Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Mimi nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mzuri na kwa maono yake makubwa aliyonayo kwa Watanzania hasa kwa kuendelea kufungua fursa kwa Watanzania kujiajiri kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze na Waziri wa maliasili na utalii pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo na kwa kweli kwa kuweza kutafsiri maono na mapenzi makubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania. Sasa tunaona kwamba sasa baada ya Mama kuleta unafuu kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji hapa nchini sasa leo ameangazia eneo la wafuga nyuki na eneo hilo sasa naona linachagizwa na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Naibu Waziri wake kwa kweli mnastahili maua yenu, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaingia kwenye mchango wangu nikupongeze wewe Spika wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Tulia kwa uongozi wako mzuri. Ni vizuri tusiwe tunasemea pembeni, tukupongeze hapa usikie na hata Wananchi wa Mbeya wasikie kwamba Wabunge tunakukubali na Watanzania wanakukubali na wewe unastahili maua yako, hongera sana kwa kazi nzuri, ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme ninaunga mkono hoja mazimio yote mawili azimio la kurekebisha mipaka ya Ruaha, vilevile azimio la kushusha Kigosi kutoka kwenye Hifadhi ya Taifa kwenda kwenye Mamlaka ya Hifadhi za Misitu Tanzania (TFS).
Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba maamuzi haya na maazimio yote haya mawili yanakwenda kuleta unafuu mkubwa sana kwa Watanzania. Mathalani kule Ruaha migogoro ilikuwa ni mingi sana Watanzania tulikuwa tunashuhudia watu wanagombania mipaka sasa azimio hili la kwenda kurekebisha hiyo mipaka huu ndio mwarobaini wa kwenda kupeleka suluhisho la kudumu kwa wananchi wale waweze kufurahia kuishi ndani ya Taifa lao.
Mheshimiwa Spika, nikija upande wa Kigosi niseme tu kwamba Mataifa ya Kongo, Rwanda na Burundi kwa sehemu kubwa yamekuwa yaki-import asali inayotoka kwenye Hifadhi ya Kigosi. Sisi wananchi wa Ngara ni watumiaji wazuri sana wa asali. Asali yote tunayoitumia Ngara tumekuwa tukinunua asali inayozalishwa pale Kigosi.
Mheshimiwa Spika, mathalani na wananchi wote wa Kanda ya Ziwa na wale wa Mkoa wa Kagera wote tumekuwa tukitegemea asali ambayo imekuwa ikilinywa pale kwenye Hifadhi ya Kigosi. Sasa kitendo cha kuondoa hifadhi hii kutoka kuwa Hifadhi ya Taifa na kwenda kuwa hifadhi ya misitu kinakwenda kufungua ajira kwa Watanzania zaidi ya 5000 ambao hawa wanakwenda kujiajiri moja kwa moja kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo ufugaji wa nyuki kwenye eneo lile la msitu.
Mheshimiwa Spia, kuna Watanzania zaidi ya 10,000 ambao wanakwenda kupata ajira indirectly kutokana na uwekezaji wa Watanzania ambao wanakwenda kuwekeza pale kufuga nyuki.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa na nia nzuri kabisa kupitia TFS ambapo viwanda vitano vimejengwa kwa ajili ya kuchakata asali mbichi na kwa siku moja viwanda hivi vilikuwa vinachakata zaidi ya tani nne ya asali ambayo inazalishwa na hawa wananchi waliojiajiri eneo lile. Kwa mwaka mmoja viwanda hivi vilikuwa vinauwezo wa kuchakata tani za asali 1460.
Mheshimiwa Spika, tani moja ya asali inauzwa shilingi 4,000,000, sasa ukizidisha kwa mwaka mmoja ni takribani eneo hili lilikuwa linazalisha shilingi 5,800,000,000 kutokana na uwekezaji ambao wananchi wanaofugia asali mle wameufanya. Lakini eneo hili mara tu baada ya kuchukuliwa na TANAPA likawa chini ya Hifadhi ya Taifa shughuli zote hizi zilisitishwa.
Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi hebu fikiri kwa mwaka huu pekee watalii waliokwenda Kigosi ni watalii kumi, imagine nchi yetu inawekeza pale tumewalipa watu mishahara watu wanaweka mafuta kwenye magari wanafanya kampeni promotion mwaka mzima wanapatikana watalii kumi huku tumezuia Watanzania kutengeneza shilingi 5,800,000,000 kwa mwaka. Kwa kweli yalikuwa ni maamuzi ambayo yanaturudisha nyuma bdala ya kwenda mbele.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi ambacho eneo hili limekaa chini ya TANAPA tumepoteza shilingi bilioni 30, ukifanya mahesabu zaidi ya bilioni 30 zimepotea. Sasa kwa kweli dhamira nzuri ya Serikali inaonekana pale ambapo Serikali inafanya cost benefit analysis inaonyesha kwamba tukiendelea hivi hasara yake ni kubwa lakini tukifanya hivi tunaenda kupata faida tunaenda kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati ya moyo wangu nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi mazuri aliyoyafanya tunakwenda sasa kuwasaidia Watanzania waweze kujiajiri kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe na watu wa TANAPA hili liwe funzo kwao yako maeneo mengine ndani ya nchi hii kwa mfano Hifadhi ile ya Manyara eneo lile la Mayoka. Eneo lile lina vein zina madini ya vito, yale Madini ya Vito uchimbaji wake hauhitaji matumizi ya kemikali ni kuruhusu mtu anakwenda na greda anachimbua analeta kadude kamoja kadogo kanauzwa mpaka Dola laki moja. Nchi yetu tuko katika wakati ambapo tunahitaji fedha lakini yaani TANAPA wakisikia mtu yoyote anazingumzia hilo eneo wanatamani kukukamata hata kabla hujafika huko. Kitendo tu cha kuzungumza kwamba eneo fulani ni potential kwa nchi hii linaweza likatumika kusaidia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kazi nzuri uliyoifanya huko Ruaha na huko Kigosi inaonekana na inaenda kuleta matunda makubwa kwa Watanzania. Katika eneo hilohilo Mheshimiwa Waziri endelea basi ruhusu hata Taasisi za Serikali ziende zifanye utafiti tujue tuna-reserve kiasi gani tujue kama Taifa madeni tunayodaiwa nje ya nchi tunaweza tukawekeza kidogo eneo lile tukapata fedha nyingi tukaingizia Serikali fedha na tukaenda kutatua matatizo ya Watanzania. Kaeneo kenyewe kako mwishoni mwa Hifadhi ya Manyara hekta zenyewe hata 2000 hazifiki hata ukikata hekta 200, 300 Watanzania wataweza kuwekeza pale na tutapata fedha. Maamuzi yaliyofanyika Ruaha na Kigosi ikawe fundisho watu wa TANAPA fungueni moyo wenu muone kwamba haya mambo yanawezekana na hii iwe ni mwanzo wa kuangalia maeneo mengine potential kwa ajili ya Taifa letu ili yaweze kuachiliwa ili uwekezaji ufanyike na nchi yetu iweze kupata faida kutokana na rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu alitujalia.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya ninakushukuru sana kwa fursa hii niseme tu ninaunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)