Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kutupa uhai siku ya leo, lakini pili nitoe shukrani zangu kwa Serikali hasa wakati huu ambapo sisi wa vijijini tunaonekana. Shukrani zangu zimwendee Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya lakini pia Mheshimiwa January Makamba, Waziri wa Nishati na Ndugu yangu Byabato Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeyasema haya makusudi kwa sababu mwaka juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja kuzindua umeme katika Mkoa wa Manyara, aliuwashia kwenye Kijiji kilichoko katika Jimbo la Mbulu Vijijini Mungahay; na kule tulikupa jina nafikiri unalikumbuka; tulikuita “Tlhaqwe”. Hilo jina ni maarufu sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Na tulikupa kwa sababu umewasha umeme kwenye vijiji ambavyo kwa kweli vilikuwa ndani sana. Sasa baada ya kuja kuwasha umeme kwa kweli mambo yamekwenda siyo mabaya ndiyo maana natoa pongezi hizi kwa Wizara. Lakini kubwa zaidi vijiji vyetu viko 76 na 43 vimepata umeme bado 33. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naona Mheshimiwa Waziri ni kijana na ni kijana mwenzangu ambaye tumefanya mengi. Wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kwanza wanafaidi sana jambo la umeme kwa sababu sisi kule bahati nzuri tuna viwanda vingi, na sisi ni wakulima, na unajua haya, na umefanya ziara mara nyingi katika eneo letu. Sasa nikuombe kabla sijasahau, hivi vijiji 33 ndugu yangu mtupatie namna ya kuvimaliza haraka. Kwa nini? Tofauti ya majimbo yetu ya vijijini yana kilometa nyingi kufikia kijiji hadi kijiji. Tuna mkandarasi kweli anafanya kazi yake lakini kwa kweli amefanya kazi taratibu mno kutoka wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, muwezesheni huyu mkandarasi. Mimi sina shida naye lakini ukweli ni kwamba anajitahidi; inawezekana lakini kwa sasa kwa kweli sitaki kumlaumu au kumtuhumu kwa sababu ni ndugu yetu anafanya kazi yake kadiri anavyoweza; lakini kwa kweli kwa sasa hajabahatika kuwasha vijiji 10. Sasa sina hakika mnafanyaje mtusaidie sisi, ni kilio cha wananchi wa Mbulu. Mtusaidie kwa kweli, muwezesheni. Matatizo yake, ninavyo sikia sina hakika, analia sana fedha hajawezeshwa sijui inawezekana vipi mumsaidie. Kwa kweli mumsimamie amalize hivyo vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lililoko kwetu sisi kutoka kijiji kimoja hadi kwenda kijiji kingine anahitaji kujenga zile nguzo kubwa kilometa 25, kilometa 20, kilometa 30 na hizo ndizo zilizobaki na kule kwangu kuna kata tatu. Kata ya Yaeda Chini, Kata ya Eshkesh; na hizo kata nazozisema Mheshimiwa Waziri ni kata ambazo kwa kweli ziko kwa Wahadzabe; na katika eneo la Tanzania hii, Wahadzabe wako kwangu. Ningefurahi, Mheshimiwa Waziri hebu weka legacy, sijui nisemaje kwa Kiswahili sanifu. Weka historia, wewe uwe Waziri wa kwanza kuwapelekea Wahadzabe umeme kwenye Vijiji vya Munguamollo, Dumanga, Yaeda Chini pamoja na Eshkesh. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo vijiji nimevitaja Mheshimiwa Waziri hivyo ndivyo vijiji vya Wahadzabe ambao kimsingi wakipata umeme, mimi naamini watatoka kule vijijini, huwa mara nyingi wanakaa kwenye mlima na wanarina asali na kupata mizizi ya miti.

Mheshimiwa Spika, na wakati wa sensa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ilibidi tuwinde wanyama wa pori waje kula na tuwahesabu. Kwa hiyo, ukishawapelekea umeme Mheshimiwa Waziri ni wazi kwamba wale ndugu zangu watakuja wakiwa wame-settle mahali, watakaa kwenye majumba yao wapate umeme. Nina hakika ukija Mheshimiwa Waziri utafurahi sana. Hawa ndugu zangu kwa kweli kwanza wameenda shule, lakini pili wanataka maendeleo na tatu kwa sababu hiyo basi utakapowapelekea maendeleo hasa haya ya umeme ni wazi kwamba nyumba zao zitawaka umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyumba zao si kama nyumba hizi za kwetu ambazo umezizoea, wana nyumba za asili ambazo naamini wakishawasha umeme kule watakaa na kuendelea kukaa maeneo hayo. Kwa hiyo niombe sana hilo. Na hizo kata kwa kweli ni muhimu sana kwa sababu tangu dunia imeumbwa hawajawahi kuona waya wa umeme, na kwa sababu hiyo basi na mimi nadhani muone namna gani utaratibu wa kuwasaidia hawa wakandarasi wanaokuja vijijini kwa sababu moja; wakandarasi wa mijini wao wanakuja na ile kushusha umeme mnaita underline. Sasa kwao ni rahisi sana kupata fedha na kuweza kujilipa na kuendelea lakini wakandarasi kwenye jimbo langu mimi wanahitaji hela nyingi kabla ya kuanza kutekeleza huo mradi. Kwa mfano, kwa vijiji hivi 33 ukiangalia urefu wao, umbali ni mkubwa sana. Ninaona wanakazana wamepeleka maeneo nguzo lakini sasa namna ya kufikisha umeme hapo imekuwa tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ombi langu lingine kubwa, nimeona kwenye bajeti yako, nikupongeze sana, bajeti imekaa vizuri na nimeona kabisa umeweka deadline unakwenda kumaliza vijiji vyote. Nimefurahi sana kusikia hivyo, na nikupongeze kwa hilo. Na ninashukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuweka fedha ambazo kila kijiji kinakwenda kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi muondoe ule utaratibu wenu wa ujazilizo. Kwa sababu ujazilizo maana yake nini; mnapeleka umeme halafu baadaye mnajaziliza sehemu ambazo hazikupata umeme. Sasa, kwa mimi wa vijijini kwa sababu sijapata kabisa kitu kinachoitwa umeme kwa hiyo ni wazi kabisa sitapata nini? Ujazilizo. Kwa hiyo, mtuone sisi wa vijijini ambao hatuna namna yoyote ya kupata huo umeme, haujafika bado, mtuwekee share au akiba kwa sababu sisi ni wananchi pia ili basi mnapopeleka umeme sisi tuwe na share yetu ya ujazilizo. Kwa sababu mnapeleka umeme aidha kilometa moja, na kwa sababu sisi pia hatukupata kwa sababu tu ya mazingira tuliyokaa, lakini basi muone mtakavyopeleka umeme huo ujazilizo ambao mjini wanapata sisi tupate na share yetu iwepo. Nimesema hivyo makusudi kwa sababu hamna namna nyingine nitaweza kupata umeme ikiwa ujazilizo utapita (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi nimeona kabisa vitongoji. Mimi vitongoji vyangu ni vingi, viko vitongoji 400, naomba Mheshimiwa Waziri uone hilo. Vitongoji kule kwangu ni sawa sawa na kijiji na tofauti kabisa na maeneo ya mjini. Na utakumbuka amechangia mchangiaji mmoja hapa, sisi wa vijijini na hali ya milima na miteremko kule inahitaji uangalifu wa kutosha sana Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo ombi langu mimi, wakandarasi walioko kule mjaribu kuwa-treat tofauti na walioko mjini. Si kwamba nawatetea bali ninaona hali ya mazingira yetu yalivyo kule. Kwa mtu wa kawaida huwezi kutekeleza mradi ambao unaonekana upo katika milima na maporomoko kutokana na hali yao ya kuwapatia fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nikuombe, ushauri wangu kwa Wizara yako, na huu nadhani ukiupokea utakusaidia. Kuna gesi tumekuwa tukiisema muda wote na muda wote tumeona mkifanya vizuri. Mtwara naona wameanza kazi nzuri, kuna majengo au nyumba 223 ambayo nafikiri yameingia gesi lakini kuna gesi ambayo tunataka kupeleka kwenye magari na mitambo hii ya kuendesha nini? tunasema kwa mfano gari. Mimi ningefurahi sana hata gari langu kupata gesi, kuondoa kitu kinachoitwa carburetor na kuweka gesi. Mimi ningeomba hapa Dodoma muweke kituo kikubwa cha ku-supply hiyo gesi, itasaidia sana. Muanze na majengo ya Mawaziri hapa na Naibu Mawaziri, itatusaidia sisi kufanya uhamasishaji na sisi tutajiunga huko. Maana kwa mfano ukijaza gesi Dar es Salaam ukija nayo Dodoma si imekwisha? Utajazia wapi? Naomba sasa muone namna gani Mheshimiwa Waziri, kwa sababu wewe ni kijana na Naibu wako wote ni vijana. Mimi nina hakika mtatupeleka kwenye ulimwengu mzuri wa kupunguza matumizi hasa haya ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kengele imelia nakushukuru sana. Ahsante kwa muda, naunga mkono hoja. (Makofi)