Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Naomba nianze kwa kumshukuru Mungu, hatimaye nitumie fursa hii kuwapongeza Wizara hii ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Balozi Pindi Chana pamoja na Naibu Waziri wake, Hamis Mohamed Mwinjuma, Mwana FA, bila kumsahau Katibu Mkuu wa Wizara hii na watendaji wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, nataka nimrejee Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mwasisi wa Taifa letu la Tanzania, alisema kwamba “Nchi isiyokuwa na utamaduni wake ni sawa na Taifa lililolokufa, yaani Taifa mfu”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana ya kuyarejea haya maneno na hapo kabla sijaipongeza Timu ya Yanga. Naipongeza Timu ya Yanga kwa hatua waliyofikia pamoja na kwamba mimi sio Yanga. Mimi naipenda Timu ya Simba lakini ninaposimama kwenye jukwaa hili au kwenye Bunge lako Tukufu, nasimama nikiamini kwamba Tanzania kwanza, ndio maana nimetumia fursa hii kuipongeza Timu yetu ya Yanga kwa hatua nzuri waliofikia, lakini Waswahili wanasema usione vinaelea bali vimeundwa. Waundaji sio wengine ni Mama shupavu, Mama hodari, Mama ambaye ana maono makubwa sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hongera sana mama kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, niongelee kuhusu utamaduni. Utamaduni ndiyo kitu kinachomtanabaisha mwanadamu, wapi alikotoka, wapi alipo na wapi anakokwenda, tamaduni ni maisha ya kila siku. Sasa kwa muktadha huo bajeti hii ambayo imepewa Wizara hii ni bajeti ndogo ndogo kupita kiasi. Hakuna chochote hapa ambacho wanaweza kufanya ndani ya Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii kwa muktadha wake ndiyo Wizara inayobeba Taifa ukiachana na Wizara nyingine. Ndiyo Wizara inayotutambulisha sisi kama Watanzania. Kuna mambo mengi na makubwa ya kufanya kwa bajeti hii wanafanya nini hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la michezo. Michezo ni lazima tuwajenge watoto wakiwa mashuleni, hapa mashuleni kote unakokwenda hakuna viwanja vizuri vya kuchezea, hakuna wataalam ambao wanaweza wakawafundisha hao Watoto, na kule mashuleni ndiko tunakoweza kuwaibua wachezaji kama leo wakina Mayele hao ndiyo tunawaibua kule. Kama bajeti ni ya namna hii tunafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hiyo kwa sababu ka muda kenyewe ni kadogo sana nataka nielezee TaSUBa. TaSUBa ni Tamasha la Utamaduni na Sanaa Bagamoyo, hapa kama ambavyo wamesema ndani ya miaka 10 bajeti haijaenda, lakini tutambue kwamba hapa ndipo wanapozalishwa vijana wenye vipaji maalum katika Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na uzalishaji huo, Mama Samia Suluhu Hassan ametangaza Royal Tour na Bagamoyo ni Mji wa kihistoria katika Taifa hili na duniani kwa ujumla, duniani kote wanaijua Bagamoyo, angalia leo unakwenda kwenye Chuo cha Sanaa Bagamoyo hata ukuta hakuna! Ukuta hakuna, hivi mtu anatoka huko anakotoka anasema anaenda kukiona chuo ambacho kinawazalisha wasanii, ndiyo chuo chenyewe hiki? Hapa ni lazima tujipange, tujipange ili tuoneshe na sisi kama Taifa kuna chemchem ya kuibua hivi vipaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekuwa mdogo nilikuwa na mambo mengi ya kusema lakini sasa nitafanya nini dakika zenyewe ni dakika saba? Basi itoshe tu hayo hayo niliyoyasema yanatosha lakini nilikuwa na mambo mengi nitaandika. Nilikuwa na mambo mengi na ushauri bila kukosa kukisemea Kiswahili. Kiswahili ni lugha, ni lugha adhimu, ni lugha yenye mashiko na lugha inayowatambulisha Watanzania, chimbuko la Kiswahili ni Tanzania. Sasa nina ushauri juu ya Kiswahili hiki. Kuna Chama kinaitwa CHAUKIDU (Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani). Hivi vyama hivi ni lazima Wizara kama Wizara kuna CHAUKIDU na CHALUFAKITA. Hivi Wizara ni lazima mviweke ndani ya bajeti yenu, Wanapofanya makongamano Wizara ishiriki katika kuvisaidia hivi vyama katika kukitangaza Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Salma Kikwete tunakushukuru sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)