Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi. Kwanza mimi natoa pongezi sana kwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wote. Kusema kweli tunachotaka sasa ni Serikali kuipa fedha zote Wizara hii ili ikatekeleze mipango kama ilivyo kwenye bajeti yao. Mimi katika mkoa wangu wa Rukwa hasa Wilaya ya Nkasi nimeshukuru sana, miaka sita barabara yetu toka Sumbawanga - Mpanda ilikuwa haijakamilika kwa bajeti hii naona barabara Disemba itakuwa lami tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilikuwa napiga kelele sana kuhusu shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kwenda kukamilisha Bandari ya Kipili. Leo naona kwenye bajeti kuna pesa ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza barabara mpaka Bandari ya Kipili. Naipongeza sana Serikali na Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe masikitiko yangu makubwa, alipokuwa hapa ndani, leo ni Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi, aliniahidi barabara ya kutoka Kirando - Kazovu - Korongwe na shahidi ni Alhaji Iyombe alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na alikubali kunisaidia. Wakati wa kampeni zake tena alipokuwa Namanyere aliniahidi hii barabara atanisaidia. Vilevile aliahidi kwamba Namanyere Mjini atanipa pesa za kilometa tatu za barabara ya lami, lakini sikuona humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni kuhusu usafiri Lake Tanganyika. Awamu ya Nne tuliahidiwa meli mbili, Awamu ya Tano hakuna cha meli, ni utengenezaji wa Liemba kwa shilingi bilioni 5.6. Ndugu zangu, tuliahidiwa meli moja leo hamna meli ni matengenezo, tuna meli kule MV Mwongozo haitajwi kabisa, ilikuwa pacha pamoja na ile iliyozama kule Bukoba, zilitengenezwa siku moja…
MBUNGE FULANI: MV Bukoba.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Ndiyo MV Bukoba, lakini sisi ile meli tunayo mpaka sasa, haina matengenezo haina chochote imekaa pale Kigoma kazi yake kukodishwa na wafanyabiashara kidogo kidogo haijulikani inafanya kazi gani. Tunaomba Serikali kama haina pesa za kutosha ya kununua meli mpya iifanyie ukarabati wa hali ya juu MV Mwongozo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kibaya zaidi ni kuhusu wafanyakazi wa Liemba, hii Marine Service inatesa watumishi. Mpaka leo mshahara wa mwezi wa nne wafanyakazi wa Liemba hawajapata, hawana bima ya afya, hawana hela ya likizo hata waliostaafu hawajalipwa mafao yao mpaka leo. Hata meli ya mtu binafsi ungesikia kelele, hii siyo meli siyo chochote na wakati wowote inaweza kutokea ajali maana hata engine zake zinazimika mara kwa mara ndani ya Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru sana Serikali, nilipiga kelele tokea bajeti ya kwanza kuhusu Bandari ndogo ya Kabwe lakini kwenye bajeti hii nimeona kwamba itaanza kutengenezwa mwezi Julai. Naomba Mheshimiwa Waziri hicho kipindi cha mwezi Julai itakuwa Bunge hapa hakuna na mimi nitakuwa Kabwe, nataka nihakikishe huo mwezi Julai bandari ya Kabwe imeanza kutengenezwa kama ulivyoahidi kwenye bajeti yako. Maana bajeti ya mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi bilioni moja kwenye bajeti kwa ajili ya Bandari ndogo ya Kabwe lakini sikuona chochote mnasema tu vifaa vimeshawasili Dar es Salaam. Mmesema bandari ya Kabwe na Lagosa zitaanza kujengwa mwezi Julai na kipindi hicho Mheshimiwa Waziri tutakuwa huko, nitakuwa kwenye jimbo langu nihakikishe bandari ya Kabwe imeanza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Serikali ni yetu wote, kuna mikoa hapa inapendelewa siyo uongo na ni mikoa ambayo iko mbele ukienda utafikiri uko Durban au uko Johannesburg na sisi wengine hata barabara za vumbi hatuna. Kuna watu wanadai viwanja vya ndege, kuna watu wanadai barabara za lami, sisi tunataka barabara za vumbi. Katika hayo maombi 3,000 watu walioomba kuhamisha barabara kutoka halmashauri kwenda TANROADS, lazima tufikirie mikoa mingapi ina lami, mingapi ina barabara za TANROADS ili tuinue mikoa ambayo iko nyuma kabisa. Kuna mikoa mingine iko kama peponi, leo unakuja kusema hapa maneno ya ajabu ajabu sijui kisungura na kadhalika, tuangalie mikoa hii.
Ndugu zangu, nchi hii tumetembea kila kona, labda ninyi hamjakwenda mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma mkaangalia jinsi tulivyokuwa nyuma katika suala la barabara…
MBUNGE FULANI: Na Simiyu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Nendeni Simiyu, ninyi mnataka mpaka lami ziwafikie kwenye majumba yenu binafsi, hilo Mheshimiwa Waziri hatutalikubali. Ni lazima tuangalie upya mkoa upi una kilometa nyingi za lami, una kilometa nyingi za TANROADS ili na sisi mikoa mingine bajeti iende kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wilaya nyingine zina lami mpaka kwenye mitaa, miji yao ina lami makao makuu ya Wilaya…
MBUNGE FULANI: Sema.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Lakini Wilaya nyingine hazina lami hata kilometa moja. Ni kweli, mwenzangu ametoka kuzungumzia hapa, utashangaa, unabandua lami unabandika lami wakati zina mashimo, sisi wengine za vumbi hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa, toka Kirando kwenda Kazovu kuna vijiji zaidi ya sita mpaka Korongwe, tangu uhuru hawajaona hata bajaji. Wananchi wanapata taabu, Ziwa Tanganyika likichafuka mitumbwi inazama, akina mama wanakufa hawana njia nyingine ya usafiri ni kwa mguu au kwa mitumbwi, Lake Tanganyika wimbi lake ni la ajabu utashangaa mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri aachane na wanaoomba viwanja vya ndege ndugu zangu hata abiria hakuna, wanapanda Wabunge, nilizungumze hapa, wanapanda Wabunge baada ya Ubunge kuisha hata tiketi hawakati, leo wanaomba viwanja vya ndege kila Wilaya atapanda nani. Akina mama na bibi zetu wanapanda magari, wanapanda treni, leo mnakwenda kuchukua mabilioni ya hela, tuchukue mfano kidogo wa uwanja wa ndege wa Mpanda nani anautumia? Tuseme ukweli nani anautumia uwanja wa ndege ya Mpanda, kuna ndege ya abiria inayokwenda Mpanda? Nimekwenda Tabora na ndege hakuna abiria anayepanda wala anayeshuka, Tabora hapo ndiyo mji mkubwa, leo unaomba kiwanja wakati abiria hakuna. Watu wa Tabora wanataka reli, watu wa Mpanda wanataka reli siyo viwanja vya ndege. Tusiwe tunadanganyana hapa, tugawane sawa hiyo keki. Mnabandua lami, mnabandika lami wengine hawajaona hata lami, ndugu zangu tunakwenda wapi, tuoneane huruma. Wengine nchi hii mpaka leo wanatembea kwa mguu hawana barabara, wewe unaomba kiwanja cha ndege, ndugu zangu, huoni hata aibu! Unakuja kuzungumza uwanja wa ndege mbele ya Bunge, mbele ya nchi hii wakati wenzako hawana barabara!
TAARIFA...
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi ninaosema reli ndiyo itakayotuletea uchumi, siyo ndege. Hayo makontena ya vifaa vya viwanda itapakia ndege? Wewe mwenyewe umelalamika ndege wanatoza shilingi 200,000 sanduku, ndege gani si unadanganya Bunge hapa, hakuna kitu kama hicho. FastJet bei yake ni rahisi kuliko ndege zote hapa leo unataka kuwapakazia FastJet begi shilingi 400,000 begi gani hilo jeneza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bandari, bandari yetu inatuletea msongamano mkubwa Dar es Salaam inatumiwa na nchi nyingi. Tuliomba bandari ya nchi kavu na kuokoa msongamano, reli ichukue mizigo mpaka Kibaha kule mbali au Chalinze ili magari yote ya kutoka nchi jirani yabebe mzigo kwenda nje. (Makofi)
Kwa kufanya hivyo, tutaondoa msongamano katika Jiji letu la Dar es Salaam. Hizi flyovers mnazoweka, sijui mnapanda mabasi yaendayo kasi haitasaidia kama bado mizigo inakwenda kuchukuliwa bandarini na magari makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mafuta lazima kuwe na mpango ili bomba la mafuta liende mbali kidogo na Dar es Salaam ili magari yote yakachukulie huko mafuta kwenda nchi za nje. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Sawa sawa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Bila kufanya hivyo msongamano utaendelea kuwa pale, magari kutoka bandari kupitia Mandela road ni foleni ya ajabu, saa tatu mpaka nne ni foleni, ndugu zangu tunapoteza muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri fanya kazi yako, wewe ni Waziri mzuri unafanya kazi, usitishwe na mtu yeyote, endelea kusaidia sehemu ambazo hazina barabara, hazina mawasiliano, lakini kusema mimi nataka uwanja wa ndege achana na viwanja vya ndege, achana kabisa havina maendeleo kwa nchi yetu bado changa vilivyopo vinatosha. Tuendelee na viwanja vya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Kigoma pembezoni kule vinatosha lakini vingine vya katikati ndugu zangu ni kupoteza wakati hakuna abiria, nimefanya utafiti hakuna abiria. Sisi wa kule Sumbawanga kiwanja cha Mbeya kinatosha sana, tusidanganye. Tunakwenda na ndege FastJet asubuhi abiria hawajahi, leo unataka kiwanja kijengwe Sumbawanga, Mpanda, Mbozi, Kibaha, ndugu zangu hela zitatoka wapi? Tuendelee kujenga barabara na reli ili nchi yetu itoke katika uchumi huu uende uchumi wa mbele, tusidanganyane! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani unakuwa Mbunge hapa unasema Morogoro wanataka kiwanja cha ndege, Tabora uwanja wa ndege, dai gauge Tabora reli itakusaidia.
Tarime uwanja wa ndege, utapanda wewe peke yako Mbunge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri ahadi ya Rais alipokuwa Waziri aliniahidi hapa akatuma na wataalam kwenda kukagua barabara kilometa 35 tu, aliniahidi atanisaidia alipokuwa Waziri na alipokuwa Rais, nakuomba itekelezwe. Shahidi ni Mheshimiwa Mzee Lukuvi alikuwa anaambatana naye na yuko humu aliahidi kujenga hiyo barabara. Kwa hiyo, naomba hiyo barabara tafuta hela popote ikatengenezwe kusaidia watu wa Kazovu na Korongwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ujumbe wangu umefika.