Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi kubwa ya Royal Tour na kwa Jimbo langu imeleta mafanikio makubwa sana. Mheshimiwa Waziri ni shahidi mwezi uliopita alikuwepo katika Jimbo langu akiwa na Makamu wa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Karatu limezungukwa na hifadhi mbili, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Lake Manyara National Park, pia Jimbo langu lina Kata 14, Kata Tisa zimezungukwa na hifadhi lakini vilevile vijiji 29 vimezungukwa na hifadhi katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wameongea changamoto kubwa ya tembo lakini niseme kwamba siku ya Ijumaa tulipoteza mwananchi mmoja katika Kata ya Oldean na leo hii siku ya Jumatatu wanampumzisha. Niseme ni kilio kikubwa kwa Jimbo langu la Karatu pia najiuliza watu hawa wa hifadhi ng’ombe wakiingia kwenye hifadhi wanakuwa makini kweli na sasa hivi ng’ombe mmoja anapigwa faini ya shilingi 100,000 lakini sasa hivi suala la faini ya 100,000 wameacha sasa hivi wamekwenda mbele zaidi wanataifisha mali za wafugaji wetu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo wakiingia kwenye shamba la mkulima hana bei. Ndiyo Mheshimiwa mchangiaji aliyetangulia amesema kwamba kwa hekari moja unafidiwa kwa shilingi 25,000 wakati huo mita 500 hawawezi kuchangia chochote. Mimi pia najiuliza Mamlaka ya Hifadhi za Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 wakati huo wananchi walikuwepo na ikaweka fire-line katika eneo hilo, ikawekwa mpaka wa Hifadhi ya Ngorongoro na ikawekwa fireline kwenye mpaka upande wa wananchi. Leo wameweka kwenye kanuni zao mita 500 hamna kumchangia hata hiyo 25,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa kama ilivyoelezwa mita 500 mpaka 1000 kama ilivyoelezwa lakini kuanzia kilometa Nne mpaka tano shilingi 75,000. Lakini kilometa Nne mpaka Tano ni shilingi 100,000. Pia, ukiwa na zaidi ya hekari tano hawakupi fidia hata zikiharibiwa hekari 50, wao wanachojua ni hekari tano tu. Huu ni uonevu kwa wananchi wetu na wametuonea kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia najiuliza hao waliopitisha shilingi 25,000 kwa heka Wizarani au TAWA hivi kweli wameangalia na hao ni wakulima kweli? Hivi mwananchi unamsaidia kwa 25,000 kwa hekari? Hata kwa kilimo tu cha trekta haitoshi wakati huo mwananchi amegharamika mpaka anakaribia kuvuna tembo nakwenda kuharibu. Kwa nini tusitunge sheria tembo hawa ni mali ya Serikali na kuna watu wameajiriwa kwa ajili ya kuchunga. Kama tembo hawa wanatoka misituni wanaingia kwenye mali za wananchi siyo kwamba wale wanaowachunga msituni wamezembea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo mpaka wanafika kwenye mali za wananchi kama ng’ombe wetu wanaingia misituni wanakuwa makini kutu–charge shilingi laki moja kila ng’ombe, hao ng’ombe wao wanaotoka misituni wanakuja kwenye mali yetu sisi wananchi halafu wanatupangia na fidia wanatoa wanavyotaka na wanayoona wao inafaa. Pia, inaweza kuchukua hata miaka mitatu mwananchi anaendelea kudai hata hiyo 25,000 anaweza kudai miaka mitatu. Hii siyo sawa. Tukuombe Mheshimiwa Waziri, uangalie kwa upya, kwa sisi tuliozunguka na hizi mbunga tumeumia kweli kwa muda mrefu na wananchi wetu wanaendelea kuteseka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme katika Jimbo langu kuna changamoto kubwa hasa katika kata tatu; Kata ya Oldean, Kata ya Daa na Kata ya Ganako. Wananchi wale wamekuwa maskini kabisa katika muda mrefu kabisa kwa miaka yote ambao wanapakana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro. Mimi sisemi kwanini tumezungukwa na hizi hifadhi, lakini tunachoomba kwa Wizara waweze kuona ni namna ipi ili waweze kuwadhibiti wanyama hawa ambao wanaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa mfano Wilaya kama hii ambayo ina vijiji 29, ina kata tisa imezungukwa na hifadhi, hamna hata gari moja la kufanya doria, Wilaya nzima hamna hata gari moja la kufanya doria. Wale watumishi wamekaa pale hawana hata kazi yoyote, kwa sababu kazi yao kubwa ilikuwa wawasaidie wananchi wetu kuzunguka lakini hawana gari, wamekaa tu ofisini wanapiga mshahara wa bure kabisa hamna kazi na wanaendelea kuwepo katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, katika Jimbo langu nina changamoto na nilikueleza siku ile ulikuwepo na Makamu wa Rais. Katika eneo la Kata ya Buger kulikuwa na changamoto kubwa na bahati nzuri nilipata bahati ya kwenda na Naibu Waziri, wanachobishainia pale wananchi na watu wa uhifadhi ikizidi sana kwa upana ni hatua 30 na maeneo mengine ni hatua 10. Hata hivyo, imekuwa ni mgogoro wa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 TANAPA waliweka alama, 2014 wakaboresha, mwaka 2018 wakaingia kwa wananchi zaidi kama ninavyoeleza hatua 30 maeneo mengine hatua 14 lakini ikizidi sana upana huo ni hatua 30. Nilienda na Mheshimiwa Naibu Waziri lilipopata bahati ya kutembelewa, badala ya kupungua kwa ule mgogoro alichokifanya Naibu Waziri, ni kwenda kuongeza ule mgogoro na aliendelea kutoa matamko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa Viongozi au Mawaziri tusiwe Mawaziri wa matamko, tujaribu kusikiliza wananchi wetu. Shida yetu kubwa ni kwamba tunawasikiliza viongozi wale ambao tunawakuta kwenye eneo lile na ambao wako upande wa Serikali. Tunashindwa kutoa fursa kama Kiongozi kuwasikiliza wananchi. Sasa kama Kiongozi wa Serikali upime sasa lile unaloambiwa na mwenzako kule chini linaendana na hali ya wananchi wa eneo husika? Mimi sioni sababu ya wananchi kuendelea kugombana na Serikali yao kwa hatua 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru uliahidi kwamba mwezi huu wa Saba unaweza kwenda kutembelea eneo lile la Buger na mimi nikukaribishe. Sioni sababu ukagawanya Kata, kaya baadhi za wananchi lakini inakata mashamba ya watu na Mheshimiwa Naibu Waziri alisema tutatoa fidia. Wananchi wale wamenituma sisi hatuna shida na fedha bali sisi tuna shida na ardhi yetu ambayo tumekaa nayo toka enzi za mababu. Hatuko tayari kuchukua fidia, kama ni mali yenu kwa nini mnatufidia sisi? Huwezi kutufidia, kama ni mali yako chukua, kama ni mali yetu usitufidie! Sisi hatuhitaji na wananchi wale wamenituma kwamba sisi fidia hatuhitaji, tunachohitaji ni ardhi yetu na siyo eneo kubwa ni eneo dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Serikali mwaka 2011 wanakuja kuweka beacon, wametumia fedha za umma, wanakuja kuweka 2014, wanakuja kuweka 2018 watu hao hao! Unajiuliza, wale waliofanya 2011 ni Serikali kutoka wapi, na hawa 2018 ni kutoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba pia ninakukaribisha katika Jimbo la Karatu, tutakwenda kwenye ile Kata, wananchi wale hawana shida, sisi tunaelewa kwa sababu tumekaa na hawa wanyama muda mrefu, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeanzishwa mwaka 1959 sisi tunakaa nao? Pia, wananchi wale hawana shida na uhifadhi ni katika eneo lile linaloonekana wananchi wetu wananyang’anywa mali yao kwa nguvu kabisa. Kwa sababu 2011 waliweka beacon, 2014 waliweka beacon na 2018 wakasogeza wakaingia kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru kwa nafasi lakini ninamuomba Mheshimiwa Waziri mwezi wa Saba karibu kwenye Jimbo langu tuweze kushusha ile pressure. Siku ile ulipotoa kauli katika eneo la Karatu wale pressure ilishuka. Nami ninaamini kwa jinsi ulivyofanya kule Tarime naamini kwamba kwa Karatu utaweza kuja kufanya vizuri, ninakushukuru na ninakukaribisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)