Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nami nijielekeze kwenye kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Nampongeza kwa sababu ameanza vizuri, ameanza kwa usikivu, ameanza kwa kujishusha kwenda kuwatumia Watanzania kwa kuwasikiliza. Mheshimiwa Mchengerwa hongera sana. Endelea kuwa humble katika kuwatumikia Watanzania hawa, endelea kuwa humble katika kumsaidia Mheshimiwa Rais kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nizungumzie hali yetu kule Mkinga. Tuna changamoto kubwa sana ya uvamizi wa tembo kwenye Wilaya yetu ya Mkinga. Wilaya ya Mkinga ina Kata 22, hivi ninavyozungumza Kata 13 tembo wanavuruga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni maeneo yaliyokuwa yanashambuliwa sana ni Daluni, Bwiti, Duga, Gombero na Mwakijembe. Haya ndiyo yalikuwa maeneo yaliyokuwa yanashambuliwa kwa kiasi kikubwa, lakini leo hii tunapozungumza Kata nyingine Barongo Kasera, Mtimbwani, Doda, Moa, Mapatano, Duga Sigaya, nasikia Maramba wamepita na vilevile Mnyenzani wamepita, hali ni mbaya sana. Hali ni mbaya kwa sababu wananchi wanapoteza…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Kuna Taarifa Mheshimiwa Kitandula.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba anavyozungumza tembo hali mbaya, kwenye Jimbo la Bunda karibu Kata zote tembo wako barabarani saa hizi, wako makundi 40, 20, 30, Kata zote toka usiku mpaka leo saa hizi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dunstan Kitandula.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge taarifa ni moja.

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda huu ni mdogo. Waheshimiwa Wabunge waache wenzao watumie muda waliouomba kuchangia. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, kuna taarifa nyingine hapa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, taarifa inakuwa ni moja. Hajaanza hata kusema taarifa inatoka wapi? Muache aseme kwanza. Mheshimiwa Kitandula naomba uendelee. (Makofi)

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, daah, mambo mengine yanaudhi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkinga wanataabika, tumeleta maombi baada ya mazao yao kuharibiwa ili waweze kupata fidia, huu ni mwaka wa tatu hakuna kifuta jasho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Kamati ya Siasa ilikuwa inafanya ziara feedback waliyoipata kutoka kwa wananchi, wananchi wamekata tamaa. Wananchi wanasema Serikali inathamini tembo kuliko wananchi, hili si jambo zuri kwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi. Twendeni tukawasaidie wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni, mazao yaliyokuwa yanaathirika ni mahindi na mikorosho, lakini sasa hali imekuwa mbaya kwenye zao la mkonge. Tembo sasa mkonge ndiyo imekuwa, sijui nisemeje, wanavuruga kwelikweli. Chama cha Wakulima wa Mkonge kule Mkinga kimeleta malalamiko haya nimeyafikisha, hali ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Kaka yangu Ngenya tukiwa kwenye bajeti hapa akawa ananitania ananiambia Mheshimiwa Mbunge, naendelea kuwa maskini. Mwaka huu nilikuwa nategemea nianze kuvuna mkonge, tembo wamemaliza shamba zima. Hali, Mheshimiwa Mchengerwa, ni mbaya!

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri, nilikuja kumueleza mwanzoni mwa mwezi Mei, baada ya siku mbili akaongeza kikosi pale Mkinga. Mheshimiwa Naibu Waziri, tunakushukuru sana, kikosi kile kilienda tarehe 19. Lakini kwa ukubwa wa tatizo hili kikosi kile hakitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tulikuwa tunazungumza asubuhi, tembo wamevamia Mavovo, wamekula mahindi ya wananchi, Kikosi kile kimeitwa kiende Muheza kwenda kufukuza simba, kwa hiyo kule shughuli inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nakuomba tukimaliza Bunge hili hebu tuende Mkinga ukaone hali. Hali ni mbaya. Mlituahidi kwamba mtakuja kufundisha vijana kumi kwenye kila kijiji, mtawapatia vifaa ili watusaidie tuwe na usimamizi wa karibu, jambo lile halijafanyika, tunaomba fanyeni jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikosi hiki kilichowekwa ni cha muda, tunahitaji kuwa na kikosi pale cha kudumu kwa sababu tatizo ni kubwa. Tunapata tembo kutoka Tsavo - Kenya, tunapata tembo kutoka Mbuga ya Mkomazi. Njooni mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni changamoto ambayo imeletwa na hili tunalolifanya la kutatua migogoro, hatujalifanya vizuri kule Mkinga. Kata ya Mwakijembe kuna kilio, ushirikishaji haukuwa mzuri. Tarehe 30, ilikuja timu kule kwenda kufanya tathmini, timu ile haikushirikisha hata wenyeviti wa vijiji, tunawezaje kufanya mambo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wale wanapita wanawaambia wananchi ukifika mwezi Julai mnaondoka. Tunazalisha taharuki bila sababu ya msingi, tunachukua maeneo yao hatuwaambii fidia tunayowapa ni ipi! Mheshimiwa Mchengerwa, nakuomba hebu tuende Mkinga tukaondoe changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya kazi nzuri sana mwaka 2017, tuliwashirikisha wananchi tukapata muafaka wa Kimkoa na Kitaifa, tukasubiri jambo lile sasa tuende tukalifanyie kazi. Kikosi kazi mlichotuma kimekwenda kutupa yale yote tuliyokuwa tumekubaliana, kimekuja na maamuzi yao tofauti ambayo hawakushirikisha wananchi, hatuwezi kufanya hivi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji kule wanazuiwa, hata sasa wanaambiwa hawatapeleka mifugo yao kwenda kunywa maji kwenye Mto Umba, mto ambao unatiririka kwenda Kenya, wenzetu wananufaika, sisi tunazuia watu wetu. Tunawezaje kufanya mambo haya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ile ya kwanza ilipokuja ilijiridhisha kwamba eneo lile hakuna uwezekano hata wa kuchimba kisima. Kwa hiyo, eneo pekee ni kwenda kunywa maji kwenye Mto Umba. Leo tunawaambia wafugaji wale kwanza tunachukua maeneo yao, hatuwaambii fidia tutakayowapa ni ipi, halafu tunawazuia wasiende kunywesha maji kwenye maeneo yale. This is…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)