Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na maarifa ambapo leo Waheshimiwa Wabunge ni zaidi ya miezi mitatu tuko hapa kujadili na kuamua bajeti iliyowasilishwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge, Katibu wa Bunge na timu yake kwa namna mlivyotuongoza vyema katika kipindi chote cha kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, pia nashukuru upande wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa namna walivyojibu maswali na kutolea ufafanuzi wa hoja zetu hapa Bungeni, asanteni sana.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Usalama wa Taifa kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda amani na usalama wa nchi yetu, kulinda mipaka, kulinda raia na mali zao kazi ambayo inafanywa na vyombo vyetu usiku na mchana kwa uzalendo na kwa kujitoa kwa kiwango cha juu na kuifanya nchi yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani.
Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoingoza Serikali na kuhakikisha maendeleo kwa Watanzania yanapatikana ambapo tumeshuhudia miradi mingi ikikamilika na mingine mingi ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwemo miradi ya Ikulu ya Chamwino, ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, bomba la mafuta kutoka Uganda, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, reli ya SGR, mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia wa LNG, Daraja la Tanzanite, Daraja la JPM-Kigongo Busisi, ujenzi wa meli ya Mv Mwanza - Hapa Kazi Tu, ujenzi uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato, ununuzi wa ndege mpya ya mizigo na miradi mingine ya elimu, afya, maji, barabara pamoja na kuanzishwa kwa Tume ya Taifa Mipango na kadhalika haya sio mambo madogo kama Taifa tuna kila sababu ya kujivunia.
Pia niwapongeze Watanzania wote wakiwemo wapiga kura wangu wa Jimbo la Kisesa kwa namna mnavyojitoa kwa hali na mali kulijenga Taifa letu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, nimepitia Mpango wa Maendeleo, Hali ya Uchumi na hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2023/2024, pia nimepitia Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti; kwa ujumla hotuba hizi zimetoa takwimu na taarifa muhimu kutuwezesha Wabunge kutoa michango yetu. Aidha, nampongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamad Hamis Chande, Katibu Mkuu na timu yote ya watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi zake za BOT, TRA, NBS na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), PPRA na kadhalika, pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa kazi nzuri mliyofanya.
Mheshimiwa Spika, mambo ya kiujumla; baadhi ya ibara katika hotuba ya Waziri wa Fedha zinahitaji ufafanuzi wa kina au kuondolewa kabisa kwenye hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa kuwa zinakwenda kinyume na Kanuni za Bunge pamoja na Sheria za nchi. Naomba kupitia mambo ya kiujumla katika vipengele vinne kama ifuatavyo:-
(i) Naunga mkono pendekezo la Kamati ya Bajeti la kutoa muda wa kutosha kuwasilisha na kujadiliwa Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) walau mwezi mmoja badala ya siku saba ilivyo sasa ili kutoa nafasi ya kutosha kwa wadau na Waheshimiwa Wabunge kupitia kwa makini kabla ya kuupitisha.
(ii) Kamati ya Bajeti kutokuwasilisha bango kitita linaloonesha hoja 17 zilizoibuliwa katika Kamati za Kisekta na majadiliano Bungeni, bango kitita hilo lingeeleza hoja, majibu ya Serikali na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti badala ya maelezo waliyoyatoa na Kamati kuwa walikubaliana na Serikali bila kueleza walikubaliana nini na kulifanya Bunge lisielewe hoja zake zimeshughulikiwaje.
(iii) Waziri wa Fedha, kutumia vibaya jina la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhihaka kinyume na Kanuni za Bunge kwa kumsingizia kuwa alianza Urais mwaka 2008, huku ni kutumia vibaya jina la Mheshimiwa Rais. Kauli hii inatolewa kwenye hotuba ya Serikali Ibara ya 9 ukurasa wa tano wa hotuba ya Waziri wa Fedha huku akijua fika kuwa wakati huo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa wakati huo mwaka 2008 alikuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, imekuwaje Waziri aweke taarifa ya aina hii? Naomba kunukuu; “Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianza mchakato wa kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (sovereign credit rating) mwaka 2008 ambapo zoezi hilo halikukamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mdororo wa uchumi pamoja na kuyumba kwa soko la fedha duniani” mwisho wa kunukuu.
(iv) Kupiga marufuku ufungaji wa biashara kwa sababu zozote zile Waziri wa Fedha katika Ibara ya 126 ya hotuba anapendekeza kutofunga biashara kwa sababu zozote zile kuanzia tarehe 1 Julai, 2023 huku akijua kuwa kufunga biashara ni sehemu ya takwa la kisheria inapobidi kufanya hivyo, mfano mgodi au kiwanda kinapokutwa kinatiririsha maji machafu na yenye kemikali za sumu kwenda kwenye makazi ya wananchi na kwenye vyanzo vya maji na kuhatarisha maisha ya watu na viumbe hai wengine.
Je, mamlaka za udhibiti zifanye nini, ziache watu wafe ili kulinda biashara? Mfanyabishara anakutwa hana vibali, hana leseni, hana nyaraka yoyote, anauza bidhaa fake/bandia na zilizokwisha muda wa matumizi zenye athari za kiuchumi na kiafya kwa binadamu na viumbe hai wengine, ashtakiwe yeye halafu bidhaa zake ziendelee kuuzwa kwa wananchi? Hata wafanyabishara wa dawa za kulevya, fedha haramu na biashara haramu zingine nao waachwe waendelee na biashara zao wasifungiwe?
Kauli hii ya Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba inaleta mkanganyiko mkubwa wa kisheria na mifumo ya udhibiti nchini, lakini pia inarudisha nyuma jitihada za Serikali zinazofanywa na Mamlaka za Udhibiti katika kusimamia ustawi wa Taifa na wananchi kwa upande mwingine wataelewa kwamba Serikali imekuwa ikiwaonea.
Aidha, ifahamike kuwa ada na tozo zinazotozwa na mamlaka za udhibiti zipo kwa mujibu wa sheria na zilikubalika kwa Waziri mwenye dhamana ya Fedha hivyo sio sahihi kusema kwamba usimamizi wao makini unasukumwa na kuongeza mapato ya taasisi husika. Lakini pia ni muhimu kuthamini kazi nzuri inayofanywa na mamlaka zetu za udhibiti katika kulinda biashara, usalama wa afya za walaji na uchumi wa nchi, taasisi kama TBS, NEMC, TMDA, TPRI, OSHA, Polisi, TRA, DCEA, LATRA, EWURA, BOT, TCRA, eGA, TCAA, FIU, WMA, NACTVET, FCC, BRELA, PPRA na kadhalika zinapaswa kupongeza kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, Waziri alipaswa kulieleza Bunge hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini (blueprint), lakini pia Waziri angeeleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi wachache wasio waaminifu ambao wamekuwa wakikiuka sheria na taratibu na kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwanyanyasa wafanyabishara badala ya kuzituhumu kiujumla taasisi za udhibiti ambazo zimekuwa zikifanya kazi nzuri kwa mujibu wa sheria na kwa ustawi wa Taifa letu.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali; mapato ya kodi, yasiyo ya kikodi na ya halmashauri yamekuwa yakiongezeka kila mwaka lakini ongezeko hilo haliendani na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Wastani wa pato la Taifa kwa makusanyo ya kodi kwa mwaka 2022 ilikuwa ni asilimia 12.3; uwiano huu ni chini ya uwiano kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao ni asilimia 15. Zipo changamoto nyingi zinazotufanya tushindwe kukusanya kodi stahiki.
(i) Malimbikizo ya kodi yenye mapingamizi Mahakamani taarifa ya TRAB na TRAT kuishia Aprili, 2023 inaonesha kuwa mashauri 1,155 ya rufani za kodi yenye thamani ya shilingi trilioni 7.35 yalipokelewa na kusajiliwa katika Mahakama za Rufani za Kodi za TRAB na TRAT ambapo mashauri 423 yenye thamani ya shilingi bilioni 849.8 yaliamuliwa sawa na 11.5% ya mashauri yote. TRA ilishinda mashauri 344 yenye thamani ya shilingi bilioni 824 sawa na 81% na walipakodi walishinda mashauri 79 yenye thamani ya shilingi bilioni 25.7 sawa na 19%. Mtiririko unaonesha kuwa nafasi ya kushinda kesi kwa TRA ni wastani wa 81%, hii ina maanisha kuwa endapo kesi zote zingesikilizwa kwa wakati TRA ingekusanya takribani shilingi trilioni sita kwa kipindi husika na kuongeza mapato ya Serikali. Hapa unaona kuwa mapato mengi ya Serikali yameshikiliwa katika mapingamizi ya kikodi bila sababu za msingi.
Je, nini kinachoifanya Serikali ishindwe kuweka mikakati ya kuzifanya Mahakama za TRAB na TRAT kuamua mashauri haya kwa wakati? Tunaacha kukusanya mapato haya ya wazi na badala yake tunakimbilia kuweka tozo na kodi kwa kuwakamua watu maskini. Nashauri iundwe Tume ya Bunge ili kubaini ukweli uliojificha na kuwezesha kukusanya mapato ya Serikali pamoja na kuondoa usumbufu ambao wafanyabishara wanaupata kwa kukaa na kesi muda mrefu.
(ii) Utakasishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi; taarifa ya Waziri inaeleza kuwa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) kuishia Aprili, 2023 kimeripoti ongezeko kubwa la taarifa shuku, kutoka taarifa shuku za fedha taslimu na usafirishaji kwa njia ya kielektroniki 724; Aprili 2021 taarifa shuku 12,651 zenye thamani ya shilingi trilioni 122.85; Aprili, 2022 hadi kufikia taarifa shuku 16,035 zenye thamani ya shilingi trilioni 280; Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 130. Aidha, Kitengo kimechambua miamala shuku 769 na kuandaa taarifa fiche 314 sawa na asilimia 40 ya miamala shuku iliyofanyiwa kazi na kuwasilisha kwenye taasisi za utekelezaji wa sheria kwa hatua za uchunguzi Aprili, 2023.
Mheshimiwa Spika, ni vigumu kwa Serikali kukusanya mapato stahiki katika mazingira ya namna hii ambapo taarifa shuku za fedha taslimu na usafirishaji wa fedha kwa njia ya kielektoniki zimeongezeka na kufikia trilioni 280 sawa na asilimia 130, hii inatupa ishara kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa kodi unaofadhiliwa na mbinu mbalimbali ikiwemo biashara za magendo, wizi, rushwa, ufisadi, utoroshaji wa fedha na rasilimali nje ya nchi (Illicit Financial Flows), Transfer Pricing, uhamishaji wa mitaji (Capital Flight) na kadhalika. Hapa kuna maswali mengi ya kujiuliza:-
a) Kwa nini FIU ifanye uchambuzi wa miamala shuku 769 tu kati ya miamala shuku 16,035 ambayo ni asilimia tano tu ya miamala yote kwa mwaka mzima?
b) Serikali inachukua hatua gani za dharura kushughulikia taarifa shuku za utakasishaji wa fedha haramu zilizofikia shilingi trilioni 280 ili kuzuia ukwepaji mkubwa wa kodi na utoroshaji wa fedha nje ya nchi unaondelea nchini.
c) Ni fedha kiasi gani zilizoshikiliwa na FIU kutokana na taarifa shuku za fedha taslimu na usafirishaji kwa njia ya kielektoniki hadi sasa?
d) Kwa nini FIU isiwe mamlaka kamili badala ya kuwa kitengo chini ya Wizara ya Fedha kama ilivyo sasa? Pamoja na taarifa hizi za FIU kutishia uchumi, mapato ya Serikali na usalama wa nchi yetu, lakini hakuna mkakati madhubuti uliowekwa na Serikali kupambana na matukio haya ya uhalifu, leo tunazungumzia taarifa shuku 16,035 zenye thamani ya shilingi trilioni 280 lakini zilizofanyiwa uchambuzi ni taarifa shuku 769 tu sawa na asilimia tano kwa mwaka mzima. Hivi sasa nchi yetu inatekeleza Mpango Kazi wa Kikosi Kazi cha Kifedha cha Kimataifa (Financial Action Task Force – FATF), matukio ya utakasishaji fedha haramu yanazidi kuongezeka kila mwaka licha ya mikakati na hatua zilizochukuliwa na Serikali kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 18 ya hotuba ya Waziri. Lakini pia sijaona mkakati wa uwezeshaji, uratibu na kufanya kazi kwa pamoja kwa taasisi zinazosimamia utekelezaji wa sheria katika hatua ya kukamata, kuchunguza na kuendesha mashtaka kwa mamlaka zinazohusika za FIU, DCI, PCCB, DCEA na DPP.
(iii) Biashara za magendo na utoroshaji wa rasilimali za Taifa nje ya nchi; tumeshuhudia matukio mengi ya kushamiri kwa biashara za magendo ambapo bidhaa nyingi za magendo zinaingia nchini lakini pia kuna utoroshaji mkubwa wa rasilimali kama madini, nyara za Serikali, mazao ya misitu, mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi hali ambayo inaathiri kwa kiwango kikubwa uchumi, ukusanyaji wa mapato ya Serikali, mfumuko wa bei na ugumu wa maisha. Magendo haya yameshamiri katika maeneo ya mipakani na kwenye bandari bubu zinazofikia 693. Licha ya Serikali kupoteza mapato mengi katika hili eneo hakuna mifumo madhubuti ya udhibiti iliyowekwa na kulifanya tatizo hili kuwa sugu. Tunao vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa na wengine wakiendelea kujitolea katika Kambi zetu JKT na Jeshi la Akiba (mgambo) waliandaliwa uzalendo na moyo wa kujituma tuwatumie kudhibiti maeneo yote tete na kuongeza mapato ya Serikali.
(iv) Mifumo ya TEHAMA; Taarifa ya Wizara ya Fedha imeonesha kuwa kuna kasi ndogo ya ujengaji na maboresho ya mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali ikilinganishwa na kasi ya mabadiliko ya TEHAMA duniani na hivyo kuhatarisha ufanisi na usalama wa mifumo ya usimamizi wa fedha za umma. Kifungu cha 24(1) na (2) cha Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 (e-Government Act No. 10 of 2019) inazitaka taasisi za umma kutekeleza miradi ya TEHAMA kwa namna ambayo itahakikisha manufaa yanayotarajiwa kupatikana na hatari zinapunguzwa kwa kuzingatia viwango na miongozo ya kitalaamu kama ilivyoagizwa na mamlaka. Aidha, hairuhusiwi kuanzisha na kutumia mifumo ya TEHAMA bila kupata kibali (clearance) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Mheshimiwa Spika, matumizi ya mifumo ya TEHAMA yamesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi ya Serikali kwa kiwango kikubwa, baadhi ya mifumo hiyo ni GePG, GIMIS, TTMS, TANCIS, ITAX, EFDMS, TAUSI, HCMIS, TANePS, MUSE, LUKU na kadhalika ingawa pia zipo changamoto zinazopunguza ufanisi kama ifuatavyo:-
(i) Miundombinu ya mifumo ya TEHAMA kuhujumiwa; baadhi ya watendaji wa Serikali kwa maslahi binafsi wamekuwa wakiharibu miundombinu ya TEHAMA ili kuficha ukweli unaowekwa wazi na mifumo katika kuzuia wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Mfano kuzima scanner bandarini, mifumo kutosomana, mtandao uko chini na kadhalika.
(ii) Baadhi ya Wizara na Taasisi za Umma zimeanzisha na kutumia mifumo ya TEHAMA bila kibali cha eGA mfano Wizara ya Kilimo (Mfumo wa Mbolea ya Ruzuku) na TANESCO (Mfumo wa Mipango wa Rasilimali za Biashara – ERP) na kadhalika.
(iii) Kukosekana kwa uunganishwaji wa mawasiliano (connectivity) kutokana na baadhi ya maeneo hawajafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, minara ya simu na umeme hivyo mifumo kutofanya kazi.
(iv) Kutokuzingatia viwango na miongozo iliyowekwa na eGA, kukosekana ushirikiano wa kitaasisi na baadhi ya taasisi kuamini zaidi wataalamu na mifumo ya kutoka nje ya nchi kupata suluhisho la changamoto za mifumo yao.
(v) Baadhi ya taasisi za Serikali kutokuwa na watalaamu wabobezi wa mifumo ya TEHAMA na hivyo kupelekea ufanisi mdogo wa mifumo na kadhalika. Serikali itatue changamoto zinazokabili ufanisi wa mifumo ya TEHAMA na kuwekeza kikamilifu katika wataalamu wabobezi wa TEHAMA, pamoja na changamoto nilizozitaja nchi yetu ya Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kushika nafasi ya 26 kidunia na ya pili Barani Afrika baada ya Mauritius kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) mwaka 2022 kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index).
(vi) Kushindwa kukusanya mapato kwa mujibu wa mikataba na sheria; baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali zimeshindwa kukusanya mapato yatokanayo na faini, tozo na CSR katika utekelezaji wa mikataba na zingine zimeshindwa kukusanya malipo baada ya kushinda mashauri mahakamani. Mfano Wizara ya Nishati na TANESCO kushindwa kukusanya faini shilingi bilioni 655 na CSR shilingi bilioni 270 kutoka Kampuni ya Arab Contractors na malipo kutoka Kampuni ya IPTL kiasi cha shilingi bilioni 342 ambapo jumla ni kiasi cha shilingi trilioni 1.268, Wizara ya Katiba na Sheria na DPP kushindwa kukusanya shilingi bilioni 170 kutokana na malipo ya kesi za plea bargain. Kwa mifano hii michache hatujakusanya jumla ya shilingi trilioni 1.438 bila sababu za msingi, tulimsikia Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba eti kutokukusanya fedha hizo za umma alitumia hekima na busara, hizo hekima na busara tunazipimaje katika fedha za umma ambazo ziko kisheria na kwa mujibu wa mkataba. Mawaziri wetu wanageuka kuwa mawakili wa makampuni halafu leo tunaenda kuweka tozo ya ushuru wa barabara na mafuta ya shilingi 100 kwa mafuta ya petroli na dizeli ili zitumike kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambapo itaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 381.8, tozo hii inakwenda kuwakamua wananchi masikini, inafikirisha sana, hapa nasema bila kumung’unya maneno Serikali haiwatendei haki wananchi katika hii tozo.
(vi) Malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani; malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yalifikia kiasi cha shilingi trilioni 7.54 mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo ilionesha uwezo mdogo wa 10% wa TRA kukusanya mapato hayo. Taarifa ya Waziri wa Fedha haijaonesha malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yalifikia kiasi gani mwaka wa fedha 2021/2022. Kama assessment ya kodi ilifanyika na hakuna mapingamizi nini kilichowafanya TRA washindwe kukusanya mapato hayo? Eneo hili hata tungeweza kukusanya 50% tu tungepata kiasi cha shilingi trilioni 3.77. Nashauri iundwe Tume ya Bunge ili kubaini ukweli uliojificha na kuwezesha kukusanya mapato ya Serikali.
(vii) Malimbikizo ya Kodi za Madini (Makinikia) mwaka wa fedha 2020/2021 inaonesha miongoni mwa kesi za rufani zilizoisha ni kesi 45 zenye thamani shilingi 5,594,675,387,242.40 ambazo zipo katika mazungumzo kati ya Serikali na kampuni za madini ambayo ni North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limited, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration. Kati ya kesi hizo jumla ya deni la shilingi trilioni 343.5 lilirejeshwa kusikilizwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hotuba ya Waziri wa Fedha haijaeleza hitimisho ya suala hili la malimbikizo ya kodi ya kiasi cha shilingi trilioni 5.594 ambapo Mamlaka za Rufani za Kodi za TRAB na TRAT ziliona Serikali inastahili kulipwa madai hayo. Pamoja na maelezo ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa madai hayo yalifutwa na sherehe ikafanyika Ikulu hadi leo ameshindwa kuleta uthibitisho na sababu za msingi za kufutwa kwa madai hayo. Kwa mujibu wa kifungu cha 43(1) cha Sheria ya Fedha za Umma Bunge linaweza kwa Azimio la Bunge kutoa idhini kwa Waziri wa Fedha kufuta hasara na upotevu wa fedha na vifaa vya Serikali, madai ya kodi pamoja na riba itokanayo na malimbikizo ya kodi. Bunge halijawahi kupitisha Azimio hilo. Kwa msingi huo wa kisheria bado naamini hakuna mamlaka yoyote iliyofuta madai ya kodi ya malimbikizo ya kodi za Makinikia kutoka kwa makampuni ya madini kiasi cha shilingi trilioni 5.594 na inashangaza kuona kwa nini Serikali haijakusanya mapato hayo hadi sasa.
Nashauri iundwe Tume ya Bunge ili kubaini ukweli uliojificha na kuwezesha kukusanya mapato ya Serikali.
(viii) Kuweka misamaha ya kodi kwenye kundi la watu wachache kupitia Finance Bill ya mwaka 2022 tuliamua kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha mamlaka ya kusamehe kodi hizo kwa wawekezaji mahiri maalum. Kuweka misamaha ya kodi kwenye kundi la watu wachache maarufu kama wawekezaji mahiri maalum, maamuzi haya yanainyima Serikali mapato pasipo sababu za msingi, kodi za namna hii ni za kibaguzi na zinaondoa ushindani wa haki, misamaha ya kodi sio kivutio pekee cha uwekezaji, kunufaisha kundi la wachache na kuwakamua wananchi masikini kwa kuwawabebesha mzigo wa tozo na kodi kubwa kufidia mapato ya Serikali yanayopotea mfano malalamiko ya wafanyabishara kule Kariakoo na maeneo mengine nchini, Waziri atuambie tangu kuanza utaratibu huo Serikali imevutia wawekezaji wangapi na imepoteza mapato kiasi gani?
Waheshimiwa Wabunge, tuamue leo kupitia Finance Bill ya mwaka 2023 kufuta utaratibu huu ili kuleta usawa katika ulipaji kodi na kuokoa mapato ya Serikali yanayopotea bila sababu za msingi. Ni hatari kwa Taifa kuwa na mfumo wa kodi wa aina hii hususan katika kipindi ambacho Taifa linavutia uwekezaji na kuingia mikataba mikubwa ya rasilimali za nchi mfano miradi ya kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG), madini, gesi, mafuta, makaa ya mawe na kadhalika na kuikosesha mapato Serikali.
(ix) Kuondoa faini kwenye miamala ya transfer pricing kupitia Finance Bill ya mwaka 2021, Waziri wa Fedha alifanya marekebisho ya Kanuni Na. 15 ya Ukokotoaji wa Kodi za Kimataifa (Transfer Pricing Regulations) kwa kufuta kifungu kinachoweka adhabu ya asilimia 100 kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya sheria. Lengo la hatua hii ni kuwaondolea walipakodi adhabu kubwa ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji nchini. Uamuzi huo aliufanya Waziri wa Fedha huku akijua kuwa TRA ina uwezo mdogo wa kukagua miamala ya transfer pricing katika Makampuni ya Kimataifa (MNCs) na Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kupitia miamala ya Kimataifa (Transfer Pricing) uamuzi huu unahamasisha uvunjaji wa sheria yaani makosa yafanyike halafu hatua zilisichukuliwe kwa wahusika na kuikosesha Serikali mapato bila sababu za msingi.
Bunge limuagize Waziri wa Fedha kuirejesha kanuni hii ili kudhibiti ukwepaji wa kodi unaofanywa na MNCs. Jitihada za Serikali za kuimarisha udhibiti na kuzuia upotevu wa mapato katika vihatarishi vilivyopo katika miamala ya uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma baina ya makampuni ya kimataifa (transfer pricing) hazitazaa matunda kama sheria ndani ya nchi haina meno ya kudhibiti wahalifu. Hatua kubwa iliyopigwa na Serikali kupitia TRA ni pamoja na kununua kanzidata ya Orbis kwa ajili ya kupata taarifa za kusaidia kufananisha bei za miamala ya kimataifa ili zisaidie kujenga hoja wakati wa ukaguzi unaofanywa kwenye kampuni za hapa nchini. Pia Tanzania imejiunga na Jukwaa la Kimataifa la Ubadilishaji wa Taarifa za Kikodi kwa lengo la kuhakikisha nchi yetu inajenga uwezo wa kubadilishana taarifa za kikodi na nchi nyingine na Serikali inatarajia kusaini mkataba ujulikanao kama Multilateral Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters ambao utaiwezesha TRA kupata taarifa mbalimbali kutoka katika nchi 146 duniani ambazo zitasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa miamala ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, mwisho katika hili eneo la ukusanyaji wa mapato Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi zingine za Serikali zinazohusika na ukusanyaji wa mapato zinapaswa kujipanga vizuri kwa kuweka programu na mikakati madhubuti ili kuweza kukusanya mapato kwa ufanisi mkubwa na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali. Wigo mdogo na ulegevu wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali unapelekea kuanzisha kodi na tozo kubwa kwa wananchi masikini, kuchochea mfumuko wa bei na ugumu wa maisha. Mfano kwa uchambuzi wangu mdogo katika vipengele tisa nilivyovitaja Serikali ingekusanya mapato ziadi ya shilingi trilioni 15. Kiasi hiki cha fedha kingewezesha kugharamia miradi yote ya kimkakati na ya maendeleo bila kuchukua mkopo kokote.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya mikopo ya ECF na LTP kutoka IMF na WB; utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za mikopo katika kipindi cha miaka mitatu ambapo mkopo kutoka dirisha la Extended Credit Facility (ECF) kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wa miaka mitatu wenye jumla ya shilingi trilioni 2.4 na Mkopo wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki ya Ardhi (LTP) kutoka Benki ya Dunia wa dola za Marekani milioni 150 sawa na shilingi bilioni 350. 65 Kamati imeeleza kuwa mikopo ya ECF na LTP kiasi cha shilingi trilioni 2.75 kimeelekezwa katika shughuli ambazo hazina manufaa ya muda mrefu. Fedha hizo zimeelekezwa katika mafunzo, ununuzi wa vifaa vya ofisi, utekelezaji wa shughuli zisizo na tija na kutokuwa na mpango wa uendelevu wa miradi pindi mkopo utakapokoma.
Mheshimiwa Spika, msimamo wa nchi yetu ni kutochukua mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida bali mikopo yote iwe ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Waziri wa Fedha alipata wapi kibali cha kuchukua mikopo isiyo na tija na alifanya kwa manufaa ya nani? Katika siku za hivi karibuni deni la Serikali limekuwa likiongezeka kwa kasi kubwa mfano katika kipindi cha Aprili, 2022 hadi Aprili, 2023 deni la Serikali limeongezeka kwa shilingi trilioni 9.84 sawa na ongezeko la 14%; huu ni ukuaji mkubwa sana wa deni la Serikali. Kila tukiuliza tunajibiwa deni ni himilivu na kwamba linaongezeka kwa sababu ya kugharamia miradi ya kimkakati ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo Busisi lakini leo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeweka wazi ukweli uliokuwa unafichwa kwa nguvu kubwa na Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amekwenda kufanya makubaliano na kukopa mikopo ya isiyo na tija ya zaidi ya shilingi trilioni 2.75, ni Waziri huyu huyu kwenye Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 ambaye amekopa zaidi ya trilioni 1.285 nje ya bajeti na bila kibali cha Bunge, lakini pia ni Waziri huyu huyu amechukua misaada na mikopo ya nje yenye masharti nafuu ya shilingi trilioni 2.531 ambayo haikupitia Mfuko Mkuu wa Serikali kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, Bunge liitake Serikali kuwasilishwa mchanganuo wa mpango wa matumizi na mgao wa fedha hizi za mikopo ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, ufadhili wa miradi kupitia utaratibu wa EPC+F; kupitia mpango wa maendeleo, hotuba ya Waziri wa Fedha na hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ilielezwa kuwa mwaka 2022/2023 Wizara ilianza taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuwapata makandarasi wa kujenga barabara saba kwa kiwango cha lami kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F). Hatua iliyofikiwa hadi sasa ni kuwa makandarasi wa miradi yote saba wamepatikana na mikataba ya kazi za ujenzi imesainiwa tarehe 16 Juni, 2023 ambapo makandarasi wanne wamepewa kazi hiyo ya barabara saba zenye urefu wa kilometa 2,035 kwa gharama ya shilingi trilioni 3.7.
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kujenga barabara zenye jumla ya kilometa 2,035 maeneo mbalimbali nchini ikiwemo barabara inayopita Jimbo la Kisesa ya kutoka Karatu-Mbulu-Sibiti-Meatu-Lalago-Maswa ni jambo la kupongezwa kwani mtandao huo wa barabara utaleta tija kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na uchumi wa nchi kwa ujumla. Hapa unazungumzia nchi kuingia mkopo wa trilioni 3.7 lakini nimepitia taarifa zote za Serikali hakuna maelezo ya kina namna miradi hii itakavyotekelezwa na makampuni yaliyopewa zabuni ya ukandarasi wa ujenzi yatakavyorejesha fedha zake na fedha hizo zitarejeshwa kwa kipindi gani.
Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa miongoni mwa Wabunge waliohudhuria hafla ya utiaji saini mikataba hiyo lakini hakuna ufafanuzi wa kina uliotolewa kuhusu suala hili na kuacha maswali mengi ya kujiuliza kama ifuatavyo:-
(i) Gharama za mradi (project costs) huandaliwa na mfadhili na baadaye shughuli za ujenzi na manunuzi hufanywa na mfadhili mwenyewe na hivyo si rahisi kwa Serikali kujiridhisha na thamani halisi ya mradi (value for money) kwani mzabuni haimzuii kufanya upandishaji wa bei na gharama. Je, nafasi ya Serikali itakuwa wapi katika usimamizi wa gharama na ubora wa miradi wakati mfadhili analipa moja kwa moja kwa Makampuni yake? Kwa nini haielezwi kilometa moja ya barabara inajengwa kwa shilingi ngapi ikilinganishwa na gharama ya kilometa moja tunazojenga barabara za lami nchini hivi sasa.
(ii) Fedha hizi haziingii kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwani mfadhili analipa moja kwa moja kwenye makampuni yake ya ujenzi. Je, nafasi ya CAG na Bunge katika usimamizi wa miradi ya aina hii itakuwaje? Na kuna hatari miradi hii ikatumika kama uchochoro wa ubadhirifu wa fedha za umma, mfano fedha trilioni 3.7 hazimo kwenye bajeti ya Wizara - sekta ya ujenzi Fungu la 98.
(iii) Tulishaweka ukomo wa mikopo katika bajeti ya Serikali mwaka 2023/2024 hizi fedha za EPC+F ziko kwenye fungu gani? Hii inaweza kuwa njia ya kutanua goli la kuchukua mikopo nje ya utaratibu maalum uliowekwa kisheria ambao unaweza kulipelekea Taifa letu kutumbukia kwenye mzigo mkubwa wa madeni yasiyolipika.
(iv) Hapa ulinzi wa ajira za Watanzania uko wapi? Kazi zote zitafanywa na mfadhili ku-design mradi, ununuzi wa vifaa vya ujenzi, kuajiri makandarasi na kadhalika. Miradi ya aina hii inavunja mnyororo wa thamani na ni hatari kwa Taifa ambalo lina vijana wengi wanaohitimu katika vyuo mbalimbali wakiwa na tatizo kubwa la ajira. Mwisho wa siku huu ni mkopo ambao kama Taifa tutalazimika kuulipa na hivyo ni lazima tujue ukweli wa masharti ya mikataba hii na Serikali iache kuweka siri katika jambo hili na iweke wazi faida itakayopatikana ya mradi huu ikilinganishwa na mikopo ya kawaida, huko nyuma tumekuwa tukikataa mikopo ya utaratibu wa EPC+F kutokana na masharti magumu na yasiyozingatia maslahi ya Taifa. Serikali ilete maelezo ya kina juu ya miradi hii ikibainisha masharti yote ya mikataba na mchanganuo wa gharama kwa kila mradi na muda wa kukamilisha miradi ili Bunge lichukue nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP); nimesoma mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2023/2024 na hotuba za Mawaziri kuhusu maeneo ya miradi itakayotekelezwa kwa utaratibu wa ubia na sekta za umma na sekta binafsi (PPP) baadhi ya miradi hiyo ni kama ifuatavyo; kuanza ujenzi wa barabara ya Kibaha – Chalinze - Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilometa 461 kwa utaratibu wa PPP na barabara ya tozo Mbeya Bypass (Uyole – Sogwe kilometa 48.9).
Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri kuhusu ujenzi wa barabara kwa kutumia utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi (Public Private Partnership - PPP), Wizara inaendelea na manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa expressway kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 205. Hadi sasa kazi inayoendelea ni uchambuzi (evaluation) wa makandarasi watano walioonesha nia (expression of interest) ya kutekeleza mradi huu kwa sehemu ya kutoka Kibaha – Chalinze yenye urefu wa kilometa 78.9. Kwa sehemu ya Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 126.1, Mshauri Elekezi anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu. Utaratibu wa PPP ni mzuri katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa barabara kwa kuwa mara nyingi huwa kuna njia mbadala (alternative roads/competing roads) ambayo sio ya kulipia, lakini hapa nina wasiwasi mkubwa juu ya masharti ya mkataba utakaoingiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inajenga reli ya SGR kutoka Dar es Salaam - Dodoma hadi Mwanza ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo na pia kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo lakini pia kuwepo kwa barabara shindani isiyo ya kulipia. Hii inanipa mashaka na maswali mengi kama ifuatavyo:-
(i) Barabara hii inakwenda kujengwa wapi kwenye eneo la hifadhi ya barabara iliyopo sasa (road reserves) au itakwenda kununua maeneo yake mengine mapya kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo? Hapa tunaambiwa mchakato wa manunuzi uko hatua za mwisho, lakini mambo muhimu yanayohusu ardhi za wananchi hayawekwi wazi kwenye taarifa zote za Serikali kuhusu mradi huu.
(ii) Je, mkataba unaoingiwa hauzuii ukarabati, maendelezo au upanuzi wa barabara iliyopo? Kwani mara nyingi mikataba ya aina hii imekuwa ikiweka mazuio, hatuwezi leo kufanya maamuzi makubwa kiasi hiki ya kuzuia uendelezaji wa barabara zetu kwa manufaa makubwa ya kiuchumi ya wananchi na Taifa letu kwa ajili ya kumnufaisha mwekezaji.
(iii) Nani atakayekuwa mwamuzi wa gharama za matumizi ya barabara hizo Serikali au mwekezaji? Mikataba ya PPP ya aina hii hupelekea barabara za bure zinazotumiwa na wananchi kutelekezwa na pengine eneo ambalo lingetumika kufanya upanuzi kuchukuliwa na wawekezaji na hivyo kupelekea ulazima wa kila mmoja kupita kwenye barabara ya kulipia hali itakayosababisha ugumu wa maisha, gharama kubwa za usafiri na usafirishaji, double taxation na anguko kubwa la uchumi.
Mheshimiwa Spika, Serikali wakati wa kuhitimisha hoja yake ilete maelezo ya kina juu ya masharti ya mikataba ya PPP ya ujenzi wa barabara, usiri mkubwa ulioko sasa utatuletea matatizo makubwa, upanuzi wa barabara za njia nane Kibaha hadi Kimara umepunguza kwa kiasi kikubwa foleni na Serikali inaweza kuendelea na upanuzi huo polepole kupunguza msongamano uliopo sasa.
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iwasilishe Bungeni masharti yote ili yapate ridhaa ya Bunge kabla ya mkataba kusainiwa.
Kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi, ada, tozo na hatua nyingine za mapato; kila mwaka tunaanzisha, tunafuta na kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali lakini Serikali imekuwa haileti tathmini ya utekelezaji wa maamuzi hayo kabla ya kupendekeza maboresho ya mwaka wa fedha unaofuata hali hii inawaweka Wabunge na wananchi kutokujua kama malengo na madhumuni ya uamuzi huo yamefikiwa. Tujiulize katika maeneo ambayo tulipunguza kodi, tozo, ushuru na ada bei za bidhaa zilipungua? Mapato ya Serikali yaliongezeka? Hivi tujiulize haya maamuzi huwa tunayafanya kumnufaisha nani? Na kwa nini Serikali haitaki kuleta tathmini ya mabadiliko ya kodi yanayofanyika kila mwaka ili iwe msingi wa maamuzi ya mwaka unaofuata, kuna uwezekano eneo hili la mabadiliko ya kodi limeingiliwa na baadhi ya maamuzi yanafanywa kwa maslahi binafsi kwani ukipima huoni tija yake.
Mheshimiwa Spika, pia napongeza hatua ya Serikali kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi, kuongeza kima cha usajili kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani kinachotakiwa kwa mfanyabiashara kusajiliwa kutoka shilingi milioni 100 hadi shilingi milioni 200, kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa kutumia pamba na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, ninapendekeza kufanya marekebisho katika baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
(i) Serikali inapendekeza kufuta adhabu ya asilimia 15 ya thamani ya bidhaa inayotozwa na Shirika la Viwango Tanzania kwa bidhaa zinazoingia nchini bila ya kuwa na Cheti cha Uthibitisho wa Ukaguzi wa Ubora (Certificate of Conformity - CoC). Aidha, bidhaa hizo zisizo na Cheti cha Uthibitisho wa Ubora zitafanyiwa ukaguzi wa ubora zinapofika nchini na kulipiwa gharama za ukaguzi pekee. Nchi yetu ilianzisha mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla hazijasafirishwa kuja nchini (Pre-shipment Verification of Conformity-PVoC) ambapo baada ya ukaguzi huo hupewa cheti cha ubora (Certificate of Conformity-CoC), utaratibu huu ulianzishwa ili kuhakikisha kuwa kuna ubora wa bidhaa na usalama wa afya za watumiaji, kuhifadhi mazingira na kukataa Tanzania kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa fake na bandia, au zilizokwisha muda wa matumizi.
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Waziri wa Fedha wa kuondoa faini ya asilimia 15 kwa bidhaa zinazoingizwa nchini bila cheti cha CoC inamaanisha kuwa amefuta utaratibu wa PVoC ambapo sehemu mbalimbali duniani TBS imeweka watoa huduma (service provider). Waziri wa Fedha amefanya utafiti wa kutosha wa kuwa na mbadala wa PVoC ili kuhakikisha nchi yetu haigeuzwi kuwa dampo la bidhaa zisizo na ubora, fake, bandia au zilizokwisha muda wa matumizi ambazo ni hatari kwa afya na maisha ya Watanzania, kuua ushindani, kuua ajira na uchumi wa Watanzania, lakini pia nchi yetu inaweza kuingia kwenye migogoro ya kimataifa kwa kushindwa kuzingatia viwango.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huu ulifikiwaje na Serikali? Kitendo cha Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kuondoa faini ya cheti cha CoC na kuondoa PVoC bila kujiridhisha na uwezo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kivifaa, kirasilimali watu na fedha ni kitendo cha usaliti kwa nchi ambacho kitalingiza Taifa kwenye matatizo makubwa ya kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa zisizo na ubora. Pendekezo hili lisikubaliwe na Bunge, lakini itafutwe namna bora itakayorahisha na kuondoa kero wanazopata wafanyabiashara kwa sasa kupitia utaratibu huu.
(ii) Waziri wa Fedha anapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 kwa kuongeza Ushuru wa Barabara na Mafuta kwa kiasi cha shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo itaiwezesha Serikali kukusanya shilingi bilioni 381.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Spika, bei za nishati ya mafuta bado ziko juu sana nchini na tozo nyingi zimewekwa na Serikali, pendekezo hili linakwenda kuongeza gharama za usafiri na usafirishaji, kupanda kwa bei za bidhaa na kuchochea mfumuko wa bei na ugumu wa maisha kwa wananchi masikini. Yapo maeneo mengi ya kukusanya kodi na kufidia eneo hili. Pendekezo hili lisikubaliwe na Bunge.
(iii) Waziri wa Fedha kupendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha shilingi 20 kwa kila kilo moja ya saruji inayotoka nje ya nchi na inayozalishwa ndani ya nchi ili kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi bilioni 147.549. Vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji bei zake ziko juu hivyo kuweka ushuru wa bidhaa wa shilingi 20 kwa kilo ni kuongeza gharama za ujenzi kwa wananchi, mapato haya yanaweza kufidiwa katika maeneo mengine. Pendekezo hili lisikubaliwe na Bunge.
(iv) Waziri wa Fedha anapendekeza kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri kwa mwaka mmoja kwenye mabasi ya abiria yanayotambulika kwa HS Codes 8702.10.99 na HS Codes 8702.20.99 yanayoingizwa nchini kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka. Hatua hii inalenga kupunguza gharama za uingizaji wa mabasi hayo ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi. Pendekezo hili linapunguza mapato ya Serikali bila sababu za msingi hivyo lisikubaliwe na Bunge.
(v) Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za Marekani 500 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (refined), hatua hizi kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.258. Pendekezo la kushusha Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 hadi asilimia 25 linaondoa ulinzi wa viwanda na kuua bei na soko la wazalishaji wa ndani wa mazao ya mbegu ikiwemo alizeti, Bunge lisikubali pendekezo hili. Uchambuzi zaidi kwenye eneo hili utafanyika kipindi cha kuujadili na kupitisha Finance Bill.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuadimika kwa dola za Marekani; taarifa ya Waziri na ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeeleza sababu za kuadimika kwa dola za Marekani na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali, lakini wananchi na wafanyabishara wanalalamika juu ya kuadimika kwa dola za Marekani, kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni na kusababisha kushindwa kuhudumia mahitaji ya malipo ya uagizaji bidhaa nje ya nchi. Pamoja na sababu zilizotajwa lakini sababu kubwa ya kuadimika kwa dola za Marekani inalotokana na kukosekana kwa mifumo imara ya udhibiti na usimamizi hafifu wa Sera za Fedha na Bajeti (Fiscal and Monetary Policy) ambapo kumesababisha mahitaji na matumizi makubwa ya dola za Marekani nchini kama ifuatavyo:-
(i) Hakuna mkakati madhubuti uliowekwa na Serikali wa kuzuia uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi zinazozalishwa nchini hali inayosababisha uhitaji na matumizi ya dola pasipo na sababu za msingi. Mfano kuruhusu biashara holela ya kuuza na kuingiza mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi nje nchi. Pia bidhaa za misitu na kadhalika, ununuzi wa chanjo za mifugo nje ya nchi wakati nchi yetu ina kiwanda kinachozalisha chanjo cha Hester Biosciences Africa Limited na Kiwanda cha TVI Kibaha na kuagiza dawa za kuogesha mifugo nje ya nchi wakati ndani ya nchi tuna kiwanda cha Farm Base Ltd.
(ii) Serikali kuajiri wazabuni na wakandarasi kutoka nje ya nchi hata kwa miradi ambayo ingeweza kutekelezwa na Watanzania ambapo hulazimika kulipa dola za Marekani badala ya shilingi ya Tanzania. Mfano ukarabati wa Kivuko cha Mv Magogoni (shilingi bilioni 7.5), Mkataba wa Tech Mahindra na TANESCO (shilingi bilioni 70) kujenga mfumo wa TEHAMA, ujenzi wa barabara ya bypass huko Maswa (shilingi bilioni 12) na miradi mingine mingi ya barabara, umeme, TEHAMA, maji, madaraja na kadhalika.
(iii) Kukosekana kwa mikakati thabiti ya kudhibiti soko haramu la kubadilisha fedha za kigeni ambapo kumepelekea soko kubwa lisilo rasmi la kubadilisha fedha za kigeni nchini (black-market).
(iv) Utoroshaji wa fedha nyingi za kigeni kwenda nje ya nchi na utakasishaji wa fedha haramu hali inayopelekea matumizi na mahitaji makubwa ya dola nchini. Taarifa FIU ya kuishia Aprili, 2023 inaonesha taarifa shuku za fedha taslimu zenye thamani ya shilingi trilioni 56.65 na usafirishaji fedha kwa njia ya kielektroniki zenye thamani ya shilingi trilioni 222.81 ikijumuisha usafirishaji wa fedha taslimu na hati za malipo kupitia mipakani. Hii ni ishara kuwa kuna ukwepaji mkubwa wa kodi na utoroshaji wa fedha nje ya nchi. Hotuba ya Waziri wa Fedha haina suluhisho juu ya changamoto hizi, ninashauri Serikali kupitia bajeti hii iimarishe mifumo ya udhibiti na uzingatiaji wa sera za fedha na bajeti ili kuimarisha hali ya uchumi na upatikanaji wa dola nchini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu usimamizi wa fedha za umma; usimamizi dhaifu wa fedha za umma ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa bajeti nchini, mamlaka za ukaguzi na uchunguzi za CAG, PPRA, FIU na PCCB na Mbio za Mwenge zimekuwa zikitoa taarifa za ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma hali inayoonesha kuwa hatuko vizuri katika usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma. Maeneo ambayo yanaripotiwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, matumizi nje ya bajeti, ukopaji holela wa mikopo, matumizi yasiyo na vielelezo, kushindwa kukusanya mapato ya Serikali bila sababu za msingi na wizi na ubadhirifu wa fedha za umma. Mfano Wizara ya Kilimo ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa mbolea ya ruzuku, lakini hadi kufikia Aprili, 2023 ilikuwa imetumia kiasi cha shilingi bilioni 218 zaidi ya shilingi bilioni 68 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge. Lakini pia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na TRC kufanya manunuzi kwa kuacha bei ya ushindani na kutumia single source na kuisababishia hasara Serikali ya takribani shilingi trilioni nne.
Mheshimiwa Spika, licha ya matukio hayo ya ubadhirifu, wizi na ufisadi wa fedha za umma, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na badala yake wahusika kuendelea kuwa katika Ofisi za Serikali na wakiendelea kutumia nguvu kubwa kila leo kujisafisha mbele ya umma. Utekelezaji wa mapendekezo na maazimio ya Bunge kuhusu hoja za CAG nao umekuwa wa kusuasua ambapo hadi sasa taarifa ya utekelezaji ya hoja za mwaka 2020/2021 na mwaka 2021/2022 hazijawasilishwa. Mamlaka za kuchukua hatua zote zimekaa kimya juu ya ripoti ya CAG na zingine kurushiana mpira mfano Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba kupitia hotuba yake Ibara ya 63 anazilaumu mamlaka zingine kwa kujidogosha na kushindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya watuhumiwa wa ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma. Haya ni maneno mazuri kutoka kwa Waziri kuona Mamlaka za DCI, TAKUKURU na DPP hazichukui hatua ingawa yeye binafsi akiwa mhusika mkuu hajaeleza amechukua hatua gani?
Aidha, awali wakati nikichangia Bungeni hotuba ya Waziri Mkuu nilieleza kuwa kwenye uchambuzi wangu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/2022 nilibaini ubadhirifu wa zaidi ya trilioni 30 lakini hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa dhidi ya hatua zilizochukuliwa kwa wahusika. Lakini pia jambo lingine la kushangaza zaidi CAG ameshindwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 47(3) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008 (The Public Audit Act) kuwafikisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) watuhumiwa aliojiridhisha pasipo mashaka kuhusika na ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani.
Kuhusu mikataba; (i) kwa nini Serikali inaendelea kuingia mikataba ya raslimali za Taifa kwa usiri mkubwa kinyume cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act, 2015 na Sheria ya The Natural Wealth and permanent Sovereignty Act No. 5 ya mwaka 2017 ambazo zinataka kuweka uwazi wa masharti ya mikataba kwenye hatua za awali na kupata kibali cha Bunge. Mfano Mkataba wa LNG, Mkataba wa IGA wa Bandari na Mkataba wa Mradi wa barabara wa PPP.
(ii) Je, kwa nini jedwali la mikataba yenye thamani ya trilioni 91 iliyofanyiwa upekuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali halijawasilishwa ili lisomwe pamoja na Mpango wa Maendeleo na hotuba ya Bajeti ya Serikali?
Waheshimiwa Wabunge, eneo hili tusipoliangalia vizuri Serikali inaweza kuingia kwenye mikataba ambayo hatujakubaliana, haimo kwenye bajeti wala kwenye Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano. Pia Serikali inaweza kuingia kwenye mikataba ambayo nchi haina uwezo wa kiuchumi kuihudumia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu sekta binafsi; (i) kuimarisha sekta za uzalishaji bidhaa za kuuza nje ya nchi ambapo Mfuko wa Dhamana kwa Wakopaji Wanaozalisha Bidhaa za Kuuza Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme - ECGS) na Mfuko wa Dhamana wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Entreprises Credit Guarantee Scheme - SMECGS) kutengewa zaidi ya shilingi bilioni 600. Hii ni hatua nzuri na ya kupongezwa ingawa fedha zilizotengwa kwenye eneo husika ni kidogo na haziwezi kukidhi mahitaji, lakini pia lazima kujipanga na usimamizi wa fedha hizi ili ziwafikie walengwa na kuleta tija iliyokusudiwa, kwani uzoefu uliopo fedha za aina hii hutumika vibaya. Mfano mabilioni ya JK, fedha za kufidia hasara iliyosababishwa na mtikisiko wa uchumi duniani (financial crisis), na asilimia 10 ya Halmashauri kwa ajili ya makundi maalum.
(ii) Utoaji wa mikopo, riba na dhamana katika mabenki; viwango vya riba vimepungua kwa kasi ndogo kutoka asilimia 16.31 Aprili, 2022 hadi kufikia asilimia 15.91 Aprili, 2023 hali inayopelekea gharama za biashara na uwekezaji kuendelea kuwa juu ingawa hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) zinatia matumaini. Niipongeze Benki ya CRDB, NMB, TIB, TCB, AZANIA, TADB, BOA, PASS na kadhalika kwa namna zinavyoendelea kutoa mikopo nchini na kuwezesha upatikanaji wa mitaji na fedha za uwekezaji. Serikali ichukue hatua zaidi za kushusha viwango vya riba ili kupunguza gharama za biashara na uwekezaji na ugumu wa maisha, pia kuwezesha Watanzania kupata dhamana ya mikopo mikubwa ili waweze kushiriki katika zabuni na kandarasi kubwa za barabara, umeme, maji na kadhalika.
(iii) Malimbikizo ya VAT refunds imekuwa ni tatizo linalolamikiwa na walipa kodi wengi nchini hali inayosababisha kuua mitaji, ajira na kudhoofisha biashara na uwekezaji nchini. Kufikia Machi, 2023 Serikali ilikuwa imelipa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 836 hii ni hatua nzuri na ya kupongeza ingawa Waziri hajaeleza ni malimbikizo ya shilingi ngapi ya VAT refunds yanadaiwa na walipa kodi nchini. Nini mkakati wa Serikali kupitia bajeti hii wa kumaliza tatizo la madai ya marejesho ya kodi?
(iv) Malimbikizo ya madeni makubwa ya wakandarasi na wazabuni; eneo hili limekuwa na malalamiko ya muda mrefu hali inayosababisha kuua ajira, mitaji, kufisilika na wengine kupoteza maisha. Kufikia Aprili, 2023 Serikali ilikuwa imelipa kiasi cha shilingi trilioni 1.2 hii ni hatua nzuri ingawa Waziri hajaeleza hadi sasa Serikali inadaiwa madeni ya kiasi gani? Nini mkakati wa Serikali kupitia bajeti hii wa kumaliza tatizo hili la madeni ya muda mrefu? Kulimbikiza madeni ni kinyume cha kifungu cha 52(1) cha Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 pamoja na Waraka Namba 4 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali wenye Kumb. CBA187/355/01/15 wa tarehe 31 Disemba, 2014.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya kuishia tarehe 30 Juni, 2022 inaonesha madeni ya wazabuni na wakandarasi ya muda mrefu yalifikia trilioni 3.4. Ucheleweshaji wa malipo na uhakiki wa madeni usio na mwisho umekuwa ukikera sana wananchi huku upande wa wazabuni na wakandarasi wa kutoka nje ya nchi wakilipwa kwa wakati na hata wakicheleweshewa malipo yao wanalipwa pamoja na faini. Mwaka wa fedha 2021/2022 malipo ya tozo za riba ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi, wazabuni, bima na mifuko ya hifadhi ya jamii bila sababu za msingi ilikuwa shilingi bilioni 418.5. Nini kinachosababisha malimbikizo ya madeni hayo wakati fedha zimeidhinishwa katika mwaka husika?
(v) Katakata ya umeme na migao isiyoisha ya umeme imekuwa kikwazo kikubwa cha biashara na uwekezaji nchini pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika sekta ya nishati na kuongeza uzalishaji wa umeme katika Gridi ya Taifa bado tatizo la mgao wa umeme ni kubwa na linaathiri uzalishaji. Majibu yanayotolewa na Wizara ya Nishati yanakinzana na hayana ukweli, lakini pia Vituo vya Miito ya Simu (Unified Call Centre) kuunganishwa na kuendeshwa na kampuni binafsi umeshusha viwango vya utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Spika, hitimisho; bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha haitoi suluhisho la tatizo la mfumuko wa bei na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi kwa sasa, udhibiti hafifu wa viwango vya riba na viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni. Bajeti imeshindwa kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti hali itakayopelekea kuimarika kwa biashara za magendo, biashara haramu na utoroshaji wa raslimali za taifa nje ya nchi. Bajeti haina mkakati madhubuti wa kudhibiti upotevu wa mapato na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, lakini pia bajeti hii haitoi ulinzi wa ajira za Watanzania, viwanda na wawekezaji wa ndani. Hivyo bajeti hii kama itapita kama ilivyowasilishwa pamoja na Finance Bill italisababishia Taifa matatizo makubwa. Bajeti hii sio pro-poor budget.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.