Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kupata nafasi hii jioni hii ya leo lakini pia naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai huu alionipa siku hii ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya katika Majimbo yetu kwa sababu kazi ambayo Rais anaifanya ni kubwa na ambayo sisi Wabunge wake na wananchi wake kwa ujumla tunamuunga mkono kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda mrefu sana uliopita wananchi wengi wamekuwa wakihadithiwa shughuli za maendeleo bila kuziona kwa macho lakini Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan wananchi wengi wameona shughuli za Serikali zinavyowafikia katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hili ni la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu anafanya kazi kubwa. Kwa hiyo, hata pale ambapo wananchi wanaambiwa kwamba walipe kodi naamini kwamba wanaweza kuwa wanahamasika kwa sababu wanaona vitu vinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mfanyabiashara na sisi huwa hatuendi darasani kujifunza namna ya kuweza kufanya biashara. Isipokuwa kufanya biashara ni namna tu ya mazingira uliyoyatokea nyumbani kwenu. Wakati mwingine umesoma au hujasoma na ukiona fursa ya kusoma hukuipata lazima uvamie fursa ya biashara. Sasa mimi ni mfanyabiashara, pia tupo wafanyabiashara wengi katika nchi hii ambao tunafanya biashara lakini hatukupata elimu ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa najaribu kufikiria na kuiomba Serikali kwamba hizi kodi nyingi, mtiririko mwingi wa kodi ni kwa nini Serikali isizitengenezee utaratibu wale wafanyabiashara wakawa wanazilipa kwa installment? kwa sababu watu wengi wanapokwenda kwa wafanyabiashara, huyu akaenda leo kwaa jambo fulani kwa ajili ya kumwambia mfanyabiashara alipe kodi ya jambo hilo, kesho akaenda mtu mwingine, keshokutwa na mwingine; zile kodi ziko zaidi karibia ya kumi ambazo mfanyabiashara mmoja anatakiwa kuzilipa. Sasa na kwa sababu pia hatuna elimu ya biashara yule mfanyabiashara anakuwa anachanganyikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi huwa najaribu kufikiri ni kwa nini Serikali haiwezi kuona kwamba zile kodi ambazo zinaweza zikaziunganisha pamoja, kwa nini zisiunganishwe pamoja na wale wafanyabiashara wakaambiwa kuwa wanazilipa kwa wakati? Kuliko hizi ambazo wanaruhusiwa watu wengi kwenda kuwasimamia wafanyabiashara aidha kuwadai vyanzo fulani vya mapato ya Serikali ambavyo na wao wenyewe wao waliotumwa kwenda kuvidai vyanzo vile vya mapato hawajui kuvielezea vizuri kwa wafanyabiashara. Lazima mamlaka ya mapato Tanzania ambayo ndiyo imepewa mamlaka hiyo ya kukusanya kodi inaweza kuwaelewesha watu vizuri wakaelewa namna ya kulipa kodi kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachoamini ni kwamba hawa wafanyabiashara wakieleweshwa vizuri kuhusiana na suala la kodi naamini watalipa vizuri. Serikali ili ikusanye kodi vizuri lazima iwaeleweshe wafanyabiashara wake vizuri waelewe ni kwa nini wanalipa kodi. Bahati nzuri kitu ninachokisema kwa sasa ni kwamba watu wengi hata mimi nimekuwa nikilalamika huko nyuma kwamba inawezekana nalipa kodi halafu kazi zinazofanywa na Serikali sizioni lakini kwa awamu hii kazi zinaonekana. Kwa hiyo hata namna ya kumwelezea mtu kwamba unalipa kodi ili kifanyike kitu gani inakuwa ni rahisi. Sasa ni kwa nini Serikali isiviunganishe vitu hivi, vyanzo vyake hivi vya mapato kuliko Serikali moja inatengeneza vyanzo vingi karibia 30 halafu unawapa watu tofautitofauti kwenda kuwaelezea hao wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wafanyabiashara kwa sababu tulio wengi hatujasomea biashara ila tumeingia tu kwenye biashara kutokana na ukata wa maisha, namna ile unavyokuja kuni-treat mimi inakuwa ni vigumu kukuelewa. Lakini kukitengenezwa mfumo mzuri ambao wafanyabiashara hawa wa chini wakaambiwa kiwango chake cha kulipa kodi kwa mwaka ni hiki kikagawika kwa awamu kama nne, ikawa kila baada ya awamu analipa kiasi kile anachokijua yeye Serikali haiwezi kupata usumbufu na wala haiwezi kuhangaishana na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata wakati nyingine mnapoona wafanyabiashara saa zingine wamegoma, wanagoma kwa sababu ya kuchanganyikiwa, yaani vitu vinakuwa vingi ambavyo vinaingia vichwani mwao na namna ya kuweza kulifanyia kazi inashindikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye wewe ni daktari wa fedha ni vizuri utusaidie sisi, uwasaidie walipa kodi wako ambao wewe unaamini kwamba unatoza kodi kwa watu ambao hawajasomea biashara lakini ndio wanaokulipa kodi. Sasa wewe lazima utumie namna yoyote inayoweza kuwezekana ili wale wafanyabiashara waweze kulipa kodi katika utaratibu ambao ni mzuri na ni nafuu na ambao ni rafiki. Bila hivyo wafanyabiashara wale bado wataendelea kukuhangaisha na bado watu wataendelea kukwepa kodi. Lakini kumbe kitu kikubwa kilichopo ni kwamba wakishaeleweshwa vizuri wakajua vizuri, na bahati nzuri sasa wanaona shughuli za maendeleo zinavyofanyika katika nchi yao kwa hiyo kigugumizi kinakwisha, na watu watakuwa wanaambiwa kulipa na wanalipa katika utaratibu ambao nil aini kabisa bila kuhangaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hilo nilikuwa naliomba sana, kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye ni mtaalam wa fedha atusaidie jambo hilo. Pia na juzi niliona hapa mchangiaji mmoja anasema kwamba mimi na taasisi yangu labla kampuni yangu nina miaka 20 nayo, halafu leo nikiambiwa kwenda kuisimamia ile taasisi yangu au kuisajili kwa ajili ya kufanya biashara labda ya microfinance naambiwa kwamba mimi siwezi kuwa kwenye bodi ya ma-director kwa sababu elimu yangu mimi haikidhi vigezo hivyo. Wakati huo huo taasisi hiyo nimeanza zaidi ya miaka 20. Sasa kwa akili za kawaida hata ukijiuliza unaona haiwezekani. Uzoefu nao una-matter katika kazi. Ingekuwa tu kusoma peke yake ndiko kunakosababisha kila jambo liweze kufanyika vizuri mimi naamini saa nyingine tusingekuwepo hapa tunahangaika na mambo mengi ambayo saa zingine yamekwenda na saa zingine hayakwenda vizuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hili nalo ni jambo ambalo unapashwa kuliangalia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo lingine nilitaka kusema tu kwamba wananchi wangu wale wa Kata ya Nyatwali wameshafanyiwa tathmini ya maendelezo yao kwenye kata yao ile ya Nyatwali. Na kwa vyovyote vile itakavyokuwa muda mfupi uliobaki watahama katika eneo lile. Sasa na kwa sababu wananchi wetu wale na unawajua wananchi walio wengi ni wakulima na wafugaji; ni ombi langu kwa Serikali kwamba ni vizuri yake malipo yao kwenye bajeti hii wakalipwa mapema ili wakajipange mapema kwa ajili ya kilimo katika maeneo mengine. Wakilipwa nje ya muda ule ambao unaendana na muda wa kilimo itawatesa kwa sababu pale walipo hawaruhusiwi kulima, pale walipo hawaruhusiwi kuendeleza chochote. Pia yule anayetakiwa kuwalipa hajawalipa, halafu anawaambia bado wako pale pale. Sasa hao watu wataishi katika mazingira gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naamini kwamba kwenye bajeti hii wale wananchi wetu watalipwa fedha zao mapema na wataondoka kwa wakati ili wakaanze maisha yao huko wanakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni lile jambo la kifuta machozi. Wananchi wetu wale maskini, wakulima, tena wakulima wa heka moja moja ya chakula na chakula chenyewe wanachokilima hata hakiwatoshi kukila kwa mwaka. Halafu chakula hicho hicho kimekuja kimeliwa na tembo halafu kulipwa fidia analipwa laki moja, halafu laki moja yenyewe anaisubiria baada ya miaka miwili, mitatu. Kwa kweli watu wale wanaumia kwa kiasi kikubwa. Ni ombi langu pia kwa Serikali kwamba jambo hili ni vizuri Serikali ikalifanyia mkakati mpya kuhakikisha kwamba kilimo cha mwaka kile ambacho hao wananchi wamekilima, mazao yao yamelishwa na tembo, muda huo huo mwaka ukiisha wawe wamepewa fedha zile ili na wao waende watafute chakula cha kununua. Hicho chakula ambacho wenzetu wanasema kwao gunia limeshuka mpaka 35,000 mikoa ya kusini. Sisi Mara gunia la mahindi ni 120,000 au 100,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakipata fedha hizo mapema wataenda huko ambako chakula kinauzwa 40,000 gunia wakanunue, halafu kitawasaidia, kuliko ile sasa kwamba fedha za mwaka huu atalipwa baada ya miaka miwili au miaka mitatu. Mwananchi huyu anakuwa ameshaumia kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba Halmashauri yangu ya Mji wa Bunda ilitoa eneo pale kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za TANAPA kanda ya magharibi; na halmashauri ile ilishatoa eneo lipo kwa muda sasa. Ni imani yetu kwamba kwa sababu tunapisha ile Kata nzima ya Nywatali ni vizuri pia Serikali na yenyewe ikahakikisha kwamba ofisi ile iliyokuwa imetengewa pale fedha za kuanza ujenzi ni vizuri ikajengwa kwa wakati kwa sababu ndio itakayokuwa inasimamia mambo hayo ya Mbuga ya Serengeti na mambo mengine. Malalamiko mengi ya wananchi wetu wakati mwingine yataishia hapo kuliko vile ambavyo tunakuwa tunapata wakati mgumu wa namna ya kupata suluhisho la matatizo hayo ambayo tunakuwa tumeyapata katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kusema kwamba fedha zile zitolewe mapema ili kwamba Ofisi ile ya TANAPA Kanda ya Magharibi ziweze kujengwa kwa wakati ili ziweze kusaidia katika Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la fedha za miradi ya barabara. Niishukuru Serikali kwa sababu imeendelea kufanya kazi kubwa lakini bado sisi kwetu Bunda pale eneo la barabara za mitaa bado tatizo lipo ni kubwa.
Ombi langu ni kuiomba Serikali iendelee kutoa fedha kwenye TARURA ili kwamba uboreshwaji wa barabara zile za mitaa uweze kukaa vizuri; na kwa sababu maeneo hayo muda mwingi yamekuwa hayapitiki kwa muda mrefu lakini kwa sasa ramani imeanza kuonekana. Ombi langu ni kwa Serikali kuhakikisha kwamba wanawapa fedha za kutosha ili kwamba barabara zetu zile ziweze kulimika vizuri na wananchi wetu waweze kupita katika maeneo yao kwa wakati wote wa masika na kiangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nakushukuru kwa kupata nafasi; ahsante sana. (Makofi)