Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa walau nichangie katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri ya Bajeti Kuu ya Serikali, kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uchapaji kazi wake mzuri, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu yake nzima iliyochakata bajeti hii ambayo hivi sasa tumeiona imetupa vipaumbele vikubwa kadhaa ikiwemo kwanza kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimepewa kipaumbele namba moja na hasa hasa kwenye maeneo ya umwagiliaji pamoja na pembejeo za kilimo. Hapohapo ile miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ndio tunasema inaenda kukomboa uchumi wa nchi yetu Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, haya mambo kwa kweli tunayo kila sababu ya kumpongeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye tunasema ndiye mbeba maono ya nchi yetu kuelekea 2025. Nimuombee Rais wetu afya njema na tumpe moyo, tumtie moyo Rais wetu kwa kazi hii anayoifanya ili aendelee kututumikia Watanzania wenzake kwa moyo na kwa upendo wa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilete shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, siku ile nilipoomba barabara ile ya Singida - Ilongero nimshukuru Waziri wa Ujenzi aliahidi kunipa kilomita 10 za lami, lakini na yeye Waziri wa Fedha akaniambia bwana tunaenda kutafuta fedha kwa barabara nzima iwekwe lami, hiyo ahadi tunaishukuru wananchi wa Singida Kaskazini lakini tunatarajia sasa tuone utekelezaji. Tunatarajia tuone utekelezaji kuanzia mwaka huu wa fedha kama Waziri Mbarawa alivyosema lakini hata wewe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama ulivyoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu kubwa ya leo pamoja na mazuri mengi niliyoyaona kwenye bajeti hii ikiwemo suala la wanafunzi wa elimu ya vyuo vya kati kusoma for free kwa mikopo kutoka Serikalini, kwa kuondolewa ada lakini pia kwa kuendelea kutoa ruzuku kwenye mbegu kwenye mbolea na pembejeo za kilimo. Nina mambo machache ambayo ningependa kuyawasilisha kwa ajili ya kuyafanyia kazi:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna suala la ule mfumo wa electronic stamp (ETS). Mfumo huu ni mzuri lakini umekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau kwamba una gharama kubwa, yule mwekezaji anayetoa hii huduma imekuwa kidogo ina malalamiko kutoka kwa wadau. Kwa hiyo, niombe Serikali ichukue fursa ya kukutana na yule mdau ili kupunguza zile gharama ili wale wananchi wanaopata hii huduma wapate huduma hii kwa urahisi.

Pili, zile stamp zilizopo kwenye chupa za maji kwenye soda na kadhalika zimekuwa zina malalamiko kwa hiyo niombe Serikali ikae na yule mwekezaji waweze kuondoa zile gharama ziwe za kawaida kwa ajili ya kupunguza hata gharama pia za maji kwenye matumizi ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme moja kubwa leo kwenye eneo la kilimo hususani zao la alizeti. Wenzangu wamezungumza sana wanaotoka Mikoa ya Kati, alizungumza sana Mheshimiwa Yahaya Massare jana amezungumza pia Mheshimiwa Kunti Majala asubuhi ya leo lakini na Wabunge wengine wanaotoka kwenye maeneo yanayozalisha Alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022, 2022/2023 Wizara ya Kilimo, Waziri Mkuu kwa ujumla wake wametuhamasisha sana kulima alizeti, tunashukuru tumeona pembejeo za kilimo, tumeletewa mbolea, mbegu zenye ruzuku lakini hatua hizo zimewezesha kwa kiwango kikubwa kuongeza tija kwenye uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alizeti imelimwa kwa kiwango kikubwa sana nchini, kuanzia Iringa, Singida Kaskazini, mpaka kule Maluga, Kiomboi kule ndani kule Shelui wanakolima alizeti, wamelima sana alizeti na sasa hivi pale barabarani tunakopita pale Maluga unaona alizeti ni nyingi kweli kweli, ukienda Iramba ndani kule Mkoa wamelima sana alizeti kwa wingi, nyingi kwelikweli nawapongeza sana wa Singida, Wanasingida, Watanzania kwa ujumla wanaozalisha alizeti. Niwapongeze na watu wa Ilongero, Mudida na kule kwingine kote walioitiia wito wa Serikali kwa kulima na kuzalisha alizeti kwa wingi, wameipokea kauli mbiu wamepokea kauli za viongozi wao kuhakikisha wanazalisha sana alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida inakoanzia ni wapi? Kwa masikitiko makubwa sana, kwa majonzi makubwa sana, sasa hivi tunavyoongea hapa bei ya gunia moja la alizeti ambalo lina ujazo wa kilo sitini mpaka sabini ni shilingi 25,000 umeuza sana 35,000. Kwa kweli ni masikitiko makubwa sana kwa mfumo huu, hili tatizo limeletwa na sisi tunaoagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu ambayo naiheshimu sana na kwa kweli suala la kilimo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo mimi niliinadi mwaka 2020, wakati tuko kwenye Uchaguzi Mkuu, kwamba tunakwenda kukipa kipaumbele kilimo na tunaenda kuki-modernize kiwe cha kisasa, kwenye ukurasa wa 33 kuendelea mpaka huko inakoenda kwamba Serikali ya CCM inakwenda ku-modernize kilimo. Sasa ku-modernize kilimo maana yake ni kuhakikisha hata kwenye masoko yetu, sisi wenyewe tu-export nje ya nchi, siyo tu import. Nashangaa inawezekanaje tuwe tunaagiza mafuta ya kula nchini wakati tuna mawese, tuna alizeti, karanga na pamba. Sisi ndio tunatakiwa tupeleke mafuta ya kula nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kunti alizungumza vizuri sana asubuhi kuhusu eneo la alizeti. Naomba mchango wake nami niutambue kwenye eneo la alizeti. Naomba Mheshimiwa Waziri kwenye eneo la alizeti, katika suala la kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, hii tunailetea nchi yetu laana. Tunawaumiza wakulima wetu, tunawaumiza wananchi wetu ambao maisha yao yanategemea kilimo. Mwananchi amelima kutoka mwezi wa Kumi na Moja mpaka leo Mwezi wa Sita ndiyo anaenda kuuza. Almost seven months yuko kwenye kilimo anahangaika kuzalisha, unakuja kumwambia leo unamwagizia mafuta kutoka nje. Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali yangu ifanye mambo mawili. La kwanza kwenye hili, ili kumsaidia mkulima, kumsaidia mwananchi wa kawaida wa nchi yetu, la kwanza tuhakikishe ile nakisi iliyopo, tunasema mahitaji yetu ya ndani ni tani 650,000, lakini tuna uwezo wa kuzalisha tani 300,000, basi tusiagize hivi sasa. Tusubiri wakati tunapoona nakisi kule mwishoni ndiyo tuagize, lakini tuagizie kwa kutumia vibali kulingana na upungufu uliopo. Sasa hivi ni soko huria, ukimwambia mtu agiza, aneleta zaidi ya hizo. Anaweza kuleta tani 1,000, tutawezaje kudhibiti hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana twende kwa takwimu. Tuangalie kwanza tuna viwanda kiasi gani vinavyozalisha mafuta? Vina uwezo gani? Tuangalie na uzalishaji tunaoufanya, kweli hii nakisi tunayosema ya tani 350,000 ndiyo iko hivyo hivyo? Maana yake wenzetu wanapoambiwa walete, wanaagiza mpaka wanakuja kuua soko letu la mazao ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana Waziri anisikie na Serikali kwa ujumla, kwamba kuendelea kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi ni kuendelea kumdidimiza mkulima ambaye maisha yake asilimia 100 yanategemea hiyo mbegu ya alizeti, yanategemea kilimo, hana mshahara, hana kitu kingine chochote kinachomwingizia mapato kwenye maisha yake. Anategemea apate dawa, apate ada ya watoto wake, na kila kitu kwenye maisha yake anategemea alizeti au mazao. Sasa sisi tunavyoendelea kuagiza kutoka nje, tunamnyanyasa, tunamuumiza huyu mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye eneo la alizeti, kuagiza mafuta kutoka nje, naomba Serikali ilisikie hili na kulifanyia kazi. Serikali ifanye tafiti, kwa nini sisi mpaka leo tunaagiza mafuta kutoka nje ya nchi wakati ardhi yetu ukianzia Kigoma uende mpaka Pwani, kote unakutana na alizeti. Ukianzia Ruvuma mpaka Arusha kote tunalima alizeti; tunalima chikichi, tunalima pamba, inakuaje mpaka leo sisi ni waagizaji wa mafuta kutoka nje? Tuna hujuma? Hatufanyi kazi ipasavyo? Tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hili Mheshimiwa Waziri alichukue, ninashukuru kwamba hata yeye ni mkulima namba moja, hata kwenye hotuba yake hapa alisema amesoma kwa kupitia mifugo, amesoma kwa kupitia kilimo, kwa sababu kilimo na mifugo vinaenda pamoja. Naamini hili ninalolizungumza analielewa kaka yangu doctor, tunatarajia baadaye awe Profesa. Sasa Uprofesa huu tuulete kwenye maisha halisi ya wananchi wale waliotuzaa sisi wakatusomesha mpaka leo tuko hapa. Mheshimiwa Waziri … (Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ABEID R. IGHONDO: …tunatarajia nao wapate manufaa na matunda.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ramadhani kuna taarifa. Iko wapi taarifa?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Kuchauka.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kuchauka.

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kutoa taarifa. Nampa taarifa mzungumzaji, anachangia vizuri sana. Nami ninazo taarifa kutoka kwa wakulima wanasema, katika kuagiza haya mafuta humu, kuna watu wananufaika, ndiyo maana wanaendelea kuagiza. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ramadhani Ighondo, unapokea hiyo taarifa?

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshaunga mkono hoja, lakini pia anachokizungumza Mheshimiwa Kuchauka ni kweli. Hili eneo la kuagiza mafuta ndiyo linalowatesa wananchi kwa sababu kuna watu wananufaika na wametundika mirija yao, wanawatesa wananchi wenzangu kule Singida Kaskazini, Iramba, Mkalama pamoja na maeneo mengine kwa sababu ya fursa wanazozitumia za kuagiza mafuta kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashukuru. Naunga mkono hoja. Naomba hili moja kubwa la leo la eneo la mafuta ambalo nimezungumza, lichukuliwe na Serikali na lifanyiwe kazi, ahsante. (Makofi)