Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na mimi niweze kutoa mchango katka Wizara hii ya Nishati na awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa baraka na neema zake na kwa kunijalia uzima na afya njema. Niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara na kazi nzuri anayoendelea kuifanya ya kuleta mabadiliko makubwa katika Taifa letu. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba, Naibu wake Mheshimiwa Stephen Byabato na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri na kubwa ya kuhakikisha nchi yetu inapata nishati ya kutosha, hongereni sana! Napenda kuwatia moyo endeleeni kuchapa kazi na sisi tupo nyuma yenu.

Mheshimiwa Spika, nitachangia maeneo yafuatayo; nianze na Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi imara wa Jemedari Mheshimiwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kuendelea kutekeleza mradi huu kwa weledi mkubwa na kuhakikisha unakamilika kwa malengo waliyojiwekea.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameonesha nia ya Serikali ya kukamilisha mradi kwa sasa mradi huu umefikia 87%; ni jambo kubwa na la kujivunia uzinduzi wa kujaza maji kwenye mradi huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere uliofanywa na Mheshimiwa Rais unatoa dira kama nchi tumeamua kuondokana na giza na kukaribisha mwanga kuliwezesha Taifa letu kupata nishati ya kutosha kwa kuwa mradi huu umegharimu fedha nyingi. Niishauri Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa mradi huu ili thamani ya fedha iweze kuonekana. Ninaamini kumalizika kwa mradi huu utakuwa ni kichocheo kikubwa cha kuleta maendeleo na kutavutia wawekezaji wa kutoka ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo ningependa kulichangia ni mradi wa REA; niipongeze sana Serikali kwa kuendelea kusambaza umeme kuhakikisha umeme unafika kila pembe ya nchi yetu vijijini, lakini bado jitihada kubwa zinatakiwa kufanyika ili vijiji vyote na vitongoji vyote viweze kupata nishati ya umeme. Katika mkoa wangu wa Singida kuna vijiji 441 kati ya vijiji hivyo vijiji 114 havijawashwa umeme, Ikungi vijiji 24, Iramba vijiji 10, Wilaya ya Manyoni vijiji 26, na Wilaya ya Singida 18. Niiombe Serikali iharakishe na vijiji hivi viweze kupata nishati ya umeme kwa haraka na wa kati.

Mheshimiwa Spika, niungane na Wabunge wenzangu pamoja na kwamba umeme umefika vijijini lakini bado vitongoji vingi havijafikiwa, niishauri Serikali ije na mpango mkakati wa kuhakikisha vijiji na vitongoji vyangu vyote vya mkoa wa Singida vinapata umeme, lakini pia Serikali iangalie upya bei za umeme hususan maeneo ya Miji Midogo kwani miji yangu ya Iguguno, Nduguti, Ikungi, Ilongero na Kiomboi hali zao ni za chini na hawana uwezo wa kulipa gharama ya shilingi 320,000 ili malengo mazuri yaliyowekwa na Serikali yaweze kutimia.

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ambalo ningependa kulichangia ni matumizi ya gesi majumbani yaani nishati safi majumbani, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa maono makubwa ya ustawi wa jamii hususan kwa kundi la wanawake kwani ndio wahusika wanaotumia gesi hii majumbani, kwa sasa ni asilimia ndogo sana ya Watanzania wanaotumia nishati safi kwa kupikia yaani gesi, niiombe Serikali ije na kampeni kubwa ya kuelimisha jamii juu ya matumizi ya nishati safi ya gesi majumbani ili wananchi wetu wengi waweze kuachana na nishati chafu ambayo kwa kiwango kikubwa imeharibu mazingira na vyanzo vya maji na ningependa kushauri kampeni hii iitwe “Achia Shoka, Kamati Gesi,” lakini niiombe sana Serikali ili maono makubwa ya Mheshimiwa Rais yaweze kutimia ni lazima gesi ipatikane kila mahala kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza watendaji wote wa TANESCO na REA wakiongozwa na Engineer Florence Godfrey Mwakasege Meneja wa Mkoa wangu wa Singida kwa kazi nzuri na naunga mkono hoja.