Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa hii, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama hapa leo.

Mheshimiwa Spika, nami naomba niwe miongoni mwa wachangiaji kwenye hoja hii ya kuridhia kuanzisha mahusiano ya nchi hizi mbili; Tanzania na Dubai kwa ajili ya suala la uwekezaji kwenye bandari yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwanza mimi naona kwamba jambo hili limechelewa, yaani kwamba mchakato huu umechelewa kuanzishwa. Nilikuwa nategemea jambo hili lingekuja mapema sana, mara tu baada ya kuanza ujenzi wa Standard Gauge Railway. Naomba tu niseme kwamba katika bandari yetu ya Tanzania mpaka sasa hivi, pamoja na kuwa bandari yetu hii imezungukwa na nchi mbalimbali ambazo kimsingi ndio wateja wetu; Uganda, Congo, Zambia, Malawi, Mozambique, Rwanda na Burundi, tuna bahati sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niseme mpaka sasa hivi katika bandari yetu ya Tanzania, uwezo wa bandari yetu kuleta makontena kwa mwaka mmoja, mwaka 2021/2022 makontena ni 820 tu ambayo yaliweza kupakuliwa kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam, ukilinganisha na nchi ya Dubai ambako ndiko mwekezaji huyu tunayemzungumzia DP World yeye yupo na anafanya kazi, Bandari ya Dubai sasa hivi inatoa makontena 24,000,000 kwa mwaka. Kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba wenzetu wako mbali sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuwa tayari tumeshawekeza fedha nyingi sana kwenye Standard Gauge Railway, zaidi ya trilioni sita ambazo zinakwenda kuwekezwa kwenye SGR. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba iko haja ya kufanya maandalizi mazuri ili kutengeneza mnyororo mzuri kwamba bandari yetu ya Dar es Salaam iweze kuongezewa uwezo na hatimaye sasa Standard Gauge Railway itakapokuwa tayari imeunganishwa vipande vyote sasa iweze kupokea mzigo kutoka kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam na kusafirisha kwenye nchi hizo nilizozitaja.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo mimi nataka niseme kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana. Wenzangu wamesema, lakini na mimi naomba niseme kidogo.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upotoshaji kwamba kwenye huu mkataba ambao tunauzungumzia leo hakutakuwa na marekebisho yoyote. Mimi naomba wapotoshaji hao wasifanye jambo hilo kwa sababu wanafanya kwa makusudi na wanatambua kwamba kwenye ule mkataba kuna Ibara ya 22 ambayo imejipambanua vizuri, imewekwa wazi kwamba marekebisho yoyote yanaweza yakafanyika wakati wowote.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwenye suala la TEHAMA; kwenye suala hili ni sehemu nyeti sana, kwa hiyo, ninashauri kwenye eneo la TEHAMA hawa wenzetu eGA wawepo, lakini pia TCRA wawepo kwa sababu mifumo hii tukiiacha iwe free kwa mwekezaji itakuwa ni hatari sana kwa usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine naomba niseme, Watanzania wenzangu, Watanzania sisi kama ambavyo mnatambua mmetupa ridhaa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuko hapa kwa niaba yenu kuhakikisha kwamba mambo yote yanakwenda vizuri na hakuna jambo litakaloharibika, kama ambavyo mlituamini tunaomba muendelee kutuamini. Lakini kama ambavyo mnamwamini Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaomba pia muendelee kumwamini kwa sababu anasimamia misingi ya sheria na misingi ya utawala bora, hakuna kitu chochote kitakachokwenda tofauti.

Mheshimiwa Spika, lakini pia umoja wetu ni lazima tuuzingatie sana, tusigawike eti kwa sababu ya suala hili la bandari hii ambayo inakwenda kupata mwekezaji baada ya michakato hii yote kwenda.

Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe sana Mheshimiwa Rais wangu, kwa kweli asitolewe kweli reli ya maandalizi na mchakato huu wa kuelekea uwekezaji mkubwa kwa Taifa hili. Wapo wanasiasa uchwara ambao wanapita kila maeneo huko kupotosha na wana kazi maalum ya kuhakikisha kwamba wanamtoa Mheshimiwa Rais wetu kwenye reli ili asiweze kusimama imara katika suala hili la uwekezaji wa bandari kama ambavyo nimezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika wapo madalali; hawa madalali wamekuwa wakitusumbua sana katika nchi yetu na wengine ni majirani zetu tuwaombe watuachie nchi yetu tufanye shughuli zetu kwa usalama na amani kwa sababu hata wakati tulipokuwa tuna mchakato wa Ngorongoro Conservation kuhamisha wananchi kule kuwapeleka kule Tanga napo ambao waliingilia, wakaanza kuleta kelele, wakaanza kuleta vurugu. Hatuhitaji mtu yeyote aje atuingilie kwenye nchi yetu, mwacheni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan afanye kazi yake vizuri ipasavyo na kwa vyovyote vile wanatuonea wivu kwa sababu Mheshimiwa Rais wetu yuko imara, anafanya kazi vizuri sana, amesimama vizuri sana katika kufungua masuala yote ya kiuchumi katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaaminim kabisa uwekezaji huu ukifanyika katika nchi yetu ya Tanzania maana yake tunaenda kuingiza pesa nyingi sana. Kwa hiyo, ni lazima wawe na wivu katika masuala mazima ya kiuchumi na hawa madalali wa kisiasa tunawaomba sana kama wamechukuliwa, wamelipwa fedha basi waangalie mambo yao wasiingilie masuala haya ambayo ni masuala yenye afya katika uchumi wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo machache naomba nichukue nafasi hii kukushukuru na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)