Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024. Kwanza kabisa, nichukue nafasi ya kuipongeza Serikali kwa kuchukua hoja nyingi sana za Wabunge katika kupanga Bajeti yake. Pia jioni ya leo nitaongelea maeneo mawili ambayo ndio hasa napenda kuyaongelea yaliyochukuliwa katika bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kabisa ni ile ambapo Serikali imedhamiria kuanzisha akiba ya dhahabu kupitia Benki Kuu. Katika ukurasa wa 18, hotuba ya Waziri inasema, naomba ninukuu: “Serikali imekamilisha taratibu za kununua dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kuanzisha akiba ya dhahabu ya Taifa.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii ni njema kwa sababu kwanza itaimarisha sarafu yetu ya Tanzania, lakini pia ni akiba kwa vizazi vijavyo, yaani hata kama migodi ya dhabu itaisha, lakini tutawapeleka watoto wetu na vizazi vijavyo kwenye vault na kuwaonesha kwamba hebu angalieni urithi wenu. Kwa hiyo, hilo ni jambo la kupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani Mheshimiwa Waziri afanye mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa kule Benki Kuu ya Tanzania kuna kilo 418 ambazo zimekuwa zikitaifishwa kwa sababu ya makosa ya utoroshaji na kwa sababu sheria inasema kwamba, ukipatikana umetorosha hiyo itataifishwa. Sasa hizi kilo 418 zina thamani ya bilioni 53.2. Pendekezo langu achukue hizi kilo 418 apeleke zikasafishwe (refinery) ili iwe kianzio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ili pendekezo la Mheshimiwa Waziri liweze kuthibitika, yaani maneno yake yathibitike kwamba Serikali inaanza, kwa nini asitaje kwamba mwaka huu anaanza na kilo ngapi katika kuanzisha akiba ya dhahabu ya Taifa? Nadhani hapo atakuwa ametenda haki kuliko yaendelee kubaki kama maneno kwenye makaratasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niongelee uanzishwaji wa Tume ya Mipango. Hili pia ni jambo ambalo limeongelewa sana na Wabunge wengi na tumeona Serikali imelichukua na hatimaye kuliweka katika utekelezaji na katika hili tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna matarajio ya wananchi katika uanzishwaji wa Tume ya Mipango. Moja kabisa, tunataka kuona kwamba Tume yetu inaondoa duplication of efforts (kurudiwa rudiwa jambo kufanywa na Wizara zaidi ya moja lakini jambo ni lile lile). Wakati fulani nilikwishasema hapa kwamba, Wizara ya Maji imekuwa ikijenga mabwawa, Wizara ya Mifugo nayo imekuwa ikijenga mabwawa, lakini Wizara ya Kilimo, kazi hiyo hiyo. Hebu tuombe sasa kwa sababu ya kuwepo kwa Tume ya Mipango hii duplication iweze kuondolewa na tuweze kupata tija kuliko mradi unaofanana ukafanywa na Wizara zaidi ya moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba tunategemea Tume yetu ya Mipango iweze kuiangalia nchi na Jiografia yake na idadi ya watu waliopo na maendeleo yaliyokwishafanyika katika eneo lile na maendeleo yanayohitajika. Mifano ambayo ni halisi, Jimbo moja unaweza ukakuta lina kata nne lakini Jimbo lingine lina kata 45, lakini wote wanasema wanapewa kilometa moja ya lami, kwa nini? Yaani kata nne, kata 45 kilometa moja ya lami? Hapana. Au VETA moja, hii inawezekanaje? Tunategemea Tume yetu ya Mipango iweze kuondoa kutokuwa na usawa katika maeneo kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta hapa nchini kuna wilaya moja ina kilometa saba tu za lami tangu iwepo, nyingine ina kilometa 200, lakini zote ziko katika nchi moja. Tunategemea Tume yetu ya Mipango iweze kuangalia mahali ambapo pako disadvantaged ili waweze kushiriki keki ya Taifa sawasawana hili linajenga umoja wa Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, wakati mwingine utakuta mikoa mingine inazungukwa na Maziwa makubwa lakini huduma ya maji ni hafifu katika maeneo hayo. Tunategemea Tume yetu ya Taifa iliangalie hili ili kuweka msawazo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, wakati mwingine zao moja linapokuwa linapata bei nzuri katika soko, utashangaa mikoa yote ya Tanzania wanataka wawe wakulima wa zao hilo hilo. Hii haiwezekani lazima kuwe na kanda za ikolojia na mazao yanayostawi katika eneo husika ndiyo yalimwe. Sio kwamba Tanzania nzima baadaye tunakuja tunakuta kwamba kuna mikorosho kila mahali, hapana hii haiwezekani. Kwa hiyo, tunategemea Tume yetu ya Mipango iangalie hali ya hewa, wingi wa mvua, joto, halafu iseme jamani hapa sio pa korosho, hapa ni pamba ni hivyo na si vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matarajio ya Tume ya Mipango, katika mipango yake ya kitaifa, napenda sana Tume ya Mipango izingatie cultural integration, nilikuwa natafuta neno zuri hapa mwingine akanishauri kwa kuniambia ni mwingiliano wa kiutamaduni. Hili naomba nilisema hivi, tulipo hapa wote, Taifa hili lina makabila 120 lakini limeweza kulinda umoja wake kama tulivyo kwa sababu ya mwingiliano ambao tumekutana JKT, vyuoni na wengine tumeoana na kuoa kwa kuingiliana hivyo na tukalinda umoja wetu wa kitaifa na ndio maana hapa hakuna mgogoro ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kuna shule za Kata. Kwa hiyo mtu atasoma primary pale pale, secondary pale pale, halafu utakuta watu wanasema naomba mkoani kwangu peleka chuo kikuu. Kwa hiyo, mtu atakuwa m-local akiwa m-local utashangaa tunajenga ukabila na ukanda. Kwa hiyo, lazima katika mipango ya kitaifa kuwe na vyuo ambavyo vitabaki katika Kanda moja ili watu tuendelee kuingiliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la sivyo, kinyume chake utakapotengeneza Taifa la wa–local wenye ukanda mmoja, wa kabila moja kwa sababu tangu primary mpaka chuo kikuu kama ni Kagera yaani ni hao wenzako tu hao hao, hapana. Lazima tuangalie cultural integration kiasi kwamba tuendelee kuingiliana. Kwa hiyo, katika mipango yao lazima waangalie kwamba inapofikia level fulani tuwaruhusu watu waende sehemu nyingine ili tuendelee kuingiliana ili tuweze kuendelea kujenga umoja wa kitaifa, tuondoe ukanda, tuondoe ukabila. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo matarajio yetu katika utendaji kazi wa Tume ya Mipango ambayo tunaamini itapewa meno na kuweza kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)