Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu, na nianze kwanza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyofanya kazi na ambavyo amejitahidi sana katika kutafuta rasilimali fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu kwa ujumla, kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli mmeweza kutafsiri maono ya Mheshimiwa Rais na kuyatekeleza mambo mengi kwa kipindi kifupi. Kazi kubwa mmeifanya, mnastahiki kwa kweli kupongezwa, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaipongeza Wizara kwa sababu ya mambo yafuatayo ambayo yamejitokeza kwenye bajeti, sitaweza kuyasema yote, lakini machache naweza kuyasema.
Mheshimiwa Spika, kwanza, ongezeko la mapato yaani makusanyo yameongezeka kwa kipindi kilichopita mpaka sasa hivi. Mmefanya jitihada kubwa mapato yameongezeka, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa bajeti za sekta za uzalishaji; kilimo, mifugo, uvuvi, bajeti imeongezeka kwa kiwango kikubwa. Haijawahi kutokea, kazi hiyo mmeifanya vizuri, hongereni sana na tunaona kwa mfano kilimo sasa hivi tena bajeti ya mwaka huu inaongezeka inakwenda kufikia shilingi bilioni 970. Kwa kweli hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini mmeleta pendekezo la kuongeza shilingi 100 kwenye mafuta ili kuwa na vyanzo ambavyo vinaeleweka katika kutekeleza miradi ya kimkakati, hili ni jambo la msingi sana. Tunayo miradi mingi ya kimkakati, tulikuwa hatuna vyanzo, sasa hiki tukikifunga yaani tuka-ringfence itasaidia sana katika kutekeleza hii miradi ya kimkakati, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TARURA imeongezewa fedha zaidi ya shilingi bilioni 370 zimeongezeka, lakini tumeshuhudia mapendekezo ya kwamba sasa vyuo vyetu vya ufundi, Chuo cha Dar Tech, Chuo cha MUST – Mbeya na Chuo cha Arusha, sasa watoto wote wanaosoma watapatiwa mikopo. Lengo tupate wataalamu katika nyanja mbalimbali, ni jitihada kubwa sana ambazo mmefanya, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini mmesema mmetenga fedha kwa ajili ya kwenda kuchimba visima/mitambo ya kuchimba visima, hii kwa kweli itachochea sana maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, tumeanzisha Tume ya Mipango; tulishauri Tume ya Mipango ianzishwe, mmesikia kilio, kwa usikivu huo Tume ya Mipango imekwenda kuanza, hii ni hatua kubwa ambayo kwa kweli tumeifanya katika kipindi hiki na mambo mengine mengi ambayo mnakwenda kuyafanya. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na timu yako tunawapa hongera sana kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli mmefanya. Yapo mengi ambayo yapo, hatuwezi kuyasema yote yakaisha, lakini mmeyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nichangie kwenye maeneo angalau mawili, kama muda utaruhusu nitaongezea labda la tatu.
Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni suala la tija; tija kwenye kilimo, tija kwenye mifugo, tija kwenye uvuvi na maeneo mengine, lakini tija kwenye viwanda yetu. Tija bado iko chini sana, lazima tuweke mkakati wa kuongeza tija, tukiongeza tija ndipo pale tutaweza kupata ufanisi na ndipo uchumi wetu utaweza kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kilimo chetu ukiangalia tija ni ndogo mno, uzalishaji ni mdogo mno. Ukienda kwenye ufedhaji tija haipo kabisa. Sasa lazima kama Serikali tuwekeze rasilimali namna tutakavyosaidia kuongeza tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na katika eneo hili Mheshimiwa Waziri huko nyuma tulikuwa na Baraza la Taifa la Tija, sasa lile tuliliondoa. Sasa kwa kuwa Tume ya Mipango imerudi, basi napendekeza na hili Baraza la Taifa la Tija lirudishwe, lianzishwe ili lisaidie katika kuchochea na kuhamasisha kuongeza tija kwenye kilimo, mifugo, viwanda na huduma mablimbali na hii itatusaidia sana katika kujenga uchumi mzuri ambao utakuwa ni imara, naamini hili eneo mtalipa uzito unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu cha tatu ambacho nataka nichangie, sasa hivi sote tunazungumzia kilimo, mifugo na kadhalika, lakini hatuweki mkazo kwenye kuongeza thamani, value addition ya hizo. Hatuwezi kusema tuendelee kuzalisha malighafi, kuzalisha mazao tunauza nje, kufanya nini, sasa hivi dunia imetoka hapo, tujitahidi sasa uzalishaji wetu tuongeze thamani. Kwenye value chain hapa ndipo tunatakiwa tuwekeze sana. Tukifanya hivyo ndipo nchi yetu itaweza kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunazalisha mahindi tunapeleka kwenda kuuza mahindi yakiwa kama mahindi, tunazalisha kahawa tunakwenda kuuza kama kahawa, tuwekeze kwenye kuongeza thamani ya hivyo ili tukauze final products maeneo mbalimbali, na hiyo ndiyo itatusafanya kwamba tupate fedha nyingi, lakini pia uchumi wetu uwe imara na ajira mbalimbali ziongezeke na umaskini katika nchi yetu uweze kupungua. Kwa hiyo, mimi napendekeza hebu tuangalie sana value addition katika products zetu, tukiwekeza hapo itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nilitaka kuchangia na nilitaka kuongeza, kwamba nimeona katika jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Serikali na nimeona kabisa kwamba kwa kweli jitihada ni nyingi zinachukuliwa. Lakini mimi nataka tulipendekeza hapa kipindi kilichopita kwamba katika ufufuaji na uimarishaji wa bandari zetu, tukasema tunataka na Bandari ya Bagamoyo sasa tuijenge, tulipendekeza mwaka jana tukasema ijengwe.
Mheshimiwa Spika, sasa kwenye hili sijaona mkakati wa kusema sasa tunaanza mikakati ya kuijenga Bandari ya Bagamoyo, kwa sababu hii ni rasilimali tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Tunataka zile bandari ziweze kuhudumia maeneo mengine. Tukiimarisha miundombinu hii ya SGR, barabara na maeneo mengine, tunataka sasa bidhaa zisafiri vizuri tuwahudumie nchi za SADC zote, nchi za Kusini mwa Afrika ambazo sisi tuna lango hili kwenye bahari yetu tuweze kuitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nataka nione mkakati, tuna mkakati gani wa kuhakikisha tunatafuta kama ni mwekezaji, kama ni nini, tujenge Bandari ya Bagamoyo ili ishirikiane na bandari zilizopo katika kuweza kuchangia uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, sanjari na hilo, pale Tunduma bado naendelea kilio changu, pale ndiyo lango la SADC, tunaomba pawe na bandari kavu, bandari kavu ile itasaidia sana katika kuweza kutoa huduma katika nchi za SADC, mizigo itasafirishwa kutoka kwenye Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine, ikifika pale basi wale wafanyabiashara watachukua kwa gharama nafuu kuliko namna sasa hivi inavyosafirishwa kwa kutumia magari na barabara zinaharibika na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, lakini zaidi hapo tunaomba mkakati mahususi wa kuimarisha reli ya TAZARA. Reli ya TAZARA ilijengwa ni reli ya uhuru, reli ya siku nyingi, reli ambayo ni muhimu sana katika uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, mlituahidi kuleta sheria hapa kwamba mtabadilisha sasa sheria ili ile TAZARA ambayo inamilikiwa na nchi mbili iweze kuboreshwa, tuweze kuwekeza, iweze kutoa mchango mkubwa. Sasa mpaka sasa hivi sijasikia nini kinaendelea kuhusiana na ufufuaji wa reli ya TAZARA. Tunataka tupate mwelekeo wa Serikali ni nini katika kuhakikisha kwamba kwa kweli tunaifufua TAZARA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, TAZAMA Pipeline ya kusafirisha mafuta nayo ni ya nchi mbili. Tumekuwa tukisafirisha yanakwenda Zambia, sasa hivi wameanza kusafirisha mafuta safi. Sasa mkakati wa Serikali uwepo ili ile TAZAMA Pipeline tusafirishe mafuta kutoka Dar es Salaam, yakifika Mbeya iwepo depot pale, yakifika Tunduma iwepo pale tupunguze gharama za uzalishaji, gharama za ongezeko la mafuta, gharama zile zitapungua, tukiweka pale yatasukumwa kwa TAZAMA, yatafika pale, yatapakuliwa na wafanyabiashara mbalimbali watachukua mafuta katika yale maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi naamini kwamba tukifanya hivyo itatusaidia sana katika kuweza kujenga uchumi wetu imara katika maeneo hayo, lakini pia tutapunguza gharama kwa watumiaji wa mafuta mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, napendekeza kuanzisha Mfuko wa Kuchochea Ujenzi wa Viwanda. Hatuwezi kuendelea kuimba tu tukasema uchumi wa viwanda, lazima tuwe na mechanism namna tutakavyochochea. Maeneo mengine tunajenga viwanda tukivikamilisha ndiyo tunatafuta mwekezaji wa kuviendesha vile viwanda, na ndipo hapo tutakapoweza kuvutia watu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, naiomba Serikali, kuhakikisha kwa kweli tunakwenda kwenye uchumi mpana, uchumi mkubwa, jitihada nzuri mmezifanya, tumeona. Sasa Mheshimiwa Waziri hapa utatusaidia kutupa majibu maana yake ukisoma kwenye taarifa yako, mwaka 2021 unasema pato la Taifa kwa nchi yetu kwa dola za Marekani ulikuwa bilioni 69.9, mwaka 2021; mwaka 2023 tunategemea itakuwa bilioni 85.5. Uki-calculate pale, ukipiga hesabu ukuaji ni zaidi karibu toka mwaka 2021 Serikali ilipoingia Awamu ya Sita hii toka wakati huo ni zaidi ya asilimia 22, ukitoa unakuta kwamba yaani kwa kweli growth rate ingekuwa ni kubwa zaidi ya pale.
Mheshimiwa Spika, sasa hebu utatusaidia, ni nini hasa ambacho kipo katika calculations. Kwa sababu IMF ndiyo wametoa hizo takwimu kwamba uchumi pato limetoka hapa limekwenda hapa, sasa ku-calculate kwa kawaida haitupi hii figure ambayo mnaisema, inaonekana nchi tumefanya vizuri zaidi kwenye uchumi kuliko ambavyo takwimu zinaonekana kwenye madaftari. Kwa hiyo, mimi nafikiri kwamba ni suala la kujipongeza, ni suala la kusema tumefanya hapa tuongeze nguvu zaidi ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)