Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Bajeti hii ya Fedha. Awali ya yote nikupongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu na Naibu Waziri lakini pia na Kamishna wa Kodi, Ndugu yangu Kidata kwa sababu ya kazi kubwa ambayo mnafanya katika Taifa hili ya kukusanya kodi. Kimsingi iko wazi kwamba ni ngumu sana mkusanya kodi kuwa popular kwa hiyo, wakati mwingine mkipigwa mawe mvumilie tu, Taifa linajua kazi kubwa ambayo mnaifanya na tunatambua kwamba mmebebeshwa mzigo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nipende kuanza na suala la microfinance; suala la microfinance huko kwa wananchi ni tatizo kubwa sana. Nakumbuka kama miaka miwili iliyopita ilikuja sheria hapa tutarekebisha sheria ili kupunguza angalau makali, kuanzia kwenye riba ambayo microfinance wanachaji kwa wananchi lakini pia na procedure mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tatizo ni kubwa, wananchi bado wanachajiwa riba kubwa na microfinance lakini pia hata ile procedure yenyewe, wanaweza wakapunguza bei ya kiasi cha riba lakini ile procedure ambayo ni application fee ni gharama kubwa kuliko hata riba yenyewe. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri suala la microfinance tuendelee kulifanyia kazi, kwa sababu huko ndiko wananchi wetu wengi wanapata mikopo kwa ajili ya biashara lakini pia na shughuli mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilikuwa naangalia napitia bado tofauti kati ya bidhaa za kutoka nje hasa kwenye vinywaji, tofauti ya kodi kati ya bidhaa za kutoka nje na ndani ni ndogo sana. Hii bado naamini tunayo nafasi ya kufanya marekebisho kama ni kushusha kodi ya bidhaa za ndani au kupandisha ya nje, lengo ili tuweze kuwainda ipasavyo na kwa vitendo viwanda vya nchi yetu. Huwezi ukaweka tofauti labda ikawa ni 200 au 100 kwa lita halafu utegemee kwamba utapata matokeo ambayo ni mazuri sana, kwa hiyo, lazima hili liwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Nchi za wenzetu unakuta tofauti ni kubwa sana kiasi kwamba mtu akitaka kwenda kununua bidhaa ya nje kama ni kinywaji anafikiria mara mbili mara tatu kwa sababu bei inakua ni kubwa sana wakati mwingine inakuwa hata mara mbili ya kile cha nyumbani. Kwa hiyo, ni lazima tuliangalie tusiogope kufanya maamuzi kwa ajili ya kulinda viwanda vya ndani na ukiwabana sana hata hawa ambao wana viwanda nje hata vifaa tunapata kwa kodi kubwa wanakuja kujenga hapa hapa kwetu, wakija kujenga hapa maana yake sasa vijana wetu wanapata ajira, tunachukua kodi zaidi na tunapata wawekezaji kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Wizara ya Fedha pia kutokana na utaraibu wake wa usimamizi wa stempu za kodi zile za ETS. Utaratibu huu umeendelea kuongeza kodi, umeendelea kuongeza kodi kwa nchi yetu lakini pia umeendelea kutupa taarifa hasa za uzalishaji maana wakati wa zamani wakati tunatumia zile stempu ambazo sio za kieletroniki kulikuwa na tatizo kubwa sana. Ilikuwa ni ngumu kuweza kujua kwa sababu forgery ilikuwa ni kubwa, ilikuwa ni ngumu kuweza kujua hasa uzalishaji ni kiasi gani lakini pia hata kodi ilikuwa ni ngumu kuweza kukusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mnafanya kazi nzuri sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hongera sana katika hili na usirudi nyuma wakati mwingine yanaweza yakaja manung’uniko yanaweza yakaja malamiko kwa sababu kama nilivyokuambia mkusanya kodi ni ngumu kuwa popular. Kwa hiyo, kanyaga na hata vetting mnayofanya kupata kampuni ambayo inafanya shughuli ile ya SICPA, mmefanya vizuri sana kwa sababu ni kampuni ambayo ukiangalia iko Dunia nzima. (Makofi)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba utulivu ndani ya Bunge.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

TAARIFA

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hapa Kingu niko…

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri sana unaotolewa na mchangiaji Kaka yangu Mheshimiwa Vuma, nilikuwa naomba nimpe taarifa kwamba pamoja na kwamba amesifia mpango mzuri wa stempu za eletroniki bado Serikali inaweza kuwa na nafasi ya kukaa na mzabuni wa SICPA kuona namna gani wanaweza wakapunguza bei, ambayo imekuwa ikionekana kidogo kwamba imeonekana kwamba ni changamoto ili kusudi Serikali ikaingia partnership na huyu mwekezaji ili Serikali iwe sehemu ya kumiliki teknolojia hii…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kingu hiyo ni taarifa au unachangia.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Naibu Spika, …na baada kuwasaidia Watanzania kupata teknolojia.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa kwa mikono miwili, kwa nini? Kwa sababu nataka niseme, kabla hatuajanza mfumo huu Serikali imepoteza mapato mengi sana na nashauri tusiiishie tu hapo kwenye stempu hizi, tusiishie kwenye bidhaa ambazo zinatozwa kodi, hata bidhaa ambazo hazitozwi kodi nashauri tubandike stempu hizi ili tuweze kujua takwimu halisi kwamba tuna zalisha kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu usirudi nyuma kanyagia hapo hapo. Tunahitaji fedha kwa ajili ya maji majimboni, tunahitaji fedha kwa ajili ya vitu mbalimbali, tunahitaji fedha kwa ajili ya barabara vijijini. Endelea kukusanya kodi na hii kampuni kama alivyonipa taarifa Mheshimiwa Kingu ni vizuri tuendelee kushirikiana vizuri kwa sababu sio kila mtu anaweza kufanya kazi hii. Kuna kampuni chache ambazo zinaweza kufanya kazi hii. Kwa hiyo, tujitahidi tuwe makini, tusirudishe nyuma, kanyagia hapo hapo ili tuendelee kukusanya fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la Benki ya Kilimo, Benki ya Kilimo hapa tumeshashauri mara nyini sana. Benki ya Kilimo ina stimulate sana uchumi wa nchi hii, kwa sababu ndio Benki ambayo inamjali mkulima kuliko benki yoyote ile huo ndio ukweli. Tumesema mara kadhaa hapa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tunaomba sana benki hii fanya consideration ya kuiongezea mtaji ili iweze kufikia Watanzania wengi Zaidi. Wananchi wengi huko hawapati mikopo ya Benki ya Kilimo kwa sababu mtaji ina maana ni mdogo. Kwa hiyo, tunaomba sana jitahidi sana uipe kipaumbele benki hii ya Tanzania ili iweze kuwafikia Watanzania ambao ni wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka kuzungumzia kuhusu maduka, utaratibu wa maduka ya kubadilisha fedha. Nadhani lazima tuangalie sheria ikoje inayo govern suala hili, kwa sababu utaratibu ni mgumu kiasi kwamba unalazimisha watu kufanya biashara hii katika namna ambayo sio halali. Yako maeneo hasa ya mpakani, maeneo ya mpakani hasa kama kule kwetu Kigoma na maeneo mengine, suala la kubadilisha dola ni suala la kila siku, watu wanatoka Congo, wanatoka Burundi, wanatoka Rwanda…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma kengele ya pili.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja.

NAIBU SPIKA: Muda wako mwingi umetumia kwenye stempu.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kw Amuda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Sekunde tano.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana nishauri Serikali iweke utaratibu mzuri kwa kuruhusu biashara hii ifanyike vizuri waweze kupata kodi kupitia maduka ya kubadilishia fedha, nashukuru sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.