Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi pia ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa kupata hii nafasi ya leo, lakini pia nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa yale ambayo ameyafanya kwenye nchi yetu, na pia tujipongeze sisi ma-baba wote kwa sababu, jana ilikuwa siku ya ma-baba duniani maana ingekuwa siku ya ma-mama ingekuwa hatari na mimi ni baba bora, naomba nijipongeze kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kidogo sisi Wana-Morogoro Vijijini tuna jambo letu, tuna malalamiko yetu, nikikumbuka wiki mbili zilizopita Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alisimama akatoa ahadi kwamba mwezi huu wa sita watasaini mikataba kwa ajili ya barabara. Jana wananchi wa Morogoro Vijijini wote wameandamana kwamba Mheshimiwa ulisimama na ukaongea na tulimsikia Waziri akiongea kwamba barabara zinakwenda kusainiwa mwezi huu wa sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukiangalia tayari mwezi upo mkiani huu, unaondoka. Wenzetu jana wamesaini, sisi Wana-Morogoro Vijijini hatujasaini, lakini tunajua labda shida yake ipo kwa Waziri mwenye dhamana ya fedha, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, niangalie kijana wako, niangalie nilivyo mdogo, niangalie majukumu ya lawama ya barabara ya Bigwa – Kisaki ni makubwa sana. Mheshimiwa Rais kwa mapenzi yake ya dhati ametugawia kilometa 78 na nikinukuu maneno yako uliyoongea juzi jambo jema ni la mama, mabaya ni ya kwenu. Sasa ikiwa hili halifanyiki wabaya ni ninyi, sio Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu naomba ungemwambia Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Mbarawa hili tatizo la kutokuwa na barabara ya Bigwa – Kisaki na mnakuja hapa mbele mnatuahidi mtasaini na hamfanyi, mnakwenda kumdhalilisha mama yangu na mimi nimesema juzi mimi ndio kipenzi cha Mama Samia, mnataka kunivunja moyo mama yangu asinipende jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi siwezi kupiga sarakasi humu ndani, siwezi kupiga msamba humu ndani, labda ni-rap tu ili wafurahi, mimi nitachana humu ndani kwa sababu hatuwezi kuwa tunazungumza jambo moja lilelile kila siku. Suala la barabara Mheshimiwa Rais ameshatoa na kama ni fedha Mheshimiwa Mwigulu unayo, tupatie tuanze kujenga barabara ya Bigwa - Kisaki, hii ni aibu ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza barabara nizungumze kuhusu michezo kidogo. Rais wetu wa Awamu ya Sita ambaye…

Mheshimiwa Spika, kama anataka kuongea muache anijibu roho yangu ifurahi.

SPIKA: Kwa sababu mimi hupenda kutenda haki, nikishamruhusu akujibu wewe na Wabunge wengine watataka kujibiwa. Kwa hiyo, tumpe nafasi ayakusanye, atayajibu. Si ndio Mheshimiwa eeh? Haya, ahsante sana. (Makofi)

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, Wabunge wengine wasubirie kipenzi cha mama kinaongea. Ungemuacha ajibu.

Mheshimiwa Spika, turudi kwenye suala la michezo; Mama Samia ndio raia ambaye ametuonesha mapenzi ya dhati ya kuipenda michezo; Mama Samia ndio Rais ambaye ametuonesha mdau mkubwa na mwekezaji kwenye Wizara ya Michezo. Wiki mbili zilizopita nilivyochangia kwenye Wizara ya Michezo nilizungumza kuhusu ile asilimia tano inayotoka kwenye michezo ya kubashiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais aliona kwamba hii Wizara inapewa pesa ndogo, shilingi bilioni 35 ni pesa mbuzi, basi akaona bora hii asilimia tano ya michezo ya kubashiri inayopatikana iende kwenye Wizara ya Michezo. Mimi nikizungumza nipo kwenye Kamati ya Michezo, hii Wizara imepata shilingi milioni 900 mwezi wa pili mwaka huu na hiyo shilingi milioni 900 iliyopata ni ya mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, narudia tena kunukuu maneno ya Mheshimiwa Waziri; mazuri ni ya Mheshimiwa Rais mabaya ni ya kwao. Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mwigulu Nchemba wewe nchi inatambua mema yako, nchi inatambua mapenzi yako na michezo, mimi nina hofu kubwa sana ukiondoka kwenye hiyo Wizara tutatetereka zaidi. Kama ikiwa leo hii wewe uko hapo tu asilimia tano ya Mama Samia haiendi kwa wakati, kama leo hii uko hapo tu, Mheshimiwa Waziri nimemuhoji juzi kwenye hii asilimia tano mnayopata mchanganuo ukoje? Hajui.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waziri anayepelekewa huo mchele wa shilingi milioni 900 hajui mchanganuo upoje. Na hiyo shilingi milioni 900 mliyopeleka ya mwaka jana huko, mwaka huu mwaka mzima, hii miezi sita, sio kama watu wanaochezesha michezo ya kubashiri hawapeleki hela kwako, bro (brother) mimi nakufahamu wewe ni mchumi, unatazama pesa zaidi, lakini hii Wizara ili tuweze kujibeba inahitaji kuwa na pesa vilevile.

Mheshimiwa Spika, mimi niombe kitu, tunapozungumza kuhusu michezo ya kubashiri ni michezo. Mheshimiwa umekumbatia mzigo mwingi, tunaomba huu mzigo wa michezo ya kubashiri uupeleke kwenye Wizara ya Michezo na ukishindwa kufanya wakati uko hapo, hakuna anayeweza kufanya. Bro (brother) mimi naamini wewe umeikuza Singida Big Star, leo hii una nuru kubwa, basi kaikuze michezo, wapelekee huu mfuko wa michezo ya kubashiri uende kwenye Wizara ya Michezo wawe wana uwezo wa kuamua jambo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kitu kimoja na ninachokiongea naongea kwa fact kwa sababu mimi nimeishi kwenye michezo, maisha yangu nimeyapata kwenye michezo, mbebeshee huu mzigo. Najua wewe ni mtaalamu wa kodi unafikiria nikiwapa Wizara ya Michezo kodi yangu wataniletea?

Mheshimiwa Spika, naamini Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake Mwana FA hawawezi kukuangusha kwenye hilo. Wapelekee michezo ya kubashiri kama ilivyo, hutasikia vilio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaona wenzetu, nchi za wenzetu zinafanya vizuri. Nilikuja na mafano hapa wa nchi kama Senegal imefanya vizuri kwenye michezo ya ndani kwenye timu zote za Taifa kwa sababu Wizara yao inapata pesa nzuri; nimetoa mfano wa nchi kama Uingereza, michezo ya kubashiri yote inaenda kwenye Wizara ya Michezo; nimekuja na mfano wa nchi kama ya Japan, michezo ya kubashiri pesa zote zinakwenda kwenye Wizara ya Michezo; nchi ya Tanzania michezo ya kubashiri iko kwenye Wizara yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunakufahamu wewe ni mchumi, lakini hebu kata hili kidogo ndugu yangu wape Wizara ya Michezo wajiendeshe. Mkikaa kwenye vikao vyenu mnapanga mipango ya kuwagawia shilingi bilioni 35, hiyo shilingi bilioni 35 waendeleze michezo yote.

Mheshimiwa Spika, tunawaona TFF wanateseka kujenga viwanja. Tumeona juzi Tanga pale wakati tunawaangalia kwenye siku ya tuzo, wametuonesha uwekezaji wao, lakini ule uwekezaji unatakiwa kufanywa na Serikali, kufanywa na Wizara. Sasa Mheshimiwa Waziri, kaka yangu na mwanamichezo tunayekutegemea ingawa timu yako imeshapoteza kocha na hivi karibuni za ndani Mayele harudi, kwa hiyo, naona wazi kabisa utaenda kutusaidia, utaenda kusaidia Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri haya maneno nayarudia mara mbilimbili kwa sababu najua siku ya wewe kufungua moyo, siku ya kubeba michezo ya kubashiri kuipeleka kwenye Wizara ya Michezo ndio siku ya Wizara hii ya Michezo kwenda kuisaidia michezo na sanaa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo siwezi kusema naunga mkono hoja mpaka nione anasema nini. Nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri, ahsante. (Makofi)