Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia hoja ya Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Dunia kwa kutujalia uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa kiongozi namba moja kuitangaza nchi yetu ya Tanzania kwenye Filamu ya Royal Tour ambayo imeiweka Tanzania katika ramani ya dunia. Napenda pia nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mary Masanja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza Wakurugenzi wote; Mkurugenzi wa Misitu, Profesa Silayo; Mkurugenzi wa TANAPA, Mheshimiwa Mwakilema, na Katibu Mkuu Mheshimiwa Dkt. Abbasi, lakini nawapongeza pia watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya bila kumsahau Mkurugenzi wa TAWA na watendaji wengine wa Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu utajikita sana kwenye migogoro ya wananchi na wafugaji lakini kwenye mambo ya malikale pia kwenye sheria ambazo zimepitwa na wakati ambazo bado zinatumika. Kwa nianze na migogoro ya wananchi kati ya wananchi na wahifadhi. Migogoro hii ukiiangalia kwa undani imesababishwa na sababu ya Wizara yenyewe kutokuweka mipaka yake. Hivi karibuni ndiyo kumekuwa na uwekaji wa mipaka hiyo. Hifadhi nyingi mipaka yake haijulikani na hili lilisababisha wananchi wengi kwenda kujenga kwenye maeneo ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ushauri wangu kwa Wizara hii ya Maliasili na Utalii ishirikiane na Wizara ya Ardhi iweze kutambua maeneo yake kwa sababu kinachojitokea sasa hivi ambacho Wizara inakuja inasema hapa ni ushoroba wa wanyama, hapa hawa wananchi wamevamia, na vijiji vingine, kwa mfano, tulikwenda kule Kilosa, tulikuta vijiji vya Ng’ombo viko katikati ya hifadhi, lakini kuna zahanati na shule, vitu ambavyo vimewekwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, unakuta kwamba hakuna ule uelewano kati ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Maliasili. Kwa sababu kijiji kinapoanzishwa kinasajiliwa na Serikali inakitambua kama ni Kijiji, inakiwekea shule, lakini kinakuwa ndani ya hifadhi. Hivyo basi, ili twende pamoja na tuache kulaumu kwamba wananchi wanavamia maeneo ya hifadhi, ni bora Wizara ya Maliasili na Utalii ikatambua hifadhi zake iweke mipaka yake kwa kujenga barabara kuzungushia hifadhi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye ushoroba. Utasema kwamba wananchi wamejenga kwenye ushoroba, wananchi hawaanzishi kijiji kwa siku moja. Kijiji hakioti kama uyoga, au mji hauanzi kwa siku moja ukasema kwamba hawa wananchi wamejenga kwenye ushoroba. Kijiji huwa kinaanza kidogo kidogo na miji pia inaanza kidogo kidogo kwa nyumba moja na ya pili: Ni kwa nini wahifadhi au Idara ya Maliasili unapoona kwamba kuna kijiji kinaanzishwa kwenye eneo la maliasili wasiwakataze wale wananchi, waambiwe kwamba hapa ni shoroba? Unangoja mwananchi amejenga nyumba yake ya thamani unakuja kubomoa kwamba hapa ni Shoroba na malipo yake yanakuwa ni kidogo? Kwa hili naomba nisiwaunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa, pia ni ile Kamati ya Mawaziri Nane. Kamati ya Mawaziri Nane ilipita, ikaainisha kwamba yale mamlaka ya kuendelea na ile kazi ibaki kwa Wakuu wa Mikoa. Niwaombe Kamati ya Mawaziri Nane mweze kurudi kwenye mikoa mliyopita mkatatue matatizo ya ardhi yaliyoko. Kuna wengine wanaambiwa mmejenga maeneo yasiyostahili, mmejenga kwenye hifadhi, au mmejenga kwenye vyanzo vya maji. Kwa hiyo, nawaomba, mlipita mkiwa mnaenda maeneo ya mjini, nawaomba mtakaporudi sasa muende site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze tu Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa kwa kwenda Tarime na kwenda Mbarali na nikuombe usiache kufanya hivyo. Usifanye kazi ya kukaka kwenye kompyuta ofisini, fanya kazi ya kwenda site ili uone maeneo yako yakoje? Ukikaa kuangalia kwenye kompyuta pori hili lina ukubwa gani, hii kazi itakuwa ngumu kwako mwanangu. Ni ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa ni kuhusu kutangaza utalii mwingine. Tunaona TV kila siku zikimtangaza tembo, zinatangaza sijui nini, tunaomba pia mtangaze utalii mwingine kama wa fukwe, utalii wa malikale na pia mweze kuangalia vivutio vingine viko wapi? Hasa hapa sasa naomba nizungumzie watu wa malikale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa malikale ni wazembe, hawafatilii malikale zilizopo kwenye mikoa. Katika yetu kuna sehemu nyingi sana ambazo ni vivutio kwa wananchi na ambavyo ambavyo pia vinaweza vikaleta pesa kwa Serikali yetu ya Tanzania, lakini wao malikale wamejikita sehemu moja. Kila mkoa una historia yake, kuna mambo ya machifu na mengine mengi. Unakuta kuna mikoa ambayo ina historia ya biashara ya utumwa, kuna maeneo ambayo wakoloni (labda niseme wageni walivyokuja kwa mara ya kwanza waliingilia pale), kuna wavumbuzi wa kwanza ambao walikwenda maeneo yale. Sehemu kama hizo, hawa watu wa malikale wanatakiwa waifatilie. Tulikwenda pale Arusha…
MBUNGE FULANI: Taarifa.
MWENYEKITI: Mchangiaji, endelea kuchangia.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, amenikoroga kidogo huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Nilikuwa nazungumzia malikale, kwamba malikale wafanye utaratibu wa kuainisha maeneo yao, washilikiane na watu wa TAMISEMI waainishe maeneo yao. Maeneo yao mengi hawana happy, maeneo yao mengi yamevamiwa kwa sababu wameyaacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la malikale limeanza tangu tulivyopata Uhuru wa nchi hii. Lakini malikale wamekuwa mambo yao hayaendi, huoni kwamba kuna msukumo hapa wa malikale lakini nafikiri sijui ni bajeti ndogo au ni kitu. Tungeomba hawa malikale waweze kuongezewa. Kuna vitu vingi kama kule Mkwawa kuna Kinjekitile, kuna mambo ya Machifu wa zamani wanatakiwa kuwa kwenye historia ya nchi hii ili sisi tutakapokwenda watoto wetu wawezi kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Taska Mbogo, ahsante sana kwa mchango wako. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nusu dakika, robo dakika. Ninaomba TANAPA iongezewe bajeti, tulikuwa na hifadhi 16 zikaongezwa hifadhi sasa hivi ziko hifadhi 22, fedha ni kidogo. TAWA pia waongezewe, kwa sababu mapoli yaliongezwa lakini pesa hazikuongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)