Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mhifadhi namba moja, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ana dhamira ya dhati kabisa ya kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inaipatia pato la uhakika nchi yetu; hongera sana kwa Mheshimiwa Rais. Tumeona kabisa kwamba ile Filamu yake ya Royal Tour imesaidia kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia na hivyo kubainisha baadhi ya vivutio ambavyo viko nchini mwetu. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, watendaji wote na taasisi zote za Wizara hii kwa kuandaa hotuba nzuri ambayo imesheheni taarifa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nizungumzie kuhusiana na suala zima la biashara ya uwindaji wa kitalii. Biashara hii ilishamiri sana miaka ya 2008 hadi 2009, kwamba Idara ya Wanyamapori iliweza kupata hadi jumla ya shilingi bilioni 60 kwa mwaka wakati biashara hii ilipokuwa ikifanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa sana, kuanzia mwaka 2013 hadi 2014, biashara hii ya uwindaji wa kitalii ilipungua na hatimaye ilikuwa ikipatikana kama bilioni 20 kwa mwaka, hapa ilisuasua kidogo. Lakini niendelee kuipongeza sana TAWA kwa kazi ambayo imekuwa ikiifanya, kwamba sasa hivi wamejitahidi tena kuweza kuoneza pato kwa biashara ya uwindaji wa kitalii kwa shilingi bilioni 60. Hii ni hatua nzuri lakini bado mimi natamani sana kwa kile kipindi cha mpito tungeweza tukafika hatua kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bahati nzuri nilishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, na kule kulikuwa kuna vitalu ambavyo vilikuwa kwa ajili ya uwindaji wa kitalii; kwa hiyo walikuwa wanakuja wageni wengi sana katika kipindi kile, na hivyo kutuletea pato la Kitaifa. Lakini pia katika yale maeneo yanayozunguka pale walikuwa wanafaidika sana wale wananchi kwa kuweza kuongeza kipato chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika yale maeneo ya kule maporini, unaweza ukashangaa kwa sababu ndege zilikuwa zinakuja, wageni walikuwa wanakuja, watu mbalimbali walikuwa wanakuja kwa ajili ya kuwinda, na hata nakumbuka ilishawahi kutokea Rais wa Panama alishawahi kuja na binti yake kwa ajili ya utalii na delegation kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba niendelee kuishauri Serikali kwamba Wizara ione umuhimu wa kuiongezea bajeti TAWA ili waweze kuweka mipango yao vizuri ili waweze kujitanua zaidi katika kuweza kugawa hivi vitalu vya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa, niendelee kuipongeza TAWA kwa sababu wameweza kutumia mfumo wa kielektroniki katika kusimamia ugawaji wa vitalu vile vya utalii; hii ni hatua kubwa. Kwa hiyo natamani wapatikane wataalamu wengi zaidi waweze kusaidia ukagwaji wa vitalu hivi ili mwisho wa siku tuweze kupata faida kubwa sana. Kwa hiyo naipongeza sana TAWA kwa hatua nzuri ambayo wameifikia. Naamini kwamba kama tutakwenda hivi vizuri basi tunaweza tukapata fedha zaidi ya bilioni 120 na kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine ni kwamba inabidi pia TAWA ibuni njia nyinginezo za mapato, kama vile utalii wa picha. Mfano ile Game Reserve ya Maswa ni nzuri kwa ajili ya utalii wa picha, kwa hiyo kama wataona huu ushauri unafaa basi waweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia hii Taasisi ya TAWA yale maeneo mengine waweze kufanya tathmini ya kina ili shirika liweze kuyatumia maeneo hayo kwa aina nyingine ya utalii badala ya kutegemea utalii wa uwindaji tu. Natambua kwamba kuna baadhi ya mataifa makubwa ambayo yamekuwa yakifanya kampeni hasi dhidi ya uwindaji wa kitalii, lakini hii ni miongoni mwa mbinu moja wapo katika utalii ambayo inaweza kuliletea pato kubwa sana Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumzia ni vivutio vinginevyo. Kuna baadhi ya vivutio ambavyo inabidi viendelezwe. Tumeona kabisa kwamba tumejikita zaidi kwa wanyamapori na mambo mengine kidogo, lakini pia sisi tuna makabila mengi sana hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna makabila zaidi ya 120, tuna mila na desturi zetu; kwa nini pia tusiwekeze kwenye utalii wa makabila ili wale watalii watakapokua wanakuja waweze pia kuona makabila yetu, mila zao na desturi wanafanya nini? Tuna makabila tofauti; tuna Wamasai, tuna Wagogo, tuna Wanyamwezi, tuna Wasukuma, tuna Waha, Wamakonde, Wangoni na makabila mengi. Kama tukiweza kuonesha zile mila zao na desturi, wote hawa mimi naamini kabisa kwamba watalii hawa wataweza kwenda wakitoka kule mbugani wataweza kuona hizi mila na desturi. Labda na sisi tupeleke watu wetu, waende Ethiopia na Afrika Kusini ambako wenzetu kule wameweza kufanikiwa sana kwenye hili suala zima la mila na desturi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri utafiti ufanyike, kwamba kwa nini asilimia 20 ya watalii ambao wanatembelea katika vivutio vyetu hurudi tena kwa mara ya pili. Kwa sababu tunatamani kwamba kama wamefurahia ile hali waliyoikuta katika mbuga zetu lakini pengine kama tukaweka kwenye suala la malikale, lakini pia tukaweka labda kwenye suala la makabila, na mengineyo mengi, watalii hawa watakuwa na hamu kwamba akitoka inawezekana kabisa akakaa zile siku alizoziweka kati ya 10 au 15, kumbe ana sababu ya kwenda maeneo mengi zaidi akaongeza zile siku za kuweza kukaa hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninashauri kwamba basi ufanyike utafiti wa kina kujua, je, ni vivutio vipi ambavyo vitaweza kuwasaidia hawa watalii waweze kurudi tena, isiwe mara moja tu, iwe mara mbili, mara tatu, mara nne, hata mara kumi? Na ikiwezekana waende wakawaambie wenzao ili waweze kufika na kuweza kufanya huo utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda si rafiki sana, mimi naomba nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa, naunga mkono hoja na ninaamini kabisa kwa jinsi hali ilivyo Tanzania itaweza kufikia zaidi ya watalii milioni tano, hata milioni 10 au milioni 15 kama katika nchi nyingine zozote duniani ambazo zimeweza kufaidika na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa fursa. (Makofi)