Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja Kuhusu Bei ya Kuuza na Kununulia Mahindi

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hoja Kuhusu Bei ya Kuuza na Kununulia Mahindi

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza, tuweke wazi kwamba Serikali hatujazuia na hatujafunga wafanyabiashara kuuza mazao nje hasa zao hili la mahindi.

Mheshimiwa Spika, hoja kubwa ambayo Serikali tunakuja nayo ni kuona namna gani tunarasimisha biashara zote kwenye sekta zote ikiwemo hii ambayo imekuwa na changamoto kubwa sana, sekta ya kilimo, kwa maana ya zao hili la mahindi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, mwaka jana kama ambavyo wachangiaji wamesema kulikuwa na changamoto kubwa sana ya bei ya mazao mbalimbali ikiwemo mazao ya chakula kupanda bei na kukithiri vile ambavyo tumezoea. Sababu mojawapo ilikuwa ni hii ya kutokuratibu vizuri biashara ya mazao ya kilimo na hasa mazao ya chakula.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tunataka tuhakikishe kwamba tunarasimisha biashara zote ikiwemo ya kuuza mazao ya chakula ili wafanyabiashara waweze kuwa na bei nzuri ya kununua kwa wakulima. Kwa sababu kumekuwa na taratibu za walanguzi na hasa wengine kutoka nje ya nchi kwenda kununua kwa wakulima kule chini kwa bei ya chini ambayo haina maslahi wala tija kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, pili, tunataka tuone kwa uratibu huu maana yake na yule mkulima wa chini anakwenda kuuza kwa vipimo na si kwa zile njia ambazo tulizoea za lumbesa, ndonya, ndoo na kadhalika. Hii imeenda kumuumiza mkulima kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, la tatu, tunataka tu–formalize kwamba, sasa hawa wanaofanya biashara wawe na leseni na sasa hivi tumerahisisha kupitia kituo cha pamoja kutoa leseni ambazo zinawasaidia wafanyabiashara kufuata taratibu zote ili pia waweze kuchangia pato la Taifa katika kulipa kodi, lakini pia kumwezesha mkulima aweze kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, nne, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, tunadhani sasa ili kusaidia wakati huu kabla ya taratibu kukamilika, NFRA nao waendelee kununua kwa bei ambayo tunadhani itakuwa haimuumizi mkulima, lakini pia ni faida kwa mfanyabiashara ambaye atakuwa amefuata taratibu zote ili aweze kuuza kokote atakakoweza kuuza. Vile vile, hata mkulima mwenyewe, kuna wakulima ambao wana mazao ya kutosha wanaweza kuuza hata nje kama watafuata utaratibu huu ambao tumesema.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.