Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwenye hili nichangie kama ifuatavyo; kwanza ni muhimu ikaeleweka kwamba watu wanaokosoa jambo wana nia njema kuliko watu wanaoona jambo na kulichukulia kama lilivyo, hilo la kwanza. (Makofi)
La pili tuna Watanzania wenzetu wako huko nje wana akili nyingi sana, pia inawezekana kutuzidi hata sisi tuliokuwa huku ndani. Kwa hiyo, ni muhimu sana kama Taifa tukajenga utamaduni wa kuheshimu kila mchango wa Mtanzania, vilevile tukauchuja pale ambapo tunaona hauna maslahi mapana kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja hazijibiwi kwa ukali, hoja inajibiwa kwa upole,…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Nani amesimama kwa ajili ya taarifa? Aah Mheshimiwa Halima Mdee kuna taarifa kwa Mheshimiwa Ummy Nderiananga.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa dada yangu Mheshimiwa Mdee kwamba hamna mchango ambao umedharauliwa au kupuuzwa ila ambacho tuna mashaka nacho ni michango ambayo ni ya upotoshaji na tunaendelea kuelimishana katika eneo hilo, ahsante. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee unaipokea taarifa hiyo.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati imesema kwamba makubaliano hayo kwa sababu tukipitisha kama Bunge maana yake yanaenda kuwa makubaliano ya Kimataifa yaani Sheria ya Kimataifa inaenda kuwa International Law. Sasa tunaambiwa makubaliano yanaweka msingi wa kisheria na sio mkataba na sisi ndio tunazungumza hapa hapa kwamba kama msingi una mashaka, kama msingi una matobo, kama msingi hauna madhara kitaifa hiyo mikataba mnayosema tutaletewa hapa Bungeni lazima iendane na sheria hapa. (Makofi)
Kwa hiyo, ni kama vile hii Katiba ya Jamhuri ya Muungano hapa, Katiba ni msingi mama wa sheria zote. Haya makubaliano hapa ndugu zangu ndio msingi wa kitakachokuja. Nitatoa mfano scope Ibara ya nne inasema; “Scope of this agreement is to facilitate the implementation of areas of co-operation set out in an Appendix I of this agreement.”
Mheshimiwa Spika, Appendix I ni sehemu pacha ya huu mkataba ama haya makubaliano. Appendix I ina phase mbili; ina phase i na ina phase II. Phase I inahusu yale magati ya bandarini ambayo pamoja na mambo mengine yanahusisha magati ambayo Tanzania tulikopa almost trilioni moja kuyafanyia maboresho. Ndugu yetu wa TPA kwa haya maelezo anapewa terminal ya maboti na anapewa na terminal ya passengers ya abiria, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili phase II inahusisha ku-develop, ku-manage na ku-operate mind you kwa sheria ya sasa hivi ya bandari ya 2014 na kama tulivyofanya marekebisho mwaka 2019, majukumu haya ni ya bandari. Kwa hiyo, tunasema kama nia ni njema kwa nini aspect ya PPP isionekane kwenye makubaliano yanayokuja kuwa sheria ya Kimataifa? Makubaliano haya bandari ni facilitator tu wa mazungumzo makubaliano haya hata umiliki wa ardhi, bandari hajulikani yuko wapi. Kwa hiyo nilisema phase II…
SPIKA: Mheshimiwa Halima subiri muda wako unalindwa, Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema, maana tuko hapa tunataka kujua vifungu vipi vina shida humu ndani. Umeeleza kuhusu scope of co-operation and implementing entities ukasoma kifungu kidogo cha kwanza, hebu kirejee tena.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kidogo cha kwanza si ndio phase I project?
SPIKA: Ndio ulioisoma, irejee tu.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, imesema development, management and operation of General Cargo Berth one to four in container terminal berth five to six. Development Dhow Wharf Terminal and Passengers Terminal of Dar es Salaam Port to be operated by TPA. This two ndio anapewa TPA ku-operate kwa mujibu wa hii hapa.
SPIKA: Kwa hiyo, kwa ulivyosoma umeanzia huku article 4 ukasoma sub-article one, ukatupeleka huku kwenye appendix I. Umetueleza kwamba Serikali ilishawekeza pesa trilioni zaidi ya moja na hilo eneo ndilo analopewa huyu DP World. Hebu nieleweshe mimi hapo anapewa kufanya nini? Kwa vifungu hivi tulivyonavyo mbele yetu anapewa kufanya nini?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba unilindie muda wangu.
SPIKA: Unalindwa kabisa usiwe na wasiwasi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nimesema hivi article 4 ni scope of co-operation ambayo article 4 inaenda sambamba na appendix I. Appendix I imeelezea maeneo ya ushirika ambayo katika appendix I specific eneo naomba niruhusu…
SPIKA: Nakusikiliza, umenisikia nimeongea, nakusikiliza. (Kicheko)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo appendix I katika moja, mbili, tatu mpaka saba kwenye appendix I TPA amepewa namba two, ndio atakayo…
SPIKA: Sawa sasa twende hapo mimi nataka pale kwenye pesa ya Mtanzania ambayo ili…
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, pesa ya Mtanzania...
SPIKA: Subiri kwanza, mimi si nakusikiliza, tunasikilizana kwa sababu jamani leo sio michango ya kawaida humu ndani, ni michango kwa ajili ya hili azimio hili. (Makofi)
Mmi nisaidie jambo moja kwenye lile eneo ambalo pesa zimetumika za Mtanzania, si ndio? Hapa phase I project na wewe uko hapo inasema hapo kwenye moja; “development, management and operation” hapo. Huku mwanzoni kwenye article 4 inasema; “The scope of this agreement is to facilitate the implementation of areas of the co-operation set out in appendix I to this agreement, co-operation between this two entities” kama hivyo ndivyo na yale maelezo ambayo umeyatoa mwenyewe kwamba Serikali imeshawekeza pale. Kwa nini wewe, mimi nauliza ili nielewe maana tunataka tujue vifungu gani tupitishe, vingine vipi tukatae.
Kwa nini usifikiri lile eneo anaenda kwenye operation maana hapa yako mambo matatu, kuna development, management and operation?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, mimi siwezi kufikiria kwa niaba ya Serikali kwa sababu hoja…
SPIKA: Ehe sasa ngoja hapo hapo umemaliza vizuri.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa sababu hapa…
SPIKA: Ngoja niweke sasa vizuri hoja yangu ili nikupe muda uendelee kumalizia. Ndio maana Waheshimiwa Wabunge sasa hivi tunatoa maoni yetu ili Serikali yale ambayo wanaenda kuingia kwenye hiyo mikataba wakayatazame. (Makofi)
Huu mkataba haujaweka msingi kwamba kwenye eneo hili la zero mpaka berth sijui saba huu mkataba hauwezi kusema anaenda kufanya nini pale, wala hausemi. Unaeleza maeneo ambayo anaweza kupelekwa sio anapelekwa. Kwa nini anaweza kupelekwa? Kwa sababu kifungu cha tano ambacho kimetajwa sana huko nje kimeweka misingi ya hayo ili waweze kukubaliana, lazima wakubaliane kamoja kamoja ambayo hawakubaliani anaweza kupewa mtu mwingine au akaendelea yeye mwenyewe TPA. (Makofi)
Sasa Mheshimiwa Halima nilitaka mimi mwenyewe nielewe vizuri maana leo lazima tuongozane vizuri humu ndani, nje mambo ni mengi. Nilitaka nielewe pale kwenye uwekezaji na maadamu umesema kwamba huwezi kujua Serikali inapeleka wapi, haya endelea na mchango wako.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, huu mkataba ni baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai na DP World ametajwa hapa specifically. Kwa hiyo, hata kama tutazunguka mbuyu kwa kiwango gani tunachozungumza hapa hivi vitu vyote viwe vitatu, kiwe kimoja, viwe viwili lazima apewe. Kwa hiyo, tukipitisha mkataba atapewa hilo ni la kwanza.
SPIKA: Lazima apewe unaitoa wapi Mheshimiwa Halima? Maana lazima tukae sawa leo ile lazima apewe yeye umeitoa wapi? (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, unajua kwa nini naitoa kwenye haya makubaliano, wamekubaliana ushirika wa mambo yote yaliyozungumzwa hapa.
SPIKA: Hapana twende vizuri, vifungu humu ndani vimetaja mambo mahususi kwamba ni lazima yeye apewe; wapi pamesema?
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa taarifa.
SPIKA: Twende tu vizuri mimi na wewe ni mwanasheria, ingawa wengine wote watatutaka sisi wanasheria tukae sawa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru wewe ni Mwanasheria tena mbobevu. Haya makubaliano Bunge leo likipitisha whether pameandikwa ni lazima apewe, ama asipewe haya makubaliano yametoa ulazima yakipitishwa kwamba chochote kitakacho…
SPIKA: Huo ulazima ndio nataka kujua unapoutoa mwanasheria mwenzangu, huo ulazima unatokea wapi? (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, ni hivi labda…
SPIKA: Mimi naweza kukuelewa sana ukisema kwamba yaani huu mkataba ama haya makubaliano yanaweka msingi ili umalizie hoja yako kwa maana ya kwamba kwa sababu haya yanaweka msingi, naishauri Serikali inapoenda kuingia mkataba itazame hapa na hapa na hapa. Ukisema inaweka ulazima hilo mimi siwezi kukukubalia kwa sababu sijapaona humu ndani panapoweka ulazima, sijapaona.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, aah come on Mheshimiwa…
SPIKA: Nani anataka kuzungumza?
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Jerry Silaa.
SPIKA: Sasa taarifa unanipa mimi au Mheshimiwa Halima?
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Halima Mdee.
SPIKA: Ngoja tumalize kwanza hoja yetu, kabisa ni uhuru wa maoni ila leo Bunge hili ni la tofauti linatoa maoni na linatoa elimu kwa umma kwa sababu kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana. Kwa hiyo, tunajadiliana kwa uhuru kabisa leo lazima tutoke humu ndani sisi wenyewe tukiwa tumeelewana, Mheshimiwa Halima. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa maneno yako mwenyewe kwamba mkataba huu ama makubaliano hayo yakipitishwa yanaweka msingi, na naweka msisitizo yanaweka msingi na huo msingi unatakiwa uzingatiwe kwenye sheria ama mikataba mingine yoyote midogo midogo itakayokuja. (Makofi)
Kwa mantiki hiyo kama msingi una matatizo na nashukuru Profesa hapa wakati anazungumza amesema kama kuna matatizo maana yake tunajua kuna matatizo…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, tunapaswa kukubali kwamba…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, hilo la kwanza, la pili,…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie.
SPIKA: Inatokea wapi taarifa?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie.
TAARIFA
SPIKA: Aah Mheshimiwa Patrobass Katambi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kumkumbusha na kumpa taarifa Mheshimiwa Halima msomi mwenzangu katika kile kwenye suala la msingi ambalo anausema, ni vizuri akajua all contracts are agreements, but not all agreement are contracts. Kwa sababu msingi wake ni kwamba ukisoma hayo anayoyaeleza, ukisoma article one ya sheria hii ambayo itasomwa pamoja na kifungu cha tano utaangalia pia na huku kwenye appendix kwenye phase I ndipo utapata tafsiri ya pamoja kwenye hili. Hata kwenye eneo ambalo amezungumza kuhusu ardhi ukienda kwenye interpretation inaeleza kwamba excluding…
SPIKA: Haya ahsante sana kwa sababu taarifa ni moja, umechagua ile ya sehemu ya kwanza, hii ni sehemu ya pili ahsante sana. Mheshimiwa Halima Mdee unaipokea taarifa hiyo.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwenye appendix hiyo hiyo ambayo inatokana na hiyo scope phase II imejumuisha ports zingine imejumuisha maziwa na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Spika, nazungumza mawanda…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa bandari ama taarifa ya bandari.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, tuna bandari kadhaa, kama hamtaki tuchangie basi mseme.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane tusikilizane, tusikilizane taarifa hiyo itakuwa ni taarifa ya tatu nafikiri sio, ni taarifa ya tatu na ya mwisho.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, ya pili hujanipa.
SPIKA: Sasa siwezi kuwapa wote wawili; Mheshimiwa Naibu Waziri.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, analolizungumza Mheshimiwa Halima la scope ya nafasi ya pili maana yake ni kwamba sisi tukishaingia makubaliano Tanzania na Dubai, tukishawapa hawa DP World wakifanya, tukijiridhisha, tukatathmini, tukajua wanaweza kufanya vizuri, tuna uwezo wa kuwapa nafasi. Tukiona hawawezi tuna uwezo wa kuwapa kampuni zingine zikafanya kazi hiyo, kwa hiyo asipotoshe, aseme vizuri. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, analolisema yeye analisema yeye, halipo hapa. Nimesema article four inazungumzia scope imerejea appendix I, appendix I ina phase mbili; phase ya kwanza ni hiyo niliyozungumza, phase ya pili, two inasema; development, management and operation of additional sea and/or lakes ports.
Mheshimiwa Spika, mawanda yamekuwa mapana kwa bandari ambazo tunazo, Bahari ya Hindi ukiacha hiyo ya Dar es Salaam, kwa sababu hili suala sio la Dar es Salaam, ni Dar es Salaam na bandari nyingine, Bahari ya Hindi tuna bandari 12, Ziwa Victoria tuna bandari 24, Ziwa Tanganyika tuna bandari 19, Ziwa Nyasa tuna bandari 11 hizi ni zile ambazo zimekamilika kisheria. Kwa hiyo, tukisema hili jambo ni la nchi linahusisha bandari, maziwa 66. Kwa hiyo, iko mbele kwa kisheria, ukija ambazo… (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Halima, hayo maeneo yote ni katika huu mkataba, yaani kwa maana ya kwamba Tanzania na Dubai moja?
MHE. HALIMA J. MDEE: Yes, mkataba huu…
SPIKA: Wapi pamesema?
MHE. HALIMA J. MDEE: Hawaja mention, wametoa ruhusa ya jumla...
SPIKA: Sasa unaona hiyo ndiyo changamoto? Kama hawajataja mbona una-speculate?
MHE. HALIMA J. MDEE: Nina speculate kwa sababu mimi ninaona mbele. Ninaona mbele kwa sababu gani? No, no, no naomba tusikilizane, naomba tusikilizane. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Halima ngoja, ngoja, ngoja muda ninaozungumza na wewe naulinda usiwe na wasiwasi, muda ninaozungumza na wewe ninaulinda.
Waheshimiwa Wabunge, tuelewane vizuri hili kwa sababu nilishasema mwanzo kwa hiyo nitazungumza nikiwa nimekaa. Kanuni zetu, Kanuni ya 111 inasema hivi; “Majadiliano wakati wa kujadili hoja ya kuridhia mkataba yatahusu masharti ya mkataba husika.” (Makofi)
Kwa hiyo, hakuna mkataba nje wa haya unaoweza kuzungumziwa kwenye ngazi hii, lakini nimwelewe yeye anasema kwamba anaona mbali. Kwa hiyo, anatoa maoni yake Waheshimiwa muyasikilize upande wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Halima Mdee.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nisikilize, unajua vitu vingine vinachosha. (Kicheko)
Kwa hiyo, mimi niseme tu mkataba huu tofauti na wengi wanavyosema kwanza haufanani kabisa na Mkataba wa TICTS, wala usifananishe, kwa sababu wa TICTS zilikuwa zinahusu zile berth nne, hii ni kubwa na ni pana kuliko TICTS. Sasa kama huu mkataba unagusa Mtwara, unagusa Dar es Salaam, unagusa Tanga, unagusa Mwanza, unagusa Kigoma na Lake Tanganyika ipo na Lake Nyasa, Lake Victoria ipo kwa nini lisizungumzwe kwa mapana yake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili kuna hiki kitu kinaitwa Exclusive Economic Zones,kwa taarifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Halima, nilikuwa najishawishi kukuongeza muda lakini sasa namna unavyosema mkataba huu unahusisha hizo bandari na kifungu huna, unasema unawaza baadaye kwa kweli kengele ya pili imeishagonga sekunde thelathini malizia sentensi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, ulisema unanilindia muda wangu...
SPIKA: Nimeshaulinda.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nasema hivi mkataba huu hili suala serious sana, na nilisema wakati ninaanza tukipitisha leo tuna nafasi ya kubadilisha, lakini hatutabadilisha, tukipitisha leo maana yake huu unaenda kuwa mkataba ama makubaliano ya Kimataifa ambayo yako legally binded. Kwa hiyo, chochote kilichotajwa humu kiujumla jumla kwa sababu kimetajwa kiujumla jumla, kinachohusu ports zetu zote kinahusika…
SPIKA: Mheshimiwa Halima, muda wako umekwisha, ahsante sana. (Makofi)