Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie maeneo manne yale yanayogusa Jimbo la Nachingwea ambalo natokea, lakini yapo ambayo yatagusia ukanda mzima wa kusini mwa Tanzania na yale yanayohusu Taifa letu kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwa hotuba nzuri nimeipitia hotuba yake vizuri sana, naomba nimpe hongera kwa kazi nzuri na tunamtakia kila la kheri katika kutimiza ahadi ya yale yote ambayo yamezungumzwa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo na pongezi hizo naomba sasa nijielekeze kwenye hoja zinazohusu barabara zetu. Uchumi wetu kwa sehemu kubwa unategemea barabara ambazo lazima ziwe katika kiwango cha lami ili tuweze kuleta maendeleo ambayo tunayakusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano lakini pia kwa Serikali ya Awamu ya Nne. Serikali ya Awamu ya Nne imefanya kazi kubwa, mimi natoka mkoa wa Lindi na wale wanaotoka mkoa wa Mtwara watakubaliana na mimi. Miaka kumi iliyopita tulikuwa tunatumia zaidi ya wiki moja kuifikia Dar es Salaam, lakini sasa hivi tunatumia saa nne au tano; unatumia gari ndogo hata taxi kufika Mtwara na Lindi. Hii yote ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambayo kwanza ilianza kufanywa wakati wa Mheshimiwa Magufuli akiwa Waziri na sasa hivi ndiye Rais wetu, kwa hiyo, hatunabudi tumshukuru na tumpongeze kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya Wabunge hapa wanachangia mimi nashangaa na nitashangaa sana, kupitia bajeti hii mtu anasimama hapa anasema tunapewa vihela vidogo hivi wakati kuna maeneo ambako wanatafuta pesa hizo waweze kujengewa miundombinu waweze kupata huduma. (Makofi)
Mimi nafikiri ifike wakati sasa tunapokwenda kutekeleza bajeti hii baadhi ya maeneo ambayo hawaoni umuhimu wa hizi kazi tunazozifanya hebu tuachane nao tuelekeze nguvu zetu sasa kwenye yale maeneo ambayo Watanzania wanahitaji kuona miundombinu bora na wanahitaji kuboresha huduma zao badala ya kukaa na kuja hapa kusema maneno ambayo kimsingi hayana mbele wala nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba sasa nirudi kwenye barabara ambayo kwa muda mrefu imekuwa inazungumzwa. Mheshimiwa Waziri Mbarawa nafikiri unakumbuka ulikuja Nachingwea mwaka jana kama sio mwanzoni mwa mwaka huu, umeona hali ya barabara ya kutoka Nachingwea kwenda Masasi na kutoka Nanganga kwenda Nachingwea. Nashukuru kupitia bajeti hii imeorodheshwa na imesemwa kwa kilometa 91; zipo kazi ambazo wakati unakuja kuhitimisha ningeomba unipe ufafanuzi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nachingwea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba maandalizi yanafanyika kwa ajili ya barabara hii, sasa sijajua maana kama ni feasibility study tayari kazi hii imeshakamilika kwa mujibu wa taarifa nilizonazo. Hapa nimeangalia imetengwa shilingi bilioni moja, sijajua hii shilingi bilioni moja ni kwa ajili ya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana ndani ya mkoa wetu wa Lindi leo tunajadili shughuli za kiuchumi, kwenda kuweka viwanda kwa ajili ya mihogo, kuona namna gani tunaboresha mazao yetu ya korosho na ufuta lakini bado hatujawa na miundombinu ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika na Serikali yetu bado nimuombe Mheshimiwa Waziri atakaposimama awaeleze wananchi wa Jimbo la Nachingwea ambao wanapakana na wananchi wa Jimbo la Ruangwa, Masasi na Liwale; lazima haya maeneo yote tuelezwe katika bajeti hii Serikali imejipanga vipi kuhakikisha tunajenga hizi barabara kwa kiwango cha lami badala ya kufanya periodical maintenance ambayo kila wakati tunalazimika kuingia gharama kubwa na barabara hizi bado zinakuwa zinaleta usumbufu mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni lile ambalo linagusa barabara zinazounganisha mkoa wetu wa Lindi. Tunayo barabara inayotoka Nanganga kwenda Nachingwea. Barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami inaenda kuunganika na mkoa wa Ruvuma kupitia njia ya Kilimarondo. Kwa muda mrefu barabara hii imekuwa ni muhimu sana kiuchumi katika maeneo yetu.
Kwa hiyo, ningeomba kupitia Wizara Mheshimiwa Waziri tuione barabara hii ili tuiweke katika mipango yetu tuweze kujenga kwa kiwango cha lami tuunganishe na mkoa wa Ruvuma ili tuweze kuunganika na mkoa wa Mtwara na tufungue maendeleo ya mikoa ya Lindi Mtwara pamoja na Ruvuma ambayo kwa muda mrefu kidogo tumekuwa nyuma katika shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimwia Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumza nje ya barabara ni eneo la viwanja vya ndege. Wapo baadhi wamezungumza kutoona umuhimu wa viwanja vya ndege. Mimi naomba niseme viwanja vya ndege ni muhimu, kwa nchi yetu hapa ilipofikia inahitaji kujenga viwanja katika maeneo yake. Hapa katika orodha ya viwanja ambavyo vitakarabatiwa kipo kiwanja cha Lindi kimetajwa hapa, kiwanja hicho kina hali ngumu
sana kwa sisi watu wa Mkowa wa Lindi. Lakini kwa Nachingwea, leo viongozi wote wanatua Nachingwea ndipo wanakwenda katika maeneo mengine. Kwa muda mrefu Mheshimiwa Benjemini Mkapa ametumia uwanja wa Jimbo la Nachingwea kwenda Masasi, na sasa hivi hata Waziri Mkuu anapokwenda Ruangwa lazima atue Nachingwea; na bado mahitaji ya watu wa Nachingwea kuweza kutumia ndege na viwanja vyake bado ni makubwa sana. Kwa hiyo wakati Mheshimiwa Waziri anakiangalia kiwanja cha Lindi bado kiwanja cha Nachingwea tungependa kuona hata ukarabati unafanyika kwa sababu ndicho kiwanja kikubwa ndani ya mkoa wa Lindi ambacho kinaweza kikaruhusu kutua kwa ndege na kuweza kufanya safari kuelekea maeneo ya pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo la mawasiliano ya simu. Naomba nipongeze Wizara, ipo kazi kubwa imefanyika lakini pia kupitia kitabu ambacho ninacho hapa Mheshimiwa Waziri naomba nikupongeze. Ninazo Tarafa za Kilimarondo, Ruponda kule kwangu Nachingwea. Tarafa hizi kwa sehemu kubwa zimeshapata mitandao ya simu na hasa mtandao wa TTCL, hata katika orodha ya vijiji na Kata ambazo zina maeneo haya mmeorodhesha. Lakini bado mtandao wa TTCL kwa wananchi au wakazi wa haya maeneo ambayo nimekutajia Mheshimiwa Waziri bado hawajapata mawasiliano ya uhakika zaidi, wanashindwa kupata huduma za fedha kwa sababu TTCL hawajaingia katika biashara hiyo. Kwa hiyo, tungeomba mitandao kama ya Vodacom, Airtel; na orodha hii tayari tumeshaleta Wizarani, tungependa katika awamu hii uweze kutoa msukumo ili tuweze kupeleka mawasiliano wananchi wale waweze kuunganika na watu wengine wa maeneo mengine ya Wilaya ya Nachingwea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na waliotangulia kusema juu ya suala la uuzaji wa nyumba za Serikali. Mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao siungi mkono utaratibu ambao ulitumika kuuza nyumba za Serikali. Utaratibu ule hauna tija kwa Taifa letu. Leo hii viongozi wanateuliwa, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, baadhi ya Mawaziri wanakwenda kukaa katika nyumba za wageni badala ya kwenda kukaa kwenye nyumba za Serikali. Hii ni hasara kwa Taifa letu na haya maamuzi kimsingi bado hatujachelewa, kupitia Serikali ya Awamu ya Tano naomba niishauri Serikali yangu, kwa heshima na taadhima hebu ifanye maamuzi ambayo ni magumu ya kurejesha nyumba zote ambazo ziliuzwa bila utaratibu ili watumishi wetu waweze kuzitumia na tuweze kuona namna bora ya kuweza kuboresha watumishi wetu na watu wa kada mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwa ufupi ATC. Naomba nipongeze jitihada ambazo Mheshimwia Waziri amezizungumza za ununuzi wa ndege japo ni ndege chache, tumechelewa na kimsingi tunapaswa tukimbie sasa kwa sababu idadi ya ndege tulizonazo ni chache na ni aibu kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaunga mkono bajeti hii lakini tunaomba watu wa Wizara wawe active waweze kuona wenzetu ambao wameendelea kwenye nchi mbalimbali ukienda kama Dubai - Emirates kule, ukiangalia katika maeneo ya Qatar, wana ndege nyingi, walitumia njia gani? Sisi tunao wasomi ambao wanaweza wakaishauri Serikali yetu na Wizara wakaona namna ya kuweza kuongeza idadi ya ndege kutoka hizi mbili ambazo leo tunazizungumza na tukawa na ndege nyingi ambazo zinaweza zikatua katika maeneo mengi ndani na nje ya nchi yetu. Kwa kufanya hivyo nafikiri tutakuwa tunatafsiri kwa vitendo uchumi ambao tunauzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe kwa kuzungumzia reli ya Mtwara, Mbamba Bay pamoja na…
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naomba kuunga mkono hoja.