Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba kuchukua kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili kuwa mchangiaji katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kama ilivyo ada na mimi naomba niungane na Wabunge wenzangu kushukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba Wizara yetu hii ya Maliasili na Utalii inachangia kwa kiwango kikubwa mapato na uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshiumiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri ameeleza kwa kina kwamba Wizara hii inachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 21 la Pato la Taifa. Hili jambo ni hongera sana kazeni buti ili mapato haya ya Serikali na Pato la Taifa liweze kuongezeka mara dufu katika mwaka ujao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tunaimani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri, kwa kipindi kifupi ambacho cha miezi mitatu na siku 22 leo juzi ilikuwa siku 19 leo siku 22, kuna mambo mengi umeyafanya ambayo yanaoesha kabisa kwamba umekuja serious kufanya kazi. Ndugu yangu hapa jirani yangu Mheshimiwa Waitara amekubali anasema huyu Mheshimiwa ana kitu ndani yake na mimi nakubali kwamba una kitu ndani yako Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza ili uweze kutumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii, ambao mimi najua hawa kwa njia moja au nyingine wameshiriki kikamilifu katika uandaaji wa bajeti hii. Kabla sijaanza kutoa mchango wangu naomba pia nimpongeze sana, sana Mtendaji Mkuu wa TAWA Kanda ya Kusini. Kwa kweli Mtendaji yule anafanyakazi nzuri sana masaa 24 Mheshimiwa Waziri Mtendaji wako yuko kazini. Mimi nilipata majanga makubwa sana ya tembo nilimpigia simu Mtendaji yule alitoa gari yake na Askari wakaja katika eneo la tukio, nampongeza sana Mtendaji yule kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nimuombe sana ndugu yangu Waziri, kuna changamoto zipo nyingi ndani ya Wizara yako, nami naomba nizieleze zile changamoto ambazo ziko ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu. Changamoto ya kwanza Mheshimiwa Waziri, ndani ya Jimbo langu kwa mwaka huu tumepata ongezeko kubwa la maafa linalosababishwa na wanyama waharibu hasa tembo. Hili ni jambo la kushangaza haijawahi kutokea ndani ya Jimbo langu watu zaidi ya 200 wamepata mashambulizi na tembo, tembo wameharibu mashamba ya watu, hili jambo kwa kweli linauzunisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kwenye Kata ya Sengenya Mheshimiwa Waziri, vijiji vya Mkumbaru, vitongoji vya Naivanga, Narunyu vimeharibiwa zaidi mashamba 73 ya wananchi yameharibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata ya Sengenya pia Kijiji cha Kinyanyila mashamba ya wananchi yameharibika, kwenye Kata ya Sengenya hiyo hiyo KItongoji cha Igunga zaidi ya wananchi 92 mashamba yao yameshambuliwa na tembo. Katika Kata ya Nangomba Kijiji cha Kiuve mashamba zaidi ya 50 ya wananchi yameshambuliwa na Kata ya Kilimanihewa Kata ya Mjini kabisa tuna Kijiji cha Mnonia mashamba ya wananchi yameshambuliwa. Sasa ninachoomba niliwahi kuchangia hapa na nikasema zaidi ya wananchi 200 wameshambuliwa, nina imani Mheshimiwa Waziri majina haya yako ofisini kwako, rai yangu wananchi hawa mashamba ndiyo ajira yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana kuchukua mwaka mzima wananchi kulipwa fidia au kifuta jasho, ni matarajio yangu Mheshimiwa Waziri utachukua kipindi kifupi wananchi hawa waweze kupewa hicho kifuta jasho.
Mheshimiwa Waziri, katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umenifurahisha sana, umekiri kwamba kifuta jasho kinachotolewa ni kidogo na uko tayari kukifanyia marekebisho. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, Mwenyezi Mungu akupe nguvu kabla ya Bunge hili hatujamaliza muda wake huu mwezi wa Saba ulete hayo mabadiliko ili wananchi waweze kupata nafuu ya vifuta jasho ambavyo vinasababishwa na hawa tembo. Jambo hili kwa kweli linaudhunisha sana Mheshimiwa Waziri na wananchi watakuombea mema sana endapo utafanya marekebisho haya ya haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa pia nikuombie ni mgogoro mkubwa uliopo juu ya sekta. Hawa Mawaziri wa kisekta Nane ambao walizunguka Tanzania nzima kutatua changamoto za migogoro. Niliwahi kuzungumza hapa ndani ya Bunge lako, ndani ya Kata ya Mkonona kuna vitongoji vya Chawanika, Kitongoji cha Nambunda na Kitongoji Namaromba, vile vitongoji vimeamuliwa wale wananchi watoke. Mheshimiwa Waziri wananchi hawana tatizo na hilo na tumekubaliana watoke. Changamoto iliyopo wanatokaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza ni Mwezi wa Sita wale wananchi ndiyo kipindi cha kuandaa mashamba. Mpaka sasa hivi hawajui watatoka wapi, watatokaje pale na watakwenda wapi? Kwa kuwa tathmini imeshafanyika na maeneo ya kwenda yameshajulikana, walipeni fidia Mheshimiwa Waziri waende huko walikopangiwa, vinginevyo wasipolipwa fidia mwaka huu, mwezi huu au mwezi unaokuja maana yake wale wananchi tunazidi kuwatia umaskini zaidi. Watakwenda wapi kama mpaka sasa hivi hawajui hatma yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wale wananchi pale walipo kulikuwa na shule wameondolewa, shule kule wanakokwenda haijajengwa. Kulikuwa na huduma za maji wale wananchi wangu walikuwa wanatoa maji Mto Ruvuma, walikuwa wanaenda kwa mguu tu kuchota maji, leo wamepelekwa mbali na Mto Ruvuma, kule wanakokwenda wanapataje huduma ya maji? Kule wanakokwenda wanapataje huduma ya afya? Mambo haya yote yangeangaliwa. Sasa mimi ninaomba Mheshimiwa Waziri nina imani na wewe, tufanye haraka iwezekanavyo wananchi hawa waweze kwenda walikopangiwa na hizi huduma muhimu zipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni changamoto ya mabucha. Mheshimiwa Waziri Wizara yako ilihamasisha wananchi wale ambao wamezungukwa na hifadhi na mbuga waanzishe mabucha ili kupunguza ujangili na wananchi wetu waweze kupata kitoweo kwa halali. Inahuizunisha wananchi wale mfano mimi kwangu pale, kuna vijana walijiunga Sahachi Company, Sahachi Group walijiunga wakatengeneza bucha, leo ni mwaka wa pili hawajapata kitoweo hata kimoja cha kuuza. Waliuza mara moja tu tena kwa bahati. Sasa Mheshimiwa Waziri, naomba maamuzi yaliyofanywa na Wizara yalikuwa ya busara kabisa ili kupunguza ujangili tuanzishe mabucha ili wananchi wapate kitoweo na wao wawe walinzi wa yale maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mpaka sasa hivi hakuna utaratibu mzuri uliopangwa wa kuwawezesha wananchi hawa kupata kitoweo, kwa kweli tunawahangaisha sana. Nina kesi pale kwangu ndugu yangu kuna bwana amehukumiwa miaka mitatu au kulipa faini 500,000 kwa kukutwa na nyama ya nguruwe pori jikoni, amekamatwa jikoni nyama inapikwa nguruwe pori amepigwa miaka mitatu au miezi mitano jela, amekaa jela mpaka ndani ya wiki moja ndugu kuchanga changa wameuza shamba ndiyo kwenda kumtoa. Hii kwa kweli ni unyanyasaji haiwezekani! Hawa Askari wako wanachokifanya siyo sawa, kamateni majangili siyo mtu anayepika, unakwendaje mpaka jikoni? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi nakuomba hiyo 500,000 nikitoka hapa unirejeshee ili nimpelekee yule mtoto.
MBUNGE FULANI: Kabisa. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo sawa, siyo sawa hata kidogo na kwa kweli tunawavunja nguvu sana wananchi wetu. Kama wananchi wetu wanalinda maliasili, leo anakutwa na nguruwe pori, mimi kwa kweli jambo hili limenihuzunisha sana, limenihuzunisha sana Mheshimiwa, na ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili uwakemee sana watu wako. Wanavyofanya siyo sawa na hiyo shilingi 500,000 naiomba ili nimrudishie yule kijana. Wameuza shamba la mikorosho ambalo wamelihudumia kwa miaka 50 lile shamba wameliuza wale wametiwa umaskini, walikuwa na shamba lao sasa wanaingoja TASAF. Maisha gani haya tunawapelekea wananchi wetu? Kwa hiyo hili nakuomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilikuwa naomba sana na mimi nichangie katika masuala mazima ya utalii ni kukupongeza sana katika hotuba yako, umeongea mambo mazuri sana jinsi ya kuboresha na kuongeza utalii na mimi naomba nichangie kidogo. Naomba tutumie Balozi zetu kikamilifu ili ziweze kuchochea utalili wetu. Kule Balozini peleka Maafisa hata Watano kutoka Wizarani kwako, wakawe waambata wa utalii ndani ya Balozi zetu, tusiwategemee Maafisa wa Ubalozi wafanye shughuli ambayo hawana taaluma nayo, peleka Maafisa kule ili wakasimamie shughuli hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo najua muda siyo rafiki nitachangia kimaandishi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)