Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Na mimi niungane na wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na viongozi wote wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi lakini bajeti ni ndogo, mambo ni mengi na muda nao ni mdogo, nitajaribu kwenda kwa harakaharaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wazo la Mheshimiwa Sanga la kuangalia namna ya kutumia CSR za makampuni kuwekeza katika michezo. Kwa kifupi tu bajeti wanayopewa leo ya milioni 35 haiwezi kujenga moja ya tatu ya ule Uwanja wa Mkapa. Nimeangalia kwenye dodoso hapa ule uwanja ni dola milioni 56, ni kama bilioni 133. Kwa hiyo hiyo bajeti yenyewe hata kiwanja kama kile haiwezi, ukiacha mambo ya watumishi huko na vitu vingine. Kwa hiyo ninaomba sana tuangalie namna ya kuiwezesha Wizara iwe na hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitoe mfano; Moshi tuna Uwanja wetu wa Majengo, kila mwaka tunatenga bajeti ikinyesha mvua kubwa barabara zikiharibika wakiangalia mahali pa kutoa tunasema toa kule kwenye michezo, yaani michezo nchi hii imeendelea kuwa nayo ni mchezo, yaani michezo ni mchezo. Lakini kwenye Baraza la Madiwani lililopo sasa Moshi Mjini, mwaka jana tumetenga milioni 300 na mwaka huu milioni 300 na Uwanja ule wa Majengo tayari tunakwenda kuutengeneza, tayari pitch imeshawekwa, tunaweka uzio na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Wizara; na kwa sababu sasa hakuna hela ya kusiadia kule Majengo nashindwa niioombeje, lakini hata kama mtatembeza bakuli mkipata chochote kwenye Halmashauri kama ya Moshi ambayo tumepeleka milioni 600 kwenye uwanja na sisi tunakuwa wa mfano, basi mtusaidie kutuongezea hela ili uwanja wetu ukamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mpango wa kujenga viwanja viwili (arenas). Naona mmoja unajengwa Dar es Salaam, mwingine walisema ni Dodoma. Mimi naomba niwaambie, ili michezo iendelee kukua ni lazima tu-diversify. Ni vizuri mmoja ukijengwa Dodoma huo mwingine ujengwe ama Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini au kule kusini Mbeya, maeneo ambayo yanafikika, ili tuweze kupanua huu mchezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Moshi Mjini sisi tuna eneo pale, lina ukubwa wa mita za mraba 157,000, unaweza kuweka arena pale. Kanda ya Kaskazini tuna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa pale Hai, Moshi Mjini tuna uwanja mdogo, ule uwanja unafikika. Kwa hiyo ni vizuri tu-diversify, siyo viwanja vyote vijengwe Dar na Dodoma halafu kwingine kusiwe na viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aspect ya kwamba michezo ni utalii, na nilikuwa nataka kulichangia hili katika Wizara ya Utalii lakini ni vizuri nililete hapa. Sisi Moshi Mjini tuna mashindano makubwa ya kukimbia, Kilimanjaro Marathon, inaleta watu karibu 8,000 kutoka nchi zaidi ya 51. Wale watu wakishamaliza kukimbia huwa wanakwenda mbugani, wanapanda mlima, wanakwenda Zanzibar, wanaingiza fedha kwenye utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yapo maeneo Wizara ya Michezo ikiwekeza vizuri inaweza kusaidia sekta nyingine na ili hizi sekta sasa na zenyewe zichangie kwenye michezo. Hii Kilimanjaro Marathon ni mfano, lakini tunaweza kuwa na Mchezo wa Golf wa kimataifa, tunakwenda ku-lobby na PGA. Kuna moja ilikuwa ifanyike kule Kili Golf, kuna kiwanja ambacho kipo katikati ya Mlima Meru na Mlima Kilimajaro, Kilimanjaro Golf, unaitwa Kili Golf; unaweza ukaleta yale mashindano pale, yatatangazwa dunia nzima lakini wale washiriki pia watapata nafasi ya kwenda kwenye mbuga za wanyama kwenda kutalii ili watuingizie fedha. Hiyo ni pamoja na cycling tour.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote hayaji tu. Kule Rwanda kuna Tour De Kigali; hayaji tu, lazima ukafanye lobbying na vile vyama vya cycling vya kimataifa. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri mkitushirikisha sisi tunaweza kuungana kuweza kufanya hiyo lobbying. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanja vya golf, na ninasema golf kama mchezo mmoja, lakini kwa michezo mingine yote. Tume-concentrate sana kwenye mpira wa miguu, ni vizuri tukumbuke kwamba ndondi nayo sasa hivi imeanza kutupia kimataifa, muziki unatuaisha kimataifa, riadha juzi kuna mkimbiaji wetu amemshinda mpaka Kipchoge. Kwa hiyo ni vizuri tuangalie namna ya kukuza hii michezo yote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye golf Moshi pale tuna uwanja wetu wa golf, Uwanja wa kwanza golf Tanzania, Moshi Club, tuna denii kubwa sana la land rent. Sisi hatutaki tusamehewe, tunaomba Mheshimiwa Waziri uongee na Waziri wa Ardhi waondoe interest, sisi tuko tayari kulipa ile land rent yote ili kuweza kusimamia ule Uwanja wa kihistoria wa Moshi Club.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la riadha. Kuna ulazima wa kutengeneza kambi maeneo ya nyanda za juu, maeneo ya Rift Valley kama kule Karatu, na maeneo ya West Kilimanjaro ili watu waje wa-train. Kule Kenya kuna eneo linaitwa Iten ambalo mpaka wakimbiaji wa nje wanakuja ku-train wiki mbili, wiki tatu kabla ya mashindano makubwa. Sisi tuna maeneo yanafaa, kule West Kilimanjaro kunafaa, kule Karatu kunafaa, itengenezwe kambi watu waje wawekeze nyumba za kulala ili wakimbiaji waje washiriki huku, na ni utalii pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye incentives, kampuni ambazo zimeshasaidia michezo mpaka sasa, sijajua Serikali inazisaidiaje; Azam kama mfano mzuri, GSM, Mohamed Enterprises, CRDB ambao wana-sponsor Mchezo wa Basketball wa Taifa, NMB; ni namna gani Serikali inatia chachu kwa kampuni hizi ili kampuni nyingine nazo ziwekeze kwenye michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Moshi tulikuwa na mashindano makubwa sana ya volley ball. Yalikuwa yanakuwa sponsored na Bonite Bottlers. Sijaona ni namna gani Serikali inasaidia makampuni binafsi ambayo yanawekeza kwenye michezo ili kuvutia makampuni mengine nayo yapate hamu ya kuwekeza kwenye michezo. Kwa hiyo nadhani kuna kitu cha kufanya ili tuweze kusukuma gurudumu hili mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)