Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji asubuhi hii katika Wizara yetu hii ya Nishati. Awali kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wa Ta'ala kwa kutujalia afya njema, uzima lakini pia kuendelea amani kutamalaki katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri January Makamba, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara kwa kweli wanafanya nzuri na mwenye macho haambiwi tazama kwa sababu ukienda kwenye maonyesho pale unajione mwenyewe. Kama leo Mtanzania Mheshimiwa Mbunge ambaye hajawahi kufika kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini ameweza kulionia akiwa Dodoma na ameliona si kwamba ameliona picha ameona kwa uhalisia kabisa. Kwa hiyo kweli huu ni ubunifa mkubwa na ni mapinduzi ya kiteknolojia na kiutendaji katika sekta yetu hii ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, mimi niende kwenye maeneo matatu makubwa na nianze tu kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuendeleza ushirikiano mzuri baina ya TANESCO na ZECO Zanzibar hali kadhalika baina ya Wizara ya Nishati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Tanzania Visiwani, ambayo ni Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli ushirikiano ni mzuri na ndiyo haya mwenzangu Kaka yangu Pondeza ameyazungumza hapa. Kwamba hivi sasa tumeweza kufika kile kilio chetu ambacho tulichangia hapa mwaka jana kwa sauti kubwa kwamba bei za Tanzania Visiwani na za Tanzania Bara ambao wote hawa ni raia wamoja na ni ndugu – kulikuwa kuna tofauti kubwa sana, na sasa hivi ni furaha kwamba tumeambiwa kwamba hii kadhia imeweza kutatuliwa.
Mheshimiwa Spika, sasa ni ombi langu tu, kwamba tuwasiliane na wenzetu wa ZECO tukaone tafsiri ya haya mazungumzo na makubaliano tafsiri yake ikaonekane kwenye bill. Kwa sababu mimi nikiwa kama mtumiaji wa umeme bado ile tafsiri na mabadiliko hali sijayaona bado. Sasa ningeliomba tu kwamba haya mabaliko ambayo yanaonekana kwamba bei imekwenda kuwa negotiated na hadi sasa bei zinafanana basi ikaonekane kwenye bill ya mwananchi, kwa sababu siyo fair kwa Mtanzania huyu huyu ambaye kwenye Tigo, kwenye Zantel, kwenye Vodacom analipia sawasawa baina ya Tanzania bara na Tanzania Visiwani lakini umeme kuwe kuna tofauti. Nafikiri tunaamini kama hilo limekaa sawa ni vizuri na kama bado kuna tofauti ndogo tukarekebishe.
Mheshimiwa Spika, suala jingine ni kwanza nitangulize shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Waziri kutokana na jitihada na tafiti ambazo zinaendelea katika vyanzo vingine vya umeme. Kwa sababu ni hatari kuendelea kutegemea vyanzo vya maji peke yake. Kama tunavyojua kwamba nchi hii iinakabiliwa kama ilivyo dunia kwa ujumla na mabaliko ya Tabianchi na hatujui siku gani utakuja ukame wa kutisha na vyanzo vyetu vya maji vije viweze kuteteleka na hapa itakuwa hatuna msalia Mtume isipokuwa tukangalie vile vyanzo ambavyo havitegemei maji moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningelimuomba tu Mheshimiwa Waziri hapa atengeneze jitihada. Mwenzangu Mheshimiwa Sanga jana amezungumza hapa, kwamba kuna maeneo tayari ameshafanyia tafiti kama Makambako, lakini yapo maeneo mengi Tanzania kuna maeneo ambayo yana-potential ya umeme wa jotoardhi, umeme wa solar na umeme wa upepo. Sasa nafikiria maeneo ambayo tayari tafiti zimeshakamilika sasa nafikiri tuende tuka-invest ili angalau tupate megawatt chache za kuweza kuziweka kama akiba ili siku ambayo tutateteleka kwenye maji basi angalau tutakuwa tuna sehemu ya kukimbilia.
Mheshimiwa Spika, sehemu ya tatu ya mchango wangu niende kwenye ile ambayo jana alizungumza hapa Mheshimiwa Waziri, ile kuhama kutoka kwenye nishati chafu ya kupikia na kwenda kwenye nishati safi na salama ya kupikia. Na hapa tena niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anayaifanya, na niombee Mungu mradi wa LNG nao uende ukafanikiwe haraka ili uende ukaongeze ufanisi katika hili.
Mheshimiwa Spika, hapa pia nafikiria nimuombe tu Mheshimiwa Waziri tujitahidi kadri inavyowezekana, kwa sababu kama tunavyojua, kwamba bado kuna jitihada nyingi zinaendelea katika nchi hii katika suala la kuhama au shifting kutoka kwenye kutumia nishati chafu hii na kwenda kwenye nishati safi na salama. Wenzetu wa misitu wanafanya kazi hiyo, wenzetu wa mazingira wanfanya kazi hiyo. Sasa hivi jitihada twende tukazichanganye kwa pamoja ili tuweze kupata ufanisi mzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Tanzania inapoteza takriban hekta laki nne kwa mwaka. Na hekta hizi laki nne ambazo zinapotea kwa mwaka ndizo ambazo zinahifadhi na zinatiririsha maji kupeleka kwenye vyanzo vyetu vya umeme vya Kihansi, Pangani, Mtera, hali kadhalika na chanzo cha umeme ambacho sasa hivi tunakitegemea cha Bwawa la Mwalimu Nyerere. Sasa iwapo misitu hii itaendelea kupotea basi ni hatari kubwa kwa investment kubwa ambayo inafanywa na Serikali kwenye miradi yetu ya maji. Kwa hiyo, ningeliomba tu Mheshimiwa Waziri akajitahidi kukaa na wenzake hawa wa sekta ya TAMISEMI ili kuangalia wanafanya jitihada hizi kwa kiasi gani ili kuzichanganya kwa pamoja ili ziweze kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, lakini pia ombi langu, tusije tukavamia tukachukua register kwamba hizi nishati mbadala ziende kwa kila mahali Tanzania zienee. Ningeliomba tu kwamba tukaangalie uwezekano wa maeneo mbalimbali ambayo yako very strategic, ambayo ni potential. Kuna maeneo ambayo yana misitu na kasi ya kupotea kwa misitu ni kubwa; twende huko tukashambulie kwanza kabla hatujaenda kuangalia kila mahali. Kwa hiyo kwa utaratibu wetu sisi hasa Wizara ya Nishati tukaangalie maeneo ambayo yanatuhusu zaidi kwanza halafu tena baadaye ndipo tukaangalie upande mwingine.
Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa promotion ambayo anaendelea kuifanya. Waheshimiwa Wabunge hawa walifanya kazi kubwa kipindi cha sensa, walifanya promotion ya sensa na Tanzania nzima ilisimama na matokeo yake matokeo ya sensa sisi tunayajua. Kwa hiyo nafikiria na hii promotion ambayo unajumuisha Wabunge katika uendelezaji wa nishati safi na salama basi hii inakwenda kuzaa matunda makubwa, kama ambayo ulitufunza.
Mheshimiwa Spika, nishukuru na niunge mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana.