Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Nianze kwa kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiona yote yanayofanyika kwenye nchi yetu ni kwa sababu ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini hawezi kufanya kazi mwenyewe lazima wawepo washauri. Kwa upande wa fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ameonekana kujipambanua na kumshauri Rais ipasavyo. Kwa hiyo nimpongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwenye bajeti yetu tumeweka vipaumbele vingi, lakini ili tuweze kutekeleza yale yote ambayo tumesema ni lazima tusimamie makusanyo na fedha na tuweke nguvu kwenye Mamlaka yetu ya Mapato (TRA). Kuna maeneo ambayo tunaona hatukusanyi vizuri na ili tuweze kutekeleza yote kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni lazima tuwe na fedha ambazo zinatosheleza kutekeleza miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja nimwombe Mheshimiwa Waziri, kila siku tumekuwa tukizungumza he is a humble person. Nimemwambia kule Loliondo tunahitaji Kituo cha Forodha eneo la Olaika, Ololosokwani ambapo wananchi wanatoka kilometa 500 mpaka Namanga ndiyo wakapate huduma. Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na unavyojua sisi hatuna barabara ya lami ni Wilaya ya Ngorongoro tu ndiyo bado hatujaunganishwa na Mkoa wa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa imagine mtu anatoka Waso – Loliondo mpaka Namanga kilometa 501.5 kwa ajili ya kufuata huduma. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nimwombe TRA walishafanya upembuzi yakinifu mwaka 2016, wameweka mpaka miundombinu ya maji, lakini mpaka leo hawajajenga, nimwombe sana atafute fedha popote atejengee kituo cha forodha. Wananchi wa Ngorongoro watamshukuru na watamshukuru Mheshimiwa Rais kwa yote ambayo wanatenda pamoja na hicho kituo cha forodha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Wilaya yetu ya Ngorongoro bado hatujaunganishwa na Mkoa wa Arusha. Ukijaribu kuangalia wilaya zingine zote saba zimeunganishwa kwa lami na mkoa, lakini sisi hatujaunganishwa. Tunahitaji na ukijaribu kwenda kule kwetu usafiri ni wa shida. Hata leo Mawaziri ukiwaambia njooni Ngorongoro, ukimwambia atatembea kilometa 300 rough road anaanza kufikiria hapo kweli nitarudi salama? Naomba basi na sisi watukumbuke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Makamu wa Rais aliagiza kwamba kilometa 39 kutoka Ngaresero mpaka Engaruka ziingizwe kwenye bajeti, zimeingizwa. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu akiona tu Barabara ya Loliondo kwa ajili ya lami naomba apitishe usiku hata asisubiri asubuhi kwa sababu wale wananchi wanateseka. Unaambiwa sisi tuna gari moja ya Loliondo Coach, ndiyo inatoka Arusha kila siku kwenda Loliondo, kwa sababu magari mengine yakija, kesho yake hayawezi kurudi kwa sababu ya miundombinu iliyopo. Kukodisha gari kutoka Arusha mpaka Loliondo kwa ajili ya huduma ya wananchi na biashara wananchi wanashindwa kufanya biashara na kuboresha maisha yao kwa sababu ya ughali wa maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipata barabara hii itatusaidia na sisi kuongeza uchumi wa wilaya yetu na huku pia tukijua kwamba barabara ile kutoka Kigongoni kupita Oldonyo Lengai mpaka Loliondo ndiyo watapita watalii wataenda mpaka Serengeti. Kwa hiyo niwaombe sana Serikali, tujaribu kuangalia namna tuharakishe barabara ile, tuweke hata kwenye mpango wa EPC+F, itatusaidia kuboresha maisha ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Wilaya ya Ngorongoro tuna kata 28, lakini mpaka leo tuna vituo vya afya sita tu, zahanati tunazo 31 kati ya vijiji 62. Tulikuwa na huduma na fly medical service, TCIAA wanasema kwamba ni lazima wasajiliwe nchini, SMS wameweza kufanya kazi kwa miaka 40. Leo Wilaya ya Ngorongoro vifo vya akinamama na watoto vimeongezeka ghafla kwa sababu ndege ile ndiyo ilikuwa inawasaidia. Kwa hiyo nimwombe sana Waziri, wanasema lazima tulipe kodi, niombe washirikiane na Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Afya, wale watu tuwape kibali cha kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo mtu amekuja, amefanya kazi miaka 40, halafu leo unakuja kumkatisha kwamba tunataka ujisajili, tunataka ulipe kodi na anatoa huduma ambayo Serikali imeshindwa kutoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)