Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja bajeti ya Wizara ya Nishati na nikiwaomba Waheshimiwa Wabunge wote muipitishe, na ni kwa sababu hizi chache kwa muda niliopata nitakazozisema.
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, namshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu, na hasa kimahsusi Mheshimiwa Rais kwa kuniruhusu sasa ninasoma Bajeti ya Wizara ya Nishati au ninahudhuria au inasomwa nikiwepo kwenye Wizara hii kwa mara ya tatu; ninamshukuru sana kwa kuendelea kuniamini. Na mimi ni moja wapo kati ya wale wachache ambao wanaweza wakaeleza jitihada na mwelekeo mzuri wa Wizara hii kwa kuwahudumia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe na ninakupongeza kwa jitihada zako na uongozi wako mzuri nakutakia kheri katika lile ambalo wenzangu wote wamelisema. Nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wenzangu, Waheshimiwa Wabunge lakini kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, January Makamba kwa malezi yake kwangu mimi kama mdogo wake lakini kwa kutuongoza vyema Wizarani mimi pamoja na wenzangu ambao tunamsaidia kazi nawapongeza pia. Mwisho lakini si kwa umuhimu, nawashukuru waajiri wangu wa Jimbo la Bukoba Mjini kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano nikiendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara imepokea shukurani na pongezi nyingi sana. Hapa mwanzo kabisa nieleze, shukurani hizi na pongezi hizi ni za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi ni wawakilishi, ni wajumbe na ni watenda kazi wake kwa niaba ya Watanzania; na tutaendelea kufanya kazi hii kwa sababu tunaipenda na tunaiweza na tuko tayari kuendelea kulitumikia Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, lakini kama raia na wananchi wa kawaida tu na mimi naomba nitoe shukurani zangu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuamua kwa mara ya kwanza kuruhusu fedha itengwe kwa ajili ya kupeleka Gridi ya Taifa kwa Mkoa wa Kagera kwa kujenga line ya kutoka Benako kwenda Kyaka. Kwa hiyo na sisi watu wa Kagera tunafurahia matunda mazuri na wito wake mzuri kwa kuwahudumia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye hoja mbili ambazo nitamsaidia Mheshimiwa Waziri kujibu na kwa muda nitakaokuwa nao naamini nitafanikiwa. Maeneo hayo ni gharama za kuunganisha umeme lakini pia nitaenda kwenye gharama za umeme vijijini au umeme vijijini kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge takribani wote wamezungumzia kuhusiana na gharama za kuunganisha umeme. Tumewasikia na tunawaelewa na tunatamani jambo hilo litokee kwa sasa, lakini si rahisi na hatuwezi kulifanya kwa haraka sana namna hiyo. Sababu ni kwamba tunahitaji fedha zaidi.
Mheshimiwa Spika, gharama za kuunganisha umeme halisi ni wastani wa shilingi 700,000 kwa wale ambao wapo ndani ya mita 30. Kwa hiyo, pale ambapo tunaunganisha umeme kwa shilingi 320,000 kwa mjini maana yake Serikali ya Awamu ya Sita imeweka ruzuku ya takribani shilingi 380,000 ili iweze kuunganisha umeme. Kwa wenzetu wa vijijini ambao wanaunganisha kwa 27,000 imewekwa takribani ruzuku ya shilingi 670,000 ili waweze kuunganisha umeme.
Mheshimiwa Spika, gharama za sasa zina ruzuku kubwa ya namna hiyo. Sasa, ruzuku maana yake ni fedha ambayo inalipwa na mwingine ili mwingine apate huduma. Kwa hiyo, it’s either ilipwe na mwananchi au ilipwe na TANESCO au ilipwe na Serikali. Tulivyofanya hesabu baada ya mabadiliko ya kurudi kwenye bei ambazo tulikuwa tukizitumia zamani Januari mwaka jana, TANESCO ilibaini ongezeko la shilingi bilioni sita katika makusanyo ya gharama za kuunganisha. Kwa maana hiyo kwa mwezi TANESCO inahitaji bilioni sita ili kuunganisha watu kwa gharama ya shilingi 27,000 kwa mjini na inahitaji takribani bilioni kama saba kuunganishwa wale wa vijijini. Kwa maana nyingine tukitaka kuunganisha Watanzania wote wanaohitaji umeme tunahitaji takribani bilioni 13 ya ruzuku ili kuweza kuunganisha kwa shilingi 27,000.
Mheshimiwa Spika, ukiipiga hii kwa mwaka ni takribani bilioni 156. Sasa jambo hili tunalielewa na tunatamani litokee lakini sasa bilioni 156 inatoka wapi? Tunawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge mturuhusu tuendeelee kuchakata tuone namna ya kujibana hapa na pale ili fedha hii ya ruzuku ipatikane, gharama hizi ziweze kupunguzwa kwa wananchi ili tuweze kupata huduma hiyo vizuri kabisa.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa Mheshimiwa Rais anayonia, na pale ambapo tumekuwa tukikabwa sana amefanya. Alitoa bilioni 100 kuweka ruzuku kwenye mafuta na amekuwa akitoa ruzuku kwenye mbolea na kwenye maeneo mengine. Tunaamini kwa kujibana na kwa kuweka viapumbele mbele hili nalo utalifanikisha. Kwa sasa shughuli ya kubaini maeneo ni yapi kwa uwezo wa wananchi kwa uwezo wa kiuchumi linaendelea, na litakapokamilika tutakuja kuliunganisha pamoja na hili ili sasa tuweze kufikia sehemu ambapo tutaunganisha wananchi wetu kwa gharama nafuu. Ni jambo zuri lenye kuleta kheri lakini linahitaji mjadala mkubwa Serikalini kuweza kubaini sehemu ya kupata fedha hiyo, na mimi naamini kwamba tutalifanikisha.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye jambo la pili la umeme vijijini. Waheshimiwa Wabunge takribani wote waliposimama wamelizungumzia jambo hili, na ni jambo la muhimu kweli na katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya uchaguzi imeelekeza ifikapo 2025 vijiji vyote viwe vina umeme. Sisi hatuna wasiwasi hata kidogo, wala 2025 hatutafika jukumu hili na sharti hili la ilani litakuwa limekamilika. Mwaka huu tutahakikisha kwamba vijiji vyote vinapata umeme. Kwa sasa overall tumefikia asilimia 72 ya Mradi wa REA III Round II. Yapo maeneo ambapo tumefanya vizuri sana. Lot namba 30 ya Simiyu yenye Wilaya ya Maswa na Meatu tumemaliza asilimia 100. Lot namba 18 ya Morogoro vijijini asilimia 100, lot namba 23 ya Pwani wilaya zote asilimia 100. Lot namba 38 ya Tanga, Wilaya ya Kilindi, asilimia 100, lot namba 14 ya Mkoa wa Mara, na wamesema hapa, asilimia 100. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tunakiri kwamba bado kuna sehemu hatujafanya vizuri. Na mpaka sasa baada ya jitihada zilizoanza Januari mwaka huu tumebakiza Lot nne ambazo tunaona hatukaa sawa. Lot namba moja, lot namba 27, lot namba 39 na lot namba 25. Waheshimiwa Wabunge humu wamesema, tunaomba mtuamini, tumeweka mikakati, tuemeweka jitihada na tunakimbizana na wakandarasi hawa, tutafanikisha. Lakini si maneno tu, Waheshimiwa humu wengine wamesema tufungue LC, LC tayari zimefunguliwa na wale ambao wanakidhi vigezo watachukua pesa ili waweze kupata vifaa kwa wakati mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongeza wasimamizi. Waheshimiwa Wabunge wote mnafahamu vijana wameripoti kwenye majimbo yetu kwa ajili ya kuendelea kutoa taarifa za siku hadi siku ili mradi uweze kusimamiwa vizuri. Tumeongeza wahandisi wa REA kwenye level za mikoa, tumeongeza speed kwenye taratibu za malipo, maana malipo yanakwenda REA, yanakwenda TANESCO na yanakwenda Wizara ya Fedha; yalikuwa yanachukua muda. Tume-develop mechanism ambayo itatufikisha kwa haraka mwishoni.
Mheshimiwa Spika, lakini hatujaishia hapo tu, tumeweka mechanism mpya ya miradi mipya inayokuja ili tusiingie kwenye matatizo ambayo tumekutana nayo. Moja wapo ya sharti ni kwamba kama hujafikia asilimia fulani za mradi mwingine hauto qualify kupata mradi mpya, na hii tayari tumeanza kuitekeleza; na katika hili hatutazamani usoni, tunahakikisha kwamba tunalisimamia vyema.
Mheshimiwa Spika, kuna mkandarasi ambaye alitajwa hadharani si vyema tukaliacha hivi hivi. Mkandarasi anayefanya kazi ya Tanga kwenye maeneo kadhaa lakini ana kazi pia Mkoa wa Kahama. Mkandarasi huyu hakufanya vizuri Tanga, anaitwa Tontan. Kwa upande wa Kahama Mheshimiwa Iddi na Mheshimiwa Cherehani wametoa Ushahidi; anajitahidi sana kufanya kazi nzuri kwenye eneo la Kahama.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa Korogwe tuna shughulika naye na hatua zimeshaanza kuchukuliwa liquidated damage tumeshaanza kukata. Kwa hiyo, tunaichukua Lot ya Korogwe kama ameshindwa kufanya kazi tunashughulika naye huko. Lot ya Kahama ambayo anafanya kazi vizuri kwa kujitahidi tunaendelea kumtazama kwa karibu. Lakini ilisemwa kwamba amepata kazi nyingine TANESCO; ni kweli amepata kazi ya kujenga line ya kutoka Ubungo kwenda Ununio, na alipata kazi kabla hatujajua haya mengine. Alikuwa ameonekana atapata kazi nyingine mbili lakini zimesitishwa kwa sababu alionekana atatusumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini aliwahi kufanya kazi nyingine, aliwahi kujenga line ya Dege kuja mpaka Kurasini, aliifanya vizuri. Kwa hiyo, matatizo aliyoyapata sisi hatuyatazami kama ni matatizo ya jumla, tunatazama kwenye mradi husika. Kwenye mradi wa Korogwe tutashughulika naye kisawasawa mpaka tupate haki yetu na yeye apate haki yake. Huko kwingine tutaendelea kuhakikisha kazi inafanyika vizuri. Hii Lot ya kutoka ubungo kwenda Ununio ameshaleta bank guarantee. Akianza kusuasua tunakula kichwa kwa sababu kazi yetu ni kuhakikisha kwamba huduma inawafaikia wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niombe mtupe nafasi tena tuendelee kusimamiana na hawa wenzetu. Umeme vijijini ni siasa kwa kila mtu lakini ni huduma kwa wananchi, na tutahakikisha tunaweza kulifanya hili vizuri. Lakini pia pale ambapo mkandarasi amesua sua leo tusifute na record zake za jana na juzi, huenda ikawa watumishi labda walikuwa wamepitia njia ambazo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, alisema mkandarasi aliyefilisika kwenye Kinyerezi I Extension, mkandarasi huyo huyo alitujengea Mradi wa Kinyerezi I vizuri kabisa na ukakamilika, unafanya kazi mpaka leo. Mkandarasi huyo huyo alitujengea mradi wa Kinyerezi II vizuri kabisa umekamilika mpaka leo unafanya kazi kwa zaidi ya dola milioni 300. Alipoingia kwenye Kinyerezi I Extension yaliyomkuta yalimkuta akapata shida. Isionekana tulikuwa na mkandarasi wa hovyo na ambaye hafai alifanya kazi nyingine lakini huko tupaache Kinyerezi I Extension imekamilika na Mega Watt 135 zimeshaingia mradi unafanya kazi vizuri na umeziba ma-gap ambayo tulikuwa tuna matatizo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, eneo la umeme wa vitongojini nitamuachia Mheshimiwa Waziri aje aliseme kwa upana wake kwa sababu lina kishindo kikubwa. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri tulisema nia ya kuendeleza Wizara ni kuifanya sekta ya nishati kushamirisha shughuli za biashara, uzalishaji na maendeleo ya sekta nyingine zote za kijamii na kiuchumi, ndivyo tunavyoiona Wizara ya Nishati. Na jukumu hilo kama nilivyotangulia kusema kazi hii sisi tunaipenda na tunaiweza. Tunaomba muendelee kutuamini na mtupe nafasi ya kufanya hii kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, waipitishe bajeti hii ambayo kama ilivyosemwa na wenzangu ina component kubwa ya miradi, ina component ndogo sana ya OC na kwa ajili ya mambo mengine. Tukishafanikiwa hili tunaamini baada ya bajeti kupitishwa shughuli itaanza kwa kasi. Ari na moyo tunao na tunaweza kufanya kazi hii kama mnavyotuona na jinsi mlivyotupongeza na kutupa hamasa na shukurani ambazo nimesema zote zielekezwe kwenye mwenye nazo, Mheshimiwa Rais. Tunawashukuru sana, na kwa nyuso navyoziona naamini shughuli ilishakamilika na namuomba Mwenyezi Mungu aibariki iwe hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo ninaomba kuunga mkono hoja na Mwenyezi Mungu awabariki wote, ahsanteni sana. (Makofi)