Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi, nishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa Bajeti ambayo hii tunaendelea nayo. Hii inatupa moyo sana na ninaanza kwa kuiunga mkono Bajeti hii mpya ambayo tunakwenda nayo kwa sababu Bajeti iliyopita imetufanyia makubwa na imewatekelezea wananchi kazi kubwa za kimaendeleo kwa maana hiyo ninaanza kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Bajeti hii kwenye vipengele vingi lakini hasa hususan hapa kwa kuondoa ada kwenye vyuo vya ufundi kwa kweli umewapunguzia, Serikali imewapunguzia sana mzigo wananchi lakini pia kwa kuweka mikopo katika vyuo vya kati kwa kweli wazazi wamepunguziwa mzigo mkubwa na watoto sasa wana uhakika wa kwenda shule. Kwa hiyo kwa ujumla niipongeze Bajeti ni nzuri na ni ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina baadhi ya ushauri wa mambo ili twende sawa. Katika utekelezaji wa Bajeti iliyopita bado kuna miradi ambayo haijakamilika kwa sababu tofauti tofauti. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba miradi ile inakamilika, tuangalie vipaumbele vyetu ambavyo tuliviweka halafu tuhakikishe vinakamilika. Mfano miradi ya maji, iko miradi ya maji ambayo inaendelea katika majimbo yetu. Ni vyema ile miradi ya maji tuhakikishe tunapoelekea mwisho huu wa bajeti tuhakikishe ile miradi inawekewa mipango mizuri ya kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya maji wakandarasi wamekuwa ni dhaifu sana, wamekuwa hawana uwezo na hata wakipewa fedha na Serikali wanakimbia kimbia. Sasa sijajua hii miradi ambayo wakandarasi wamepewa hela na Serikali wanakuwa na visingizio. Mfano kuna miradi miwili ya maji visingizio vikubwa vinakuwa ni ukosefu wa mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii inachukua muda mrefu sana. Mradi wa shilingi milioni 800 unatekelezwa toka Bajeti ya mwaka wa kwanza, mwaka wa pili na mwaka huu unakwenda ni wa tatu lakini Bajeti hiyo inaendelea kutekelezwa, kutekelezwa mpaka sisi sasa wawakilishi wa wananchi tunashindwa kwenda kufanya mikutano kule kwa sababu kila siku ukienda hadithi ni hiyo hiyo. Kwa hiyo, nataka hili hebu lifanyiwe kazi na liishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano pale kwetu kuna wakandarasi wawili walipewa hela na Serikali lakini visingizio mwaka mzima mabomba hakuna. Sasa kama mabomba hakuna lazima Serikali ione namna ya kuikwamua hii miradi ili wananchi waanze kufikiria miradi mingine. Lakini miradi mingine kama mradi ule wa mjini tunaishukuru Serikali juzi imetoa shilingi milioni 600, certificate ya yule mkandarasi na amepata matumaini ya kuendelea na mradi. Mradi uko 72% na zaidi lakini alikwama kwa sababu fedha zilichelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba miradi hii ambayo ni muhimu sana, ni miradi ya kimkakati ambayo Mheshimiwa Rais ameweka ahadi ya kuwatua ndoo wakina mama kichwani tuiangalie lakini miradi mingine ni miradi ile ya visima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Bajeti mwaka wa kwanza, mwaka wa pili na huu ni mwaka wa tatu. Mwaka wa kwanza tunachimba visima, mwaka wa pili tunafanya feasibility study, mwaka wa tatu ndiyo tunaanza usambazaji. Jambo hili linatukatisha tamaa, ni bora miradi hii yenyewe siyo gharama kubwa sana. Mradi wa kuchimba kisima na kusambaza kwenye mitaa yetu yawezekana shilingi milioni 150.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri Serikali inapokuja na miradi ya namna hii ya muhimu ya maji basi ije na mradi uliokamilika, wachimbe kisima kwa wakati huo huo wakati wana chimba kisima, basi wataalamu wawe wameshafanyia feasibility study ili waanze kusambaza kuliko kisima kinakaa mika mitatu hakijapelekewa fedha za usambazaji. Kwa maana hiyo tuna visima zaidi ya 10 kwenye Jimbo la Kondoa Mjini vinahitaji usambazaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, safari hii kwa Bajeti hii tutachimba tena visima vingine, vile vya mwanzo hatujavisambaza. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri Serikali hebu iangalie miradi yote ambayo tayari imekwisha peleka fedha nyingi basi tuimalizie kwa kuikamilisha ili iweze kuanza kutumika na tuanze kubuni miradi mingine kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo jingine la kukumbusha. Ilani ya CCM bado nazungumzia Barabara inayotoka Tanga kuja Mrijo kwenda Kwa Mtoro kwenda Singida. Ninaamini Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiyo Mwenyekiti wa CCM anaifahamu barabara hii ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na imetamkwa vizuri sana itatoka Mondo itakuja Mpaka Bicha. Sasa tumeweka juzi tulihudhuria sherehe ya kusaini mkataba wa hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matamko ya Mheshimiwa Waziri kile kipande hakijatajwa. Ninashukuru kwenye Hotuba ya Bajeti kipo nimekiona. Kwa hiyo, nadhani Serikali izingatie ule Mpango uliopo kwenye Ilani ya CCM kwa maana hiyo ninaomba wakati tuanendelea kujenga ile barabara tujue kabisa barabara iliyotajwa kwenye Ilani ya CCM inatoka Mondo kuja Bicha na yenyewe izingatiwe katika hii hatua hii ambayo tumesaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tumekuwa tukizungumza mara kwa mara hili Daraja la Munguri B. Ni muhimu sana daraja hili likajengwa mapema kwa sababu sisi Wanakondoa na Watu wa Hanang’ tunalitegemea sana kwenye shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi alikuwepo Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo katika Jimbo langu kuzungumzia na alimwita mtaalamu kuzungumzia. Sababu ambazo zinatolewa haziridhishi kusema kwamba daraja lile lisijengwe. Wamekwenda kufanya feasibility study kwenye eneo refu la mita 500 wakati daraja la awali lilikuwepo mita 100 ambalo linaweza likatumia fedha ndogo ambayo walikuwa wanaangalia kwamba economic not viable wakashindwa kulijenga kwenye hiyo mita 500 ilitakiwa wale wataalamu wangeenda kuchukua vipimo kwenye eneo la zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa lazima wataingia gharama mara mbili. Wamekwenda kufanya uchunguzi lakini wamekwenda wamekuja na matokeo ambayo Serikali wanasema haiwezi kujenga daraja kwenye eneo lile ni refu wanatakiwa waanze tena upya kuja kupima kwenye eneo la zamani ambalo ni mita 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa kwa nini kwa gharama ile ile wasingepima kule pafupi ili wafupishe huu mlolongo mrefu wa kujenga hiyo daraja? Daraja hiyo inapoteza magari ya watu yanazama, watu wana umia, watu wanaingia gharama kuvushwa kwenye daraja lile hata kama haifai kiuchumi lakini Serikali yetu lazima ijue maeneo yale ni maeneo ya wananchi na wananchi wanaingiza vipato kwa kilimo ng’ambo ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishapeleka fedha eneo lile kwenye Pori la Swagaswaga. Wamejenga mageti, wamejenga hosteli unasemaje sasa tena kiuchumi haifai wakati tayari umekwishapeleka fedha upande ule? Kwa hiyo, lile daraja likijengwa hata hao watalii ndiyo watapita, vinginevyo masika yote hata kama tutakuwa na watalii hawawezi kupita kwa sababu daraja linapitisha maji na mto unapitisha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara ya Ujenzi ichukulie serious ujenzi wa daraja hili ambalo linaunganisha mikoa miwili Dodoma pamoja na Mkoa wa Manyara. Kwa hiyo nilikuwa nakumbusha hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na ujenzi wa sekondari unaendelea huu wa mradi wa SEQUIP, tulikuwa na ile awamu ya kwanza tunashukuru Serikali ilituletea fedha. Jimboni kwangu tumekamilisha ile sekondari na leo wanafunzi wanasoma kidato cha kwanza na kidato cha pili, tunasubiria basi ile awamu nyingine ya pili. Na sasa hivi halmashauri ndio hivyo zinakwenda kufungiwa yao tunakwenda kumaliza. Sina uhakika kwamba hizo fedha zitakuja katika kipindii hiki kabla mwaka wa bajeti haujaisha ama tutatarajia zitakuja kwa mwaka mwingine unaofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tujenge sekondari nyingine hiyo Kata ya Bolisa ambayo miaka mingi wamekuwa wakisubiri kata yao wanakwenda kusoma kata nyingine. Kwa hiyo tunataka tujue sasa ile fedha itaingia sasa au tutaivusha kwenda kwenye bajeti? Na kama tukiiivusha mwaka unaofuata sekondari tutajenga nyingine? Kwa hiyo nilitaka nifahamu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kufanya kazi nzuri ya uhifadhi. Leo ukiona Waheshimiwa Wabunge wote wanalalamika tembo wamekuwa wengi maana yake Wizara imefanya kazi kubwa ya kuwalinda hao tembo ambao walikuwa wanakwenda kupotea kutokana na majangili. Tunawapongeza sana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa namna walivyoweza kulinda hifadhi zetu mpaka leo sisi Wabunge wote takriban, maeneo mengi tunalalamika tembo wamekuwa ni kero maana yake kazi yao wameifanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kinachotakiwa kufanyika ni lazima sasa ipangike mikakati kama Serikali tumeweza kupanga mikakati mizuri ya kuhifadhi hifadhi zetu wanyama wetu leo wameongezeka basi wasije wakawa tena kero kwa wananchi. Bajeti hizi zinatakiwa zizingatie mambo haya. Kwamba tumeweza kuhifadhi sasa, tembo wamekuwa wengi ni namna gani tunaweza kuwadhibiti tena isiwe ni dhahma kwa wananchi. Maeneo mengi na Serikali inatumia fedha nyingi sana kwenda kulipa vifuta jasho na vifuta machozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa kwenye jimbo la dada yangu Dkt. Ashatu Kijaji juzi wakati wa Katibu Mkuu, mwananchi anaongea kana kwamba sasa anajua kabisa anakwenda kulima, nikishalima tembo watakuja kula Serikali ijiandae kulipa kifutamachozi sio sawa. Kwa sababu kifutamachozi chenyewe kinachotoka tunafahamu wote hakitoshi. Mtu analima heka kumi analipwa hela za kununua gunia mbili; hii haifai. Kwa hiyo Serikali iweke mikakati mizuri ya kuwadhibiti hawa tembo kwa sababu wamekuwa waharibifu. Ikiwezekana kama wanauzika watangaze soko, wawauze tembo kwa mwenye kuwataka ili wapungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nashukuru sana ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. (Makofi)