Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nitakuwa na sehemu kama tatu. Kwanza, pongezi; pili, nitazungumzia Baraza la Kiswahili la Taifa; na tatu, soka letu na nne, nitazungumzia uingiaji salama katika Uwanja wa Taifa na mwisho utawala bora katika michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameongeza hamasa katika michezo. Zile shilingi milioni tano, tano alizokuwa anazitoa kwa magoli yanayofungwa kwenye club bingwa na kwenye shirikisho, imeleta heshima sana na ikaleta hamasa kubwa sana. Kwa hiyo, tunampongeza sana na tunapongeza vilabu vyote ambavyo vimeshiriki kimataifa, Simba pamoja na Yanga ambao walituheshimisha kwa kufika fainali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza utajielekeza kwenye Baraza la Kiswahili la Taifa. Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza sana. Tumesema kwamba tutafanya Kiswahili kuwa bidhaa na watu wengi wanadhani kwamba ukijua tu Kiswahili kama hivi ambavyo tunaongea, basi unaweza ukawa Mwalimu wa Kiswahili au mkalimani. Kumbe sivyo, lazima ujifunze Kiswahili kama lugha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka pia kukifanya Kiswahili bidhaa kwa maana ya kwamba kikafundishwe huko nje, lazima pia tujifunze na lugha za mataifa mengine. Kwa hiyo, nawapongeza sana BAKITA, wana kitabu hapa English, Kiswahili na Portuguese cha mtu ambaye anajifunza Kiswahili ambaye ni Mreno. Sasa ili aweze kufundishika vizuri, ndani yake pia kuna sehemu ya Kiingereza. Pia wamekuja na Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni hatua ya awali, kati na juu. Hii kweli wanathibitisha kwamba BAKITA wapo kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, wana kitabu kinaitwa furahia Kiswahili, Kiswahili kwa wageni. Kwa hiyo, tunaona jitihada ambazo BAKITA wanazifanya katika kuhakikisha kwamba Kiswahili kweli kinakuwa ni bidhaa kama ambavyo tumesema. Sasa nami nitoe wito kwa Wizara ya Elimu na Vyuo Vyetu Vikuu, navyo viwekeze nguvu katika kufundisha siyo tu Kiswahili, lakini kufundisha Kiswahili kama lugha ambayo baadaye inakuwa bidhaa, kufundisha wakalimani wa kutosha, na kufundisha katika namna ile ambayo kweli watu watapata nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tulisikia South Africa wanataka walimu 1,000 lakini huwezi kwenda South Africa kufundisha Kiswahili kwa sababu tu unajua Kiswahili, lazima ujue Kiswahili kama lugha, lazima ujue Kiingereza, lakini ikibidi lazima ujue lugha za wenyeji wa maeneo yale. Kwa hiyo, nawapongeza sana BAKITA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nilisema kwamba suala la pili nitazungumzia kuhusu soka letu. Katika timu nne ambazo zimeingia fainali ya shirikirikisho na fainali ya club bingwa Afrika, Al Ahly wao katika timu yao first eleven walikuwa wana wachezaji wa kigeni watatu tu. Wale Wydad ambao waliwatoa Simba walikuwa na wachezaji wawili tu. Hawa USM Alger, walikuwa na wachezaji wawili tu. Yanga walikuwa na wachezaji wazawa sita. Maana yake ni nini? Hatusemi kwamba vilabu visiwe na wachezaji wa kigeni, lakini hii ni kwa sababu hatuwekezi kwenye soka la vijana kuanzia under seventeen, under twenty, under twenty-three. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ushiriki World Cup au Afcon kila mwaka, uwe na uhakika, ni lazima tuwekeze kwenye soka la vijana. Hapa kuna mambo mawili; kuna Serikali na wadau. Kwa hiyo, Serikali wajibu wake: moja, kujenga miundombinu ya viwanja; pili, kupitia sera za kikodi kuhakikisha kwamba tunapunguza kodi katika vifaa vya michezo. Leo hii ukimpeleka mtoto kama pale Fountain Gate au Magnet au Kambiyaso, ile kit yake tu, kwamba vifaa kwa maana ya viatu, soksi, jezi na mpira wa kuchezea, minimum labda unazungumzia Shilingi laki moja na nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tuweze kuwa na Timu ya Taifa itakayokuwa shindani, lazima tuwe na wachezaji wazawa wa kutosha, lakini ili tuwe na wazawa wa kutosha, lazima tuwekeze kuanzia hiyo under seventeen na kuendelea. Kwa hiyo, hilo nimeona niliseme vizuri. Kwa hiyo, kuna wajibu wa Serikali na wajibu wa wadau. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo ni muhimu niliseme ni kuhusu uingiajia wa pale uwanjani. Mmeona juzi tunatoa pole kwa ile familia, lakini lazima tufike wakati tujifunze wakati wa mechi kubwa management ya namna ya kuingia uwanjani iwe ni salama. Haiwezekani mechi inachezwa saa 10.00, unatakiwa uende uwanjani saa 12.00 asubuhi. Tuwekeni utaratibu mwema wa jinsi ya kuingia pale uwanjani.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cosato, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kapinga.
TAARIFA
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji juu ya uingiaji salama katika Uwanja wetu wa Taifa. Kwa utaratibu wa uwanja ule, una mageti, lakini kwa bahati mbaya sana utaratibu uliozoeleka, mageti yanayofunguliwa ni matatu tu; lile la Simba, lile la Yanga, na lile kubwa, lakini uwanja ule wote umezungukwa na mageti, lakini sasa wananchi wanasongamana kiasi kwamba wanasababisha ile hali inayotokea pale na mauaji.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cosato, taarifa hiyo unaipokea?
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa sababu inaboresha namna ya kuingia katika uwanja na kwa usalama na kwenda uwanjani isiwe kama kero, isiwe kama adha. Maana yake tunasema kuna kitu Mheshimiwa Jesca huwa anasema afya ya akili. Michezo na burudani ni mojawapo ya tiba nzuri sana ya hiyo mnayoita afya ya akili. Kwa hiyo, mtu kwenda uwanjani ni kutaka kupata entertainment. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema lingine nitazungumzia utawala bora katika soka. Nilisema mwaka 2022, Chama cha Mpira cha Wanawake mpaka leo hawajafanya uchaguzi. Walipofanya uchaguzi, ulivurigika, walisema kwamba wapigakura wamekuwa wengi, wakasema watafanya baada ya miezi mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, wewe kama mama kwa kukosekana ule uchaguzi maana yake tunakosa uwakilishi wa wanawake kwenye Kamati ya Utendaji wa TFF. Kwa hiyo, nawaomba Baraza la Michezo, Msajili wa Vyama za Michezo na Wizara kwa ujumla, jambo hili ni muhimu. Kama tunazungumzia kunyanyua wanawake, na timu zetu za wanawake zinafanya vizuri, tufanye uchaguzi wa chama cha soka cha wanawake hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.