Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Naomba nianze kwa kutambua kazi kubwa ambayo wenzetu wanaifanya, na hasa nataka kutambua uamuzi wa Serikali na wa Rais wetu na Mheshimiwa Waziri wa kuweza kuwapitisha wenzetu wawili kwenda kugombea kwenye nafasi kubwa sana huko duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumzia Mheshimiwa Spika wetu, Dkt. Tulia Ackson, anayegombea Urais wa IPU, na mimi naamini, ninamfahamu tangu chuo kikuu, ni mtu sahihi sana kwa nafasi hiyo. Kwa hiyo tuiambie dunia kwamba amepatikana mtu sahihi wa kuongoza chombo chetu hiki muhimu na wasitie shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini imezungumzwa hapa kwamba Mheshimiwa Ambassador Liberata ni mtu mahiri, muhimu sana, na hiyo nafasi itakuwa imepata mtu sahihi. Kwa hiyo niishukuru sana Serikali kwa uamuzi sahihi sana wa kuwatanguliza hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni swali kwa kweli, kwamba kwenye zile hatua nne za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, tulianza na customs union, tukaja soko la pamoja, lakini tarehe 31 Novemba, 2013, tukasaini protocol ya monetary union, ni miaka kumi, inaisha mwaka huu. Nataka kujua tupo hatua gani; na je, hatuoni haja ya kuharakisha mchakato huo tukizingatia kwamba sasa hivi tunazungumzia Dola ya Marekani ikienda kusambaratika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mnafahamu, sasa hivi duniani, Middle East, hapa BRICS wanazungumzia kuanzisha fedha yao. Hatuoni ni muda sahihi sisi kuwa na fedha yetu Jumuiya ya Afrika Mashariki; East African Currency, hatuoni kama muda umefika? Ningeshukuru sana Mheshimiwa Waziri kama hili nalo ungeweza kulitolea ufafanuzi wakati una-wind up.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka niongeze sauti kidogo, mimi sizungumzii uraia pacha kivile, na hili jambo lilizungumzwa vizuri sana kwenye hotuba ya Mwalimu Nyerere. Mara baada ya nchi yetu kupata uhuru na kuwa Jamhuri, tarehe 10, Desemba, kwenye Bunge letu, Mwalimu alitoa hotuba moja muhimu sana ambapo alieleza tunakwenda kujenga Taifa la namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wakati huo kulikuwa na matabaka makubwa kati ya Wazungu, Wahindi, Waarabu na Waafrika. Na alijaribu kuwatia moyo, kwamba ninyi Wazungu hamjapoteza chochote kwa sababu bado uchumi upo mikononi mwenu, mna elimu zaidi; na Waafrika akawaambia mna political control, kwa hiyo tukiunganisha hizi forces mbili tunaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kweli wakati huo kulikuwa na wasiwasi, suala la uraia lilikuwa kubwa, na Mwalimu alilizungumzia kwa kirefu sana. Lakini hoja ya msingi kwa upande wangu, suala kiuchumi ni zuri, lakini kwa kweli ni secondary, hoja ya msingi hapa tunalindaje haki za asili, haki za Kimungu? Kitila Mkumbo kuwa Mtanzania si chaguo lake, ni jambo la asili, jambo la Kimungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kati yetu hapa ambaye amechagua awe Mtanzania, au Mganda au Mkenya, uraia wa kwanza ni wa asili, unazaliwa kuwa raia wa nchi fulani. Mambo mengine ya kujitakia unaweza ukaamua uende kutafuta uraia wa nchi nyingine. Lakini kwa kweli jambo la msingi kuliko yote ni kwamba huyu mtu ambaye kwa Kimungu kabisa amezaliwa kuwa Mtanzania, na baadaye ameamua kwenda kusaka fursa, na kwa mujibu wa Katiba yetu Ibara ya 17(1) inasema hivi; 17.-(1)Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nimekaa hapa, mmenisomesha, nimeamua kwenda kutafuta kazi Afrika Kusini, nimepata. Lakini kule Afrika Kusini kuna hati fulani ili uzipate lazima uchukue mambo yao fulani; kitendo hicho kinaninyan’anya haki yangu ya Kimungu ya kuwa Mtanzania kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukisoma nchi nyingi ambazo zinapinga, hazitaki uraia pacha, zipo, hata Sweden. Lakini kitu kimoja ambacho wamekilinda ni haki ya uraia wa watu wao. Kwa hiyo wewe kachukue uraia wowote, lakini wewe ni Mtanzania, wewe ni Mswiden, wewe ni Mwingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hakuna mtu anayezungumzia hapa kwamba eti atoke mtu kutoka nchi nyingine aje apewe Uraia wa Tanzania, hilo hatulipiganii, tunachopigania na kinachozungumzwa hapa; kwa nini turuhusu Mtanzania apoteze haki yake ya Kimungu kwa sababu tu amekwenda kutafuta fursa katika nchi nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sasa hivi tunazungumzia, duniani, takwimu zinaonesha kabisa, moja ya njia za kutatua tatizo la graduate unemployment, tatizo la ajira ni kubwa, lakini tatizo kubwa la ajira kuliko yote ni tatizo la ajira ya watu ambao wamekwenda shule, wa vyuo vikuu hawa, hilo ndilo tatizo kubwa. Kwa hiyo njia ambayo zinafanya nchi nyingi ni kuwaandaa watu wao kuwa global citizens ili wakatafute kazi huko duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukisukuma hilo unaondoa vikwazo. Kwa hiyo hili jambo kama litakuja kwa uraia pacha, ama hadhi maalum, kwangu siyo hoja kubwa, hoja kubwa ni tunalindaje haki za watu wetu ambao ni Watanzania wanapokwenda kutafuta fursa kwenye nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata kiuchumi, uchumi watu wengi wamesema hapa, vitu gani vinakwamisha watu wetu? Sisi watu wetu wengi wanakaa nje vizuri tu, ukiangalia idadi ya Watanzania, Waganda, Wakenya, hatutofautiani sana kwa walioko nje, lakini kwa nini remittance za wenzetu ni kubwa kuliko za kwetu? Kwa hiyo zimefanyika studies na zinaonesha, ya kwanza ni kwamba Mtanzania akiwa nje anakuwa hana confidence, kwa hiyo ni jambo ambalo lipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile hata watu wetu kutoka nje ni changamoto, inaonesha kwamba kwa East Africa Watanzania ndio watu ambao wanaongoza kwa kutokupenda kutoka nje, ambayo siyo faida kwa leo. Kwa leo ungetaka kuwa na watu ambao wanachangamkia fursa duniani na ndani ya nchi yao. Kwa hiyo nadhani hili ni jambo la msingi la kiliangalia, whatever form we are going to decide, kama ni uraia pacha, kama ni hadhi maalum, lakini ni jambo ambalo lazima tuliangalie kwa umakini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita nadhani Daily News wametoa taarifa, walikuwa wanamnukuu Mheshimiwa Rais, inaonesha kwamba ukiangalia hizo hela kutoka nje (remittance) na uwekezaji kutoka nje kwa Watanzania imefikia 2.5 trillion shillings; ni pesa nyingi. Kwa hivyo lazima Mheshimiwa Waziri uangalie ni namna gani utatengeneza mazingira mambo mawili yatokee; Watanzania wengi wachangamkie fursa za kiuchumi zilizopo duniani, lakini pia waliopo kule duniani wachangamkie fursa hapa nyumbani kwa maana ya uwekezaji. Hiyo lazima tuweke mazingira mazuri ya kufanya hivyo kwa sababu ni jambo la msingi. Kwa hiyo hili jambo likamilishwe mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kabisa kwamba wameshazidisha, hela ambazo zinakuja kutoka kwa hawa zinazidi hela ambayo tunapata ya kahawa, cashewnuts, tumbaku na chai ukiunganisha. Hela za watu waliopo nje (diaspora), ni kubwa, kwa hiyo siyo jambo ambalo kwa kweli tunaweza kuendelea kuliangalia kwa jicho ambalo siyo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo kwa kweli hoja yangu kubwa ni hiyo, kwamba muda umefika hili jambo lifanywe likamilike. Na tutumie fursa ambayo naisema kila siku; Mheshimiwa Rais amekuja na mambo hayo manne, suala la reform ni muhimu, kama kuna eneo la kufanya reform kubwa kuliko yote ni suala hili. Kwa saabu kwa kweli hata kama tunazungumzia Katiba mpya, itakapofika mjadala hili ni suala ambalo lazima tuliangalie kwa makini sana ili Watanzania haki zao za asili zilindwe popote walipo, iwe ni ndani ama nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)