Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa hotuba nzuri ya Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ile ya Bajeti Kuu ya mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, michango yangu itajikita kwenye mambo yafuatayo nikianza na migogoro ya Ushirika Mkoani Kilimanjaro; kumekuwepo na migogoro mingi inayohusisha uporaji wa mashamba au matumizi mabaya ya mashamba yanayomilikiwa na vyama vingi vya ushirika mkoani Kilimanjaro. Mengi ya mashamba haya ni yale yaliyotaifishwa na Serikali kufuatilia kuanzishwa ka Azimio la Arusha na kukabidhiwa vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Spika, migogoro hii inasababishwa na viongozi wa ushirika na imezidi kutafuna wananchi masikini hususani wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro. Kwa kiasi kikubwa migogoro hii husababishwa na viongozi wa bodi za vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Spika, utafiti niliofanya unaonesha kuwa katika Wilaya za Siha, Hai, Rombo na Moshi kuna migogoro ambayo Serikali inapaswa kuweka jicho ili kulinda mali za wakulima maskini ambao wanatapeliwa mashamba yao na wajanja wachache. Kwa mfano, katika Wilaya ya Siha upande wa West Kilimanjaro kuna shida kubwa na wananchi wanaishi kama wakimbizi kwa sababu ardhi imehodhiwa na watu wachache kinyume cha matakwa ya wanaushiriia wengi.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ichukue hatua ya makusudi kuyanusuru mashamba haya kwa manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pili ni kuhusu ukataji holela wa miti ya asili na uharibifu wa vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro; huku mkoani Kilimanjaro katika Wilaya za Siha, Hai, Moshi na Rombo kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa kukata miti ya asili kama vile Mikufi katika maeneo ya mtoni ambako kuna vyanzo vya maji. Majangili hutumia chainsaw kuangamiza rasilimali za asili za Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limekuwa ni changamoto inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na tayari limesababisha mito kukauka na kuathiri upatikanaji wa maji ya kunywa na ya kumwagilia mashamba. Ninaishauri Serikali ichukue hatua kali mapema za kulinda maeneo haya. Katika jambo hili kubwa sheria za nchi zizingatiwe ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika kusababisha uharibifu kwa kuzishirikisha idara za misitu, mamlaka za maji na jeshi kulinda na kutunza vyanzo hivyo.
Kuhusu migogoro katika vyanzo vya maji mkoani Kilimanjaro; baadhi ya maeneo ya Jimbo la Moshi Vijijini yanakabiliwa na shida kubwa ya majisafi na salama ya kunywa. Juhudi kubwa zimefanywa na mamlaka husika kuwapelekea wananchi maji kupitia miradi inayofadhiliwa na Serikali mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha kuona kwamba baadhi ya wananchi walio karibu na vyanzo vya maji katika maeneo ya Moshi Vijijini (Kimochi, Oldmoshi Mashariki, Kibosho Kati) wanapinga miradi hiyo isijengwe pamoja na wenzao kukabiliwa na shida kubwa ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana kuhusu umiliki wa rasilimali hizi za maji. Kuna wanaofikiria hizo rasilimali ni mali zao binafsi na si za Taifa kama sheria inavyotamka.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, kumekuwepo na changamoto kwenye ujenzi wa miradi ya maji. Kwa makusudi, baadhi ya wananchi wenye nia ovu wamekuwa wa kuzuia na kuhujumu ujenzi wa miradi katika maeneo niliyotaja. Kwa mantiki hii, ninaishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu rasilimali za maji na umuhimu wa kushirikiana ili kulinda na kupeleka huduma ya maji kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, changamoto zinazokikabili Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka; kuna changamoto zinazokikabili Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka ambazo kwa kiwango kikubwa zimeshusha hadhi yake ya kuwa Chuo cha Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto hiyo ni kupungua kwa idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaojiunga na Chuo hicho kila mwaka. Changamoto iliyopo ni ile ya masharti magumu kwenye mfumo wetu yanayosababisha baadhi ya masomo yanayotolewa na nchi nyingine yasitambuliwe chuoni hapo kwa wanafunzi wanaotoka nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hili, ni vyema vyombo vyetu vya udhibiti na usimamizi wa elimu hapa nchini (TCU na NACTE) viangalie namna ya kurekebisha kanuni ili kuruhusu wanafunzi kutoka mataifa ya nje kuja na kupata elimu hapa nchini. Hii ni pamoja na kutambua sifa, vyeti na masomo yanayotolewa na nchi nyingine katika udahili hapo chuoni Mweka.
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango yangu hapo juu, naunga mkono hoja.