Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru.
Kwanza nimshauri tu Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, usiige utamaduni wa mtangulizi wako wa kutuletea vitabu vikubwa ambavyo mtu akisoma between the lines kuna maneno mengi kuliko uhalisia.
Ushauri wangu kwako tu, inawezekana huu ni mwaka wa kwanza bado una mihemko ya aliyekutangulia, kuanzia mwaka ujao uje na kitabu ambacho kinaeleza tumepanga nini na tutatekeleza nini kwa huo mwaka, hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili watu ambao mnaongea sana, sijui Mheshimiwa Magufuli alivyokuwa Waziri kafanya nini, mwaka jana mwenyewe amekiri hapa, katika miaka kumi ya Ilani ya CCM, 2005 – 2015 ameweza kutekeleza asilimia 31 ya kile mlichotakiwa mkifanye. Sasa hivi nyie mtoto akifanya mtihani akipata 31 chini ya 100, hivi huyo amefeli amefaulu?
Kwa hiyo, tuache kujikomba, unafiki, tusaidie Serikali ndilo jukumu letu kama Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina barabara zangu Jimboni, najua kuna wengine huko wanapata shida na barabara zao zimechokachoka, sisi wa town tuna nafuu kidogo. Lakini nimeahidiwa hapa, miaka mitatu iliyopita na Mheshimiwa Waziri, naomba utoe majibu. Kuna barabara za kupunguza foleni mkoa wa Dar es Salaam; barabara ambazo zinaunganisha Jimbo la Kibamba na Jimbo la Kawe; barabara ya Goba – Tanki Bovu; Goba – Wazo Hill –Tegeta, Gao – Goba – Makongo – Mlimani City.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mkiwa mnanijibu hapa, msiniambie ujenzi umeanza, ninajua hizi ni barabara tatu tofauti zinazounganishwa na kipande kimoja. Sasa nataka leo msiniambie kwa sababu ukiangalia vitabu vya bajeti, na ndio maana nawaambia Waheshimiwa Wabunge,
tuwe tunasoma, tukiwa hatusomi Mawaziri hawa wanakuja wanatudanganya. Miaka mitatu mfululizo hizi barabara zimetengewa fedha, kipande cha kuunganisha Jimbo la Kibamba na Kawe, Goba – Mbezi, Goba – Wazo Hill, Goba – Mlimani City, lakini leo ni mwaka wa tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona kuna hela zimetengwa hapa, zipo, kama ambavyo mwaka wa jana Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa maneno haya haya kama ya kwako zilikuwepo lakini mwaka mmoja baadaye hakuna barabara. Sasa Waziri kesho ukiwa unajibu naomba uniambie kwa uhakika wananchi wa Kawe wasikie, kwa sababu wewe ni mwananchi wangu pia na Mbunge wako nikiwa nazungumza lazima usikilize hizi barabara zinakamilika lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa juzi, wakati wanajenga hii barabara ya Mwenge – Tegeta – Kibaoni niliishauri Serikali nikaiambia wakati wa mvua kuna kiwango kikubwa cha maji kinachotoka ukanda wa Wazo huku juu Goba na ili barabara iweze kudumu kuna maeneo ambayo lazima mapokeo na matoleo ya maji yawe makubwa Ili tuweze kuelekeza maji baharini. Leo barabara imejengwa, mvua ikinyesha ukiwa pale Afrikana, Goigi ni majanga, hii barabara itakatika miaka mitano haitimii, kuna faida gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi namuomba Mheshimiwa waziri akiwa anajibu, kwa sababu niliandika barua kama Mbunge nikiwaomba; mkasema ooh! huyu mjapani ambaye tumepewa msaada ana masharti tutatumia fedha za ndani kujenga mapokeo ya maji makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo naomba niambiwe maana mvua ikinyesha yakitokea maafa Mheshimiwa Jenista Mhagama huyo, halafu mvua ikikauka na yeye anasepa, barabara iko vilevile. Sasa leo nataka mniambie mna mikakati gani, dhahiri, shahiri, kuweza kuokoa ile barabara ya mabilioni ya shilingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Rais ambaye watu tunaambiwa tusimtajetaje, tutamtaja tu kama alichemsha, msitutishe. Wakati tunapitisha bajeti ya barabara ya Mwenge – Tegeta ya shilingi bilioni 88 tuliambiwa hii barabara itajengwa vipande viwili, kwa matukio mawili. Moja ni Mwenge kwenda Tegeta ya pili ni Mwenge kwenda Morocco, bilioni 88. Sasa leo kuna uchafu unaendelea pale, kutoka Mwenge kwenda Morocco sijui mnatengeneza kichochoro, sijui mnatengeneza kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka nijui zile shilingi bilioni 88 ambazo Mheshimiwa John Pombe Magufuli, katika Bunge hili akiwa Waziri alisema kazi yake ni kujenga hizi barabara mbili, ziko wapi? Nataka majibu. Na ule uchafu mnaojisifia sijui fedha za Uhuru, sijui fedha za nini, ile barabara ilikuwa na pesa; kwa hiyo msitafute ujiko kwa kuwa mmezitafuna zile pesa mnatuletea uchafu. Si hadhi ya Dar es Salaam kujengwa ibarabara zile na kama mnatuambia mnajenga kwa muda, hilo pia ni tatizo linguine, misuse of resources. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuriko. TANROADS walifanya upembuzi yakinifu sijui mnavyoita ninyi, wakatengeneza na michoro kwa ajili ya mfereji mkubwa kuzuia mafuriko ukanda wa Kunduchi, miaka minne imepita. Mwaka juzi alienda Mheshimiwa Pinda, akaambiwa mchoro huo upo, wakati wananchi wanaelea kwenye bahari ya mafuriko, mkasema itajengwa, itatengewa fedha, hakuna kilichofanyika, naomba nipate majibu kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Serikali. Naomba niseme hivi, haya majipu yanayotumbuliwa tutaona huyu bwana mkubwa ana maanisha akitekeleza Azimio la Bunge la mwaka 2008. Bunge lilisema nyumba ambazo zilipewa watu ambao si sahihi zirejeshwe, nyumba ambazo zilikuwa za maeneo ya kimkakati ya watumishi zirejeshwe. Sasa kuna maneno mengi ya mtaani yanasemwa kuhusiana na watu waliopewa nyumba hizi. Sasa tukiona bwana mkubwa anashindwa kufanya utekelezaji yale maneno ya mtaani tutaanza kuyaamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka hatua zichukuliwe, ukaguzi ufanyike kwa kina, CAG aagizwe ili hizi nyumba 7,921 zilizouzwa, tujue mbivu zipi, mbichi zipi, na kama kuna watu walipewa kinyume na utaratibu nyumba zirejeshwe (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa jana Mheshimiwa Samuel John Sitta akiwa Waziri nilizungumza juu ya nyumba za TAZARA zilizouzwa kinyemela, kinyume na utaratibu. Kuna audited report ya mwaka 2014 aliniomba nakala nikampatia; nyumba zaidi ya 500 ziko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa nyie kawaida yenu mnaendana na mihemko, maana kipindi kile aposhinda Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ari mpya, kasi mpya, yaani kila mtu akija hapa ni swaga tu za ari mpya, maisha kwa Watanzania yamekuwa fresh. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameenda na ya kwake, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ametengeneza asilimia 31 tunakuja huku, hapa kazi, story tu, yaani ninyi ni watu wa mapambio. Sasa mimi nitakupatia hii audited report ili umuulize na Mheshimiwa Samuel John Sitta aliifanyia nini, ili kesho unipe majibu juu ya hizi nyumba zilizouzwa. Kwa mtindo ule ule wa nyumba zile za Serikali utaratibu wake uko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru, lakini niwaombe Wabunge wenzangu mtanikumbuka miaka mitano ikiisha. Pitieni vitabu vya ujenzi mtanikumbuka maneno yangu. Ninyi kaeni, mnaona majina yenu hapa mnacheka cheka tu, itakula kwenu big time. Asanteni sana Mheshimiwa.