Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu ya mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametupa uzima kuwepo katika ukumbi huu siku ya leo, kuendelea kujadili bajeti ya Taifa letu kwa maana ya hatma ya wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akijishughulisha kwa hali na mali kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma mbalimbali katika afya, elimu, barabara, maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiache kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, kwa kazi nzuri na njema ambayo ameendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais, Naibu wake pamoja na Wizara nzima Watumishi wa Wizara ya Fedha ambao wanahakikisha kwamba anafanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba huduma inapatikana kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kumpongeza tena Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo kwenye bajeti hii amehakikisha kwanza watoto wanaokwenda katika vyuo vya kati sasa wanakwenda kusoma kwa kupata mikopo. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwetu Wabunge kwa sababu kila mtoto analia kwamba tunaomba ada. Mheshimiwa Mbunge naomba ada, kwa hiyo hii kwa kweli tunampongeza Mheshimiwa Rais, tunakupongeza na Mheshimiwa Mwigulu kwa sababu mmefikiria jambo la msingi sana kwa Watanzania ambao wana familia maskini. Pia mmeenda kuondoa ada kabisa kwenye vyuo vingine hivi vya technical, kwa kweli mmefanya jambo la maana na jambo la muhimu kwa Watanzania na mnapaswa kushukuriwa, Mheshimiwa Rais anapaswa kushukuriwa na Mheshimiwa Mwigulu na timu yako nzima mnapaswa kushukuriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msamaha huu utaenda kuondoa vilio vya Watanzania walio wengi ambao hawakuwa na uwezo kwa ajili ya kupata elimu ya vyuo vikuu hasa vyuo vya kati na itaenda sasa kuleta faraja katika familia ambazo walikuwa wanafikiri kusoma haiwezekani, leo watakwenda kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu Mheshimiwa Waziri kwamba basi bajeti hii itakapoanza kutekelezwa katika kipengele hiki cha kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi hawa, tuweke utaratibu ambao hatutasikia tena kwamba huyu kapata, huyu kakosa maadam tu ana vigezo na amekidhi vigezo vyote na amechaguliwa kwenda kwenye chuo husika. Basi ile azma ya Rais wetu na Serikali yetu chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ikaendelee kutimia na wananchi waendelee kufurahia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niingie kwenye suala la miundombinu. Kama tunavyojua TARURA tumeiongezea fedha. Mimi kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi hivi karibuni kama alivyoeleza huko awali, nimekubwa na mafuriko makubwa sana ambayo yameharibu miundombinu ya barabara, imeharibu madaraja na hata kupelekea kabisa wananchi hawawezi kwenda hospitalini hawawezi kupata huduma za jamii, kwa sababu hali siyo nzuri kwa miundombinu kuharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu tumeomba fedha za dharura kwa madaraja kama manne. Daraja la Sekei kwa maana ya Kiutu - Naurei, daraja ambalo tumepata zaidi ya milioni 400 kwa fedha za dharura, daraja la Loning’o - Ilboru kwenda Kiranyi tumepata milioni 200 karibu na 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kuna madaraja matatu sasa ambayo wananchi hawapiti kabisa. Daraja la TPRI - Likamba kwenda Musa kwenda kutokea Jeshini Monduli. Kwa kweli hali siyo nzuri, hilo daraja halipitiki tena, hali ni mbaya. Vile vile daraja la kwenda Hospitali ya Oturmeti, maeneo yameharibika sana kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile barabara ya Mnadani – Mwandeti, Mnadani – Mindo kwenda Hospitali hali ni mbaya. Naomba sana Mheshimiwa Mwigulu kwa kuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alishaongea na wewe, utusaidie hizo fedha za dharura kwa sababu, kwa kweli hali kule ni mbaya. Nami kurudi jimboni bila kunisaidia hilo, utakuwa umeniumiza, umewaumiza wale wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi hasa kwa upande wa huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mifumo. Katika Halmashauri zetu Tanzania kumekuwa na changamoto kubwa sana inapofika mwezi wa sita, mifumo yote inafungwa. Mifumo mwezi wa Sita haifanyi kazi, mwezi wa Saba haifanyi kazi, mpaka mwezi wa Nane. Hii nayo ni changamoto kubwa. Kwa sababu, inakwamisha utoaji wa huduma kwenye Halmashauri, inakwamisha utekelezaji wa shughuli za miradi mbalimbali, inakwama kwa sababu mifumo imefungwa. Zaidi ya hapo, mifumo hii ingesaidia wananchi kuendelea kulipa kodi ndani ya Halmashauri na pia kulipa kodi kwenye Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalo Wizara ya Fedha iliangalie kwa makini na mapana namna ambavyo litaweza kupunguza kadhia hii ya wananchi kulipa kodi kwa sababu, bila kulipa kodi ina maana uchumi utakuwa umedorora kwa wananchi na Taifa. Kwa hiyo, naomba sana hili nalo liangaliwe kwa makini ili basi wananchi wasione kero katika kulipa kodi na utoaji wa huduma mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupitisha bajeti hii, bajeti hii ikipitishwa tunategemea Serikali na yenyewe inahakikisha inasimamia mapato hayo, ukusanyaji na matumizi. Kila mwaka kumekuwa kukitokea taarifa ambazo CAG anakuja hapa anatuambia umefanyika ubadhirifu hapa, umefanyika ubadhirifu kwenye taasisi fulani, umefanyika ubadhirifu kwenye Wizara fulani, hii haipendezi. Ni kwa nini sasa Serikali isiweke mkakati? Pamoja na kwamba, kuna mechanism kwa maana ya vyombo mbalimbali vinavyozuia suala hili la watu kujiunga na kufanya mbinu ya kujipatia fedha zisizo halali katika miradi mbalimbali na kuanzisha masuala ya rushwa, wizi, ufisadi na mambo mengine kama hayo, kwa nini Serikali isione haja ya kuondoa jambo hili kabisa la CAG kuja kila mwaka na maajabu na maajabu na masikitiko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitisha bajeti hii, lakini Serikali ina mzigo mkubwa. Mheshimiwa mwigulu ana mzigo mkubwa wa kumsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba masuala haya ya rushwa na ufisadi katika miradi mbalimbali inatoweka kabisa. Tufurahie taarifa ya CAG inapotolewa, basi tuone CAG anasema mambo madogo madogo ambayo hayaleti karaha na hayawezi kumuudhi Rais, hayawezi kumuudhi mtu yeyote na Watanzania wanafurahia Serikali yao kwa sababu, inasimamia mapato ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu hatua kuchukuliwa kwa wale ambao wanahusika. Kama kweli mtu kabainika kwa mujibu wa sheria na taratibu, basi wahusika wachukuliwe hatua. Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali wachukue hatua, sio mpaka wasubiri labda Mheshimiwa Waziri au Mheshimiwa Rais ndio aongee, labda ndiyo ionekane, hapana. Kuna watu wanaomsaidia Mheshimiwa Rais, kuna watu ambao wanamsaidia Waziri, kwa nini wasichukue hatua? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)