Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwanza naomba kusema naunga mkono hoja zote mbili; hoja ya kuibadilisha Kigosi kuwa Hifadhi ya Misitu na hoja ya Kurekebisha Mipaka ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, nimepata bahati ya kufika Kigosi na ukubwa wake wa hizo takribani square kilometer 8,000 lakini nimepata bahati pia ya kufika Ruaha. Nafahamu mateso waliyokuwa wanayapata wananchi wa vijiji vinavyozunguka Ruaha hasa inapotokea mgongano wa kifikra kati ya Wahifadhi na wananchi na lengo ni jema.

Mheshimiwa Spika, kazi tuliyowapa wahifadhi ni kuhakikisha kwamba maeneo tuliyowapa yanalindwa, lakini pia lazima tukubali kwamba kutokana na nchi yetu kuendelea kuongezeka kwa watu imekuwepo haja ya watu kwenda kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ambako kweli ndio maeneo yenye rutuba na maeneo yenye uzalishaji wenye uhakika kwenda kutafuta maeneo ya kilimo. Kwa hiyo kuridhia kurekebisha mipaka ni kuepuka kesi zisizo za lazima, lakini pia kuridhia kurejesha Pori la Kigosi kwa TFS ni kuruhusu shughuli zingine za kiuchumi ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo ambayo Kigosi ilikuwa inazunguka wanarudishiwa maeneo yao kwa sababu historia inaonesha mwaka 1983, Serikali ndio ilibadilisha kuwa Game Reserve na baadae imekuja tukabadilisha ikawa National Park na Sheria zetu zilivyo hazitambui sana kwamba wananchi wa asili ya maeneo haya walikuwa wanafanya kazi gani.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa asili ya maeneo yale ambao kwa asili, maeneo yale ninayoyazungumzia yana watu wa Makabila ya Wasumbwa, Wasukuma, Waha, Wanyamwezi na Wasubi. Hawa ni wafugaji wa nyuki na walinaji wa asali. Kwa hiyo tulipobadilisha sheria tukaweka kizuizi na hii ilikuwa ni kazi kubwa ya kiuchumi na ukiangalia ndio maeneo ambapo Wizara pia ilipeleka Viwanda vingi vya asali kwa ajili ya ku-capture soko la China. Kwa hiyo tulikuwa tumezuia kazi za kiuchumi lakini tulikuwa tumetengeneza mradi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa haiwezekani kabisa watu wakaacha kwenda, walikuwa wanaingia na wakiingia wanakamatwa, kwa hiyo tukajikuta tumegeuza makosa kuwa chanzo cha mapato na kwa sababu watu hawawezi kuacha ndio kazi ya uchumi walikuwa wanaingia. Kwa hiyo maamuzi haya ni maamuzi sahihi, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Kamati kwa kuridhia jambo hili liweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, tunapobadilisha kuwa msitu, hatumaanishi kwamba tunakwenda kuua uhifadhi, bado TFS wana wajibu wa kuendeleza ikolojia ya eneo lile kwa sababu hata TFS wana utalii unaitwa eco-tourism ambao unahusisha utalii wa ikolojia na katika maeneo yote yaliyohifadhiwa wanyama wamo. Kwa hiyo bado TFS wanaweza kulilinda eneo hilo likaendelea kuwa na wanyama na likaendelea kufanya utalii, lakini likaendelea kuruhusu wananchi kufanya kazi ambazo hazina athari kubwa kwenye misitu.

Mheshimiwa Spika, wito wangu hapa ni kwamba utaratibu huu uangaliwe pia na maeneo mengine. Nataka kutoa mfano, niliwahi kutembelea Ugala nikakuta kuna mto pale ambao ni mto unao-feed Ziwa Tanganyika. Wakati wa kiangazi ule mto unakauka unaacha mabwawa, yale mabwawa yanakuwa na samaki wengi sana, kwa hiyo wananchi wanavizia kwenda kuvua kwa kuiba, lakini wale samaki wasipovuliwa wanakufa kwa sababu maji yanakauka na wanakufa wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sasa unaona sheria inazuia watu wasiende kuvua samaki, kiangazi kikiwa kikali samaki wanakufa wenyewe, kwa hiyo tuangalie utaratibu ambapo hata ndani ya National Park kama kinachoenda kufanyika hakina madhara kama ni uvuvi wa samaki watu wakavue samaki. Kwa sababu kwa nature ilivyo hata usipowavua wewe watakufa, kwa hiyo jambo hili litufundishe.

Mheshimiwa Spika, la pili, mchango mkubwa wa wananchi kwa maeneo husika. Tunatarajia kwamba baada ya kuwa limerudishwa TFS wananchi wa maeneo yale kwa sababu ni misitu mikubwa watafaidika pia kwenye mazao mengine ya misitu.

Mheshimiwa Spika, nitoe angalizo kidogo, Kigosi ni catchment area kubwa ya Malagarasi…

SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu hicho kisemeo chako ukishika na mkono wa kulia kinazuiwa, kwa hiyo sauti haitoki vizuri. Ukishika na mkono wa kushoto unatusaidia tunakusikia vizuri zaidi.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nilikuwa nasema kwamba pamoja na kuunga mkono nataka kuishauri Serikali mambo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, Kigosi ni catchment area ya Malagarasi ambayo Malagarasi ndio inayotengeneza maji yanayokwenda mpaka Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, tunapoirudisha TFS jukumu la kuendelea kulinda ikolojia ile na uasili wake, lifanyike kama ambavyo lilikuwa linafanyika lilipokuwa chini ya TANAPA.

Mheshimiwa Spika, la pili, Kigosi ni makazi ya wanyamapori na hawa wanyamapori hawatajua kwamba tumebadili Sheria tumewatoa TANAPA, watabaki kwenye misitu na wataendelea kuingia kwa wananchi. Tuliwahi kuishauri Serikali kwamba TFS lazima wajiandae kuthibiti wanyamapori walio kwenye misitu yao. Kuna tembo wa kutosha, kuna simba wa kutosha ambao wakiondoka TANAPA, wakaondoka wale watu wa Game Reserve wakabaki TFS lazima wajiandae kisaikolojia kwamba hawa simba waliokuwa wanazungumzwa hapa wataingia kwenye hizo wilaya zingine. Kwa hiyo lazima jambo hili lifanyiwe uwekezaji wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, la tatu, kuna misitu minene ambayo ndio chanzo cha mvua cha Mikoa ya Kigoma, Geita, Kagera na Tabora. Kwa hiyo aina yoyote ya matumizi lazima iwe rafiki kulinda ikolojia hii kwa sababu tunapofurahia mvua lazima tujue mvua inatoka kwenye misitu.

Mheshimiwa Spika, la nne, niipongeze kwa kweli Wizara, eneo lile tuna hifadhi nyingine nyingi. Tunazo Hifadhi Burigi Chato, Rubondo, Ugala, kuna Game Reserve ya Moyowosi, sasa ni muda wa kuwekeza kwa nguvu kubwa Ugala kwenye National Park ili watalii waweze Kwenda. Nasema hivi kwa sababu hatuwezi kujisifia kwamba kuna watalii kumi tu walienda, hapana, lazima tujue kwa nini watalii hawaendi. Kama watalii wanasafiri kwenda kuangalia magofu Vietnam na wapi, tuwalete Ugala ili waweze kufaidika na ikolojia iliyopo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)