Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, na mimi pia nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia maoni yangu kwenye Azimio hili la Bunge ambalo tunategemea kulipitisha muda mchache unaokuja.
Mheshimiwa Spika, labda mimi nianze pia kama wengine waliochnagia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanaya ya uwekezaji. Nakumbuka mwaka jana kwenye Dubai Expo ilisainiwa Memorandum of Understanding takribani 35 yenye thamani ya trilioni 17.5. Zimesaini Wizara nyingi tu, Wizara ya Nishati ilisaini na Wizara nyinyine. Sasa tunapoona mikataba hii inatekelezwa na ilisainiwa Watanzania tukajulishwa tukafurahi halafu wananyanyuka wengine wanaanza kusema imekosewa nadhani iko haja ya kuelimishana vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia nichukue nafasi hii kuomba sana Watanzania, hili Bunge ni Bunge lao, wametutuma humu kwa ajili ya kuwawakilisha, yapo mambo mengi sana yamesemwa huko nje tumeyasikia na wamesikilizwa kwenye mitandao na sehemu nyingine. Tuwasihi watupe nafasi na sisi pia, maana kama wametuamini kama wawakilishi wao kwenye kupitisha miradi ya maendeleo, kwenye kufanya uwakilishi ambao wamekuwa wanategemea tunaufanya vuizuri na kwenye hili pia watupe nafasi ya kutusikiliza na kutuamini. Siyo pale tunapochangia mitandao iko macho, Bunge la CCM, Bunge la hivi hapana, Bunge la CCM hili limejenga madarasa, limefanya shughuli nyingine zote ambazo zinaendelea watupe nafasi tutoe ushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya haya, mimi kwa upande wangu ni engineer kwa hiyo nitaenda zaidi kwenye vitu vyangu vya kihandisi ambavyo vinahusu bandari, mambo haya mengine ya mikataba wengi mmeongea sana kwa kiasi kikubwa mimi nataka nuiongelee stage hii ya engineering na hasa mambo haya ya uhandisi ambayo yanafanyika pale.
Mheshimiwa Spika, wengi kwanza wameuliza kile kiambatanisho au appendix number one. Naielezea appendix number one tu kwa haraka ya maeneo yale ya kimkakati ambayo uki–refer article namba tano right to develop, manage or operate. Kwa hiyo, kuna mojawapo kati ya hao yanaweza yakafanyika. Wameelezea appendix namba moja na specifically phase one. Kwa hiyo, ukiangalia scope ilitaja appendix yote, lakini development inataja phase one ya appendix ile. Kwa hiyo, phase two ukija kuisoma ni pale TPA atakapoamua ndio maana kule mwisho ukisoma phase two kwa mwisho, mambo ya maziwa mambo ya nini endapo TPA mwenyewe ataamua atawashirikisha. Kwa hiyo, siyo sehemu ya scope. Kwa hiyo, tukienda namba tano hii ndiyo inayoelezea maeneo ambayo tutashirikiana ambayo amepewa haki yeye ya kwamba amepewa ile exclusive kwa phase one for twelve months, sasa wengi walikuwa wanauliza hapa.
Mheshimiwa Spika, kwanza ukiongelea phase one ni sehemu ambayo nchi hii tumewekeza kwa kiasi kikubwa pale, lakini ukweli uliopo ni kwamba hatukuwa na vifaa kwenye bandari hii. Tumechimba kina cha bandari yetu imefika mita 15 leo kina kilipo unaweza ukashindana na Mombasa. Mombasa nao wana mita 15, tulikuwa na mita 11 sasa tumeenda mita 15. Gati Namba 8 mapaka 11bado lina mita 11. Mwekezaji huyu Gati Namba 8 mpaka 11 kuna vifaa vilivyokuwa na mwekezaji yule aliyepita, huwezi kumleta mtu ukamuweka kwenye sehemu ambayo tayari una vifaa, lakini kwa sababu sisi upande wa kwetu pamoja na kwamba tulikuwa na kina cha mita 11 tulikuwa tuna-miss vifaa vingi sana.
Mheshimiwa Spika, mimi nikiongea hapa sehemu hii tunahitaji tuwe na ship to shore gantry crane sita, lakini tulikuwepo nayo moja na gantry crane moja inauzwa shilingi bilioni 42 za Kitanzania. Tulitakiwa tuwe na rubber tag, gantry crane ziko 20 tulizotakiwa tuwe nazo, tunazo mbili tu. Vifaa vyote nilikuwa nimepiga hapa hesabu na moja inauzwa bilioni saba. Ukienda kwenye mobile harbor crane zinatakiwa ziwe 11 tulikuwa nazo sita, moja inauzwa shilingi bilioni 15 kwa haraka na hesabu za kawaida tu za haraka haraka tunahitahji uwekezaji wa vifaa vya shilingi bilioni 435 sehemu hii tu ambayo mmempa huyu mtu aje kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sehemu hii ilikuwa muhimu mpe yeye aje na vifaa aje awekeze. Hatuwezi kwenda benki kuchukua shilingi bilioni 435 unaenda kuweka pale halafu unampa mtu aende kwenye kina kifupi. Kina hiki cha mita 15 leo tuko kwenye position ya kushindana na Bandari ya Mombasa. Meli kubwa zilizokuwa haziwezi kuja hapa zinashusha Mombasa zitaanza kuja hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo cha kwanza efficiency ya bandari yetu inakwenda kuongezeka kwa hili tu. Nadhani niliweke sawa hilo ndio maana nikasema ile exclusivity tunayosema kwanza ni ya twelve months ndugu zangu. Tangu kusainiwa mkataba huu, tuliposimama hapa exclusivity ya phase one kwao imebaki ikifika tarehe 28 Oktoba ule uhalali wa kwao wa kutoa phase one walioi-operate wao utakuwa umeisha endapo hatujakubaliana. Kwa hiyo itakuwa wazi kwa TPA kuweza kutafuta wawekezaji wengine au yeye mwenyewe aombe, lakini bila exclusivity, liko wazi hili.
Mheshimiwa Spika, sasa sielewe wanasheria wanakwama wapi wanatafsiri vitu vingine ambavyo havipo. Kwa hiyo mimi niombe Watanzania wanaotusikiliza huko nje muelewe Bunge hili lina wanasheria, Bunge hili lina wahandisi, Bunge hili lina madaktari, hatuwezi kwenda kupeleka nchi sehemu ambayo sisi wengine bado ni vijana wadogo tunataka tuone Taifa hili likisonga huku tuki-enjoy na watoto wetu na vizazi vyetu vikiwa vinaenda mbele. (Makofi)
Kwa hiyo tuombe hili tuwe na imani na Bunge hili tuwe na imani na Serikali yetu, kuna wengine wamenda mbali zaidi anasema mkataba huu huwezi kujitoa, lakini vifungu hivi viko wazi.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu umeelezewa kabisa kwamba duration and determination iko hapa namba 23 imeeleza; subject to paragraph two ukienda namba two hii the expiration of all HGAs and all projects agreements subject to any additional or extension, ikisha-expire hii mikataba midogo tunayosaini huu mkataba mkubwa, hii agreement hii kubwa haina kazi tena it is obvious na iko hapa, sasa hatuelewi hawa watu haya mambo wanayatoa wapi na tumeenda mbali zaidi mtu anasema huu mkataba huwezi kujitoa mkataba mpaka umekupa room ya kufanya amendment article 22 kwamba kama kuna jambo hata leo kama limeshapita bado states wanaweza wakakaa wakafanya amendments ya baadhi ya mambo, ipo hapa.
Mheshimiwa Spika, tukienda article 23 namba nne ambayo imeongelewa sana na watu wengi, mimi siyo mwanasheria lakini usisome ukaishia hapa tu, kulikuwa na kipengele kimeendelea; notwithstanding the foregoing, any dispute between State Parties in respect of such circumstances shall be dealt with in accordance with the requirements of Article 20 of this Agreement. Unarudi nyuma article 20 inasemaje; kutakuwa na mazungumzo kati ya viongozi wetu endapo tutashindwana kwenye hiyo article 20 ndio twende kwenye arbitration. Sasa kwa nini mtu anasema mkataba huu ni kifungo hauwezi kutoka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi tu sasa niongee with experience pia. Kwa nini tumeenda Dubai? Hilo ndiyo jambo la muhimu pia wananchi wajue why Dubai today?
Mheshimiwa Spika, wote mnajua mizigo inayokuja kwenye Bandari ya Dar es Salaam, wafanyabiashara wanajua, sehemu kubwa ya mizigo yetu unapoongelea kutoa kontena moja Shanghai, China kuja Dar es Salaam, 20 feet kontena inaenda dola 2,500 mpaka dola 2,800 na kontena la 40 feet mpaka inaenda dola 4,500. Unapoongelea kutoa mzigo ule ule kuja Mombasa 20 feet dola 1,200 wao kati ya 20 feet na 40 feet kontena, zinatofautiana kati ya dola 300 na dola 400; hawafikishi kontena hata la 40 feet kwa dola 2,000; utashindana vipi mtu anayepeleka mzigo Congo atakubali kuleta Dar es Salaam hapa?
Mheshimiwa Spika, ndugu zangu kama tunaipenda hii nchi tuache siasa, mimi siyo mwanasiasa, mimi ni mhandisi mambo yangu yamenyooka hivi. Mbili jumlisha mbili ni nne haibadiliki. Tukitaka kwenda mbele tuache siasa, tukileta siasa kwenye masuala makubwa kama ya Taifa hili, ndugu zangu Taifa hili tunaliangamiza, unapoenda mbele kwa nini mizigo yetu imekuwa inachelewa kwa sababu cha kwanza mfanyabiashara anachotaka other than saving cost anachotaka na mzigo aupate kwa uharaka zaidi. Wote ni mashahidi trans-shipment ya mizigo ya Tanznaia ni Jebel Ali Dubai. Mizigo mingi inayotoka Bara la Asia, inayotoka Ulaya mingi inapita Dubai Jebel Ali, ikishafika Jebel Ali ndio wanai–consolidate kutafuta meli ya kuileta huku kwetu. Mizigo imekuwa ikichelewa Jebel Ali not less than three to two weeks sometimes. Mfanyabiashara ambaye ameagiza mgigo mwenzake ameshapokea Kenya yeye yuko Congo anasubiira mzigo umekaa Dubai wiki mbili unauleta Dar es Salaam, utoke Dar es Salaam uje huku, nani atapitishia mizigo kwenye bandari hii?
Mheshimiwa Spika, no wonder ukisema wenzetu wale majirani zetu kwenye nchi wanazozihudumia mpaka wameweka kwamba na Tanzania wanaihudumia, sasa unaposoma profile ya mwenzetu mwenye bandari kama sisi, competitor wetu, anasema anatuhudumia na sisi kama Taifa na sisi ndiyo tuna bandari maana yake ni nini? Anatuondolea baishara, sometimes tusiingie kwneye mkumbo.
Mheshimiwa Spika, ameongea vizuri sana Mheshimiwa Jerry pale, sisi tunaowakilisha hii nchi kwenye Mabunge ya nje tunajua upinzani tulionao na wenzetu wa jirani. Ni lazima kama Taifa ifikie stage tusimame, hawezi kuja mtu anayeongea lafudhi ya nchi jirani, mnamuita mmbobezi na mtaalamu wa sheria, mlitaka Bunge tujadili kitu kabla ya kuja humu? Leo kimekuja, Serikali imesema, Wabunge tumeona kazi imeishia hapa leo, tusingeweza kwenda kwenye mitandao Wabunge na Serikali tukaanza kujibu kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi kwa kuomba tunapoenda kumalizia hasa kwenye utekelezaji, nimefika katika bandari ya Suez nchini Misri mwaka 2019 pale kwenye Suez Special Economic Zone. Wale watu wamefanya uwekezaji mkubwa sana, pale kazi anayofanya anafanya APM, hii kazi anakuja kufanya DP World hapa Suez anafanya APM. APM ni kampuni ya Uholanzi kutoka Maersk Group, wao walichokifanya...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa Muda wa Mzungumzaji)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, namalizia; wao wamekodisha miaka 45 kwenye upande ule wa makubaliano, sasa mimi nilikuwa nataka niweke maoni. Maoni yangu ni mawili; cha kwanza, kwenye contracts ambazo mnaenda kuingia kati ya TPA na DP World tunaomba tupate specific time, nilikuwa na suggest not more than 25 years kwa kuanzia na mikataba iwe revisited after every five years.
SPIKA: Mheshimiwa muda wako umeisha, ahsante sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.