Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kuiwezesha Wizara hii lakini pia kuhakikisha angalau miradi mingi ya kimkakati na miradi ambayo kimsingi ndiyo msingi wa uchumi na uzalishaji wa umeme inakwenda kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili nami naungana na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa dhati kabisa kwa namna ambavyo anaendelea kuwashika mkono na kuhakikisha angalau Wizara hii inaweza kutimiza yale ambayo ni malengo halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo kwanza ulivyo mbunifu, ulivyo mpole, namna ambavyo unasikiliza hoja za Wabunge, pia naamini kabisa namna ambavyo umeamua kutengeneza mfumo upya na kuliunda Shirika (TANESCO) kwa maslahi mapana ya Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukuomba sana kama kijana mwenzetu uendelee kuwa hivyo, ninaamini kabisa kwamba ukiendelea kuwa hivyo basi utatufikisha mbali sana kwenye hili ambalo ni kusudio letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kwanza pia kukushukuru sana, pamoja na kwamba mwanzoni tulianza kusuasua katika utekelelezaji wa umeme wa REA kwenye Wilaya yangu na Mkandarasi anayeitwa GIZA Cable, nitumie nafasi hii kukushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ulivyoingilia. Leo mimi nazungumza, katika vijiji 13 vilivyokuwa vimesalia kwa ajili ya kupeleka umeme wa REA, vijiji vyote sasa ninavyozungumza tayari umeme umefika na amebakiza vijiji viwili tu kuweza kuwasha umeme huo. Kwa hiyo, ni jambo la heri na mimi niendelee kuwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe Vijiji vya Nyihara, Kenyamsama, Borere, Wamaya, Urio, Tabati, Nyamusi, Nyahera pamoja na Masike, tayari umeme umeshafika, vimebaki vijiji viwili tu kwa ajili ya kuwasha. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana watendaji wa TANESCO kwa kusimamia hili na kuhakikisha angalau linatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya ambayo tunakupongeza na kukushukuru, nadhani leo tukushauri, ninatamani nikushauri maeneo mawili ili angalau uendelee kufanya mazuri zaidi kwa maslahi mapana ya Taifa. Kwanza, nimesikiliza hotuba yako na nikiangalia kwenye aya ya 22 ya hotuba yako ambapo ulikuwa unazungumzia hali ya uzalishaji wa nishati umeme na mahitaji halisi ya wananchi juu ya uzalishaji kutumia nishati ya umeme, mwenyewe kabisa kwenye hotuba yako kwenye aya ya 22 umekiri hadharani kwamba haiendani na kasi na namna ambavyo wananchi wanahitaji umeme na uzalishaji wenyewe ulivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda kwenye vipaumbele vyako kwenye hiki kitabu ulichotupatia, kipaumbele cha kwanza kabisa umezungumzia hilohilo, kwamba ni kuhakikisha angalau vile vitongoji vyote vilivyosalia, vitongoji 36,101 vinapata umeme safi na salama. Pia ukienda kwenye aya ya 113, mpango maalum wa kuhakikisha kwamba angalau umeme wa REA unafika kwenye maeneo ya vitongoji vyote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza haya yote maana yake kuna jambo ambalo nadhani unakusudia kulifanya lakini kwenye hotuba yako humu ndani labda hujaliweka sawa. Ninatamani sana utakapopata nafasi ya kufanya majumuisho kesho utuambie mpango mkakati uliojipanga kuhakikisha angalau vitongoji vyote 36,101 vinafikiwa na umeme nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka na utakubaliana na mimi kwamba kila wakati ukisimama ndani ya Bunge unaona Wabunge namna wanavyohoji umeme ndani ya vitongoji. Nami mwenyewe ndani ya Jimbo langu nina vitongoji 507, lakini vitongoji ambavyo vina umeme havizidi 200. Kwa hiyo, maana yake zaidi ya asilimia 60 ya vitongoji vilivyosalia havina nguzo wala miundombinu yoyote ya umeme, na ndivyo ilivyo katika maeneo yote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu dhamira yako umeionesha kwenye hotuba yako, ningetamani mwishoni Mheshimiwa Waziri utuambie, na usiogope, kama kuna namna nyingine bora ya kupata fedha, tuambie Bunge hili lijue, kama kuna namna ya ku-impose hata rate kidogo kwenye gharama za mafuta kwa maana ya shilingi 50 mpaka shilingi 100 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba umeme unapata fedha nyingi, zaidi ya shilingi trilioni 6.7, kwenda kutatua vitongoji vyote nchi hii, wewe tuende huko useme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Rais amekuwa akilizungumza hili, kwamba ndani ya miaka mitano matarajio yetu ni kwamba vitongoji vyote 36,000 vinakwenda kupata umeme. Sasa Mheshimiwa Waziri ukiliacha hili likawa fumbo na kuendelea kututesa maana yake inawezekana ndani ya miaka mitano usilifikie. Nenda fanya kazi, fanya utafiti, kaa na Wizara ya Fedha, hata ikibidi kama unaweza kuweka shilingi 50 mpaka shilingi 100 kwenye nishati ya mafuta ili angalau iweze kuzunguka nchi nzima ili vitongoji vyote viweze kupata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ambacho ninatamani nikushauri pia ni namna ya utekelezaji wa umeme kwenye maeneo ya Miji ambayo inakua. Mimi nina Mji pale unakua unaitwa Shirati, tumekuwa tukiuita Mamlaka ya Mji Mdogo lakini ni mamlaka ambayo haina GN, haipo kisheria, hata uki-google hapo Mamlaka ya Mji Mdogo Shirati hautaiona, lakini rates wanazochajiwa wale wananchi, wanalipa zaidi ya shilingi 321,000 kwa nguzo moja wakiambiwa kwamba ile ni Mamlaka ya Mji Mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hawajapata usajili hakuna GN, hakuna mratibu na wala haijiendeshi iko chini ya Halmashauri, ninaomba sana Mamlaka ya Mji Mdogo, kwa maana ya Shirati, Kata za Mkoma na Raranya, tuendelee kuwaungia umeme kwa bei ileile ya zamani, shilingi 27,000, badala ya kuwaongezea bei. Kwa sababu tunawaongezea bei kwa sababu ile ni Mamlaka ya Mji Mdogo lakini mamlaka haipo, kwa hiyo inatengeneza taharuku na sababu ambazo hazipo. Ningetamani sana kesho wakati wa majumuisho utamke tu kwamba wananchi wa maeneo haya, hizi Kata mbili, kwa sababu bado mamlaka haijaanza kufanya kazi, haipo na haijasajiliwa, basi waendelee kuunganishiwa umeme kwa bei ileile wenzao wa vijiji vingine wanayounganishiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika hilo ni fidia ya wahanga wangu ambao walikubali toka 2011. Nilikwambia hili kwamba waliridhia kwa hiari yao kupisha umeme mkubwa uwe maeneo mengi, vijiji vingi tu. Zaidi ya wananchi 200 toka mwaka 2011 hawajalipwa fidia. Ninaomba pia kesho ukipata nafasi utamke juu ya hawa wananchi. Kwa nini toka 2021 Mkoa mzima wa Mara vijiji vyote vimelipwa kasoro Wilaya yangu ya Rorya. Wilaya zote zimelipwa kwa ajili ya kupisha umeme ule kasoro Wilaya yangu ya Rorya. Hawa wananchi wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu, kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilikuambia mwaka jana ninaamini kesho ukipata ridhaa ya ku-conclude utatoa tamko juu ya adha hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu katika hilo ni hawa watu wa ETDCO hii kampuni tanzu ambao wanafanya kazi. Yawezekana ikawa inafanya kazi vizuri sana, nimeona humu wanazungumza wanapata faida mpaka bilioni mbili na pointi kwa mwaka, lakini kwangu nadhani kuna sehemu hawajafanya vyema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, toka mwaka 2021 leo ni 2023, wamepewa miradi mitano, hawajawahi kufika hata mradi mmoja. Sasa haya ndiyo yanaleta manung’uniko mengi, wakati mwingine Mheshimiwa Waziri unaweza ukavishwa mzigo ambao siyo wa kwako. Kama ETDCo hawana uwezo bado wa kufikisha umeme maeneo haya, apewe Mkandarasi mwingine ili apeleke vitongoji hivi vyote alivyopewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ana miradi maeneo matano, na nitakutajia, anayo Kasino, Kongo, Isegere, Buturi, Kyamwama na Nyamunga. Maeneo haya toka 2021, leo tunazungumza 2023/2024 hakuna Mkandarasi site wala chochote kinachoendelea. Kwa hiyo, unaweza ukaona wananchi wana haki ya kulalamika lakini kuna mtu mwingine tu ambaye amepewa mradi inawezekana anashindwa kutimiza. Niombe na lenyewe hili utakapopata nafasi kesho uweze kulisemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kukatikakatika kwa umeme. Mimi Wilayani kwangu, kama nilivyokuwambia sehemu kubwa ya uzalishaji inategemea umeme. Kwa sababu umesema kwamba sasa hivi unaweka fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu, niombe sana Wilaya ya Rorya uingalie, kwa sababu mpaka sasa ninapozungumza na wewe haiwezi kupita wiki, siku tatu umeme haujakatika, unakatika kwa sababu ya miundombinu inawezekana ikawa imechoka sana. Kwa hiyo, nikuombe kwenye hili nalo uone namna unavyoweza kunisaidia kwenye upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, unafanya kazi vizuri sana, maeneo haya yote unayofanya kazi unafanya kazi kwa ushirikiano na Wabunge, kwa sababu bado ni mtu ambaye unasikiliza maoni na ushauri wa Wabunge, niendelee kukuomba endelea hivyohivyo kwa sababu msingi na dhaminra yako ni njema huko mbele utakapokwenda. Kwa hiyo, ninaomba haya niliyoyasema kwa nia njema kabisa kwa maslahi ya watu wangu wa Rorya ili uweze kuwakumbuka, ninatamani sana kesho, kama nilivyosema utoe angalau majibu kwa sababu haya yamekuwa yakilalamikiwa miaka nenda rudi. Suala la Shirati, kama nilivyosema, walipe 27,000 kama wanavyolipa maeneo mengine, kwa sababu bado hakuna mamlaka, hii ndiyo imekwamisha sasa shughuli za kiuchumi na kuvuta umeme pale limekuwa dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)