Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya mimi kutoa mawazo yangu kwenye bajeti hii. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri ambayo kwa kweli, inatupa mwanga wa kile kinachokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa nimesimama hapa leo, kwa kweli naomba kwa nafasi ya pekee kabla sijachangia bajeti hii, nipongeze Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania ambayo kwa mara ya kwanza wamekamata cocaine pamoja na heroin kilo 250. Naipongeza mamlaka hii kwa sababu kazi hii inataka uzalendo wa hali ya juu. Nikisema uzalendo, unaweza ukawa mzalendo kwenye mambo mengine, lakini kwenye suala la pesa uko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, kazi hii inataka uzalendo uki¬-base kwenye kutokupokea rushwa. Ninaipongeza sana mamlaka hii na ninampongeza kwa nafasi ya kipekee Kamishna Mkuu wa Mamlaka hii Bwana Aretas Lyimo. Kwa kweli, ninampongeza sana, wamekamata bangi kavu magunia 978 ambayo ilikuwa tayari kusafirishwa. Wamekamata bangi mbichi magunia 5,495, wamefyeka ekari 1,093. Kwa kweli, taasisi hii ambayo iko chini ya jemadari wetu Mheshimiwa Jenista Joachim Mhagama, kwa usimamizi wenu, tunawapa pongezi nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu, hapa tunazungumzia masuala ya bajeti kwa maana ya kile tunachopata pamoja na matumizi, lakini dawa za kulevya, athari zake ni kwamba, zikizidi kwenye nchi, hata uchumi kwanza unaharibika. Hakuna mtu ambaye ataweza kuwekeza kwenye sehemu ambayo uhalifu uko kwa kiwango kikubwa. Wahalifu wengi ni hawa ambao wanavuta bangi na kutumia dawa za kulevya. Kwa hiyo, uhalifu ukiongezeka, hakuna mtu; hata hao wawekezaji ambao leo hii tunawapigia kelele kuwaita, hawataweza kuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nijaribu kusema kwa sisi wanawake ambao hasa ndio walezi, imagine una mtoto wako ambaye pengine anaweza akawa mmoja au una watoto wako ambao unawapenda. Hakuna mzazi ambaye hampendi mtoto wake. Umemzaa mtoto wako, umemlea vizuri, umemsomesha; wakati unasema kwamba sasa ndiyo umefika wakati wa yeye kuwa angalau akulee wewe, anakuja kuangamia kwenye suala hili la dawa za kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya uteuzi wa watu makini. Kwa sababu, tumeona baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yamefyekwa haya madawa ya kulevya, kwa maana ya bangi, ni maeneo ambayo bangi ilikuwa inalimwa. Arumeru hapo Arusha kuna viongozi, kuna watu, kuna Wenyeviti. Kwa hiyo, yataka moyo wa kijasiri wewe kutoka pale ulipo kwa maana ya Kamishna Lyimo kutoka pale alipo kwenda kufyeka zile dawa. Ninampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilikuwa naomba kwanza kuwapa hongera Waheshimiwa Wabunge kwa msimamo mliokuwanao. Wabunge wanawake asanteni sana kwa kura nyingi za kishindo mlizonipa za Ujumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa. Asanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie bajeti. Bajeti hii ni pro-growth kwa maana ya kwamba huko inakokwenda tunaona kabisa inakwenda kuinua uchumi, lakini zaidi ime-base kwenye biashara. Biashara ndiyo hazina kubwa katika maendeleo ya nchi yoyote ile. Serikali haifanyi biashara, lakini uzalishaji wowote ule, hata juzi kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anazungumza, alikuwa anazungumzia kuhusu masuala ya biashara na jinsi ilivyo wakulima kule, viwanda, kiwango cha uchakataji wa mazao pamoja na kadhalika. Kwa hiyo, naomba kupongeza sehemu moja. Sehemu kubwa moja ambayo naomba kuipongeza ni suala zima la kuitoa Capital Gain Tax kwenye share transfer za makampuni yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine kama tunavyojua kwamba soko la hisa Afrika Mashariki liko wazi, hii itasaidia sana kuweza kukaribisha wawekezaji wengi zaidi waweze kuja kwenye nchi yetu na kuwekeza wakijua kwamba hili suala la Capital Gain Tax ni zero rated. Kwa sababu, hapo zamani ilikuwa ni asilimia 10, lakini napata mashaka kidogo, huu utaratibu wa kuileta Finance Bill dakika za mwisho (last minutes), mapendekezo ambayo sisi kama Wabunge tunayabadilisha, ni wakati gani yanapata nafasi ya kuingizwa kule kwenye mabadiliko? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua, bajeti inaanza utekelezaji tarehe 01 Julai. Kama ni hivyo, leo tarehe 20, tunapiga kura tarehe 27, tarehe 28 pengine ni Finance Bill, tarehe 30 hapo hapa katikati Finance Bill isomwe, mabadiliko yafanyike, Rais asaini. Ni muda mfupi sana. Kwa hiyo, sana sana ambacho naweza kukisema hapa kutokana na timeframe, naomba sasa tuwe wazalendo, yale ambayo tunayapendekeza kubadilishwa yaweze kubadilishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kutokana na hilo, muda ni mfupi. Baadhi ya nchi za wenzetu wameweza kufanya mabadiliko kwamba, bajeti inasomwa, Finance Bill inakuja kusomwa baadaye au wengine wanasoma kabla. Mabadiliko mengi ambayo yanakuja kuwekwa, watu wanaweza kuyaona, lakini hivi hivi unakuwa hujui kipi kitakwenda kusainiwa na kipi kitakwenda kufanyiwa kazi. Kidogo inaleta shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri kwa suala zima la kuondoa ada kwa watoto wetu, lakini changamoto kubwa ambayo naiona kwenye nchi yetu na hasa kwenye nchi nyingi za kiafrika ni ongezeko la watu (population). Hivi hatua hizi tunazoendelea kuzifanya, mwisho lini? Au tutazifanya kwa kiwango gani? Kwa sababu idadi ya watu ni kubwa. Yaani wakati hawa wengine wanamaliza, tunachukua measures hizi, bado kuna wengine wanazaliwa, bado kuna wengine wako vyuoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani hatuna budi kukaa chini na kuangalia matumizi ya Serikali, ili fedha ambazo zinapatikana na zinaminywa ziweze kwenda kusaidia kwenye vitu kama hivi. Naomba sana kwa sababu kelele nyingine za watu huko nje, siyo wakati mwingine labda ni kwa sababu ya jambo fulani, lakini watu wanataka waone fedha zinakwenda kule ambako kunatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu suala zima la bandari. Yapo mengi yamesemwa. Suala hili limekuwa lina mambo mengi sana, lakini mimi nilikuwa naomba kusema hivi, nyakati kama hizi ambazo kila mtu anakuwa na ya kwake ya kusema, hatuna budi sisi kama Wabunge kukaa chini na kutafakari yale ambayo yanasemwa na kuangalia ni kitu gani tunaweza kuki-push ili Serikali iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, mimi kwa imani yangu na ninafahamu kwamba ni imani ya wengi, kwanza kwenye hili suala kuna mistake ilitokea somewhere. Kuna vitu ambavyo huwa inatakiwa sisi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lucy muda wako umeisha. Malizia mchango wako, nakupa sekunde 30.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Eeh, amesemaje?
MBUNGE FULANI: Muda umeisha. (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa unga mkono hoja.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)