Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi ya kuchangia hoja ya mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, na wote tuliopo humu ndani tumepewa uhai na Mwenyezi Mungu, tunatakiwa tumshukuru wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuendeleza miradi mbalimbali ya zamani na kuanzisha miradi mipya. Kwanza kuna miradi ya kuchochea uchumi; pili, kuna miradi ya huduma za jamii. Mama huyu amefanya kazi kubwa na kazi zote zinaonekana, mama huyu tumpe maua yake kwa kweli. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha, kwa kazi zao nzuri ambazo wamezifanya kwa kutuletea bajeti yenye mashiko. Bajeti hii ni bajeti nzuri ambayo inakidhi kwa mwananchi wa kawaida, kwa kweli ni bajeti nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi tunampongeza na kumshukru sana mama Dkt. Samia kwa mradi wa EPC+F wa barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale. Barabara hii kwa kweli kila siku nilikuwa nikiinuka, nikisimama hapa nalia na hii barabara. Maswali yangu ya msingi kila siku ilikuwa ni hii barabara. Lakini tunamshukuru sana mama huyu kwa kutukubalia sisi watu wa Mkoa wa Lindi, tumesaini mkataba tarehe 16 Juni; kwa kweli tunashukuru sana, mama ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunamshukuru mama Dkt. Samia kwa kutuletea Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko. Tunashukuru sana, kazi zimeanza kufanywa pale, hatua za mwanzo za ujenzi zinaendelea; tunamshukuru sana mama Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwenye maeneo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna wastaafu kwenda kuhakikiwa mkoani. Sisi wote hapa, asilimia kubwa sisi ni wastaafu, tuko hapa ndani wastaafu wa Serikali. Tunajua kuna wastaafu wengine walistaafu miaka mingi, hali zao za uchumi ni mbaya. Fedha wanayopata ni ndogo sana. inakuaje hili suala la kuhakikiwa kila mwaka watoke kule vijijini wapite wilaya, waende mkoani? Kitu gani kinashindikana Wizara ya Fedha kufanya utaratibu wakafuatwa kwenye wilaya zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hela walizokuwa nazo za mafao yao ni ndogo sana jamani. Niombe sana, kwa mfano umtoe mtu wa Kilima Rondo afike Nachingwea, aende Lindi, aisee, ni mbali sana. Umtoe mtu wa Kilwa huko ndani ndani, afike mjini, aende Lindi, nafikiri hii siyo sawa. Hebu tufanye marekebisho watumishi waende kila wilaya kuwasaidia hawa watu kuhakiki taarifa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kulizungumzia ni ajira ya maafisa ustawi wa jamii, siyo maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii. Sasa hivi kuna matatizo sana ya afya ya akili, watu wengi kutokana na msongo wa mawazo wamekuwa na matatizo ya afya ya akili. Lakini cha kushangaza kwenye nchi yetu hawa maafisa ustawi wa jamii wako wachache sana. Mbaya zaidi hao wachache waliokuwepo wanapewa kazi za maendeleo ya jamii kuzifanya badala ya kazi za ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ndiyo consultants ambao wanatakiwa kuwasaidia watu wenye msongo, watu wenye matatizo ya afya ya akili. Sasa inakuaje badala ya kufanya kazi zao au watu wengine waongezeke, wale wanakwenda kufanya kazi za maendeleo ya jamii? Nafikiri hii siyo sawa. Kwanza tujitahidi maafisa ustawi wa jamii waajiriwe wa kutosha, waongezeke, wako wachache sana. Wale ni watu hot cake, wanatakiwa sana kwa matatizo tuliyokuwa nayo kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine kwa Serikali ni kwa ajili ya tembo. Huyu tembo huyu, kwa jina lingine ndovu, anatuchanganya sana akili. Naona maeneo mengi ya Tanzania wanalalamika kuhusu ndovu. Sasa huko kwetu Mkoa wa Lindi ndiyo kichekesho, maana yake sasa imekuwa ni too much, mpaka saa 12 asubuhi wako nyumbani kwa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekula mazao yote mashambani yamekwisha, wanachofanya sasa hivi wanabomoa nyumba za watu. Juzi kuamkia jana kuna Kijiji kinaitwa Nambalapala huko Wilaya ya Nachingwea, wameingia ndovu wametafuta mashambani mtama, wameshamaliza kila kitu, kilichofuatia wamekwenda kubomoa nyumba kutafuta vyakula ndani. Hivi sasa tutakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, nitoe ushauri wangu mdogo kama wataweza kuusikiliza ili tunusuru wananchi wa Tanzania. Naomba tuweke solar electric fences. Kuna nchi mbalimbali ambazo wamefanya hiki kitu kama India, South Africa, hata hapo Kenya kidogo wameanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoijua Serikali yetu inaweza hiki kitu. Kama tumeweza kuweka umeme sasa hivi tunategemea kila kijiji kutakuwa na umeme, sidhani kama tutashindwa kuweka hiki kitu. Kwa sabbu hizi solar electric fences siyo kila sehemu, ni sehemu zile ambazo zinazungukwa na mbuga za wanyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi solar electric fences zikifungwa vizuri, mnyama yeyote hawezi kuvuka. Wanavyotengeneza pale yule mnyama akisogelea tu karibu na ile fensi kuna kashoti fulani kanatokea, mnyama anaogopa, anarudi ndani. Niombe sana Serikali yangu, najua hii Serikali ni sikivu – iweke hizi solar electric fences kwenye mbuga za wanyama ili kunusuru wananchi hawa ambao tunasumbuliwa na tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yaliyochukuliwa na vikosi vya jeshi 41KJ Nachingwea na kikosi cha JKT hapohapo Nachingwea. Kulikuwa na mashamba ya muda mefu ambayo yanahudumiwa na wananchi pale tangu mababu na mabibi zetu wanahudumia yale mashamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali yetu sikivu iwalipe kiinua mgongo angalau wale watu wapate pesa za kwenda kuanzia sehemu nyingine kununua mashamba. Hali ni mbaya, watu hawana uwezo wa kununua mashamba, hela imekuwa ngumu, ndovu ndiyo kama hao, vyakula mashambani hakuna, hali ni mbaya. Tunaomba wasaidiwe watu hawa walipwe ili waweze kusaidiwa kupata hela kwenda kununua maeneo mengine. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Chinguile, karibu.
TAARIFA
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza sasa kwamba haya maeneo ambayo wananchi wana mgogoro na Jeshi letu la Wananchi, siyo tu kwamba wanapaswa kulipwa, maeneo haya kumekuja na taarifa mbili tofauti. Taarifa za awali ni kwamba walielekezwa watapata malipo, lakini taarifa nyingine walivyokuja maafisa wengine wa Jeshi wakaeleza kwamba eneo hili hawatalipwa. Kwa hiyo kwa sasa wananchi wamebaki bila kujua hatma yao ni nini. Naomba kumpa taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, taarifa unaipokea?
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matengenezo ya viwanja vya ndege; Kiwanja cha Ndege cha Lindi Mjini na Nachingwea. Tunaomba viwanja vile vitengenezwe. Nimeangalia kwenye bajeti sijaona, sijui labda kama macho yangu yamekuwa yana matatizo. Tunaomba viwanja hivi vitengenezwe kwa sababu sasa hivi tunategemea mradi mkubwa sana wa gesi pale Lindi tusije tukatia aibu viwanja vikiwa vibaya jamani. Tunaomba tuangaliwe kwa macho mawili, tutengenezewe viwanja hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia pia suala la ofisi za CAG. Kila mwaka na kila siku tunazungumza masuala haya, tukiangalia kwenye ripoti za CAG makosa mara nyingi ni yaleyale yanajirudia kila mwaka. Leo utaona kosa hili, ikija ripoti ya mwakani kosa ni hilohilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipendekeze kitu kimoja; hawa ma-internal auditors walioko kule nafikiri wanashindwa kufanya vizuri kazi zao. Ombi langu kwa Serikali, hawa maafisa wa CAG sasa wapelekwe kila Wizara ili waende kushauri kule na kupunguza haya matatizo. Tupunguze hoja nyingi zinazojirudia kila siku kuja Bungeni. Tunaona makosa yanayotokea kwenye ripoti zile za CAG kila siku yanarudi yaleyale. Mnashauri vizuri, Bunge tunakaa tunashauri lakini inapokuja ripoti ya mwaka mwingine yaleyale tena. Sasa inakuaje?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)