Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia Wizara hii ya Fedha. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anazoendelea kufanya pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoendelea kusimamia Wizara yetu ya Fedha na kuhakikisha kwamba Sera zinatekelezwa vizuri kwa ajili ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo moja au mawili ambayo natamani kuyazungumza siku ya leo kuishauri hii Wizara. Kuna sehemu aliyochangia kaka yangu Mheshimiwa Mbunge wa Handeni, habari ya Kitengo cha Internal Audit katika Halmashauri zetu pia kwenye Wizara mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna shida ipo kwenye kitengo hiki. Kwanza kabisa, lazima tufahamu kwamba bado kuna tatizo kubwa sana la uhuru. Wakaguzi wetu wa Ndani hawana uhuru kwa sababu wanaripoti moja kwa moja, sehemu kubwa wanawezeshwa na Maafisa Masuuli. Unakuta Afisa Masuuli huyo ndiyo anaeombwa gari kwa ajili ya Mkaguzi wa Ndani kwenda kufanya ukaguzi site. Akipenda anaweza akatoa gari, asipopenda anaweza asitoe gari, at the same time Mafungu bado yapo kwa Afisa Masuuli kwa sababu kazi hizi zinafanywa na mapato ya ndani lakini pia na mapato ya OC kutoka Serikali Kuu. Sasa hapa uhuru lazima ukosekane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshauri Mheshimiwa Waziri sasa, kuhakikisha kwamba wanatengeneza vote, mwaka jana tulipitisha hapa tukakubaliana kwamba watengeneze vote kwa ajili ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ili aweze kupeleka rasilimali huku chini kwa Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri lakini Wakaguzi wa Ndani wa Wizara mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kitakachopatikana hapa? Wakaguzi wa Ndani watakuwa na uhuru wa kufanya kazi zao bila kumtegemea Afisa Masuuli. Afisa Masuuli atakuwa anapewa taarifa za kiukaguzi kama Meneja wa sehemu husika kwa sababu ndiye anayetakiwa kujibu zile hoja za Mkaguzi wa Ndani. Tukilifanya hilo tutawapa uhuru mkubwa kwa sababu sasa hivi hawana uhuru wa kusema wakati wanatekeleza majukumu yao ya ukaguzi wa fedha zetu ambazo tunapeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri na tunapeleka fedha nyingi kwenye Wizara zetu lakini Wakaguzi hawa wa Ndani hawana ule uhuru wa kutekeleza majukumu yao kwa sababu Maafisa Masuuli ndiyo wanaowawezesha kutekeleza yale majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawawezi kufanya kwa sababu Afisa Masuuli huyo huyo unamwandikia kwenda kukagua mradi wakati anajua mradi huo una matatizo, atakuchenga wala hatakupatia fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu hayo. Fedha zitoke moja kwa moja kwa Vote ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani zishuke chini ili waweze kufanya kazi kwa uhuru mkubwa na tutaweza kuona matokeo ya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuziimarishe hizi Kamati za Ukaguzi za taasisi husika. Mheshimiwa Waziri, kuna sehemu nyingine hata hizi Kamati hazipo, kuna baadhi ya Halmashauri hata hizi Kamati hazipo, hazijaundwa. Ukisoma Public Finance Act ya Mwaka 2010 Cap. 348 inaeleza vizuri kabisa lakini kuna baadhi ya sehemu Kamati hizi hazipo, sasa ufanisi wao unakosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili ufanisi wao upatikane ni lazima pia mzifuatilie Kamati hizi na kuona kama zinafanya kazi. Vilevile, nazo pia bado zinakumbwa na tatizo la uhuru kwa sababu Kamati zinategemea posho kutoka kwa Afisa Masuuli, ni lazima tutengeneze vizuri hapa ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwa ajili ya hizi Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni rasilimali watu. Bado Wakaguzi wa Ndani ni wachache, ongezeni Wakaguzi wa Ndani kwenye Taasisi za Serikali ili tuweze kupata ufanisi wa kazi ambazo wao wanazifanya. Unakuta kwenye Halmashauri kuna Mkaguzi wa Ndani mmoja lakini kazi ziko nyingi, atafanyaje kuhakikisha kwamba hizi kazi zinafanyika na kudhibiti huu ubadhirifu unaoendelea katika kazi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nimekiona na kimekuwa kikija kwenye Kamati na nimekiona ni kizuri ambacho kinafanywa na CAG na tunatamani pia kifanywe na Idara hii ya Ukaguzi wa Ndani, ni zile kaguzi za performance audit (Value for money) lakini pia real time audit. Kaguzi hizi zikifanyika kwa wakaguzi wa ndani zitatusaidia pia kuhakikisha kwamba tunalinada rasilimali zetu tulizo nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninataka kuomba nini? Mheshimiwa Waziri sasa ni lazima mfikirie kuajiri professionals nyingine zaidi ya professional za kihasibu katika hizi kaguzi zetu za ndani, lazima pia tuwe na Engineers kwenye Idara ya Ukaguzi wa Ndani ili anapokwenda kukagua miradi awe anajua anakwenda kufanya nini, kwa sababu kinachofanyika sasa hivi Mkaguzi wa Ndani ni Mhasibu anakwenda kukagua kwenye jengo fulani, anapokuwa anafanya kazi za value for money, inabidi sasa kwa sababu anakuwa hajui chochote kuhusu Engineering amuulize Engineer wa halmashauri kwamba hivi ilitakiwa kuwa nondo ngapi? Wakati huyo Engineer ndiye mkaguliwa! Sasa hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuweke professional zingine kwa hiki kitengo cha internal audit ili kiweze kufanya kazi vizuri. Vilevile Mheshimiwa Waziri tuwape mafunzo. Mambo yanabadilika lakini bado hatuwapi mafunzo. Tuwape mafunzo Wakaguzi wa Ndani, Wahasibu wa Halmashauri na Wahasibu wa Taasisi zetu ili waweze kufanya kazi sawa sawa na miongozo mipya pamoja na miongozo ya kiuhasibu inayotoka ili watekeleze majukumu yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Mhasibu yuko Halmashuri miaka 15 anaandika voucher, voucher kila siku halafu unaita tuna Mhasibu! Hapana. Uhasibu siyo kuandika voucher tu peke yake, afanye na majukumu mengine. Mpelekeni kwenye training, mpelekeni kwenye mafunzo ili ajue ni mabadiliko yapi ya kiuhasibu ambayo yanatokea katika miaka mbalimbali ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukiangalia kama sikosei ni mwaka 2022 au 2021 kuna mabadiliko ya hizi IPSAS, Hisa na vitu vingine lakini ukuwauliza wale Wahasibu walioko kwenye Halmashauri na walioko kwenye Wizara kuna wengine hawajui kabisa kama kuna mabadiliko lakini mabadiliko yapo. Unakuta kuna mabadiliko ya watu kusaini, kuna mabadiliko mbalimbali ya kifedha lakini wao wanatengeneza vitabu vyao vya hesabu ukilinganisha na sera zilizokuwepo toka mwanzo bila kufuata mabadiliko ambayo yametokea hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nikuombe tenga fungu kwa ajili ya mafunzo kwa Internal Auditors, tenga fungu kwa ajili ya mafunzo kwa Wahasibu ili waweze kuendana na kasi ambayo inatakiwa na kuweza kufanya kazi katika nchi yetu na kazi zenye ufanisi. Tunataka kuona kazi zenye ufanisi katika Halmashauri zetu, tunataka kuona kazi za ufanisi katika Wizara zetu ili tumrahisishie CAG, muda mwingine tunampa CAG kazi kubwa bila sababu wakati kuna Wakaguzi wa Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)