Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kupata nafasi ya kuweza kuchangia bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, mimi nitazungumza zaidi kwenye kilimo; tunafahamu sote kwamba tulikuwa na slogan kama Taifa kwamba kilimo ni uti wa mgongo na bado hata kama hatutaji lakini kiekweli kilimo ndio kinashiikilia maisha ya Watanzania nusu walioko hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu kilimo cha kizamani cha kutegemea mvua au kutumia akili za babu zetu kimepitwa na wakati. Tunahitaji kuwa na kilimo cha kitafiti. Kule Mbeya tuna Chuo cha Kilimo Uyole takribani zaidi ya miaka minne, mitano walikuwa hawajapata fedha kwa ajili ya utafiti na sisi tunaamini katika utafiti.
Mheshimiwa Waziri ni lazima tuwekeze katika elimu kwa watafiti wetu ambao wamekwishakusoma ili kuweza kuwasaidia wakulima wetu. Ninaomba sana sana Wizara yako Mheshimiwa Waziri imeweze kutoa fedha kwa wakati hasa pale Uyole, lakini tukienda SUA wanahitaji kupata fedha tuweze kufahamu namna gani kama udongo unafaa, tunafahamu tunahitaji mitamba mizuri, tunahitaji wawe na fedha ili wafanye utafiti. Mheshimiwa Waziri kwa hilo naomba uwekeze sana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia utafiti huo huo leo hii tuna kilimo cha parachichi. Kilimo hiki kimeleta watu wengi sana toka nje ya nchi sitataja kwa ajili ya mambo ya kidiplomasia, lakini mwisho wa siku kwenye mashamba, vijijini unakutana na wateja ambao wanakuja kununua parachichi hizi. Hicho ni kitu kizuri mimi sikatai, lakini mwisho wa siku tunapata kiasi gani fedha za kigeni kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali inasimamia hawa wateja wanaokuja, wanatenda haki kwa wakulima wetu? Tumekuwa na tabia mbaya sana ambayo inafanywa na wanunuzi hawa, wananunua parachichi halafu wanaziita reject, ni nani anasimamia kama kweli hizi ni reject? Kwa sababu babu anayelima parachichi kijijini kule Rungwe na sehemu zingine za Njombe hawezi kujua kama hii ni reject au siyo reject, kwa sababu yeye kama mnunuzi anaamua kusema hii ni reject na utakuta hiyo reject ni kubwa kuliko yale mazuri na anaondoka na ile reject Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba sana sana usimamizi kwa wakulima wa parachichi, tunaona kuna madalali wengi sana hapo katikati, tunaomba msimamie kama Serikali. Mwisho wa siku kazi hii ni ngumu ambayo mwananchi wa kawaida amejiwekeza, amelima, ametaka kupata faida na familia yake anakuja dalali anakubaliana na mnunuzi kihuni na mwisho wa siku watu wetu hawapati haki anayostahili kuipata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri tunajua kabisa tunasema parachichi ni dhahabu ya kijani, tunafahamu kabisa kule kwetu tulipotoka, tumetoka katika mia zote parachichi kumi kwa shilingi 1,000 sasa hivi angalau zimeongezeka bei, lakini bado Wizara ya Fedha mtusaidie…
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, hawa watu wanapokwenda kuagiza parachichi…
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Sophia ulipaswa uendelee kuongea nilitaka umalize sentensi yako. Maadam umekaa ngoja upokee basi taarifa manake unao huo utayari, Mheshimiwa Cosato David Chumi.
TAARIFA
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi naomba kumpa taarifa mzungumzaji dada yangu Sophia kwamba kwa muktadha huo kama Taifa maana na mimi natoka tunakolima parachichi, tunahitaji kuwa na kitu kama bodi kwa ajili ya ku-regulate zao hili la parachichi. Bodi ya Parachichi kama ambavyo tuna bodi katika mazao mengine.
SPIKA: Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda unapokea taarifa hiyo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ninaipokea taarifa hii kwa mikono miwili na naiongezea Mheshimiwa Waziri uichukue hiyo taarifa ya Mheshimiwa Chumi na kuifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kabisa kwamba parachichi tumesema ni dhahabu ya kijani, inawapatia wananchi wetu fedha, lakini kumekuwa kuna tozo nyingi ambazo hazina maana kwa mkulima wa kawaida. Ni lazima Halmashauri zetu ijapokuwa sisi Wabunge ni Madiwani katika Halmashauri zetu, lakini tuwe tuna uniform moja ya utozaji wa parachichi. Ukienda Njombe wana aina yao ya utozaji, ukienda Rungwe hivyo hivyo. Tunataka sasa na ndio maana ya bodi sasa ikiwepo inaweza ikatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii wale wanaobeba zile parachichi wenye magari yale ya cooling system yale wanasimamishwa kila mahali, kila wakati na tozo nyingi sana. Mwisho wa siku tutakimbiwa na hawa wanunuzi na wakulima wetu watalima tutarudi kule kwenye mia zote tunakuwa hatujafanya sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba sana, sana, sana, Mheshimiwa Waziri ninarudia tena kusisitiza suala la reject ninaomba Halmashauri uziambie zisimamie watu wetu waweze kupata haki yao, mambo ya reject iwe kweli, mtu wa Serikali pale halmashauri amtetee mkulima ili kujua kama kweli kaonewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakuja kwenye suala la chai, ninafahamu Mheshimiwa Bashe ulikuwa na kikao kwa ajili ya kuhakikisha tunakuwa na mnada kwa ajili ya chai. Pia tunahitaji maabara, lakini mwisho wa siku tunataka tufenye zao la chai liwe la thamani zaidi. Chai inanyweka nchini, chai inanyweka dunia nzima. Leo hii kuna nchi za Ulaya zinanunua sana chai, tunaomba tuwekeze zaidi. Wenzetu wa nchi za jirani, mkulima wa chai ni tajiri lakini leo mkulima wa chai kwenye mikoa yetu hata kumiliki baiskeli ni kazi. (Makofi)
Kwa hiyo, sisi kama Taifa tunahitaji tuwatetee watu wetu, ninafahamu juhudi za Waziri wa Kilimo anazozifanya kwa zao la chai, lakini bado tunahitaji kuongeza nguvu, tunahitaji kuwa na mnada wa chai ambao mlituahidi kama utakuwepo labda unaweza ukatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba sana kuzungumzia suala la kahawa. Tunafahamu kahawa baada ya petroli duniani kunyweka, kahawa inatumia sana sana sana na wananchi dunia nzima. Tunaomba kahawa ruzuku iwepo kwa wakulima wa kahawa pia tozo ndogo ndogo kwa wanao-export kahawa zipungue ili tuwe sawa na wenzetu wa nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, tunapoingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tunahitaji kuwa na uwiano sawa hata tunapoingia kwenye mambo ya ushindani tusiwe tunakabwa sana sisi kwa kodi nyingi kuliko wenzetu ambao wako mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zao la vanilla Mheshimiwa Waziri; vanilla ni zao zuri lakini limeleta utapeli mwingi sana katika Taifa hili. Sote tunafahamu na tunalalamika katika Bunge hili. Wanakuja kuelezea vanilla inauzwa milioni moja, mkulima analima vanilla halafu mwisho wa siku inauzwa shilingi 25,000 hadi 30,000. Naomba msimamie hawa watu wanaojiita wao ndio viongozi wa vanilla wanaposema uongo Serikali iweze kupambana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie barabara za vijijini. Leo hii TARURA tunaomba muiongezee fedha na hasa maeneo ya milimani yenye Nyanda za Juu Kusini kule kwetu Mbeya kwa mfano, fedha huwezi kumpa sawa na mtu ambaye anatoka sehemu ambayo hakuna milima. Tunafahamu maeneo ya kwetu Mheshimiwa Waziri yana mvua za mwaka mzima almost, barabara zinaharibika zaidi na kwetu ndio tunalima zaidi na tunalisha Taifa hili. Tunaomba TARURA walioko Nyanda za Juu Kusini kote waongezewe fedha kwa kuwa barabara zao zina changamoto nyingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka kwenye barabara niende kwenye TAZARA. Mheshimiwa Waziri TAZARA ni reli ambayo inasaidia sana hasa watu wa Nyanda za Juu Kusini. Tunafahamu mazao yetu hata bila ya kupitia kwenye malori wakati mwingine tunatumia treni ya TAZARA, lakini bado Sheria ya TAZARA inatubana. Tunafahamu kwamba ilianzishwa kwa Zambia na Tanzania, lakini tunaona wenzetu kidogo kama wanaenda wanasuasua. Tunaomba muweze kuibadilisha TAZARA ikibidi ipate wawekezaji kwa kupitia Tanzania na nchi yetu iweze kunufaika kwa sababu bado sisi tunauhitaji sana na reli hii. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri tuisimamie kirahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie fedha za mikopo ya wanawake. Ninafahamu nia njema ya Serikali ya kusema sasa fedha zipite kwenye mabenki, lakini bado ninalo swali. Kule kwetu vijijini maana watu wengi wanaamini benki inakuwa na utaratibu wake, ili upate mkopo benki lazima uwe na document, uwe umesoma na ujaziwe na vitu viko kisomi. Je, mtaweka utaratibu wa kibenki kwa maana ya kupitisha fedha lakini mfumo ule ule wa upatikanaji wa vikundi au mtafanyaje?
Mheshimiwa Spika, si tu hivyo bado tunaomba mfanye haraka kwa sababu mnavyochelewa kuleta majibu haraka kuna wanawake walikuwa wameshakopa ambao tayari wana mikopo hiyo pia wanaendeleza biashara kwa sasa wamesimama hawafanyi kitu chochote. Tunaomba Serikali ije kwa haraka sana iweze kuwarudishia hizo fedha kama mfumo wa benki, lakini uwe kwa haraka na waweze kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nitaunga hoja nikiona kama umekuja na majibu haya ambayo mimi nimeyasema, ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)