Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii kuchangia katika Azimio hili hasa la Kurekebisha Mpaka katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye baada ya kuingia tu madarakani jambo la kwanza lilikuwa ni kupitia ile migogoro 975, mmojawapo ukiwa ni huu wa Hifadhi ya Ruaha na alielekeza Kamati ya Mawaziri Nane kutumia busara na hekima katika utatuzi wa migogoro hiyo. Pia akatuasa tusilete taharuki katika suala nzima hili. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, niwashukuru Wabunge ambao walianza kwa kuleta hoja hizi ambazo zilikwenda kuzaa hiyo Kamati ya Mawaziri Nane. Vilevile niishukuru Kamati, kwanza kwa kuunga mkono Azimio la Serikali lililoletwa hapa kwa sababu Kamati pia imeunga mkono na wachangiaji wengi walikuwa wanaunga mkono. Kwa hiyo, nawashukuru pia kwa kuliona hilo.

Mheshimiwa Spika, katika hoja za Kamati ambazo zimeletwa pamoja na wajumbe waliochangia nitajikita katika chache ambazo nataka kuzitolea ufafanuzi ambazo wameulizia. Jambo la kwanza ni suala la fidia ambayo wamelizungumzia. Nataka tu niseme ya kwamba kazi ya fidia mpaka sasa hivi imeshafikia karibu asilimia 80, watu wameshafikiwa kwa ajili ya kuweza kutathminiwa maeneo yao watakaokwenda kulipwa.

Mheshimiwa Spika, malipo watakayokwenda kulipwa ni pamoja na posho ya makazi ambayo watapewa posho ya pango la nyumba kwa miezi 36, kwa maana ya kufika kipindi kile atakachokuwa anaandaa makazi mengine aweze kupata pesa za kupanga, lakini atalipwa posho ya usumbufu, atalipwa posho ya usafiri atalipwa thamani ya ardhi yake pamoja na thamani ya nyumba. Haya yote yanafanyiwa tathmini na tayari asilimia zaidi ya 80 wameshafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwatoe hofu tu Waheshimiwa Wabunge walikuwa wamesema kazi hii ikamilike haraka, nadhani tunaenda nayo vizuri. Vile vile, jambo lingine ni suala zima la ule mpaka, baada sasa ya kubadilisha mipaka ya GN 28, zoezi la kuweka zile beacon katika mpaka limekamilika. Beacon zaidi 671 zimewekwa katika mpaka wa urefu wa kilometa 344, lakini na mkuza pia ambao wamesema uwekwe, mpaka sasa umewekwa kwa kilometa 177. Haujakamilika wote kwa sababu tu ya hali halisi ya hewa, kulikuwa eneo lingine lina maji hawawezi kuweka mpaka ule, kwa hiyo sasa hivi kwa sababu pameanza kukauka baadhi ya maeneo basi watamalizia. Kwa hiyo, mkuza nao umebaki asilimia kidogo kuweza kumalizia. Kwa hiyo, haya yote yanafanyika kwa sababu ni masuala ambayo ni maelekezo pia ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa, lakini wakaomba pia na ile suala zima la kutenganisha maeneo hayo ili yasilete mtafaruku mwingie.

Mheshimiwa Spika, katika zoezi hili zima hasa katika kuweka mpaka, wananchi kule wameshirikishwa sana kwa maana ya kwamba Uongozi wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa Ndugu Homela alikuwa pale kwa muda wote katika suala zima hilo lakini uongozi wa wilaya pia wameshirikishwa. Kwa hiyo, mpaka huu mpya uliowekwa umeshirikisha hawa wengine. Kwa yale ambayo sasa hivi pengine Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanaona labda hayajakaa sawa sana, kama Serikali nadhani bado tunao muda wa kuweza kutafakari vizuri kuyafanyia kazi. Kwa sababu kazi hii tumeifanya kwa muda mrefu, mpaka kufikia hapa kazi imefanyika vizuri.

Mheshimiwa Spika, rai yangu ambayo naitoa tu na kuwaomba Waheshimiwa Wabunge waelewe kwamba, kazi tuliyotoa ile ya hekta zaidi ya 74,000 kwa wananchi tukienda kuifanyia mpango wa matumizi bora ya ardhi tutaweza kubaini nani anapata heka ngapi na nani atapata za kilimo na kwa maana ya wafugaji. Kwa hiyo zile hekta mpaka sasa hivi bado hazijagawiwa katika yale maeneo, kwa sababu ukikamilisha hili moja basi na mpango wa matumizi ya ardhi unaanza. Tusingeweza kufanya mpango wa matumizi ya ardhi kama hata azimio lenyewe halijapita na hatuweza kujua mipaka imefikia wapi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe rai tu kwamba, tupitishe azimio hili ii twende kule tuwapange wananchi vizuri, wale wafugaji ambao wameachiwa eneo la Ruaha kule waweze kupangwa vizuri, lakini na wananchi hawa ambao wanatakiwa pia kupangwa katika yale maeneo yaliyoachiwa, kwa sababu katika kuondoka ni jumla ya vijiji vitano ambavyo vinatakiwa kuondoka katika yale maeneo lakini kuna vitongoji kama kumi na kitu ambavyo navyo vinatakiwa kuondoka. Sasa wale wote tunawapangia mahali pa Kwenda.

Mheshimiwa Spika, katika hili pia tayari tumeshabainisha vijiji kumi na mbili ambako watakwenda kule lakini pamoja na hayo watapewa ile gharama ya usafiri kwa kule wanapokwenda kwa mujibu wa kisheria. Kwa hiyo, tunasema hakuna mwananchi ambaye hatatendewa haki katika hili, kwa sababu tunajua walikuwa kwenye vijiji ambavyo vinatambulika kisheria, Serikali ilikuwa imevisajili. Kwa hiyo kuwaondoa kwao pale sio kwamba ni wavamizi kwa maana ya uvamizi, lakini vilitambuliwa vijiji, kwa hiyo mipaka ndio ilikuwa inaleta taharuki kutokana na ule uhifadhi. Pia, kwa sababu wote tunaona kwamba uhifadhi ni muhimu iendelee kuwepo, basi nadhani wote tutakuwa na dhamira njema ya kuweza kupitisha azimio hili ili kazi iweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, naomba tu niwaombe Waheshimiwa Wabunge walipitishe azimio hili wote, kwa ujumla wao kwa sababu linakwenda kuondoa changamoto kubwa ambayo imekuwepo, lakini linakwenda kuwapa nguvu za uchumi wale wananchi ambao wataondoka. Kwa sababu maeneo watakayopangiwa yatapimwa na kila mmoja atamilikishwa kwa hati yake katika lile eneo ambalo atakuwa amepangiwa. Kwa hiyo, hapo tayari kiuchumi tutakuwa tumeshawaongezea nguvu. Kwa hiyo niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira njema na ndio maana tunaongeza kasi ya kukamilisha michakato ya maeneo yenye migogoro ili watu waweze kuishi kwa amani, watu waondokane na kukimbiakimbia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niseme tu azimio hili limekuja kwa wakati muafaka, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge waikubali. Dhamira njema ya Serikali ni kuhakikisha tunalinda hifadhi zetu, lakini vile vile hatuleti changamoto kwa wananchi kwa sababu wao ni sehemu ya ulinzi wa zile hifadhi, wakipata maeneo wakakaa vizuri maana yake pia watakuwa ni sehemu ya uhifadhi na hapatakuwa na changamoto zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono azimio. Ahsante sana. (Makofi)