Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tandahimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Allah Subhanahu Wa Ta'ala lakini nikushukuru wewe kwa kuchangia siku hii ya leo.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa shukrani kama sikumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kumpa nafasi ya Uwaziri ndugu yangu January Yusuf Makamba kwa kweli Mheshimiwa Rais ametutendea haki sana Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, katika Wizara ambayo watendaji wake wana-combination sawa sawa ni Wizara hii ya Nishati na Madini. Ukianza na Waziri mwenyewe Mheshimiwa Makamba, Naibu Waziri Stephen Byabato, Katibu Mkuu Engineer Mramba, Mkurugenzi wa TANESCO Maharage Chande Mkurugenzi wa REA Engineer Hassan Said, ukienda kwa Mkurugenzi wa EWURA, Daktari James Andilile mambo ni bambam kabisa kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, katika mambo watu wa kusini Mtwara, Lindi na Ruvuma tutayaandika kwenye historia yetu ya miaka na miaka ni mradi huu wa LNG ambao leo mazungumzo yamekwisha kamilika. Tangu miaka ya 2011 huko, tulikuwa na matumaini makubwa ya kupata mradi huu wa LNG tukatarajia sasa mambo ndiyo yanakimbia Mikoa ya Kusini, katikati mambo yalisimama. Ujio wa Daktari Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, mambo yamefunguka Kusini. Hakuna tunachoweza kumlipa Mheshimiwa Rais zaidi ya kumuombea dua kwa Allah subhannah wasubuhanah ampe maisha marefu neema ya Kusini tuione. Aendelee pia kumuamini Mheshimiwa January kwa sababu anayasimamia haya ambayo ndio dhamira ya ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika Wizara yenye watu wasikivu ni Wizara hii ya Nishati. Mtwara kwenye suala la REA tumekuwa miongoni mwa watu ambao kama Wizara ilivyosema kwenye taarifa yake, umeme wa Taifa ile asilimia 70 unatoka Mtwara lakini Mkoa wa Mtwara ndiyo Mkoa ambao vijiji vingi havina umeme, kwa usikivu wa Waziri na Mkurugenzi wa REA tumeshafanya na vikao Mkoani Mtwara, tukakaa na Wakandarasi lakini na juzi tumekaa tena na Wizara pamoja na Waziri, ametupa ahueni hapa ya siku 90 kwenda kukimbiza mambo Mkoa wa Mtwara ambao vijiji vingi havijapata umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupa vijana hawa ambao wanasikia. Tuliwaomba watupeleke kule mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kumbe wakati tunaomba wenzetu walishakimbia hatua mia mbele hatukujua, yale tuliyoyaona jana na juzi unapelekwa Bwawa la Mwalimu Nyerere ukiwa Dodoma basi mpeleke na Mikoani watu waone taaluma ile. Kuona ni kuamini Watanzania wengi tunapozungumza mafanikio ya Bwawa la Mwalimu Nyerere wengi hawajaona kama haya ambayo Wabunge tumeyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwako Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla, pelekeni vile vifaa basi Mikoani, Wilayani tuwaoneshe Watanzania kazi mnayoifanya, kwamba Rais amewaamini na ninyi mnafanya, mnatekeleza na leo mmetupa ahueni nyingine kwamba mwakani mambo ni bambam, sasa tunataka nini tena Watanzania, eeh?
Mheshimiwa Spika, kama bwawa likijaa na mkaanza kutupa umeme ndiyo faraja yetu sisi, ndiyo faraja kubwa. Mheshimiwa Waziri nchi jirani ya Msumbiji sisi tunapakana na Mkoa wa Cabo Delgado sisi watu wa Mtwara lakini hatuko mbali na Mkoa wa Emba wenzetu nao wanayo gesi. Huu mchakato wa LNG ambao wewe umeuchangamkia, kama kuna namna ya ku-fast track hebu tuanze sisi kabla ya wenzetu kwa sababu na wenyewe wanautaka. Uone namna sahihi ambayo mnaweza ku-fast track hii LNG iweze kukimbia kwa haraka sana. Ni ni majirani sana sasa tukianza tutakuwa na fursa kubwa ya kuwauzia wenzetu wa nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, tuliopata bahati ya kwenda kwenye bwawa kwa kuona kabisa, zamani Daktari siyo Daktari kama wewe Dkt. Tulia wa Falsafa tunao Madaktari wasio wa Falsafa ndani humu. Daktari Musukuma alikuwa haelewi mambo ya Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini ulitupa ujumbe wa Kamati na yeye, katika vitu ambavyo tunaweza kumpongeza Waziri January Makamba ni utashi wake wa utayari wa kuwa Mwalimu wa kufundisha na kueleza uhalisia.
Mheshimiwa Spika, tulikuwa site kule Daktari Musukuma, Daktari wa Heshima, walikuwa hawakujui kwa nini amepewa Udaktari wa Heshima leo nikuambie kwa uwezo wa Musukuma mpaka kuanzisha biashara kubwa ametunukiwa Udaktari wa jambo hilo, kwa hiyo usipate shaka na Udaktari wake. Alikuwa haelewi kwamba January anafanya nini lakini tulipokwenda Bwawa la Mwalimu Nyerere tukakaa kwenye chumba akatupa mpango wa Serikali, nini kilisimama, nini kinaendelea, leo kati ya Mabalozi wazuri wa Wizara hii, Musukuma atasema hapa atachangia, amekiri kwa sababu kuona ni kuamini, aliyoyaona leo nadhani katika bajeti ambayo tusingechangia wengi, maana mambo mengi tumeshayaona tayari, kila kitu kipo tayari, ilikuwa watu sita, saba ipite watu wakaendelee kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kazi iliyofanywa na Wizara kuanzia semina tulizopata bora kabisa, kuelezwa mipango mizuri ya Serikali, jana tukapelekwa Bwawa la Mwalimu Nyerere, mimi nilitamani nikimaliza hapa tumalize mambo. Tumalize tu tupitishe hawa wakubwa wakafanye kazi tunataka matokeo. Tukipitisha hii bajeti tunataka matokeo 2024 kesho tunapokwenda hata marafiki zetu hawa basi wanaweza wakaja huku tukaungana nao kwa sababu wanaona matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama kuna jambo limetendewa haki kabisa ni hotuba na bajeti ya Wizara hii kwa namna ilivyoandaliwa kwa utashi mkubwa kwa umakini mkubwa, ubora mkubwa, umakini mkubwa, sina namna ya kuongeza zaidi ya kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)