Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuipongeza Wizara kwa ushirikiano wao mzuri na pia kwa kusogeza huduma hasa za Taasisi kama vile REA na TANESCO hapa Bungeni, hii imetusaidia sana Wabunge kupata ufafanuzi wa papo kwa papo katika masuala ya majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, nina masuala mawili tu; moja ni kuhusu bei hasa maeneo ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji yanasomeka kuwa yapo mjini, lakini uhalisia wa maisha na kipato ni maisha ya kijijini. Kwa mfano Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ni mji lakini ina vijiji kumi na moja rasmi katika kata tatu. Lakini pia yapo maeneo ya pembeni mwa mji ambako maisha na kipato ni ya kijijini. Mfano wa maeneo haya ni mengi, hapa Dodoma ni Jiji lakini katika kata 41 ni kata kama 20 tu ndizo maisha ya mjini, kata nyingine 21 maisha na kipato ni ya kijijini. Kwa sababu hiyo mara kadhaa kupitia maswali na majibu nimeshauri kwamba tutizame upya bei ile ya shilingi 340,000 ndani ya mita 30.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwa maeneo ya vijiji yanayohudumiwa na REA bei ni shilingi 27,000. Naomba nieleweke vema, simaanishi kwamba maeneo ya vijiji lakini ambayo kwa mujibu wa sheria yanasomeka kuwa ni miji yatozwe shilingi 27,000, hapana, ushauri wangu ni kwamba tuwe na makundi kwa mfano ziwepo bei tofauti tofauti, tunaweza kusema kwa mfano maeneo ya pembezoni ya mji ikawa Kundi A bei shilingi 150,000; Kundi B ikawa ni vijiji ambavyo kwa mujibu wa sheria viko mjini lakini kimaisha na kipato ni kijiji, mfano pale Mafinga maeneo kama Ndolezi, Luganga, Mkanzaule na kadhalika maisha yao ni kijiji, kundi hili tukasema walipe shilingi 97,000.

Mheshimiwa Spika, hizi bei ni mfano tu lakini ninyi kupitia wataalam wenu mnaweza kuchakata mkaona namna bora ya kulifanikisha suala hili ambalo kwa mujibu wa majibu hapa Bungeni, mara kadhaa tumeelezwa na Wizara kwamba suala hili liko katika hatua za mwisho za kufanyiwa kazi. Naomba kama litawezekana basi tupate majibu kamilifu na kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni kuhusu nguzo; Kamati ya kupitia sekta ya uzalishaji na upatikanaji wa nguzo za umeme; kwanza nawapongeza Serikali kwa ushirikishwaji pale ilipokuja taharuki kwamba Serikali itaanza kuagiza nguzo kutoka nje ya nchi. Tulikaa na Waziri na timu yake pamoja na viongozi wa Serikali na Chama wa Mikoa ya Iringa na Njombe, kikao hiki kilihusisha Waziri, Katibu Mkuu, Kamishna wa Nishati na watendaji wa TANESCO na REA kwa upande wa Wizara na kwa upande wa mikoa ilihusisha Wenyeviti wa CCM wa Mikoa ya Iringa na Njombe na Wenyeviti wa Wilaya zote, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, baadhi ya Waheshimiwa Madiwani na wadau wa sekta kwa mana ya wazalishaji na wasambazaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uzito wa suala hilo na jinsi ambavyo linagusa maisha ya watu na uchumi wao, ilishauriwa paundwe Kamati ya Wizara na wadau ili kupitia mnyororo mzima wa suala la nguzo kuanzia upatikanaji wake na suala zima la ubora. Kamati hiyo iliundwa kwa nia njema yq kupata muafaka kuhusu suala la nguzo kuhusu upatikanaji, masuala ya manunuzi, ubora na kadhalika. Nia miradi ipate nguzo kwa wakati na kwa ubora na wakati huo huo wananchi waendelee kunufaika kama ilivyo katika suala zima la local content.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu Kamati hiyo ikamilishe kazi yake ili mapendekezo ya Kamati yawafikie wadau na Serikali kwa nia ile njema ya kuhakikisha nguzo zinapatikana kwa wakati na kwa ubora. Bado naamini tunaweza kuzalisha nguzo hapa nchini, kwa hiyo, Kamati hiyo kuhitimisha kazi yake ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, naomba.