ili watoto wetu waweze kuishi kwenye mazingira mazuri na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mazingira. Upande wetu wa Mpanda eneo kubwa ni misitu. Misitu ile imevamiwa na watu, wameingia wanakata miti kama mchwa, mazingira yanaharibika. Tunaomba mikakati mizuri ya Serikali kutunza mazingira kwa ajili ya afya zetu za mvua ili tuweze kupata mahitaji muhimu ndani ya jamii yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuja upande wa bibi maendeleo. Hatuna mabibi maendeleo ndani ya Wilaya zetu na Kata zetu. Akina mama wanapata shida sana jinsi ya kuweza kufundishwa ujasiriamali na jinsi ya maendeleo kutokana na kutokuwa na mabibi maendeleo, hatuna mabwana shamba kila kata. Tunao mabwana shamba wachache sana. Sasa unakuta akina mama wanaohitaji kufundishwa jinsi gani ya kulima kilimo bora hakuna watalaam ambao wanaweza kuwafundisha. Tunaomba jitihada za Serikali tuongeze mabibi afya, tuongeze mabibi maendeleo, tuongeze mabwanashamba kwa ajili ya huduma nzuri ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji. Ndani ya vitongoji vyetu na vijiji vyetu akina mama wanapata shida sana ya maji. Maji wanafuata maeneo ya mbali ambapo wakati mwingine maeneo mengine akina mama wanaamka usiku sana, saa nane za usiku, saa tisa za usiku kwenda kutafuta maji. Ninaomba mikakati ya maji iwe mikubwa na mipana zaidi kwa ajili ya akina mama ambao wanapata shida ya kutafuta maji. Maji yenyewe wanapoenda kuyatafuta ni maji machafu, siyo maji salama. Ninaomba Serikali yangu sikivu iweze kupanga mikakati mizuri ili iweze kupata maji salama kwa ajili ya wananchi wetu waweze kupata manufaa ya sera yetu ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ninaomba niunge mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.